Kutakaswa kwa Toba
Kwa sababu ya mpango wa Mungu na Upatanisho wa Yesu Kristo, tunaweza kutakaswa kupitia mchakato wa toba.
Katika maisha hapa duniani tupo chini ya sheria za mwanadamu na sheria za Mungu. Nimekuwa na uzoefu usio wa kawaida wa kuhukumu tabia mbaya chini ya sheria hizo zote mbili—awali kama hakimu wa Mahakama Kuu ya Utah na sasa kama mshiriki wa Urais wa Kwanza. Tofauti niliyopata kati ya sheria za mwanadamu na sheria za Mungu imeongeza shukrani yangu ya uhalisia na nguvu ya Upatanisho wa Yesu Kristo. Chini ya sheria za mwanadamu, mtu aliyepatikana na hatia kubwa ya uhalifu anaweza kuhukumiwa maisha gerezani bila ya uwezekano wa msamaha. Lakini ni tofauti chini ya mpango wa huruma wa Baba mpendwa wa Mbinguni. Nimeshuhudia kwamba dhambi kama hizi zinaweza kusamehewa katika maisha haya kwa sababu ya dhabihu ya Mwokozi kwa ajili ya dhambi za “wale wote walio na moyo uliopondeka na roho iliyovunjika” (2 Nefi 2:7). Kristo anakomboa, na Upatanisho Wake ni halisi.
Huruma ya upendo ya Mwokozi wetu inaonyeshwa katika wimbo mkuu ulioimbwa na kwaya.
Njoo kwa Yesu, Yeye milele atakusikiliza,
Ingawa katika giza umepotea.
Upendo wake utakupata na kwa upole kukuongoza
Kutoka giza la usiku hadi katika mwangaza.1
Dhabihu ya upatanisho wa Yesu Kristo hufungua mlango kwa “watu wote [ku]tubu na kuja kwake” (Mafundisho na Maagano 18:11; ona pia Marko 3:28; 1 Nefi 10:18; Alma 34:8, 16). Kitabu cha Alma kinazungumzia toba na msamaha hata wa wale ambao walikuwa waovu na wenye kiu ya kuua (ona Alma 25:16; 27:27, 30). Ujumbe wangu leo ni moja ya tumaini kwetu sote, ikiwa ni pamoja na wale ambao wamepoteza uumini wao Kanisani kwa kufutwa uumini au kuondoshwa jina. Sisi sote ni watenda dhambi ambao tunaweza kutakaswa na toba. “Kutubu dhambi siyo rahisi,” Mzee Russell M, Nelson alifundisha kwenye mkutano mkuu uliopita. 2 “Lakini tuzo ina thamani kubwa.”2
I. Toba
Toba inaanza kwa Mwokozi wetu, na ni furaha, si mzigo. Kwenye mkutano wa Krismasi wa Desemba, Rais Nelson alifundisha: “Toba ya kweli siyo tukio. Ni fursa isiyo na mwisho. Ni msingi wa maendeleo na kuwa na amani ya akili, faraja, na furaha.”3
Baadhi ya mafundisho makuu juu ya toba ni katika mahubiri ya Alma ya Kitabu cha Mormon kwa waumini wa Kanisa ambao baadaye alielezea kuwa wamekuwa katika hali ya “kutoamini,” “wamejiinua kwa … kiburi,” na mioyo yao kuwekwa “katika utajiri na vitu vya ulimwengu” (Alma 7:6). Kila muumini wa Kanisa hili la urejesho ana mengi ya kujifunza kutoka kwenye mafundisho yenye ushawishi ya Alma.
Tunaanza na imani katika Yesu Kristo, kwa sababu “ni yeye ambaye anakuja kuondoa dhambi za ulimwengu” (Alma 5:48). Lazima tutubu kwa sababu, kama Alma alivyo fundisha , “msipotubu hamuwezi kuuruthi kwa vyovyote ufalme wa mbinguni” (Alma 5:51). Toba ni sehemu muhimu ya mpango wa Mungu. Kwa sababu wote watatenda dhambi katika maisha yetu ya mwili wa kufa na kutengwa na uwepo wa Mungu, mwanadamu asingeweza “kuokolewa” bila toba (Alma 5:31; ona pia Helamani 12:22).
Hili limefundishwa toka mwanzo. Bwana alimuamuru Adamu, “Wafundishe watoto wako, kwamba watu wote, kila mahali, lazima watubu, au vinginevyo hawataweza kuurithi ufalme wa Mungu, kwa maana hakuna kitu kilicho kichafu kinachoweza kukaa huko, au kukaa mbele zake” (Musa 6:57). Lazima tutubu dhambi zetu zote—matendo yetu yote au shughuli ambazo ni kinyume na amri za Mungu. Hakuna ambaye haitajiki kufanya hivyo. Jioni iliyopita Rais Nelson alitupatia changamoto, “Ndugu, sisi sote tunahitaji kutubu.”4
Ili kutakaswa kwa toba, lazima tuziache dhambi zetu na kuziungama kwa Bwana na kwa Waamuzi Wake pale inapohitajika (ona Mafundisho na Maagano 58:43). Alma pia alifundisha kwamba lazima “tutende kazi za haki” (Alma 5:35). Hii yote ni sehemu ya mwaliko wa mara kwa mara wa kuja kwa Kristo.
Tunahitaji kupokea sakramenti kila siku ya Sabato. Katika ibada hiyo tunaweka maagano na kupokea baraka ambazo zinatusaidia kushinda vitendo vyote na tamaa ambazo zinazuia ukamilifu ambao Mwokozi wetu anatualika kuufikia (ona Matthayo 5:48; 3 Nefi 12:48). Tunapo “jinyima [wenyewe] ubaya wote, na kumpenda Mungu kwa mioyo [yetu], akili na nguvu,” ndipo, tunaweza “kukamilika katika Kristo” na “kutakaswa” kupitia damu Yake iliyomwagika, ili “kuwa watakatifu, bila waa” (Moroni 10:32–33). Ni ahadi iliyoje! Ni muujiza ulioje! Ni baraka iliyoje!
II. Uwajibikaji na Hukumu ya Kibinadamu
Lengo moja la mpango wa Mungu kwa ajili ya uzoefu wa maisha haya ni “kutujaribu” sisi “ili kuona kama tutafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu [wetu] ata[tu]amuru” (Ibrahimu 3:25). Kama sehemu ya mpango huu, tunawajibika kwa Mungu na kwa watumishi Wake wateule, na uwajibikaji huo hujumuisha vyote maisha haya na hukumu takatifu.
Katika Kanisa la Bwana, hukumu katika maisha haya kwa waumini au waumini watarajiwa inatolewa na viongozi ambao wanatafuta mwongozo mtakatifu. Ni wajibu wao kuwahukumu watu wanaotafuta kuja kwa Kristo ili kupata nguvu ya Upatanisho kwenye njia ya agano kuelekea uzima wa milele. Hukumu katika maisha haya huamua iwapo mtu yupo tayari kwa ubatizo. Je, mtu anastahili kupata kibali cha kuhudhuria hekaluni? Je, mtu ambaye jina lake liliondolewa kutoka kwenye kumbukumbu za Kanisa ametubu kwa dhati kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo ili kurudishwa tena kupitia ubatizo?
Wakati hakimu mwanadamu aliyeitwa na Mungu anamuidhinisha mtu kwa maendeleo zaidi, kama vile fursa za hekaluni, hamaanishi kwamba mtu huyo ni mkamilifu , na hasamehi dhambi yoyote. Mzee Spencer W. Kimball alifundisha kwamba baada ya kile alichokiita “kufuta adhabu,” “lazima pia mtu atafute na apate kutoka kwa Mungu wa mbinguni toba ya mwisho, na yeye pekee anaweza kuihisi.”5 Na kama matendo ya dhambi na hamu ya kutotubu vitabaki hadi Hukumu ya Mwisho, mtu asiyetubu atabaki mchafu. Uwajibikaji wa mwisho, ikijumuisha utakaso wa mwisho unaotokana na toba, ni kati ya kila mmoja wetu na Mungu.
III. Ufufuo na Hukumu ya Mwisho.
Hukumu iliyoelezwa kwa kawaida katika maandiko ni Hukumu ya Mwisho inayofuata baada ya Ufufuo (ona 2Nefi 9:15). Maandiko mengi yanaeleza kwamba “sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo” (Warumi 14:10; ona pia 2 Nefi 9:15; Mosia 27:31) “kuhukumiwa kulingana na vitendo [ambavyo] vilitendwa katika miili inayokufa” (Alma 5:15; ona pia Ufunuo 20:12; Alma 41:3; 3 Nefi 26:4). Wote watahukumiwa “kulingana na matendo yao” (3 Nefi 27:15) na “kulingana na matamanio ya mioyo yao” (Mafundisho na Maagano 137:9; ona pia Alma 41:6).
Dhumuni la Hukumu hii ya Mwisho ni kuona iwapo tumefikia yale aliyoyaelezea Alma kama “badiliko kuu ya moyo” (ona Alma 5:14, 26), ambapo tumekuwa viumbe wapya, kwamba “hatuna tamaa ya kutenda maovu tena, lakini kutenda mema daima” (Mosia 5:2–2). Hakimu wa haya ni Mwokozi wetu, Yesu Kristo (ona Yohana 5:22; 2 Nefi 9:41). Baada ya hukumu Yake sote tutakiri “kwamba hukumu zake ni za haki” (Mosia 16:1; ona pia Mosia 27:31; Alma 12:15), kwa sababu Ajuaye yote (ona 2 Nefi 9:15, 20) amempa Yeye uelewa mkamilifu wa matendo yetu yote na hamu zetu, yote ya haki au yale yaliyofanyiwa toba na ambayo hayakufanyiwa toba au hayakubadilishwa.
Maandiko yanaelezea mchakato wa Hukumu hii ya Mwisho. Alma anafundisha kwamba haki ya Mungu wetu inahitaji kwamba katika Ufufuo “vitu vyote virudishwe kwa hali yake ya kawaida” (Alma 41:2). Hii ina maana kwamba “ikiwa vitendo vyao vilikuwa vizuri kwenye maisha haya, na nia za mioyo yao zilikuwa nzuri, … katika siku ya mwisho, [wata]rejeshwa kwa kile ambacho ni kizuri” (Alma 41:3). Sawa na hilo, “ikiwa matendo yao [au nia zao] ni mbovu yale yaliyo maovu yatarejeshwa kwao” (Alma 41:4–5; ona pia Helamani 14:31). Vivyo hivyo, nabii Yakobo alifundisha kwamba katika Hukumu ya Mwisho “wale wenye haki watakuwa wenye haki, na wale walio wachafu watakuwa wachafu” (2 Nefi 9:16; ona pia Mormoni 9:14; 1 Nefi 15:33). Huo ndio mchakato unaotangulia kusimama kwetu mbele ya kile Moroni anachokiita “kiti cha enzi cha kupendeza cha yule Yehova mkuu, Mwamuzi wa Milele wa wanaoishi na waliokufa” (Moroni 10:34; ona pia 3 Nefi 27:16).
Kuhakikisha kwamba tutakuwa wasafi mbele za Mungu, lazima tutubu kabla ya Hukumu ya Mwisho (ona Mormoni 3:22). Kama Alma alivyomweleza mwanaye mwenye dhambi, hatuwezi kuficha dhambi zetu mbele ya Mungu, “na isipokuwa utubu zitakuwa ushahidi dhidi yako katika siku ya mwisho” (Alma 39:8; msisitizo umeongezwa). Upatanisho wa Yesu Kristo unatupa njia pekee ya kufikia utakaso unaohitajika kupitia toba, na maisha haya ya duniani ni muda wetu wa kufanya hivyo. Japokuwa tunafundishwa kwamba toba nyingine zinaweza kutokea katika ulimwengu wa roho (ona Mafundisho na Maagano 138:31, 33, 58), hilo siyo la kutegemea. Mzee Melvin J. Ballard alifundisha: “Ni rahisi sana kushinda na kumtumikia Bwana wakati vyote mwili na roho vinapokuwa kitu kimoja. Huu ndio wakati ambapo watu wanaweza kubadilika na kupokea vitu. … Maisha haya ni wakati wa kutubu.”6.
Tunapotubu, tuna uhakika wa Bwana kwamba dhambi zetu, yakiwemo matendo na matamanio yetu, yatasafishwa na mwamuzi wetu wa mwisho mwenye huruma, “hatazikumbuka tena” (Mafundisho na Maagano 58:42; ona pia Isaya 1:18; Yeremia 31:34; Waebrania 8:12; Alma 41:6; Helamani 14:18–19). Tukiwa tumesafishwa kwa toba, tunaweza kustahili uzima wa milele, ambao Mfalme Benyamini aliuelezea kama “kuishi na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho” (Mosia 2:41; ona pia Mafundisho na Maagano 14:7).
Kama sehemu nyingine ya mpango wa Mungu “wa urejesho” (Alma 41:2), Ufufuo utarejesha “vitu vyote … kwenye umbo lake sahihi na kamilifu” (Alma 40:23). Hii inajumuisha ukamilifu wa mapungufu yetu yote ya kimwili na ulemavu uliopatikana katika maisha haya, ikiwa ni pamoja na wakati wa kuzaliwa au kwa mshituko au ugonjwa.
Je urejesho huu unatutakasa kwa uovu wetu au tamaa zilizoshindikana au uraibu? Hilo haliwezekani. Tunajua kutoka kwenye ufunuo wa siku hizi kwamba tutahukumiwa kwa matamanio yetu pia kwa matendo yetu (ona Alma 41:5; Mafundisho na Maagano 137:9) na kwamba hata mawazo yetu yatatutia hatiani (ona Alma 12:4). Hatutakiwi “kuahirisha siku yetu ya toba” hadi kifo, Amuleki alifundisha (Alma 34:33), kwa sababu roho ile ile ambayo inamiliki miili yetu katika maisha haya—iwe ya Bwana au ya ibilisi—“itakuwa na uwezo wa kumiliki mwili [wetu] katika ulimwengu ule wa milele” (Alma 34:34). Mwokozi wetu ana nguvu na yupo tayari kutusafisha kutokana na uovu. Sasa ndio muda wa kutafuta msaada wake ili kutubu uovu au matamanio na mawazo yasiyofaa ili kuwa safi na kuwa tayari kusimama mbele za Mungu kwenye Hukumu ya Mwisho.
IV. Mikono ya Huruma
Mpango wa Mungu wa milele na amri zake zote ni upendo wake kwa kila mmoja wetu, ambao ni “wakutamanisha kuliko vitu vyote … na “wenye kuleta furaha katika nafsi” (1 Nefi 11:22–23). Nabii Isaya aliwahakikishia hata waovu kwamba pale “watakapo mrudia Bwana, … atawahurumia … [na] kuwasamehe kabisa” (Isaya 55:7). Alma alifundisha, “Tazama, yeye huwatumia wanadamu wote mwaliko, kwani mikono ya huruma imenyoshwa kwao” (Alma 5:33; ona pia 2 Nefi 26:25–33). Bwana aliyefufuka aliwaambia Wanefi, “Tazama, mkono wangu wa rehema umenyoshwa kwenu, na yeyote atakayekuja, Nitampokea” (3 Nefi 9:14). Kutoka kwenye mafundisho haya ya kimaandiko na mengine mengi, tunajua kwamba Mwokozi wetu mpendwa anafungua mikono Yake kuwapokea watu wote wanaume na wanawake kwa masharti ya upendo Aliyoyaeleza ili kufurahia baraka kuu ambazo Mungu amewawekea watoto Wake.7
Kwa sababu ya mpango wa Mungu na Upatanisho wa Yesu Kristo, ninashuhudia kwa “mng’aro mkamilifu wa tumaini ” kwamba Mungu anatupenda na tunaweza kusafishwa kwa mchakato wa toba. Tumeahidiwa kwamba, “kama [tu]tasonga mbele, tukila na kusherehekea neno la Kristo, na kuvumilia hadi mwisho, tazama, hivi ndivyo asema Baba: Mtapokea uzima wa milele.” (2 Nefi 31:20). Naomba wote tufanye hivyo, ninasihi na kuomba, katika jina la Yesu Kristo, amina.