Mtegemee Yesu Kristo.
Tukimtegemea Yesu Kristo, Yeye atatusaidia kuishi maagano yetu na kukuza miito yetu kama wazee katika Israeli.
Wakati Yesu akitembea katika mtaa karibu na Kapenaumu1 pamoja na kundi kubwa la watu waliomzunguka, mwanamke aliyekuwa akiteseka kwa hali mbaya kwa miaka kumi na miwili alijinyoosha na kugusa pindo la vazi lake. Mara moja aliponywa.2
Maandiko yanaandika kwamba Yesu, akitambua “kwamba [nguvu zimemtoka].”3 “aligeuka katika msongamano”4 na “akatazama … kumwona yule ambaye amefanya kitu hiki.”5 “Yule mwanamke, alipoona ya kwamba hawezi kusitirika,”6 “akaanguka mbele yake, akamweleza kweli yote.”7
Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya: enenda zako kwa amani.”8
Yesu Kristo alimwokoa mwanamke. Alikuwa ameponywa kimwili, lakini wakati Yesu alipogeuka kumwangalia, alitangaza imani yake kwa Yesu na Yesu aliponya moyo wake.9 Alisema naye kwa upendo, alimhakikishia juu ya kukubaliwa, na alimbariki kwa amani Yake.10
Akina kaka, kama wenye ukuhani mtakatifu, tunashiriki katika kazi ya wakovu. Katika mwaka uliopita, Bwana emeweka uongozi wa kazi hii kwa uaminifu juu ya mabega ya wazee katika Israeli.11 Tunalo jukumu kutoka kwa Bwana—kufanya kazi na dada zetu, tunatakiwa kutumikia katika njia takatifu zaidi, kuongeza kasi ya kukusanya Israeli katika pande zote za pazia, kuweka imara nyumba zetu kama mahali pa madhabahu ya imani na kujifunza injili, na kuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili wa Yesu Kristo.12
Kama katika vitu vyote, Mwokozi ametuonesha njia: tunahitaji kumtegemea na kumtumikia Yesu Kristo kama Yeye alivyo mtegemea na kumtumikia Baba Yake.13 Mwokozi alilisema kwa njia hii kwa Nabii Joseph:
“Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope.
Tazama majeraha yaliyoko yaliotobolewa ubavuni mwangu, na pia alama za misumari katika mikono na miguu yangu; kuweni waaminifu, zishikeni amri zangu, na mtaurithi ufalme wa mbinguni.”14
Katika ulimwengu kabla ya maisha ya duniani, Yesu alimwahidi Baba Yake kwamba angefanya mapenzi ya Baba Yake na kuwa Mwokozi na Mkombozi wetu. Wakati Baba yake alipouliza, “Nimtume Nani?”15 Yesu alijibu:
“Niko hapa, nitume mimi.”16
“Baba, mapenzi yako yafanyike, na utukufu uwe wako milele.”17
Katika maisha yake yote ya duniani Yesu aliishi ahadi hiyo. Kwa unyenyekevu, upole, na upendo, Alifundisha mafundisho ya Baba Yake na alifanya kazi ya Baba Yake kwa nguvu na mamlaka Baba Yake aliyompa.18
Yesu aliutoa moyo wake kwa Baba yake. Alisema:
“Nampenda Baba.”19
“Ninafanya siku zote vitu hivyo ambavyo vinampendeza Yeye.”20
“Nilikuja … sio kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi ya [Baba ambaye] alinituma mimi.“21
Katika mateso yake huko Gethsemane, aliomba, “Hata hivyo sio mapenzi yangu, bali yako yatimizwe.”22
Wakati Bwana anapowaita wazee katika Israeli “nitegemeeni katika kila wazo” na “Tazama majeraha” katika mwili Wake uliofufuka, ni mwito wa kukataa dhambi na ulimwengu na kumgeukia Yeye na kumpenda na kumtii. Ni mwito wa kufundisha mafundisho Yake na kufanya Kazi yake katika njia Yake. Kwa hivyo, ni wito wa kumwamini Yeye kikamilifu, kuacha mapenzi yetu na kutoa mioyo yetu Kwake, na kupitia nguvu Yake ya kukomboa kuwa kama Yeye.23
Akina kaka, kama tutamtegemea Yesu Kristo, Yeye atatubariki tuwe Wazee Wake katika Israeli—wanyenyekevu, wapole, watiifu, waliojawa na upendo Wake.34 Na tutaleta shangwe na baraka za injili Yake na Kanisa Lake katika familia zetu na kwa kaka na dada zetu pande zote za pazia.
Rais Russell M. Nelson, ametuita kumtegemea Yesu Kristo katika njia hii: “Hakuna kitu rahisi au kinachotokea chenyewe kuhusu kuwa wafuasi wenye nguvu namna hiyo. Fokasi yetu lazima ikazwe kwa Mwokozi na injili Yake. Ni vigumu kiakili kujitahidi kumtegemea Yeye katika kila wazo. Lakini tunapofanya hivyo, mashaka yetu na hofu hutoweka.”25
Kaza ni neno kuu. Inamaanisha kufungwa imara, kuvutia na kushika kikamilifu.26 Tunakaza fokasi yetu kwa Yesu Kristo na injili yake kwa kuishi maagano yetu.
