Kitabu Chako cha Michezo cha Ukuhani
Tengeneza kitabu chako mwenyewe cha michezo cha jinsi utakavyojithibitisha mwenyewe kama mfuasi wa Kristo.
Desemba iliyopita, Urais wa Kwanza ulitoa tamko lililotangaza kwamba wavulana wa miaka 11 “wangeanza kuhudhuria … akidi za Ukuhani wa Haruni … mwanzoni mwa Januari katika mwaka wanapofikisha miaka 12.”1
Kama matokeo, katika sehemu ya kwanza ya mwaka huu, kulikuwa na wachache wa miaka 11 walioshtushwa ambao walidhani wangebaki katika Msingi mpaka siku yao ya kuzaliwa lakini walikuwa sasa wakipitisha sakramenti Jumapili kama mashemasi wapya wa Kanisa waliotawazwa.
Najiuliza nani alishangazwa zaidi na badiliko—mashemasi au wazazi wao. Kati ya hawa takriban mashemasi wapya80,000, wengi wako nasi usiku huu katika Kituo hiki Kikuu cha Mikutano au wanashiriki kupitia teknolojia. Karibuni katika undugu mkuu wa ukuhani!
Badiliko hili linaufanya mkutano huu kuwa wa kihistoria—yawezekana ni kundi kubwa zaidi la wenye Ukuhani lililowahi kuhudhuria kikao cha ukuhani cha mkutano mkuu. Katika nuru ya tukio hili muhimu, ninaelekeza mazungumzo yangu hasa kwa wavulana wa Ukuhani wa Haruni.
Masomo Niliyojifunza kwenye Michezo
Kama wanafunzi, wengi wenu pia mnakuza vipaji vyenu, matamanio, na mambo ya kupitisha muda kupitia shughuli za nje ya masomo shuleni au kwenye masomo ya binafsi, timu, na makundi nje ya shule, ikijumuisha michezo.
Nikiwa nimefurahia michezo maisha yangu yote, mara zote nimevutiwa na wale wanaokuza uwezo wao wa mchezo kwa kiasi ambacho wanatenda kwa kiwango cha juu. kwa mtu kuwa mzuri hasa kwenye kitu chochote, inahitaji, pamoja na kipaji chake asilia, nidhamu kubwa, dhabihu, na masaa yasiyo na idadi ya kujifunza na mazoezi. Wanamichezo kama hao mara nyingi husikia ukosoaji wa kuchukiza wa makocha na kwa hiari huweka kando kile wanachotaka sasa kwa jambo kubwa la siku za usoni.
Tunawajua waumini wa Kanisa na wenye ukuhani ambao wamepata mafanikio ya kiwango cha juu ya wanamichezo wa kulipwa. Kuna mifano mingi ya kuvutia, lakini ninaweza kuorodhesha michache tu kutokana na muda. Ungeweza kuwatambua baadhi ya wanamichezo hawa: katika baseball, Jeremy Guthrie na Bryce Harper; katika mpira wa kikapu, Jabari Parker na Jimmer Fredette; katika mpira wa mikono, Ricardo Rojas; na ligi ya ragbi, William Hopoate; na katika mpira wa miguu, Taysom Hill na Daniel Sorensen. Kila mmoja ameleta michango muhimu katika mchezo wake.
Wakati wamefanikiwa sana katika michezo yao, wanamichezo hawa wangekuwa wa kwanza kukubali kutokuwa wanamichezo wakamilifu au wanadamu wakamilifu. Wanafanya bidii kuwa wazuri zaidi katika michezo yao—na katika kuishi injili. Wananyanyuka ikiwa wamejikwaa, na kujitahidi kuvumilia hadi mwisho.
Soma Kitabu cha Michezo
Katika timu za michezo, majukumu hutengenezwa kwa ajili ya hali ya mchezo fulani na kuwekwa pamoja kwenye kitabu cha michezo. Wanamichezo hujifunza wajibu wao na jukumu maalumu kwa kila mchezo. Wachezaji wenye mafanikio husoma kitabu cha michezo kwa bidii sana kwamba, mchezo unapoitishwa, wanajua barabara, karibu bila kusita, wapi pa kwenda na nini cha kufanya.
Katika njia sawa na hiyo, sisi wenye ukuhani pia tuna timu (akidi) na kitabu cha michezo (maandiko matakatifu na maneno ya manabii wa leo).
Je unawaimarisha wana timu wenzako?
Ni vizuri kiasi gani umesoma kitabu chako cha michezo?
Je, unaelewa kikamilifu jukumu lako?
