Mzee Ronald A. Rasband: Kiongozi Mwenye Kipaji, Baba Mwaminifu
Ron Rasband kamwe hakuwa na shaka kwamba angetumikia misheni. Swali pekee ambalo kijana huyu wa miaka 19 alikuwa nalo alipokuwa akifungua barua ya wito wake wa kutumikia kama mmisionari lilikuwa ni wapi angehudumu.
“Baba yangu alikwenda misheni huko Ujerumani. “Kaka yangu mkubwa alikwenda misheni huko Ujerumani. “Shemeji yangu mtarajiwa alikwenda misheni huko Ujerumani,” anakumbuka. “Nilidhani nilikuwa naenda Ujerumani.”
Lakini Bwana alikuwa na mipango tofauti. Badala yake, Ron alikuwa ameitwa, katika Misheni ya Eastern States, iliyokuwa na makao makuu yake kule Jijini New York, Marekani. Akiwa amesikitika, alichukua barua ya wito wake hadi chumba chake cha kulala, akapiga magoti kando ya kitanda chake, akaomba, bila mpangilio maalumu akafungua maandiko yake, na akaanza kusoma:
“Tazama, na lo, ninao watu wengi katika eneo hili, katika maeneo ya jirani; na mlango wenye kuleta matokeo yanayotakiwa utafunguliwa katika maeneo ya jirani katika nchi za mashariki.
“Kwa hiyo, Mimi, Bwana, nimewaruhusu ninyi kuja mahali hapa; na hivyo niliona ni muhimu kwa wokovu wa wanadamu” (M&M 100:3–4; mkazo umeongezwa).
Mara moja, Roho Mtakatifu akamthibitishia Ron kwamba wito wake katika Misheni ya Eastern States haukuwa makosa.
“Niligeuka kutoka kuwa mwenye masikitiko hadi kuwa na msukumo wangu wa kwanza kati ya misukumo mingi ya kimaandiko kuwa huko ndiko Bwana alikohitaji mimi niende,” anakumbuka. “Hilo lilikuwa tukio la muhimu sana kwangu.”
Misheni yake kule Eastern States ilikuwa ya kwanza kati ya miito kadhaa ya Kanisa ambayo ingempeleka sehemu ambazo kamwe hangetarajia kwenda. Na kila wito—kama mwalimu, askofu, mjumbe wa baraza kuu, rais wa misheni, mshiriki wa Sabini, Rais Kiongozi wa Sabini, na Mtume wa Bwana Yesu Kristo—Mzee Ronald A. Rasband amekubali mapenzi ya Bwana na ameendelea kumtegemea Roho wake akiwa anawahudumia watoto wa Mungu.
Alizaliwa na Wazazi Wema
Katika Mahubiri yake kama Mtume wa Yesu Kristo, Mzee Rasband alionyesha shukrani zake za dhati kwa ukoo wake. “Nilizaliwa na wazazi wema katika injili,” alisema, “na wao pia walitokana na wazazi wema vizazi sita vilivyopita.”1
Mama yake, Verda Anderson Rasband, alikuwa kiongozi mpendwa ambaye aliulea upendo wa maandiko wa kijana Ron. Baba yake, Rulon Hawkins Rasband, alikuwa mwenye ukuhani mwaminifu ambaye alionyesha mfano wa maadili ya kufanya kazi kwa bidii.
Alizaliwa Februari 6, 1951, jijini Salt Lake, Utah, Marekani, Ronald A. (Anderson) Rasband alikuwa mtoto wa pekee wa muungano wa wazazi wake. Wote wawili walikuwa wameshawahi funga ndoa na kutalikiana, Ron alilelewa chini ya utunzaji ulioongezeka wa kaka wawili wakubwa na dada mmoja mkubwa.
“Alikuwa kiunganishi cha wazazi wetu, kwa hivyo sisi sote tulimpenda,” anasema dada yake, Nancy Schindler. “Ron hakuwaruhusu Mama na Baba kusimama pamoja au kuketi pamoja bila yeye kuwa katikati yao.”
Ron kwa kawaida alikuwa mvulana mzuri, lakini anakiri kuwa kwa upande mwingine alikuwa na utundu.
“Zaidi ya mara chache, walimu wangu [wa Msingi] walimwendea mama yangu, rais wa Msingi wa kigingi, na kusema, ‘Yule Ronnie Rasband ni mtoto mdogo mtukutu,’” anasema. “Lakini kamwe hawakufa moyo juu yangu. Walinionyesha upendo mkubwa na kunialika tena darasani.”2
Kitovu cha utoto wa Ron kilikuwa Kanisa—mikutano ya kata, sherehe za kata, karamu za kata, na timu za michezo za kata. Wakati alipokuwa hana shughuli katika jumba la mikutano la Kata ya Kwanza ya Cottonwood, alikuwa anafanya vibarua, akifanya shughuli za maskauti, na akishinda na marafiki zake. Nyumbani, kitovu cha familia kilikuwa maandiko, michezo, na kazi za nyumbani.
Baba yangu alinifundisha kazi kwa njia ya mfano wake,” alisema. “Mama yangu alinifundisha kazi kwa kunifanya niifanye.”
Baba yake Ron aliendesha gari la kusambaza mikate, akiamka kila siku 10:00 alfajiri na kurejea nyumbani usiku kila siku. Mama yake alikaa nyumbani kuwalea watoto, akiongezea mapato ya familia kwa kutengeneza na kuuza wanasesere waliotengenezwa kwa kauri zenye lesi.
Uwezo wa Ron wa kuzaliwa nao katika kuongoza, kukasimisha na kufanya mambo yafanyike—ambao ungemsaidia sana katika majukumu yake ya kikazi na kanisani—ulithibitisha kuwa na manufaa mapema sana.
“Ron alipewa jukumu la kukata nyasi,” dada yake anakumbuka. Lakini Ron, kama Tom Sawyer wa Mark Twain, alikuwa na njia ya kuwashawishi wenzake kutoa usaidizi.
“Ningetazama nje, na kungekuwa na rafiki yake mkubwa akikata nyasi kwa niaba yake,” Nancy anasema. “Wiki inayofuata mmoja wa marafiki zake alikuwa akikata nyasi. Aliketi tu mbele barazani na kucheka na kufanya utani nao huku wakifanya kazi yake.”
Wazazi wake Ron walikuwa na shida kifedha, lakini familia ilikuwa na injili. “Kamwe hatukuwa na pesa nyingi,” Ron anakumbuka, “Lakini hilo halikuathiri furaha yangu.”
Aliwaamini Marafiki na Viongozi
Alipokuwa akikua, Ron alibarikiwa kuwa na marafiki wazuri na viongozi wa ukuhani waaminifu, pamoja na rais wa kigingi wakati wa ujana wake kwa miaka 14—James E. Faust (1920–2007), ambaye hatimaye alihudumu katika Akidi ya Mitume Kumi na Wawili na katika Urais wa Kwanza. Familia ya Ron ilikuwa na uhusiano wa karibu na Rais Faust na familia yake. “Siku zote alinitambua kama mmoja wa vijana wake wa Cottonwood kwa sababu alisaidia katika kunilea,” anasema.
Ron hakuwa na wakati kwa michezo ya shule alipofika katika shule ya upili kwa sababu alikuwa na kazi siku zote, lakini alitengeneza muda kwa urafiki wa kuaminika ambao umedumu maisha yake.
“Siku zote nimetazama na kupendezwa na Ron kwa vile alivyo, lakini hakuwa mkamilifu,” anasema rafiki yake wa utotoni Kraig McCleary. Kwa tabasamu, anasema, “Siku zote nimemwambia kama ataingia mbinguni, pia na mimi nitaingia kwa sababu tulifanya mambo yaliyo sawa tukiwa tunakua.”
Ron alienda misheni yake mapema 1970 lakini Kraig alikuwa akifikiria kuhusu kuahirisha misheni yake hadi baada ya msimu wa mawindo ya majira ya kupukutika majani. Hapo ndipo Ron alipompigia simu kutoka kwenye misheni yake.
“Sijui jinsi ambavyo alipata ruhusa ya kupiga simu, lakini alinishutumu kwa kukosa kusisimka zaidi juu ya kwenda kuhudumu misheni mara moja,” Ndugu McCleary anasema. “La hasha, sikuahirisha.”
Ron huita misheni yake kuwa ni tukio la “ajabu.” “Bwana alinibariki na matukio mengi ya miujiza, matukio ya kujenga imani,” anasema. “Misheni yangu ilikuwa na maana kubwa kwa maisha yangu ya kiroho.”
