2010–2019
Majibu ya Maombi
Mkutano Mkuu wa Aprili 2019


Majibu ya Maombi

Baba anatufahamu sisi, anajua mahitaji yetu, na atatusaidia kikamilifu.

Fundisho muhimu na la kufariji la injili ya Yesu Kristo ni kwamba Baba yetu wa Mbinguni ana upendo mkamilifu kwa watoto Wake. Kwa sababu ya upendo huo mkamilifu, Anatubariki siyo tu kwa haja na mahitaji yetu lakini pia kulingana na hekima Yake isiyo na mwisho. Kama ilivyoelezewa na nabii Nefi, “Ninajua kwamba [Mungu] anawapenda watoto wake.”1

Kipengele kimoja cha upendo huo mkamilifu ni ushiriki wa Baba wa Mbinguni katika maelezo ya maisha yetu, hata wakati hatuwezi kujua au kuelewa. Tunatafuta mwongozo wa kiungu wa Baba na msaada kupitia maombi yenye hisia za moyoni, ya dhati. Tunapoheshimu maagano yetu na kujitahidi kuwa zaidi kama Mwokozi wetu, tuna haki ya kuendelea2 kupata mwongozo mtakatifu kupitia ushawishi na msukumo wa Roho Mtakatifu.

Maandiko yanatufundisha: “Maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba,”3 na Yeye “anajua vitu vyote, kwani vitu vyote vipo mbele ya macho [Yake].”4

Nabii Mormoni ni mfano wa hili. Hakuishi kuona matokeo ya kazi yake. Hata hivyo alielewa kwamba Bwana alikuwa mwangalifu katika kumwongoza. Alipohisi kutiwa msukumo kuongeza bamba ndogo za Nefi kwenye kumbukumbu zake, Mormoni aliandika: “Na ninatenda haya kwa madhumuni ya busara; kwani ninanong’onezewa, kulingana na kazi za Roho wa Bwana aliye ndani yangu. Na sasa, sijui mambo yote; lakini Bwana anajua vitu vyote vitakavyokuja; kwa hivyo, anafanya kazi ndani yangu ili nitende kulingana na nia yake.”5 Japokuwa Mormoni hakujua kuhusu kupotea baadaye kwa kurasa 116 za muswada, Bwana alijua na aliandaa njia ya kushinda kizuizi kile mapema kabla hakijatokea.

Baba anatufahamu sisi, anajua mahitaji yetu, na atatusaidia kikamilifu. Wakati mwingine msaada huo unatolewa mara moja au muda mfupi baada ya kuomba msaada wa kiungu. Wakati mwingine matamanio yetu makuu na yenye kustahili hayajibiwi kwa njia tunayotarajia, lakini tunaona kwamba Mungu ana baraka kuu katika hazina. Na wakati mwingine, matamanio yetu ya haki hayajibiwi katika maisha haya. Nitaelezea kwa mifano, kupitia matukio matatu tofauti, njia ambazo Baba yetu Mbinguni anaweza kujibu maombi yetu ya dhati Kwake.

Mwana wetu mdogo aliitwa kuhudumu kama mmisionari katika Misheni ya Ufaransa Paris. Akijiandaa kuhudumu, tulienda nae kununua mashati ya kawaida, suti, tai, soksi, na koti kubwa refu. Kwa bahati mbaya, koti kubwa refu alilolitaka halikupatikana wakati ule kwa saizi aliyoitaka. Hata hivyo, muuza duka alieleza kwamba koti lingepatikana wiki chache baadaye na lingepelekwa kwenye kituo cha mafunzo ya umisionari huko Provo kabla kijana wetu hajaondoka kwenda Ufaransa. Tulilipia lile koti na hatukufikiria chochote kiingine kulihusu.

Mwana wetu aliingia kwenye kituo cha mafunzo ya umisionari mwezi Juni, na lile koti kubwa refu lililetwa siku chache kabla ya kuondoka kwake mwezi wa Agosti. Hakulijaribu lile koti bali aliharakisha kuliweka kwenye begi lake pamoja na nguo zake na vitu vingine.