Kukabiliana na Upinzani
Kuipeleka analojia mbali zaidi, makocha wazuri wanajua nguvu na udhaifu wa timu zao vilevile ule wa wapinzani. Wanatengeneza mpango wa mchezo ambao utawapa nafasi nzuri zaidi ya ushindi. Vipi kuhusu wewe?
Unajua ni majaribu yapi yanakudhuru zaidi, na unaweza kutabiri jinsi mjaribu atakavyojaribu kukuangusha na kukuvunja moyo. Je umetengeneza mpango binafsi wa mchezo na kitabu cha michezo ili kwamba ujue jinsi ya kujibu wakati umekabiliwa na upinzani?
Unapokabiliwa na majaribu mbalimbali ya uadilifu—iwe ni katika uwepo wa wengine au ukiwa peke yako umeangalia sikirini—unajua mpango wako wa mchezo. Ikiwa rafiki anapendekeza unywe kilevi au ujaribu madawa, unajua jukumu. Umefanya mazoezi na unajua jinsi ya kujibu kabla.
Ukiwa na mpango wa mchezo, kitabu cha michezo, na ari imara ya kutimiza jukumu lako, utakuta kwamba jaribu lina nguvu ndogo juu yako. Utakuwa tayari umekwishafanya uamuzi jinsi utakavyojibu na kile utakachofanya. Hutahitaji kufanya uamuzi kila mara unapokabiliwa na jaribu.
Mmoja wa Kumi na Wawili karibuni alishiriki hadithi ambayo inaelezea kanuni hii. Kama kuhani katika shule ya upili, alikuwa akipumzika na rafiki zake. Baada ya kupata chakula, walikuwa wakiendesha gari wakati mmoja alipopendekeza waende kwenye sinema fulani. Tatizo lilikuwa alijua ilikuwa ni sinema ambayo hakupaswa kuitazama. Japokuwa haraka alihisi msukumo na shauku kuhusu hali, alikuwa amepanga kwa ajili ya hili. Hili lilikuwa ukurasa wa moja kwa moja kutoka katika kitabu chake cha michezo cha ukuhani.
Akivuta pumzi ndefu na kukusanya ujasiri wake, alitangaza, “sivutiwi na sinema hiyo. Nishusheni tu nyumbani kwangu,” ambacho walifanya. Mchezo rahisi unapelekea ushindi! Miaka kadhaa baadaye, mmoja wa rafiki aliyekuwa naye usiku ule alielezea jinsi mfano huu ulivyothibitisha kuwa nguvu kubwa kwake kwa ujasiri kukabiliana na hali kama ile katika maisha yake mwenyewe.
Kurasa kutoka Kitabu cha Michezo
Niliwauliza baadhi ya Akina kaka kupendekeza majukumu ambayo ungeweza kujumuisha katika kitabu chako cha michezo. Hapa ni baadhi ya mapendekezo yao yenye msukumo:
-
Omba kila siku kwa nuru kubwa zaidi na ushuhuda wa Yesu Kristo.
-
Sikiliza kwa makini mafundisho ya wazazi wako, askofu wako, na viongozi wako wa Wavulana na akidi.
-
Epuka ponografia na maudhui yasiyo na maadili ya mitandao ya kijamii.
-
Kumbuka ahadi ulizofanya kwa Mungu, na fanya kazi kuzitunza.
-
Soma hadithi za maandiko za manabii wakuu, na fuatisha sifa zao nzuri.
-
Bariki watoto wa Baba wa Mbinguni kupitia huduma.
-
Tafuta marafiki wema wa kukusaidia kuwa mtu unayetaka kuwa.
-
Kuwa mtaalamu kwenye app ya FamilySearch na fanyia utafiti historia yako mwenyewe ya familia.
-
Panga sehemu za kimbilio ambapo unaweza kukimbia ushawishi mbaya.
-
Penda na saidia kuimarisha waumini wengine wa akidi yako ya ukuhani.
Niliwasiliana pia na wanamichezo ambao picha zao tumetoka kuzitazama. Nilikuta ni ya kufurahisha kwamba hawajitambulishi tu kwa kile wanachofanya, kama wanamichezo wa kulipwa,bali pia wao ni nani, kama wana wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo na wenye ukuhani wa Mungu.
Sasa acha tusikilize mawazo yao:
-
Jimmer Fredette, hapa kama shemasi akijifunza kufunga tai yake, anasema: “Nimejifunza kutegemea kwa kiasi kikubwa uelewa na imani yangu ya ukweli wa injili. Hii imeniongoza kuwa … mwenye ukuhani anayestahili na zaidi ya yote—mfano chanya.”