Ron alitumikia sehemu ya misheni yake katika visiwa vya Bermuda. Rais wa misheni yake, Harold Nephi Wilkinson, alituma tu “wamisionari mishale mikali” huko kwa sababu angeweza tu kuwatembelea mara chache.
“Tulikuwa tumeachwa peke yetu kabisa, lakini rais hakuwa na sababu ya kuwa na wasiwasi juu yetu,” Ron anakumbuka. “Kazi ilifanyika.”
“Msichana wa Ndoto” wa Delta Phi
Baada ya kumaliza misheni yake mwaka 1972, Ron alipata kazi, na akajiunga na Chuo Kikuu cha Utah majira hayo ya kupukutika majani, na kujiunga na Delta Phi Kappa, udugu wa wamisionari waliorejea kutoka misheni zao. Katika shughuli za kijamii za udugu, hakukosa kumwona mwanamke kijana aliyependeza aliyeitwa Melanie Twitchell. Melanie alikuwa mmoja wa “wasichana wa ndoto,” wa Delta Phi waliochaguliwa na waliosaidia katika shughuli za huduma za udugu.
Kama Ron, Melanie alitoka katika familia ya Watakatifu wa Siku za Mwisho walio wahudhuriaji kamili. Baba yake, alikuwa ofisa wa kijeshi wa kudumu, na mama yake hakuruhusu kuhamahama kwa kila mara kuwa kisingizio cha kukosa kuhudhuria Kanisani.
Melanie alivutiwa na ukarimu wa Ron, hisani, na elimu yake ya injili. “Nilijisemea mwenyewe, ‘Huyu ni mwanaume wa kushangaza na katu sitajali hata kama sitawahi kuwa na miadi naye. Ninataka tu kuwa rafiki yake mkubwa.’”
Kadiri uhusiano wao ulivyokuwa ukikua, Roho alithibitisha hisia zake juu ya Ron na kujitoa kwake kwa Bwana. Punde uhusiano wao ulichanua na kuwa kile Melanie anachokiita “kitabu cha hadithi, hadithi ya mahaba ya vichimbakazi.”
Mzee Rasband anasema kuwa alilingana naye kikamilifu. “Melanie alikuwa katika kila njia sawa nami katika mapenzi ya injili na katika urithi. Tulikuja kuwa marafiki wa dhati, na hapo ndipo nilipomwomba nimuoe.”
Walioana Septemba 4, 1973, katika Hekalu la Salt Lake. Kutoka wakati huo, anasema, “mwandani wake wa milele asiye na ubinafsi … amesaidia kunifinyanga kama udongo wa mfinyanzi hadi kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo aliyekwatuliwa zaidi. Upendo na msaada wake, na ule wa watoto wetu 5, na wandani wao, na wajukuu wetu 24, unaniimarisha.”3
“Na Twende zetu.”
Akiwa anahudumu kama rais wa akidi ya wazee wa kata yake ya wanafunzi waliofunga ndoa, Ron alikuja kumjua Jon Huntsman Sr., mshauri wa kata kutoka baraza kuu. Mara moja Jon alivutiwa na namna Ron alivyokuwa akiiongoza akidi hiyo.
“Alikuwa na ujuzi mkubwa wa uongozi na wa kuratibu,” anakumbuka Mzee Huntsman, ambaye alihudumu kama Sabini wa Eneo kutoka 1996 hadi 2011. “Nilifikiri ilikuwa sio kawaida kwa kijana ambaye alikuwa angali katika chuo kikuu kuweza kuendesha akidi kwa namna hii.”
Kwa muda wa miezi kadhaa, Jon alimtazama Ron akigeuza dhana kuwa vitendo alipokuwa akikamilisha majukumu ya ukuhani. Wakati nafasi ya afisa masoko mwandamizi ilipokuwa wazi katika kampuni ya Jon—ambayo ingekuja kuwa Huntsman Chemical Corporation—aliamua kuwa Ron alikuwa na ujuzi aliohitaji na akampa kazi hiyo. Nafasi hiyo ilianza wiki iliyofuata kule Ohio, Marekani.
“Nilimwambia Melanie, ‘Sitaacha shule na nihame,’” Ron anakumbuka. “Nimefanya bidii maisha yangu yote kuhitimu kutoka chuo kikuu, na sasa niko karibu kutimiza lengo langu.”
