Kutafuta Maarifa kupitia Roho
Tunapaswa kujifunza kutambua ukweli si tu kupitia akili zetu kimantiki lakini kupitia sauti ndogo na tulivu ya Roho.
Akina kaka na akina dada wapendwa, Bwana ametueleza mara kwa mara “tafuteni maarifa hata kwa kujifunza na pia kwa imani.”1 Tunaweza kupokea nuru na uelewa si tu kupitia kutafakari kimantiki kwa akili zetu, lakini pia kupitia mwongozo na misukumo ya Roho Mtakatifu.
Chanzo hiki cha maarifa ya ziada hakijawa sehemu ya maisha yangu siku zote.
Mke wangu mpendwa, Irene, na mimi, tulijiunga na Kanisa miaka 31 iliyopita wakati tulipokuwa wanandoa wapya. Sote tulikuwa tumekulia kule Kolombia, lakini miezi michache baada ya ndoa yetu, kazi yangu ilitupeleka kuishi Ujerumani. Tulikuwa vijana na tulikuwa na matumaini makubwa na matarajio; ilikuwa hasa wakati wa kusisimua na wa furaha kwetu.
Wakati nilikuwa nimejikita kwenye kazi yangu, Irene alikuwa akihisi kwamba tungepokea aina fulani ya ujumbe kutoka mbinguni, bila kujua jinsi gani au lini. Ka hivyo, alianza kuruhusu waingie nyumbani kwetu aina zote za wauzaji wa kutembea kutoka nyumba moja hadi nyingine wakiwa na ensaiklopidia, vivuta vumbi, vitabu vya mapishi, vifaa vya jikoni, na kadhalika, daima akisubiria ujumbe ule wa kipekee.
Jioni moja aliniambia kwamba wavulana wawili waliokuwa wamevalia suti nyeusi walikuwa wamebisha kwenye mlango wetu na alikuwa amehisi msukumo dhahiri kabisa kuwaruhusu waingie. Walikuwa wamesema kwamba walitaka kuzungumza naye kuhusu Mungu lakini wangerudi tena wakati ningekuwa pia nyumbani. Je, ingewezekana kwamba huu ndio ujumbe uliotarajiwa?
Walianza kututembelea, na kupitia mwongozo wao, tulisoma katika maandiko na tulikuja kuelewa umuhimu mkubwa wa Yesu kristo kama Mwokozi na Mkombozi wetu. Punde tulijuta kwamba tulikuwa tumebatizwa kama watoto wadogo, ambalo halikuwa agano tulilofahamu moyoni. Hata hivyo, kubatizwa tena kungemaanisha pia kuwa waumini wa Kanisa hili jipya, kwa hivyo kwanza kabisa tulihitaji kuelewa kila kitu juu yake.
Lakini ni kwa njia gani tungejua ikiwa kile ambacho wamisionari walikuwa wakituambia kuhusu Kitabu cha Mormoni, kuhusu Joseph Smith, na kuhusu mpango wa wokovu kilikuwa ukweli hasa? Vyema, tulikuwa tumeelewa kutoka kwenye maneno ya Bwana kwamba tungeweza “kuwatambua kwa matunda yao.”2 Kwa hivyo, katika njia yenye utaratibu, tulianza kuchunguza Kanisa kwa kutafuta yale matunda kwa kutumia macho ya akili zetu kimantiki kabisa. Ni nini tulichoona? Vyema, tuliona:
-
Watu wema na wenye furaha na familia za ajabu zilizoelewa kwamba tunapaswa kuhisi shangwe katika maisha haya na si tu mateso na taabu.
-
Kanisa ambalo halina wachungaji wa kulipwa bali ambalo waumini wenyewe hukubali miito na wajibu.
-
Kanisa ambalo Yesu Kristo na familia ni kiini cha kila kitu, ambapo waumini hufunga mara moja kwa mwezi na hutoa msaada kwa ajili ya kusaidia maskini na wenye shida, ambapo tabia za afya zinadumishwa, zikitufundisha kuepukana na vitu vinavyodhuru.
Kwa kongezea:
-
Tulipenda mkazo uliowekwa juu ya kukua kibinafsi, juu ya elimu, juu ya kufanya kazi kwa bidii na kujitegemea.
-
Tulijifunza kuhusu mpango wa kusifika wa msaada wa kibinadamu.
-
Na tulivutiwa na mikutano mikuu, pamoja na muziki mzuri na kanuni za kiroho za kina zilizoshirikiwa pale.
Baada ya kuona haya yote, hatukupata kasoro yoyote katika Kanisa. Kinyume na hayo, tulipendezwa sana na kila kitu tulichoona. Hata hivyo, hatukuweza kuamua kubatizwa kwa sababu tulitaka kufahamu kila kitu kabla ya kufanya hivyo.
Lakini, hata katika kusita kwetu, Bwana alikuwa akitutayarisha kwa subira, Alikuwa akitunyoosha, na Alikuwa akitusaidia kugundua kile tulichopaswa kujifunza ili kutambua ukweli si tu kupitia akili zetu kimantiki lakini pia kupitia sauti ndogo na tulivu ya Roho, ambayo huzungumza hasa na mioyo yetu.
Sauti hiyo na hisia inayoambatana nayo vilikuja jioni moja baada ya miezi 10 ya kujifunza injili, wakati tuliposoma Mosia 18: “Kwa vile mnatamani … kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine, … na kufariji wale ambao wanahitaji kufarijiwa, … ikiwa hili ndilo pendo la mioyo yenu, ni nini mnacho dhidi ya kubatizwa kwa jina la Bwana?”3
Kifungu hicho kutoka katika Kitabu cha Mormoni kiliingia ndani ya mioyo na nafsi zetu, na ghafla tulihisi na kufahamu kwamba kwa kweli hakukuwepo na sababu yoyote dhidi ya kubatizwa. Tuligundua kwamba matamanio yaliyotajwa katika mistari hii yalikuwa pia matamanio ya mioyo yetu na kwamba vitu hivyo vilikuwa kwa kweli kile kilicho muhimu zaidi. Vilikuwa muhimu zaidi kuliko kuelewa kila kitu kwa sababu tayari tulifahamu vya kutosha. Daima tulikuwa tukitegemea mkono wa kuongoza wa Baba Mpendwa wa Mbinguni na tulikuwa na ujasiri kwamba Angeendelea kutuongoza.
Kwa hivyo, siku hiyo hiyo, tulipanga tarehe yetu ya kubatizwa, na baada ya muda tulibatizwa, hatimaye!
Je, tulijifunza nini kutokana na uzoefu huo?
Kwanza, tulijifunza kwamba tunaweza kuamini kikamilifu katika Baba mpendwa wa Mbinguni, ambaye daima anajaribu kutusaidia kuwa mtu ambaye Anajua tunaweza kuwa. Tulithibitisha ukweli wa kina wa maneno Yake wakati aliposema, “Nitawapatia watoto wa watu mstari juu ya mstari, amri juu ya amri, hapa kidogo na pale kidogo; na heri wale wanaosikiliza kanuni zangu, … kwani watasoma hekima; kwani kwa yule atakayepokea nitampatia zaidi.”4
Na pili, tulijifunza kwamba, zaidi na akili zetu za kimantiki, njia nyingine ya kupata maarifa inaweza kutupatia mwongozo na uelewa. Ni sauti tulivu na nyororo ya Roho Wake Mtakatifu ikizungumza na mioyo yetu na pia akili zetu.
Napenda kulinganisha kanuni hii na uwezo wetu wa kuona. Baba yetu wa Mbinguni ametupatia si tu moja bali macho mawili ya kimwili. Tunaweza kuona vya kutosha kwa jicho moja, lakini jicho la pili linatupatia mtazamo tofauti. Wakati mitazamo yote miwili inapowekwa pamoja katika bongo zetu, inatoa picha ya vipimo vitatu ya mazingira yetu.
Vile vile, tumepewa vyanzo viwili vya habari, kupitia uwezo wetu wa kimwili na kiroho. Akili yetu hutoa utambuzi mmoja kupitia hisia zetu za kimwili na kupitia mantiki zetu. Lakini kupitia kipawa cha Roho Mtakatifu, Baba pia ametupatia mtazamo wa pili, ambao kwa kweli ni muhimu zaidi na wa kweli zaidi kwa sababu unakuja moja kwa moja kutoka Kwake. Lakini, kwa vile minong’ono ya Roho mara nyingi huwa migumu kutambua, watu wengi hawafahamu vizuri chanzo hiki cha nyongeza.
Wakati mitazamo hii miwili inawekwa pamoja ndani ya nafsi zetu, picha moja kamili inaonesha ukweli wa vitu jinsi vilivyo. Kwa hakika, kupitia mtazamo wa ziada wa Roho Mtakatifu, “kweli,” fulani, kama zinavyoonekana kupitia uelewa wetu wa kiakili, zinaweza kuwekwa wazi kama za kupotosha au dhahiri kwamba si sahihi. Kumbuka maneno ya Moroni: “Na kwa uwezo wa Roho Mtakatifu mtajua ukweli wa vitu vyote.”5
Katika miaka yangu 31 ya kuwa muumini wa Kanisa, nimepata uzoefu wa muda mrefu kwamba ikiwa tutategemea tu akili zetu za kimantiki na kukana au kupuuza uelewa wa kiroho ambao tunaweza kupokea kupitia minong’ono na misukumo ya Roho Mtakatifu, ni kana kwamba tulikuwa tukiishi na jicho moja tu. Lakini tukizungumza kistiari, kwa kweli tumepewa macho mawili. Ni muunganiko tu wa mitazamo yote miwili unaweza kutupatia picha ya kweli na kamili juu ya ukweli wote na juu ya kila kitu tunachopitia katika maisha yetu, vile vile uelewa wote na wa kustaajabisha wa utambulisho wetu na lengo letu kama watoto wa Baba mpendwa wa Mbinguni.
Ninakumbuka kile ambacho Rais Nelson alitufundisha mwaka mmoja uliopita aliposema kwamba “Katika siku zijazo, haitawezekana kunusurika kiroho bila uzoefu wa mwongozo,uelekezi, faraja, na ushawishi wa kudumu wa Roho Mtakatifu.”6
Nimekuja kujua kwa uhakika kamili kwamba:
-
Tuna Baba mpndwa wa Mbinguni, na sote tulikubali kuja hapa duniani kama sehemu ya mpango mtakatifu.
-
Yesu ndiye Kristo; Yuko hai na ni Mwokozi na Mkombozi wangu.
-
Joseph, kijana mkulima mnyenyekevu, alipewa mwito na kuwa nabii mkuu ambaye alianzisha haya, maongozi ya Mungu ya nyakati jalivu, pamoja na funguo zake zote, nguvu, na mamlaka ya ukuhani mtakatifu wa Mungu.
-
Kitabu cha Mormoni ni ushahidi wa pili wa Yesu Kristo, na familia zimekusudiwa kuwa pamoja milele.
-
Bwana wetu, Yesu Kristo, analiongoza hili, Kanisa Lake lililorejeshwa, kupitia nabii wetu aliye hai, Rais Russell M. Nelson, leo hii.
Hizi na kweli zingine nyingi za thamani zimekuwa matofali ya kiroho ya kujenga kile ambacho Mungu ananisaidia kuwa. Na ninatazamia kwa hamu mafunzo mengi mapya ambayo Angali ananitaka mimi—na wewe—tupokee wakati tunapoishi maisha haya ya kupendeza na “kupata maarifa … hata kwa kujifunza na pia kwa imani.”
Yote haya nayajua kuwa kweli na ninashuhudia juu yake katika jina la Yesu Kristo, amina.