Ibada za Wokovu Zitatuletea Nuru ya Ajabu
Kushiriki katika ibada na kuheshimu maagano husika kutakuletea nuru ya ajabu na ulinzi katika dunia hii inayozidi kuwa na giza kila wakati.
Akina kaka na akina dada, ninafurahi pamoja na nanyi katika injili, au mafundisho ya Kristo.
Rafiki wakati mmoja alimuuliza Mzee Neil L. Andersen, wakati huo akiwa wa Sabini, jinsi unavyojihisi kuzungumza mbele ya watu 21,000 katika Kituo cha Mikutano. Mzee Andersen alijibu, “Si wale watu 21,000 ambao wanakufanya uwe na hofu; ni wale Ndugu 15 walioketi nyuma yako.” Nilicheka wakati huo, lakini ninahisi hivyo sasa hivi. Jinsi gani ninavyowapenda na kuwaidhinisha hawa wanaume 15 kama manabii, waonaji, na wafunuaji.
Bwana alimwambia Ibrahimu ya kwamba kupitia uzao wake na kupitia ukuhani, familia zote za dunia zitabarikiwa “kwa baraka za Injili … hata za uzima wa milele” (Ibrahimu 2:11; ona pia aya za 2–10).
Baraka hizi za injili na ukuhani zilizoahidiwa zilirejeshwa duniani, na kisha mwaka wa 1842, Nabii Joseph Smith alitoa endaumenti kwa idadi ndogo ya wanaume na wanawake. Mercy Fielding Thompson alikuwa mmoja wao. Nabii alimwambia, “Hii [endaumenti] itakuondoa gizani hadi kwenye nuru ya ajabu.”1
Leo hii ningependa kuzingatia kwenye ibada za wokovu, ambazo zitatuletea wewe na mimi nuru ya ajabu.
Ibada na Maagano
Katika Kweli kwa Injili tunasoma: “Ibada ni kitendo kitakatifu, rasmi, kinachofanywa kwa mamlaka ya ukuhani. [Zile] Ibada [ambazo] ni muhimu kwa ajili ya kuinuliwa kwetu … zinajulikana kama Ibada za wokovu. Zinajumuisha ubatizo, uthibitisho, utawazo katika Ukuhani wa Melkizedeki (kwa wanaume), endaumenti ya hekalu, na ufunganishaji wa ndoa.”2
Mzee David A. Bednar alifundisha, “Ibada za wokovu na kuinuliwa zinazotolewa katika Kanisa la urejesho la Bwana … zina mikondo iliyoidhinishwa ambayo kwayo baraka na nguvu za mbinguni zinaweza kutiririka kwenye maisha yetu binafsi.”3
Kama pande mbili za sarafu, ibada zote za wokovu zinaambatana na maagano na Mungu. Mungu alituahidi baraka ikiwa tutaheshimu maagano hayo kwa uaminifu.
Nabii Amuleki alitamka, “Huu … ndiyo wakati wa … kujitayarisha kukutana na Mungu” (Alma 34:32). Ni kwa jinsi gani tutajitayarisha? Kwa kupokea maagizo kwa ustahiki. Ni lazima pia, katika maneno ya Rais Nelson, “baki katika njia ya agano.” Rais Nelson aliendelea, “Wajibu wako wa kumfuata Mwokozi kwa kufanya maagano Naye na kisha kuyaishi maagano hayo kutafungua mlango kwa kila baraka ya kiroho na fadhila iliyoko kwa wanaume, wanawake, na watoto kila mahali.”4
John na Bonnie Newman, kama wengi wenu, ni wapokeaji wa baraka za kiroho Rais Nelson alizoahidi. Jumapili moja, baada ya kuhudhuria kanisani pamoja na watoto wao wadogo, Bonnie alimwambia John, ambaye hakuwa muumini wa Kanisa, “Siwezi kufanya haya peke yangu. Unahitaji kuamua ikiwa utakuja kanisani letu pamoja nasi au uchague kanisa ambalo tunaweza kwenda pamoja, lakini watoto wanahitaji kujua kwamba baba yao anampenda Mungu pia.” Jumapili iliyofuata na kila Jumapili baada ya hiyo, John hakuhudhuria tu; alihudumia pia, alicheza kinanda katika kata nyingi, matawi, na Msingi kwa muda wa miaka mingi. Nilikuwa na heshima ya kukutana na John mwezi wa Aprili 2015, na katika mkutano ule, tulijadiliana kwamba njia bora ambayo angeweza kuonyesha upendo wake kwa Bonnie ilikuwa ni kwa kumpeleka hekaluni, lakini hilo lisingetokea bila yeye kubatizwa.