-
Bryce Harper, hapa kama mume, anaandika: “Nilidhani umaarufu, mali, na tuzo ya MVP vingenipa furaha. Kuna kitu kilikuwa kinakosa. Hivyo, nili … jiandaa na [kuingia] hekaluni. Sasa niko kwenye njia ya [kurudi] kwa Baba yangu wa Mbinguni na kuwa na familia ya milele—ambayo ndiyo furaha kuu zaidi ulimwenguni!”
-
Daniel Sorensen, hapa kama mmisionari, anasema: “Kitabu kizuri cha michezo ni mpango ambao hutumia vipaji na nguvu za kila mshiriki wa timu. … Ninaposoma na kufanyia kazi mafundisho ya injili ya Yesu Kristo, ninaweza kujua jinsi ya kutumia uwezo wangu kutumikia katika ukuhani.”
-
Jeremy Guthrie, hapa kwa sasa akitumikia kama rais wa misheni, alishiriki: “Kama shemasi wa miaka 12 … [Nilihisi] Roho akinishuhudia [kwamba] ‘Maisha haya ndiyo wakati … wa kujitayarisha kukutana na Mungu.’2 Mpango wa mchezo ni imani katika Mungu kwenye matendo [na] toba kupitia Mwokozi. … Kitabu cha michezo kinapatikana katika maandiko matakatifu na kupitia manabii wanaoishi.
-
Jabari Parker, hapa katika utawazo wake kwenye ofisi ya mzee, anasema: “nisingeweza kufikiria mtu ambaye ningekuwa kama nisingefanya uamuzi wa kubatizwa nilipokuwa mdogo. … Ninashukuru kwamba nina Mungu katika maisha yangu kuniongoza kila siku.”
-
Ricardo Rojas, hapa kwa sasa akitumikia kama rais wa tawi, alisema: “Kupitia ukuhani wa [Mungu] [sisi] tunaweza kusaidia katika kazi yake. Tumeitwa kuwa ‘hodari na moyo wa ushujaa’3 katika kutetea ukweli.” Hii imemsaidia kufanikiwa kote uwanjani na kama mwenye ukuhani.
-
Taysom Hill, hapa kama mmisionari, anahisi kwamba injili ya Yesu Kristo imetumika kama kitabu cha michezo kwake katika maisha yake. Alishiriki, “Kuamini katika mpango wa [Mungu] na kufanya kadiri niwezavyo kutimiza jukumu langu kwenye mpango huo kumenipa hisia nzito ya amani na furaha katika maisha yangu, kwa kujua Mungu anapendezwa na juhudi zangu.”
-
William Hopoate, hapa akiwa kwenye ubarikisho wa mjukuu wake kama sehemu ya kizazi cha nne, anasema kwamba injili humsaidia yeye “kutambua mbinu za mpinzani na kutoa majibu yanayofaa kiroho ili kustahimili mishale ya moto na kuwatumikia vizuri wengine.”
Vipi kuhusu wewe? Je unatambua utambulisho wako wa juu na mtakatifu kama mwana wa Mungu, mwenye ukuhani Wake mtakatifu? Ukiwa na utambulisho huu wa milele akilini, tengeneza mpango wako wa mchezo na kitabu cha michezo cha ukuhani ambacho kitakuongoza kipindi cha nyakati za majaribu na taabu. Fikiria mbinu zote za kushambulia na kujilinda.
Mbinu za kushambulia husaidia kuimarisha shuhuda na kukuza ari ya kubaki katika njia nyembamba na iliyonyooka. Mifano hujumuisha maombi ya mara kwa mara, kusoma maandiko, kuhudhuria Kanisani na hekaluni, kulipa zaka, na kufuata ushauri unaopatikana katika kijitabu cha Kwa Nguvu ya Vijana.
Mbinu za kujilinda hujumuisha kupanga kabla jinsi ya kukabili jaribu. Unapojaribiwa kuhatarisha viwango vyako binafsi, unajua kabla nini utafanya.
Unahitaji kitabu cha michezo kwa ajili ya hilo.
Hujisikii kuomba leo? Muda wa kufanyia kazi jukumu ambalo tayari umelipanga kwenye mchezo.
Je unahisi ushuhuda wako unafifia? Una jukumu kwa ajili ya hilo. Unajua nini cha kufanya.
Wote ni Nyota Machoni pa Mungu
Ninyi ni wabebaji wa ukuhani mtakatifu wa Mungu. Kujitolea kwako kushikilia kwa uimara fimbo ya chuma kutakubadilisha kuwa kiumbe wa milele ambaye uliumbwa uwe.
Mungu anakujua na anakupenda. Atakubariki na kuongoza hatua zako.
Unaweza kudhani kwamba wewe si mtu muhimu, kwamba huna sifa ya kuwa nyota. Lakini hiyo si kweli. Je hujui kwamba Mungu ametangaza, “Mambo dhaifu ya dunia yatakuja kuyavunja yale yaliyo makubwa na yenye nguvu”?4
Hivyo je unahisi mdhaifu? usiyeonekana? Hongera, umekwisha ingia kwenye mstari!
Je unahisi usiye na umuhimu? duni? Unaweza kuwa yule ambaye Mungu anamuhitaji.
Ni mfano mkuu ulioje zaidi ya Daudi kukanyaga uwanja wa vita dhidi ya mpinzani wa kutisha, Goliati? Akimtegemea Bwana, pamoja na mpango, Daudi hakujiokoa tu yeye mwenyewe bali jeshi la Israeli!5 Fahamu kwamba Bwana atakuwa pamoja nawe unapokusanya ujasiri wako kuwa upande Wake. “Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?”6
Yeye anaweza kufungua milango na kutusaidia kupata nguvu na uwezo ambao hatukujua tuko nao.7
Wasikilizeni makocha wenu walioaminiwa, kama vile wazazi wenu, askofu, na viongozi wa Wavulana. Someni kitabu cha michezo. Someni maandiko. Jifunzeni maneno ya manabii wa leo. Tengeneza mpango wako mwenyewe wa mchezo wa jinsi utakavyojithibitisha mwenyewe kama mfuasi wa Kristo.
Fahamu kabla majukumu utakayotumia kuimarisha roho yako na kuepuka mitego ya mjaribu.
Fanya hili na Mungu atakutumia wewe.
Sasa, kuna baadhi ambao hujitenga kutoka kwenye injili na kutangatanga mbali. Baadhi hukaa majukwaani na kutazama mchezo kutokea mbali. Baadhi huchagua kukaa benchi, hata kama kocha amejaribu kuwaweka mchezoni. Ninawaalika kuokoa, kuunga mkono, na kuwapenda kama washiriki wenzenu wa timu!
Wengine wanataka kuingia mchezoni—na wanaingia. Kile chenye maana zaidi si jinsi gani wana kipaji bali jinsi gani wako radhi kujiweka uwanjani. hawasubiri namba zao ziitwe, kwa sababu wanajua andiko linalosema, “Kama unayo tamaa ya kumtumikia Mungu wewe umeitwa kwenye kazi.”8
Unaweza kujipanga kwenye mstari.
Unafanya hivyo kwa kusoma na kutimiza kitabu chako cha michezo cha ukuhani.
Njiani utajikwaa na kuanguka—pengine mara nyingi sana. Wewe si mkamilifu; kushindwa ni sehemu ya mchakato wa kustahili ambao hukuruhusu kurekebisha tabia yako na kutumikia katika njia ya huruma zaidi. Mwokozi na Upatanisho Wake usio na mwisho hutoa njia ya kushinda makosa yetu kupitia toba ya kweli.
Wanamichezo wakubwa hutumia mamia ya masaa kukamilisha kipengele kimoja kidogo cha mchezo wao. Kama mwenye ukuhani, unahitaji dhamira sawa na hiyo. Ikiwa utashindwa, tubu na jifunze kutokana na hilo. Fanya mazoezi ili uweze kufanya vizuri zaidi wakati ujao. Mwishowe, hiyo ni juu yako. Je, utasoma kitabu cha michezo?
Ninakusihi: Amini katika Bwana. Vaa silaha zote za Mungu9 na ingia mchezoni.
Kuna wachache ambao hawachezi michezo ya kulipwa kwa kiwango cha juu, lakini linapokuja suala la ufuasi, kuna wengi wanaochagua kumfuata Kristo.
Hakika, hiyo ndiyo misheni yako katika maisha haya—kujifunza njia za Bwana, kuingia njia ya ufuasi, na kujitahidi kuishi kulingana na mpango wa Mungu. Mungu atakuunga mkono na kukubariki pale unapomgeukia. Unaweza kufanya hili kwa sababu wewe ni nyota katika macho Yake.
Ninaomba kwamba mtaweka msimamo wa kuishi kwa kustahili ukuhani mtakatifu ambao mnao na kujitahidi kutimiza majukumu yenu matakatifu kila siku. Ninawabariki kwa uwezo na matamanio ya kufanya hivyo. Ninaongeza ushuhuda wangu wa nguvu ya ukuhani ambao mnao, wa manabii wanaoishi, na wa Yesu Kristo na jukumu Lake kama Mwokozi na Mkombozi wetu. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.