Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Usipige Risasi!
Kaylee Baldwin, Arizona, Marekani
Mara ya kwanza nilipokutana naye, nilikuwa nimeshikilia fidla yangu.
Alijiburuza hadi karibu nami wakati nilipokuwa nikitembea kuelekea chumba cha chakula cha mchana, sanduku langu la fidla likipigapiga mguu wangu.
“Fidla,” alisema huku akinikaribia.
“Ndio,” nilisema.
Kwa kweli sikuwa nimewahi kuzungumza na mtu ye yote mwenye ulemavu na sikujua kipi kingine cha kusema. Alinifuata na hadi kwenye meza yangu na kuketi kando yangu, akiashiria sanduku la fidla yangu.
“Fidla,” alisema tena.
Nilifungua sanduku langu na macho yake yakang’aa. Kwa fujo sana, akakwaruza nyuzi zake. Moyo wangu ulipiga kwa mshindo nilipofikiria uzi ukikatika kutoka fidla yangu, na polepole nikafunga sanduku. Alinizingira kwa kumbatio kabla ya kuondoka.
Nilimuona mara nyingi baada ya hii.
Kila aliponiona, angeviringisha mikono yake mabegani mwangu huku akibusu juu ya kichwa changu.
Kwa muda ulisalia katika shule ya upili, kila mara nilijaribu kumkwepa nilipomwona akija. Aliponipata na kunigubika na kumbatio na busu zake zilizolowa mate, nilizivumilia kwa sekunde chache na tabasamu la kulazimisha kisha ningeondoka haraka bila ya kusema lolote.
“La, hasha,” nilisemea mashavuni nilipomwona kwenye burudani yangu ya okestra ya mwisho wa shule ya upili. Baada ya burudani, alipindapinda kuelekea nilipokuwa nimesimama na marafiki zangu nje ya ukumbi.
Marafiki zangu walirudi nyuma aliponikaribia akitabasamu, mikono yake ilikuwa wazi tayari kukumbatia.
“William!”
Niligeuka na kumwona mwanamke akikimbia pole pole kuelekea tulipokuwa.
“Pole,” alisema, wakiunganisha mkono yao. “William anapenda fidla. Aliniomba nimlete katika burudani ya usiku wa leo. Twende, mpenzi.”
Hadi wakati huo, sikuwa nimegundua kuwa hata sikujua jina lake. Nilikuwa nimekutana na William miaka miwili kabla lakini nilitumia muda mwingi nikimkwepa kiasi cha kwamba sikuwa nimefanya jitihada ya kweli ya kumjua. Nilipomtazama William na mamake wakiondoka, mawimbi ya aibu yalipita juu yangu.
Miaka kadhaa baadaye, baada ya kuolewa, nilijifungua mvulana mzuri mdogo aliyekuwa na Down’s Syndrome ambaye tulimwita Spencer. Mara nyingi nilipata mawazo yangu yakiwa juu ya William kwa muda mrefu nikiwa namwangalia mwanangu, na nikawa najiuliza ikiwa Spencer angekuwa na matukio sawa na yake. Watu wangemkwepa kwa sababu alibusu sana au alibana sana alipokumbatia? Rika lake wangekuwa hawana faraja kwa sababu ya udhaifu wake?
Spencer alipokuwa na umri wa miezi minne, nilimpeleka katika hospitali ya mtaani kwetu ili kumwona tabibu. Nilipokuwa namuondoa kwenye gari, niliwaona watu wawili wakiondoka hospitalini. Kwa mshangao, niligundua ilikuwa William na mamake.
“William!” Nilimwita tulipokaribia, moyo wangu ukipiga kwa nguvu.
“Halo!” Alitembea kwa mapozi katika maegesho, na tabasamu kubwa usoni. Alinyoosha mkono wake mbele na kushika wangu kwa salamu za shauku kubwa.
“Hujambo?” Nilimwuliza.
“Fidla,” alisema, msisimko ukionekana machoni mwake.
Fidla. Alinikumbuka pia. “Ndio,” Nilisema kwa sauti ya kwikwi machozi na kicheko, “nilipiga fidla.”
Tulipokuwa tukizungumza, moyo wangu uliinuka kwa maombi kwa ajili ya huruma nyororo za Baba mpendwa wa Mbinguni ambaye alijua kiasi gani nilitamani kukutana na William tena. Ninashukuru kwamba Mungu aliniona—mama kijana aliyekuwa amezidiwa na changamoto za afya ya mwanangu na wasiwasi wa siku za usoni—na kunipa jambo ambalo lilinikumbusha kuwa Yeye anatufahamu.