Wakati msimu wa baridi ulipokaribia huko Paris, ambako mwana wetu alikuwa akihudumu, alituandikia kwamba alilitoa koti kubwa refu na kulijaribu lakini likawa dogo. Hivyo ilitulazimu tuweke pesa ya ziada kwenye akaunti yake ya benki ili aweze kununua koti huko Paris, na alifanya hivyo. Kwa hasira ya kiwango fulani, nilimwandikia na kumwambia aligawe lile koti, kwa sababu asingeweza kulitumia.

Baadaye tulipokea barua pepe hii kutoka kwake: “Kuna baridi kali hapa. … Upepo unaonekana kuvuma kati yetu, japokuwa koti langu ni zuri na zito sana. … Nilimpa koti langu la zamani [mmisionari mwingine kwenye nyumba yetu] ambaye alisema kwamba alikuwa akiomba njia ya kupata koti linalofaa zaidi. Yeye ni muongofu wa miaka kadhaa na mama yake pekee … na mmisionari aliyembatiza ndio wanaomsaidia katika misheni yake na hivyo koti lilikuwa jibu la maombi, hivyo nilihisi furaha kuhusu tendo hilo.”6

Baba wa Mbinguni alijua kwamba mmisionari huyu aliyekuwa akihudumu huko Ufaransa yapata maili 6,200 (kilomita 10,000) mbali na nyumbani, angeweza kuhitaji koti jipya kwa ajili ya kipindi cha baridi huko Ufaransa lakini kwamba mmisionari huyu asingekuwa na uwezo wa kununua. Baba wa Mbinguni pia alijua kwamba mwana wetu angepokea kutoka duka la nguo la Provo, Utah, koti kubwa refu ambalo kwake lingekuwa dogo. Alijua kwamba wamisionari hawa wawili wangeweza kuhudumu pamoja huko Paris na kwamba koti lingekuwa jibu la maombi ya unyenyekevu na ya dhati ya mmisionari ambaye alikuwa na uhitaji wa haraka.

Mwokozi alifundisha:

“Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu.

“Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.

“Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro wengi.”7

Kwa nyakati tofauti, wakati matamanio yetu ya haki hayapatikani kwa njia tuliyo itarajia, yawezekana ikawa ni kwa faida yetu. Kwa mfano, Yusufu mwana wa Yakobo alikuwa akionewa wivu na kuchukiwa na ndugu zake kiasi cha kusuka njama za mauaji ya Yusufu. Badala yake, walimuuza kama mtumwa huko Misri.8 Kama ilitokea mtu akahisi kwamba maombi yake hayakujibiwa kwa njia aliyo tarajia, basi angekuwa Yusufu. Katika uhalisia, bahati mbaya yake iliyoonekana dhahiri ilimletea baraka nyingi na kuokoa familia yake kutokana na njaa. Baadaye, baada ya kuwa kiongozi aliyeaminika huko Misri, kwa imani kubwa na hekima aliwaambia ndugu zake:

“Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku: maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu.

“Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi: na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna.

“Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu.

“Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu;.”9

Akiwa chuoni, mwana wetu mkubwa aliajiriwa katika kazi nzuri ya muda ambayo ilikuwa na uwezo wa kumuongoza kwenye kazi nzuri, ya kudumu baada ya kuhitimu. Alifanya kazi kwa bidii kwenye kazi hii ya uanafunzi kwa miaka minne, akawa na sifa nzuri sana, na aliheshimiwa sana na wenzake na wasimamizi. Mwishoni mwa mwaka wa mwisho, ikionekana kana kwamba iliandaliwa na mbingu (angalau kwa mawazo ya kufikiri ya mwana wetu), nafasi ya kudumu ilijitokeza, na yeye alikuwa mgombea aliyeongoza, kwa kila dalili na matarajio ya kwamba, hakika, angepata kazi.