Wakati tunapoishi maagano yetu, yanaathiri kila kitu tunachosema na kufanya. Tunaishi maisha ya agano27 yaliyojaa matendo rahisi, ya kila siku ya imani ambayo inayotuelekeza sisi kwa Yesu Kristo: sala kutoka moyoni katika Jina lake, tukisherehekea kwenye neno Lake , tukimgeukia Yeye kutubu thambi zetu, tukishika amri Zake , kushiriki sakrament na kuitunza Sabato Yake takatifu, tukiabudu katika hekalu Lake takatifu mara nyingi kadiri tunavyoweza, na kutumia ukuhani Wake mtakatifu kuhudumia watoto wa Mungu.
Vitendo hivi vya kimaagano hufungua mioyo yetu na akili kwenye nguvu ya ukombozi ya Mwokozi na ushawishi wa utakaso wa Roho Mtakatifu. Mstari juu ya mstari, Mwokozi anabadili asili yetu hasa, tunaongoka kwa kina Kwake, na maagano yetu huwa hai katika mioyo yetu.28
Ahadi tunazofanya kwa Baba yetu wa Mbinguni zinakuwa kujitolea kuliko imara kama mwamba, nia zetu za dhati. Ahadi za Baba wa Mbinnguni kwetu zinatujaza na shukrani na furaha.29 Maagano yetu yanakoma kuwa sheria tunazozifuata na kuwa kanuni za upendo ambazo zinatutia moyo na kutuongoza na kukaza fokasi yetu kwa Yesu kristo.30
Vitendo hivi vya dhati vinapatikana kwa wote, vijana na wazee. Ninyi wavulana wenye ukuhani mtakatifu wa Haruni, kila kitu nilichosema usiku huu kinawahusu nyinyi. Namshukuru Mungu kwa ajili yenu. Mnafanya ibada takatifu na maagano yanayopatikana kwa mamilioni ya Watakatifu wa siku za Mwisho kila wiki. Mnapoandaa, kubariki, au kupitisha sakramenti; kuhudumu; kubatizwa katika hekalu; mnapomualika rafiki kwenye shughuli; au kumuokoa muumini wa akidi yenu, mnafanya kazi ya wokovu. Ninyi pia mnaweza kumtegemea Yesu Kristo na kuishi maagano yenu kila siku. Ninawaahidi kwamba kama mtafanya hivyo, mtakuwa watumishi wa kuaminika wa Bwana sasa na, katika siku zijazo, wazee wenye nguvu katika Israeli.
Akina kaka, Ninajua kwamba haya yote yanaweza kuonekana yanakatisha tamaa. Lakini tafadhali kumbukeni maneno haya ya mwokozi: “Siko peke yangu, kwa sababu Baba yupo pamoja nami.”31 Hivyo ndivyo ilivyo kwetu. Hatuko peke yetu. Bwana Yesu Kristo na Baba yetu wa Mbinguni wanatupenda, na Wako pamoja nasi.32 Kwa sababu Yesu alimtegemea Baba Yake na akakamilisha dhabihu kuu ya upatanisho, tunaweza kumtegemea Yesu Kristo kwa imani kwamba Atatusaidia.
Hakuna kati yetu aliye mkamilifu. Wakati mwingine tunakwama. Tunavurugwa mawazo au kukatishwa tamaa. Tunajikwaa. Lakini kama tutamtegemea Yesu Kristo kwa moyo wa toba, Yeye atatuinia, kutuosha kutoka dhambi, kutusamehe, na kuponya mioyo yetu. Yeye ni mwenye subira na mpole; upendo wake wa ukombozi kamwe hauna mwisho na haushindwi.33 Atatusaidia kuishi maagano yetu na kukuza miito yetu kama wazee katika Israeli.
Na Baba atatubariki kwa vitu vyote vinavyohitajika kukamilisha azma Zake: “vitu … vyote vilivyo mbinguni na duniani, maisha na nuru, Roho na nguvu, iliyotumwa mbele kwa mapenzi ya Baba kupitia Yesu Kristo, Mwanaye.”34
Wakati nuru takatifu na nguvu vinatiririka kwenye maisha yetu vitu vitatu vya kimiujiza vinatokea:
Kwanza, tunaweza kuona! Kupitia ufunuo tunaanza kuona kama Yesu alivyomwona mwanamke: kupita mwonekano wa nje mpaka moyoni.35 Tunapoona kama Yesu anavyoona, Anatubariki kuwapenda wale tunaowatumikia kwa upendo Wake. Kwa usaidizi wake, wale tunaowahudumia watamwona Mwokozi na kuhisi upendo Wake.36
Pili, tuna nguvu za ukuhani! Tuna mamlaka na nguvu ya kutenda katika jina la Yesu Kristo “kubariki, kuongoza, kulinda, kuimarisha, na kuwaponya wengine na kuleta miujiza kwa wale [tunao] wapenda na kuweka ndoa [zetu] na familia salama.”37
Tatu,Yesu Kristo huenda pamoja nasi Kule tuendako, Yeye anakwenda. Wakati tunapofundisha, Yeye hufundisha. Wakati tunapofariji, Yeye hufariji Wakati tunapobariki,Yeye hubariki.38
Akina kaka, je, hatuna sababu ya kufurahia? Tunayo! Tunao ukuhani mtakatifu wa Mungu. Tunapomtegemea Yesu Kristo, kuishi maagano yetu, na kukaza fokasi yetu kwake, tutajumuika na dada zetu na kutumikia katika njia takatifu zaidi, kukusanya Israeli iliyotawanyika kutoka pande zote mbili za pazia, kuimarisha na kuunganisha familia zetu, na kuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili wa Bwana Yesu Kristo. Itatokea. Nashuhudia hivyo.
Ninafunga kwa sala hii kutoka moyoni mwangu, kwamba sisi sote, kila mmoja, atamtegemea Yesu Kristo katika kila wazo. Usitie shaka. Usiogope. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.