Baada ya kuhudhuria Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa miaka 39, John alibatizwa mwaka wa 2015. Mwaka mmoja baadaye, John na Bonnie waliunganishwa katika Hekalu la Memphis Tennessee, miaka 20 baada ya Bonnie kupokea endaumenti yake. Mwana wao wa miaka 47, Robert, alisema kuhusu babake, “Baba kwa kweli, kweli kabisa amesitawi baada ya kupokea ukuhani wake.” Bonnie aliongezea, “John daima amekuwa mwenye furaha na mtu mchangamfu, lakini kupokea ibada na kuheshimu maagano yake kumezidisha upole wake.”
Upatanisho wa Kristo na Mfano Wake
Miaka Mingi iliyopita, Rais Boyd K. Packer alionya, “Tabia nzuri bila ibada za injili haitawakomboa wala kuwainua wanadamu.”5 Kwa kweli, hatuhitaji tu ibada na maagano ili tuweze kurudi kwa Baba yetu, lakini pia tunamhitaji Mwanawe, Yesu Kristo, na Upatanisho Wake.
Mfalme Benjamin alifundisha ya kwamba ni katika na kupitia jina la Kristo pekee ndipo wokovu waweza kuwashukia watoto wa watu (ona Mosia 3:17; ona pia Makala ya Imani 1:3).
Kupitia Upatanisho Wake, Yesu Kristo alitukomboa kutokana na athari za Kuanguka kwa Adamu na kufanya kuwe na uwezekano wa toba yetu na hatimaye kuinuliwa kwetu. Kupitia maisha yake, alitoa mfano kwa ajili yetu kupokea ibada za wokovu, ambazo “nguvu za uchamungu hudhihirishwa” (M&M 84:20).
Baada ya Mwokozi kupokea ibada ya ubatizo ili “kutimiza utakatifu wote” ona (ona 2 Nefi 31:5–6), Shetani alimjaribu. Kadhalika, majaribu yetu hayaishi baada ya ubatizo au kuunganishwa, lakini kupokea ibada takatifu na kuheshimu maagano matakatifu husika kunatujaza na nuru ya ajabu na kutupa nguvu za kupinga na kushinda majaribu.
Onyo
Isaya alitabiri ya kwamba katika siku za mwisho, “tena dunia imetiwa unajisi … kwa maana wame … ibadili amri” (Isaya 24:5; ona pia M&M 1:15).
Onyo sawa na hili, lililofunuliwa kwa Nabii Joseph Smith, ilikuwa kwamba baadhi “husogea karibu nami [Bwana] kwa midomo yao, … wao hufundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu, yenye aina ya uchamungu ndani yake, lakini wakikana nguvu zake” (Joseph Smith—Historia 1:19).
Paulo pia alionya ya kwamba wengi watakuwa “wenye mfano wa utauwa, lakini [wakikana] nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.”(2 Timotheo 3:5). Nitarudia, hao nao jiepushe nao.
Wasiwasi mwingi na majaribu ya dunia ni kama “mbwa-mwitu wakali” (Mathayo 7:15). Ni mchungaji wa kweli ambaye atatayarisha, atalinda, na kuonya kondoo na kundi wakati mbwa-mwitu hawa wanapokaribia (ona Yohana 10:11–12). Kama wachungaji wasaidizi wanaotafuta kuiga maisha kamilifu ya Mchungaji Mwema, je, sisi sio wachungaji wa nafsi yetu wenyewe pamoja na za wengine? Pamoja na ushauri wa manabii, waonaji, na wafunuaji ambao tumetoka tu kuwaidhinisha, na pamoja na nguvu na kipawa cha Roho Mtakatifu, tunaweza kuwaona mbwa-mwitu wakija ikiwa tutakuwa waangalifu na kuwa tayari. Kinyume na hayo, wakati tunapokuwa wachungaji wasiojali sana juu ya nafsi zetu na nafsi za wengine, majeruhi watakuwepo. Kutojali kunasababisha majeruhi. Ninawaalika kila mmoja wetu kuwa mchungaji mwaminifu.
Uzoefu na Ushuhuda
Sakramenti ni ibada ambayo inatusaidia sisi kubaki katika njia, na kushiriki kwa ustahiki ni ushahidi ya kwamba tunaweka maagano yetu husika na ibada zingine zote. Miaka michache iliyopita, wakati mke wangu, Anita, pamoja nami tulikuwa tukihudumia katika Misheni ya Arkansas Little Rock, nilienda kufundisha pamoja na vijana wamisionari wawili. Wakati wa somo, ndugu mzuri tuliyekuwa tukimfundisha alisema, “Nimeshiriki kanisani mwenu; ni kwa nini mnashiriki mkate na kunywa maji kila Jumapili? Katika Kanisani letu, tunafanya hivyo mara mbili katika mwaka, Pasaka na Krismasi, na hiyo ni ya maana sana.”
Tulishiriki naye ya kwamba tumeamriwa kwamba “[tu]kutane pamoja mara kwa mara kushiriki mkate na divai” (Moroni 6:6; ona pia M&M 20:75). Tulisoma kwa sauti kubwa Mathayo 26 na 3 Nefi 18. Alijibu kwamba bado hakuona umuhimu wake.
Kisha tulishiriki ulinganishi ufuatao: “Hebu fikiria kuwa umehusika katika ajali mbaya ya gari. Umeumia na umepoteza fahamu. Mtu fulani anapita, anapogundua kwamba umepoteza fahamu, anapiga nambari ya dharura, 911. Unahudumiwa na unapata fahamu.”
Tulimwuliza ndugu huyu, “Wakati utakapoweza kutambua mazingira yako, ni maswali gani utakuwa nayo?”
Alisema, “Nitataka kujua ni vipi nilifika pale na nani alinikuta. Nitataka kumshukuru kila siku kwa maana aliokoa maisha yangu.”
Tulishiriki na ndugu huyu mzuri jinsi Mwokozi alivyookoa maisha yetu na jinsi tunahitaji kumshukuru kila siku, kila siku, kila siku!
Kisha tukamwuliza, “Ukifahamu ya kwamba alitoa maisha yake kwa ajili yako na sisi, ni mara ngapi ungependa kushiriki mkate na maji kama ishara za mwili na damu Yake?”
Alisema, “Naelewa, naelewa. Lakini kitu kimoja zaidi. Kanisa lenu sio changamfu kama letu.”
Kwa hilo tulijibu, “Ungelifanya nini ikiwa Mwokozi Yesu Kristo ataingia katika mlango wetu?”
Alisema, “Mara moja, nitapiga magoti.”
“Tuiuliza, “Je, si hivyo unavyohisi wakati unapoingia katika majumba ya Watakatifu wa Siku za Mwisho—heshima kuu kwa Mwokozi?”
Alisema, “Naelewa, naelewa, naelewa!”
Alikuja kanisani Jumapili ile ya Pasaka na akaendelea kurudi.
Ninamtaka kila mmoja wetu ajiulize, “Ni ibada ipi, ikiwa ni pamoja na sakramenti, ninayohitaji kupokea, na maagano yapi ninahitaji kuyafanya, kuyaweka, na kuyaheshimu?” Ninaahidi ya kwamba kushiriki katika ibada na kuheshimu maagano husika kutakuletea nuru ya ajabu na ulinzi katika dunia hii inayozidi kuwa na giza wakati kila wakati. Katika jina la Yesu Kristo, amina.