Melanie alimkumbusha Ron kwamba kupata kazi nzuri ndiyo sababu iliyomfanya kuwa shuleni.
“Ni kipi kinachokupa wasiwasi?” Aliuliza. “Ninajua jinsi ya kupakia na kuhama. Nimekuwa nikifanya hivyo maisha yangu yote. Nitakuruhusu uzungumze na mama yako kila usiku. Twende zetu.”
Imani ya Jon katika Ron ilidhihirika kuwa sawa. Chini ya ushauri wa Jon, Ron alipanda vyeo kwa haraka sana katika kampuni hiyo iliyokuwa ikizidi kukua, akaja kuwa rais wake na ofisa mkuu mwendeshaji mwaka wa 1986. Alisafiri sana kwa niaba ya Kampuni—nyumbani na kimataifa. Licha ya ratiba yake yenye shughuli nyingi, Ron alijaribu kuwa nyumbani wakati wa mwishoni mwa wiki. Na aliposafiri, mara nyingine angesafiri pamoja na wanafamilia.
“Wakati alipokuwa nyumbani, kwa kweli aliwafanya watoto wajisikie kuwa ni watu muhimu na wenye kupendwa,” Melanie anasema. Alihudhuria shughuli zao na matukio ya spoti wakati ilipowezekana. Jenessa MacPherson, mmoja wa wasichana wanne wa wana ndoa hawa, anasema kuwa majukumu ya baba yao kidini kwa siku ya Jumapili mara nyingi yalimzuia kuketi pamoja na familia yake wakati wa mikutano ya Kanisani.
“Tungepigania juu ya yule ambaye angepata kuketi pembeni yake Kanisani kwa sababu ilikuwa ni jambo geni sana kuwa naye pale,” anasema. “Ninakumbuka nikiweka mkono wangu mkononi mwake na kuwaza, ‘Ikiwa tu nitaweza kujifunza kuwa kama yeye, nitakuwa katika njia sahihi na nitakuwa nikikaribia kuwa kama Mwokozi.’ Alikuwa shujaa wangu siku zote.”
Mwana wa wanandoa hawa, Christian, anakumbuka kumbukumbu nzuri za “wakati wa baba na mwana.” Marafiki walikuja na kwenda kwa sababu ya familia kuhama sana, anasema, “lakini baba yangu siku zote alikuwa rafiki yangu wa dhati”—ijapokuwa ni wa mashinano sana.
Iwe ni kurushiana mpira wa vikapu na Christian, kucheza mchezo wa ubao na mabinti zake, au kuvua samaki na familia na marafiki zake, Ron alipenda kushinda.
“Tulipokuwa tukikua, kamwe hangeweza kumwacha mtu yeyote ashinde,” Christian anasema. “Tulihitaji kuchuma kwa kufanya kazi, lakini hilo lilitufanya kuwa bora. Na desturi hii inaendelezwa na wajukuu wake wapendwa.”
Kwa muda wa miaka mingi, familia yake Ron hawakukosa kuona jinsi kuhudumu katika uongozi Kanisani kulikuza uwezo wake wa kuonyesha upendo na huruma, kuonyesha hisia za roho, na kuwatia wengine moyo ili wafanye vyema. Baada ya kuzaliwa kwa Paxton, mjukuu wa Ron na Melaine, familia ilitegemea pakubwa sana nguvu za Ron za kiroho na kuhimili.
Paxton, alizaliwa na ugonjwa nadra sana wa kurithiwa, aliteseka kutokana na matatizo mengi sana ya kiafya ambayo yaliijaribu familia kimwili, kimawazo, na kiroho. Mzee Rasband aliita safari iliyofuatia kuzaliwa kwa Paxton “majaribu makali ya kujifunza masomo maalumu yanayounganishwa na milele.”4
Wakati wa miaka mitatu mifupi ya Paxton ulimwenguni—wakati maswali yalipokuwa mengi na majibu yakiwa machache—Mzee Rasband alisimama kama nguzo ya kiroho, akiongoza familia yake katika kutegemea nguvu ya Upatanisho wa Yesu Kristo.
Kwa kutangazwa kwa wito wake mpya, wana familia kadhaa na marafiki hawakushangazwa. “Wale kati yetu wanaomfahamu vyema,” Christian anasema, “tuliinua mikono yetu juu zaidi wakati alipopigiwa kura ya kukubalikawa kama Mtume.”
“Nitaenda Kuhudumu”
Mwaka 1996, akiwa na umri wa 45, Ron alikuwa katikati ya kazi yenye mafanikio wakati wito ulipokuja aende kuhudumu kama rais wa misheni ya New York, New York Kaskazini. Kama Mitume wa zamani, “mara moja akaziacha nyavu [zake]” (Mathayo 4:20).
“Kukubali wito kulichukua chini ya sekunde moja tu,” Mzee Rasband anasema. Alimwambia Bwana, “Unataka niende kuhudumu, nitaenda kuhudumu.”
Ron alichukua somo kubwa alilokuwa amejifunza kutoka katika matukio yake ya kikazi: “Watu ni wa maana kuliko kitu kingine chochote.”5 Na elimu hiyo na ujuzi wake wa kuongoza ulionyooka, alikuwa tayari kuanza huduma ya umisionari katika Ufalme wa Mungu.
Ron na Melanie waligundua kazi ya umisionari kule New York ikiwa na changamoto na ya kusisimua. Ron alikuwa mwepesi kugawa majukumu kwa wamisionari—na kutia moyo uaminifu wao, na kufundisha, kujenga, na kuwainua katika mchakato huo.
Katika mwaka wa 2000, miezi minane tu baada ya Ron na Melanie kukamilisha misheni yao, Ron aliitwa kuwa Sabini, mahali ambapo matayarisho yake, uzoefu wake, na vipaji vyake vingi vimelibariki Kanisa. Kama mshiriki wa Sabini, alihudumu kama mshauri katika Urais wa Eneo la Kati la Ulaya, akisaidia kusimamia kazi katika mataifa 39. Ingawaje aliondoka chuoni zaidi ya miaka 40 iliyopita, bado angali mwanafunzi mwenye bidii, akikubali ushauri endelevu kutoka kwa Ndugu zake wakubwa katika Ukuhani alipokuwa akisimamia maeneo ya Kaskazini mwa Amerika ya Magharibi, Kaskazini Magharibi, na maeneo matatu ya Utah; alihudumu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Mahekalu; na akahudumu katika Urais wa Sabini, akifanya kazi kwa karibu sana na wale Kumi na wawili.
Hivi majuzi, Mzee Rasband alisema, “Ni heshima na fadhila kubwa iliyoje kwangu kuwa mdogo miongoni mwa hawa Kumi na Wawili na kujifunza kutoka kwao katika kila njia na kila fursa.”6
“Waliyoyajua, Ninayajua”
Michoro miwili inapamba kuta za ofisi ya Mzee Rasband. Moja ni ya wamisionari wa Mormoni wakifundisha familia fulani kule Denmaki miaka ya 1850. Ya pili ni ya mmisionari wa mwanzoni Dan Jones akihubiri kutoka juu ya kisima katika Visiwa ya Uingereza. Michoro (juu kulia) inamkumbusha Mzee Rasband kuhusu ukoo wake.
“Hawa watangulizi wa mwanzoni walitoa vyote vilivyokuwa vyao kwa ajili ya injili ya Yesu Kristo na wameacha urithi kwa wazao wao kuendeleza,” ameshuhudia.7 Kilichowasukuma mababu wa Mzee Rasband kusonga mbele licha ya kuwa kati kati ya shida na mateso ndicho kinachomwezesha zaidi yeye katika wito wake mpya: ufahamu na ushuhuda wa kweli wa Bwana na kazi Yake.
“Nina mengi sana ya kujifunza katika wito wangu mpya,” amesema. “Ninajisikia mnyonge kuhusu hilo. Lakini kuna kipengele kimoja katika wito wangu ninachoweza kukifanya. Ninaweza kutoa ushuhuda ‘wa jina la Kristo ulimwenguni kote’ (M&M 107:23). Yeye yu Hai!”8
Kama kitukuu cha waanzilishi, anaongeza: “Walivyojisikia nami ninajisikia. Waliyoyajua ninayajua.”9
Na yale waliyotarajia katika watoto wao yamedhihirishwa katika maisha, mafunzo, na huduma ya Mzee Ronald A. Rasband, ambaye anafuata mfano wao na kuheshimu urithi wao anaposonga mbele kama mmoja wa mashahidi maalumu wa Bwana.