Acha Sote Twende Mbele
Hamu yenu ya kutii itazidishwa mnapokumbuka na kutafakari juu ya kile mlichohisi siku hizi mbili zilizopita.
Akina kaka na akina dada zangu wapendwa, tunapokaribia tamati ya mkutano huu wa kihistoria, ninaungana nanyi katika kumshukuru Bwana kwa maelekezo Yake na ushawishi wa kutia msukumo. Muziki umekuwa mzuri na wa kuinua. Sio tu kwamba jumbe zimekuwa za kuadilisha, bali pia zimekuwa za kubadili maisha!
Katika kusanyiko takatifu tuliidhinisha Urais wa Kwanza mpya. Wanaume wawili wa ajabu wamewekwa katika Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Na wale Sabini Viongozi Wakuu wenye Mamlaka wanane wameitwa.
Sasa wimbo unaopendwa sana unafanya muhtasari maazimio yetu tuliyofanya upya, changamoto yetu, na wajibu wetu kusonga mbele:
Acha twende mbele na kazi ya Bwana,
Ili tupate tuzo mwishoni;
Na tupiganie haki kwa upanga,
Upanga mkuu wa Ukweli
Usimuogope adui;
Kwa ujasiri, kwani Bwana yu nasi.
Hatutasikiliza wasemayo,
Bali Bwana pekee tutamtii.1
Ninawahimiza mjifunze jumbe za mkutano huu kila mara—hata tena na tena—kwa muda wa miezi sita ijayo. Kwa makini, tafuta njia za kujumuisha jumbe hizi katika jioni zenu za familia nyumbani, kufundisha kwenu injili, mazungumzo yenu kati ya familia na marafiki, na hata majadiliano yenu na wale wasio wa imani yetu. Watu wengi wazuri wataitikia kweli zilizofundishwa katika mkutano huu wakati zinapotolewa kwa upendo. Na hamu yenu ya kutii itazidishwa mnapokumbuka na kutafakari juu ya kile mlichohisi siku hizi mbili zilizopita.
Mkutano mkuu unashiria mwanzo wa enzi mpya ya kuhudumu. Bwana amefanya marekebisho muhimu katika njia tunayotunzana. Akina dada na kina kaka—wazee kwa vijana—watahudumiana mmoja kwa mwingine katika njia mpya, takatifu. Akidi za wazee zitaimarishwa kubariki maisha ya wanaume, wanawake, na watoto kote ulimwenguni. Akiaa dada wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama wataendelea katika njia zao za kipekee na upendo, wakitoa nafasi kwa kina dada wadogo kuungana kama inavyopangwa ifaavyo.
Ujumbe wetu kwa ulimwengu ni rahisi na wa kweli: tunawaalika watoto wa Mungu wote kutoka pande zote mbili za pazia waje kwa Mwokozi wao, wapokee baraka za hekalu takatifu, wawe na furaha ya kudumu, na kustahili uzima wa milele.2
Kuinuliwa mwishowe kunahitaji uaminifu wetu kamili sasa kwa maagano tunayofanya na ibada tunazopokea katika nyumba ya Bwana. Wakati huu, tuna mahekalu 159 yanayofanya kazi, na zaidi yanaendelea kujengwa. Tunataka kuyaleta mahekalu karibu na idadi ya waumini wa Kanisa inayoongezeka. Sasa tunafurahia kutangaza mipango ya kujenga mahekalu saba zaidi. Mahekalu hayo yatakuwa katika maeneo yafuatayo: Salta Ajentina; Bengaluru, India; Managua, Nicaragua; Cagayan de Oro, Philipines; Layton, Utah; Richmond, Virginia; na jiji kuu katika Urusi ambalo halijachaguliwa.
Akina kaka na kina dada wapendwa, ujenzi wa mahekalu haya hautabadilisha maisha yenu, lakini muda wenu hekaluni hakika utabadilisha. Katika roho hiyo, ninawabariki muweze kutambua vile vitu ambavyo mnaweza kuviacha ili muweze kutumia muda zaidi hekaluni. Ninawabariki na uwiano mkuu na upendo majumbani mwenu na tamaa ya dhati ya kujali mahusiano ya familia zenu za milele. Ninawabariki na ongezeko la imani kubwa katika Bwana Yesu Kristo na uwezo mkubwa zaidi wa kumfuata kama wafuasi Wake wa kweli.
Ninawabariki mpaze sauti zenu katika ushuhuda, ninafanya hivi sasa, kwamba tujishughulishe katika kazi ya Mwenyezi Mungu! Yesu ndiye Kristo. Hili ni Kanisa Lake, analoliongoza kupitia watumishi Wake waliopakwa mafuta. Nashuhudia hivi, pamoja na upendo wangu kwa kila mmoja wenu, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.