Naam, hakuajiriwa. Hakuna hata mmoja wetu aliweza kuelewa. Alikuwa amejiandaa vizuri, alifanya usaili vizuri, alikuwa mtu mwenye sifa zaidi, na alikuwa ameomba kwa matumaini na matarajio makubwa! Alikuwa amechukizwa na kuumizwa, na tukio hilo lote lilituacha sisi wote tukikuna vichwa vyetu. Kwanini Mungu alimtelekeza katika matamanio yake ya haki?

Haikuwa hadi miaka kadhaa baadaye ambapo jibu lilikuwa wazi kabisa. Kama angepata kazi ile ya ndoto yake baada ya kuhitimu, angekosa fursa moja muhimu sana ambayo sasa imedhihirisha kuwa ni kwa faida yake ya milele na baraka yake ya milele. Mungu alijua mwisho kutokea mwanzo (kama vile Ajuavyo wakati wote), na katika jambo hili, jibu la maombi mengi ya haki lilikuwa hapana, kwa faida ya matokeo ya juu ya baadaye.

Na wakati mwingine, jibu la maombi ambalo tunalitafuta kwa haki, kwa hamu kubwa, na kwa dhati halipatikani katika maisha haya.

Dada Patricia Parkinson alizaliwa akiwa anaona kawaida, lakini akiwa na miaka saba alianza kupofuka. Akiwa na miaka tisa, Pat alianza kuhudhuria Shule za Utah za Viziwi na Vipofu huko Ogden, Utah, yapata kilomita 145 (maili 90) kutoka nyumbani kwake, hali iliyomlazimu kukaa bwenini shuleni—ambayo ilijumuisha mawazo mengi kuhusu nyumbani ambako mtoto wa miaka tisa angeweza kupitia.

Akiwa na miaka 11, alipoteza kabisa uwezo wa kuona. Pat alirudi nyumbani moja kwa moja akiwa na miaka 15 ili ahudhulrie shule ya upili kwenye eneo alilokuwa akiishi. Aliendelea mpaka chuo kikuu na alihitimu shahada ya kwanza katika matatizo ya mawasiliano na saikolojia, na baada ya mapambano ya kishujaa dhidi ya maafisa usajili wa chuo ambao walikuwa na mashaka naye, aliingia shule ya juu na kuhitimu shahada ya uzamili katika lugha ya sayansi ya magonjwa. Pat sasa anafanya kazi na wanafunzi 53 wa shule ya msingi na anasimamia mafundisanifu wanne wa lugha katika shule ya wilaya yake. Anamiliki nyumba yake mwenyewe na gari yake, ambayo rafiki na ndugu zake wanaendesha wakati Pat anapohitaji usafiri.

Picha
Dada Patricia Parkinson

Akiwa na miaka 10, Pat alipangiwa kupata matibabu mengine ya kuangalia hali yake ya kutoona vizuri. Wazazi wake mara zote walimwambia nini kitakwenda kutokea kuhusu matibabu yake, lakini kwa sababu fulani hawakumwambia kuhusu utaratibu huu maalumu. Wakati wazazi wake walipomwambia kuwa utaratibu huo ulipangwa, Pat, kwa maneno ya mama yake, “alikuwa vurugu.” Pat alikimbilia chumba kingine lakini akarudi baadaye na akawaambia wazazi wake kwa hasira fulani, “Hebu niwaambie. Ninajua, Mungu Anajua, nanyi pia mnaweza kujua hili. Nitakuwa kipofu kwa maisha yangu yote!”

Miaka kadhaa baadaye, Pat alisafiri kwenda California kutembelea wanafamilia waliokuwa wakiishi kule. Akiwa nje na mpwa wake wa miaka mitatu, alimwambia,“Shangazi Pat, kwanini usimwambie tu Baba wa Mbinguni akupe macho mapya? Kwa sababu kama utamwomba Baba wa Mbinguni, Atakupa chochote utakacho. Unapaswa tu kumwomba Yeye.”

Pat alisema alikumbushwa nyuma kwa lile swali lakini alijibu, “Sawa, wakati mwingine Baba wa Mbinguni hafanyi kazi hivyo. Wakati mwingine Anakutaka wewe kujifunza kitu, na hivyo hakupi kila kitu unachotaka. Wakati mwingine unatakiwa kusubiri. Baba wa Mbinguni na Mwokozi wanajua vyema kilicho kizuri kwetu na nini tunahitaji. Hivyo, Hawatakupa wewe kila kitu unachotaka wakati unapokitaka.”

Nimemjua Pat kwa miaka mingi na hivi karibuni nilimwambia kuwa nilifurahia kwamba yeye daima ana mtazamo chanya na ni mwenye furaha. Alijibu, “Sawa, hujawahi kuwa nyumbani pamoja nami, si ndiyo? Huwa nina nyakati zangu. Nimekuwa na mapambano makali ya mfadhaiko, na nimelia sana.” Hata hivyo, aliongeza, “Kuanzia wakati nilipoanza kupoteza uoni wangu, ilikuwa ni ajabu, lakini nilijua kwamba Baba wa Mbinguni na Mwokozi walikuwa pamoja na familia yangu na mimi. Tulilishughulikia kwa njia tuliyoweza, na kwa maoni yangu, tulilishughulikia kwa njia sahihi. Nimeishia kuwa mtu mwenye mafanikio ya kutosha, na kwa ujumla nimekuwa mtu mwenye furaha. Ninakumbuka mkono Wake ukiwa katika kila kitu. Kwa wale wanaoniuliza kama nina hasira kwa sababu ni kipofu, ninawajibu, ‘Ningemkasirikia nani? Baba wa Mbinguni yupo pamoja nami katika hili; siko peke yangu. Yeye yupo pamoja nami wakati wote.’”

Kwa hali hii, matamanio ya Pat ya kutaka kuona hayatajibiwa katika maisha haya. Lakini kauli mbiu yake, aliyojifunza kutoka kwa baba yake, ni “Hili nalo litapita.”10

Rais Henry B. Eyring alisema, “Baba katika wakati huu anawajua, hisia zenu, na mahitaji ya kimwili na kiroho ya kila mtu anaye wazunguka.”11 Ukweli huu mkuu na wa kufariji unaweza kupatikana katika zoefu tatu nilizozielezea.

Akina kaka na akina dada, wakati mwingine maombi yetu yanajibiwa haraka kwa matokeo tunayo yategemea. Wakati mwingine, maombi yetu hayajibiwi kwa njia tunayo itarajia, hata hivyo kulingana na muda tunajifunza kwamba Mungu ana baraka kuu zilizoandaliwa kwa ajili yetu zaidi ya sisi tunavyo tarajia. Na wakati mwingine maombi yetu ya haki kwa Mungu hayatajibiwa katika maisha haya.12 Kama Mzee Neal A. Maxwell alivyosema, “Imani pia inajumuisha kuamini wakati wa Mungu.”13

Tuna uhakika kwamba katika njia Zake mwenyewe na wakati Wake mwenyewe, Baba wa Mbinguni atatubariki na kutatua matatizo yetu, udhalimu na kukata tamaa.

Nikimnukuu Mfalme Benyamini: “Na zaidi, ningetamani mtafakari juu ya hali ya baraka na yenye furaha ya wale wanaotii amri za Mungu. Kwani tazama, wanabarikiwa katika vitu vyote, vya muda na vya kiroho; na kama watavumilia kwa uaminifu hadi mwisho watapokewa mbinguni, kwamba hapo waishi na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho. Enyi kumbukeni, kumbukeni kwamba vitu hivi ni vya kweli; kwani Bwana Mungu ameyazungumza.”14

Ninajua kwamba Mungu anasikia maombi yetu.15 Ninajua kwamba kama Baba ajuaye yote, mwenye upendo, Yeye anajibu maombi yetu kwa ukamilifu, kulingana na busara Zake zisizo na mwisho, na katika njia ambazo zitakuwa kwa faida yetu na baraka yetu ya juu. Nashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha