2010–2019
Wema wa Mungu Ulio Kamili
Mkutano Mkuu wa Aprili 2019


Wema wa Mungu Ulio Kamili

Hata wakati tunamsubiri Bwana kwa uvumilivu, kuna baadhi ya baraka ambazo huja kwetu papo hapo.

Miaka kadhaa iliyopita, mwana wetu wa miaka mitano alinijia na kunifahamisha, “Baba, nimegundua jambo. Nimegundua kwamba punde kwako ni muda mrefu sana kwangu.”

Wakati Bwana na watumishi Wake wanaposema mambo kama, “Siyo baada ya siku nyingi” au “Wakati hauko mbali,” inaweza kiuhalisia kumaanisha maisha yote au zaidi ya hapo.1 Muda Wake, na mara nyingi mpangilio Wake, ni tofauti na wetu. Subira ni muhimu. Bila hiyo, hatuwezi kuendelea wala kuonyesha imani katika Mungu kwenye maisha na wokovu. Lakini ujumbe wangu leo ni kwamba, hata wakati tunamsubiri Bwana kwa uvumilivu, kuna baadhi ya baraka ambazo huja kwetu papo hapo.

Wakati Alma na watu wake walipotekwa na Walamani, waliomba kwa ajili ya ukombozi. Hawakukombolewa papo hapo, lakini waliposubiri ukombozi kwa uvumilivu, Bwana alionyesha wema Wake kwa baadhi ya baraka papo hapo. Yeye papo hapo alilainisha mioyo ya Walamani ili kwamba wasiwaue. Yeye pia aliwaimarisha watu wa Alma na kufanya miepesi mizigo yao.2 Wakati hatimaye walipokombolewa, walisafiri kwenda Zarahemla, ambapo walielezea uzoefu wao kwa hadhira iliyostaajabu. Watu wa Zarahemla walistaajabu, na “walipofikiri kuhusu wema wa Mungu ulio kamili, na uwezo wake katika kuwakomboa Alma na ndugu zake kutoka … utumwani, walipaza sauti zao na kumshukuru Mungu.”3

Wema wa Mungu ulio kamili huja kwa wote wanaomlilia Yeye kwa kusudi la kweli na lengo kamili la moyo. Hii hujumuisha wale wanaolia kwa kukata tamaa, pale ukombozi unapoonekana kuwa mbali na maumivu kuendelea, hata kuongezeka.

Ndivyo ilivyokuwa kwa nabii kijana ambaye aliteseka kando ya unyevu wa kutia kinyaa wa gereza la chini ya ardhi kabla ya hatimaye kulia: “Ee Mungu, uko wapi? … Ni kwa muda gani mkono wako utazuiliwa … ? Ndiyo, Ee Bwana, ni kwa muda gani … ?”4 Katika kujibu, Bwana hakumkomboa Joseph papo hapo, lakini papo hapo alitamka amani.5

Mungu pia hutoa tumaini la papo hapo kwa ukombozi wa baadaye.6 Bila kujali chochote, bila kujali popote, katika Kristo na kupitia Kristo daima kuna tumaini angavu mbele yetu.7 Papo hapo mbele yetu.

Zaidi, Yeye ameahidi, “wema Wangu hautaondoka kwako.”8

Juu ya yote, upendo wa Mungu ni wa papo hapo. Pamoja na Paulo, ninashuhudia kwamba hakuna kinachoweza “kututenga na upendo wa Mungu, ulio katika Kristo Yesu.”9 Hata dhambi zetu, japo zinaweza kututenga na Roho Wake kwa muda, haziwezi kututenga kutoka kwenye uaminifu na ukamilifu wa upendo Wake.

Hizi ni baadhi tu ya njia na jinsi ambavyo “anatubariki [sisi] papo hapo.”10 Sasa, kuleta kanuni hizi leo na karibu, ninashiriki nanyi uzoefu wa watu wawili ambao maisha yao yanasimama kama ushuhuda wa wema wa Mungu ulio kamili.

Tangu alipokuwa kijana mdogo, Emilie alihangaika kwa matumizi mabaya ya vitu. Majaribio yakapelekea tabia, na tabia hatimaye ilijenga kwenye uraibu ambao ulimfanya mateka kwa miaka, licha ya nyakati fulani za kuwa na ahueni. Emilie kwa makini alificha tatizo lake, hasa baada ya kuwa mke na mama.

Mwanzo wa ukombozi wake haukuwa kama ukombozi hata kidogo. Dakika moja, Emilie alikuwa akipitia ratiba ya vipimo vya afya, na iliyofuata, alikuwa akiendeshwa kwa gari la wagonjwa kwenda kwenye vifaa vya wagonjwa waliolazwa. Alianza kupata hofu alipofikiria juu ya kutenganishwa na watoto wake, mume wake, na nyumba yake.

Usiku ule, peke yake kwenye chumba chenye baridi, na giza, Emilie alijikunja juu ya kitanda chake na kulia. Uwezo wake wa kufikiri ulififia mpaka hatimaye, akizidiwa na wasiwasi, hofu, na giza zito ndani ya chumba na katika nafsi yake, Emilie kwa kweli alifikiri angekufa usiku ule. Peke yake.

Katika hali ile ya kukata tamaa, Emilie kiasi fulani alikusanya nguvu za kubingirika kutoka kitandani kwake na kwenye magoti yake. Bila mkao wowote ambao wakati mwingine ulikuwa sehemu ya sala zake za nyuma, alijikabidhi kikamilifu kwa Bwana pale aliposihi kwa hitaji kubwa, “Mungu Mpendwa, ninakuhitaji Wewe. Tafadhali nisaidie. Sitaki kuwa peke yangu. Tafadhali, nivushe nipite usiku huu.”

Na papo hapo, kama alivyofanya kwa Petro wa kale, Yesu alinyoosha mkono Wake na kuiokoa nafsi yake iliyozama.11 Hapo ulikuja kwa Emily utulivu wa kimiujiza, ujasiri, hakikisho, na upendo. Chumba hakikuwa tena cha baridi, alijua hakuwa peke yake, na kwa mara ya kwanza tangu alipokuwa na umri wa miaka 14, Emilie alijua kila kitu kingekuwa sawa. “Alipojitambua kwa Mungu”12 Emilie alisinzia kwa amani. Na kwa hivyo tunaona kuwa “ikiwa mtatubu, na msishupaze mioyo yenu, mara moja mpango mkuu wa ukombozi utatimizwa kwenu.”13

Picha
Familia ikiwa hekaluni

Uponyaji wa Emilie na hatma ya ukombozi vilichukua muda mrefu—miezi ya tiba, mafunzo, na ushauri, kipindi ambapo aliidhinishwa na wakati mwingine kubebwa na wema Wake ulio kamili. Na wema huo uliendelea kuwa naye pale alipoingia hekaluni pamoja na mume wake na watoto wake kuunganishwa pamoja milele. Kama watu wa Zarahemla, Emilie sasa anatoa shukrani pale anapokumbuka wema wa Mungu ulio kamili na nguvu Yake katika kumkomboa kutoka utumwani.

Sasa, kutoka kwenye maisha ya shujaa mwingine mwaminifu. Mnamo Desemba 27, 2013, Alicia Schroeder kwa furaha aliwakaribisha rafiki zake wapendwa Sean na Sharla Chilcote, ambao bila taarifa walifika mlangoni kwake. Sean, ambaye pia alikuwa askofu wa Alicia, alimpa simu yake ya mkononi na kwa makini alisema, “Alicia, tunakupenda. Unahitaji kupokea simu hii.”

Mume wa Alicia, Mario, alikuwa amepiga. Alikuwa mbali pamoja na baadhi ya watoto wao kwenye safari iliyotarajiwa kwa muda mrefu ya kuendesha juu ya theluji. Kulikuwa kumetokea ajali mbaya. Mario alikuwa ameumia vibaya, na mwana wao wa miaka 10, Kaleb alikuwa amefariki. Wakati Mario kwa machozi alipomwambia Alicia juu ya kifo cha Kaleb, alizidiwa na mshtuko na huzuni ambayo wachache wetu wanaweza kufahamu. Ilimdondosha. Akifadhaishwa kwa uchungu usioelezeka, Alicia hakuweza kuongea wala kusogea.

Askofu na Dada Chilcote kwa haraka walimwinua na kumshikilia. Walilia na kuomboleza pamoja kwa muda. Kisha Askofu Chilcote alijitolea kumpa Alicia baraka.

Kilichofuatia baadaye hakielezeki bila uelewa kiasi juu ya Upatanisho wa Yesu Kristo na wema wa Mungu ulio kamili. Askofu Chilcote taratibu aliweka mikono yake juu ya kichwa cha Alicia na, kwa sauti ya kutetemeka, alianza kuzungumza. Alicia alisikia mambo mawili kana kwamba yalisemwa na Mungu Mwenyewe. Kwanza, alisikia jina lake, Alicia Susan Schroeder. Kisha alisikia askofu akiomba mamlaka ya Mwenyezi Mungu. Katika wasaa ule—katika kutaja tu jina lake na nguvu ya Mungu—Alicia alijazwa na amani isiyoelezeka, upendo, faraja na kiasi fulani shangwe. Na iliendelea kuwa naye.

Sasa, ndiyo, Alicia, Mario, na familia yao wanaendelea kuomboleza na kumkosa Kaleb. Si rahisi! Kila ninapozungumza nao, macho ya Alicia yanaloa kwa machozi pale anaposimulia jinsi anavyompenda na kumkosa mwanaye. Na macho yake yanabaki na unyevu anaposimulia jinsi Mkombozi Mkuu alivyomvusha kupita kila hatua ya majaribu, akianza na wema wake ulio kamili wakati wa mateso yake makali na kuendelea sasa kwa tumaini angavu la muunganiko wa kupendeza ambao “haukuwa baada ya siku nyingi.”

Ninajua kwamba uzoefu wa maisha wakati mwingine huleta zahama na kuchanganyikiwa ambako hufanya iwe vigumu kupokea, kutambua, au kutunza aina ya usaidizi ambao ulikuja kwa Emilie na Alicia. Nimepitia nyakati kama hizo. Ninashuhudia kwamba, kipindi cha nyakati hizo, ulinzi wetu ni onyesho rahisi tu na lenye nguvu la wema wa Mungu ulio kamili. Kumbuka, Israeli ya kale hatimaye ilikombolewa “na yule Mungu ambaye alikuwa amewahifadhi”14 siku hadi siku.

Ninatoa ushahidi kwamba Yesu Kristo ni Mkombozi Mkuu, na katika jina Lake, ninaahidi kwamba unapomgeukia Yeye kwa kusudi halisi na lengo kamili la moyo, Atakukomboa kutoka kila kitu kinachotishia kupunguza au kuangamiza maisha au furaha yako. Ukombozi huo unaweza kuchukua muda mrefu kuliko ambavyo ungependa—pengine maisha yote au zaidi. Hivyo, kukupa faraja, ujasiri, na tumaini, kukuidhinisha na kukuimarisha hadi siku hiyo ya hatimaye kukombolewa, ninawasifu na kushuhudia juu ya wema wa Mungu ulio kamili katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha