Kitu Ambacho Kila Mwenye Ukuhani wa Haruni Anahitaji Kufahamu
Kutawazwa kwenu katika Ukuhani wa Haruni ni muhimu katika kuwasaidia watoto wa Mungu kupokea nguvu za Kristo za kulipia dhambi.
Ndugu, ni jambo la fadhila kuwa nanyi kwenye mkutano huu wa kihistoria. Nilipokuwa rais mpya wa misheni, nilikuwa na shauku kubwa ya kupokea kikundi cha kwanza cha wamisionari wetu wapya. Wakati wachache wa wamisionari waliokuwa na uzoefu walipokuwa wakijitayarisha kwa ajili ya mkutano mfupi na wao. Niliona kuwa walikuwa wamepanga viti vya watoto kwenye nusu mduara.
“Je, ni nini kinachoendelea na viti hivi vidogo? Niliuliza.
Wamisionari, kwa aibu, wakasema, “Kwa ajil ya wamisionari wapya.”
Ninaamini kuwa namna tunavyowaona wengine huathiri mtazamo wao kuhusu wao ni nani na kile wanachoweza kuwa.1 Wamisionari wetu wapya walikalia viti vya watu wazima siku hiyo.
Wakati mwingine, ninahofia kuwa tunawapa kwa mfano, vijana wetu wa Ukuhani wa Haruni viti vya watoto kukalia badala ya kuwasaidia kuona kwamba Mungu amewapa wao jukumu takatifu na kazi muhimu ya kufanya.
Rais Thomas S. Monson alitushauri kwamba vijana wanahitaji kuelewa “inamaanisha nini … kuwa wenye ukuhani wa Mungu. Wanahitaji kuongozwa kwenye utambuzi wa kiroho wa utakatifu wa wito wao waliotawazwa.2
Hivi leo, ninaomba kuwa Roho Mtakatifu atuongoze kila mmoja wetu tufike kwenye ufahamu zaidi wa nguvu na utakatifu wa Ukuhani wa Haruni na kutupa mwongozo wa kiungu ili kuzingatia kwa makini zaidi majukumu yetu ya ukuhani. Ujumbe wangu ni kwa wenye Ukuhani wa Haruni, ikijumuisha pia wale wenye Ukuhani wa Melkizedeki.
Mzee Dale G. Renlund alifundisha kwamba makusudi ya ukuhani ni kuwaletea watoto wa Mungu nafasi za kunufaika kutokana na nguvu za Yesu Kristo za upatanisho.3 Ili kupokea nguvu za Yesu Kristo za kupatanisho maishani mwetu, ni sharti tuamini katika Yeye, kutubu dhambi zetu, kufanya na kushika maagano matakatifu kupitia njia ya ibada, na kumpokea Roho Mtakatifu.4 Hizi si kanuni tunazojishughulisha nazo mara moja tu, bali, zinafanya kazi pamoja, zikijiimarisha na kujijenga moja juu ya ingine kwenye mchakato unaoendelea wa kuelekea juu ili “kuja kwa Kristo, na kukamilishwa ndani Yake.”5
Hivyo basi, nafasi ya Ukuhani wa Haruni ni ipi? Je, ni kwa namna gani hutusaidia sisi kupata nguvu ya Yesu Kristo za upatanisho? Ninaamini kuwa jibu lipo kwenye funguo ambazo Ukuhani wa Haruni hushikilia—funguo za huduma za malaika na injili ya matayarisho.6
Huduma ya Malaika
Tuanze na huduma ya malaika. Kabla ya wana wa Mungu kuwa na imani katika Yesu Kristo, wanahitaji kumjua na kufundishwa injili Yake. Mtume Paulo alisema:
“Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? tena wamsikieje pasipo mhubiri?
“Tena wahubirije, wasipopelekwa? …
“Basi, imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Mungu.”7
Tangu mwanzo wa nyakati, Mungu “amewatuma malaika kuhudumu kwa watoto wa watu, kuwajulisha kuhusu kuja kwa Kristo.8 Malaika ni viumbe wa mbinguni wanaobeba ujumbe wa Mungu.9 Katika Kiebrania na Kiyunani, mzizi wa neno malaika ni “mjumbe.”10
Kwa njia iliyo sawa na ambavyo malaika hutumwa na Mungu kutangaza neno Lake na kujenga imani, sisi tulio na Ukuhani wa Haruni tumetawazwa “kufundisha na kuwaalika wote kuja kwa Kristo”11 Kuhubiri injili ni jukumu la kikuhani. Na nguvu inayohusishwa na jukumu hili si ya manabii au kwa ajili ya wamisionari pekee yao tu. Ni kwa ajili yako!12
Hivyo basi, tunaipataje nguvu hii? Shemasi wa miaka 12 —au yeyote kati yetu—anawezaje kuileta imani katika Kristo kwenye mioyo ya watoto wa Mungu? Tunaanza kwa kulithamini neno Lake ili nguvu Zake zipate kuwa ndani yetu.13 Ameahidi kuwa tukifanya hivyo tutakuwa na “uwezo wa Mungu hata kuwashwishi wanadamu.”14 Inaweza kuwa fursa ya kufundisha kwenye mkutano wa akidi, au kutembelea nyumba ya muumini. Inaweza kuwa jambo lisilo rasmi, kama mazungumzo na rafiki au mwana familia. Kwa yoyote kati ya mazingira haya kama tumejitayarisha tunaweza kufundisha injili kama vile malaika afanyavyo: kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.15
Hivi majuzi nilimsikia Jacob, mwenye Ukuhani wa Haruni huko Papua New Guinea akishuhudia nguvu za Kitabu cha Mormoni na jinsi kilivyomsaidia kukinza uovu na kumfuata Roho. Maneno yake yalizidisha imani yangu na imani ya wengine. Imani yangu pia imekua kadiri ninavyowasikiliza wenye Ukuhani wa Haruni wakifundisha na kushuhudia kwa heshima katika mikutano yao ya akidi.
Vijana ninyi ni wajumbe wenye mamlaka. Kupitia kwa maneno na matendo yenu, mnaweza kuleta imani katika Kristo kwenye mioyo ya wana wa Mungu.16 Kama alivyosema Rais Russell M. Nelson “ Kwao mtakuwa kama malaika wanaohudumu.”17
Ukuhani wa Matayarisho
Ongezeko la imani katika Kristo kila mara hutupeleka katika hamu ya kubadilika au kutubu.18 Kwa hivyo kuna mantiki kwamba funguo za huduma ya malaika, ikaambatana na funguo za injili ya matayarisho, “injili ya toba, na ya ubatizo, na ya ondoleo la dhambi.19
Mnapojifunza majukumu yenu ya Ukuhani wa Haruni mtaona wajibu dhahiri wa kuwaalika wengine kutubu na kuwa bora.20 Hiyo haimaanishi kusimama kwenye pembe za barabara na kupaza sauti “Enyi tubuni!” Mara nyingi, inamaanisha kuwa sisi tunatubu, tunasamehe, na tunapohudumu kwa wengine tunatoa matumaini na amani inayoletwa na toba—kwa sababu tumepata uzoefu wake sisi wenyewe.
Nimekuwa na wenye Ukuhani wa Haruni wanapowatembelea washiriki wa akidi wenzao. Nimeshuhudia mioyo yao laini yenye kujali na wakiwasaidia kaka zao kuuona upendo wa Mungu. Nilimsikia wakati mmoja mvulana akitoa ushuhuda kwa wenzake kuhusu nguvu za toba. Alipofanya hivyo, mioyo ililainishwa, ahadi zilifanyika na nguvu za Kristo za uponyaji zilionekana.
Rais Gordon B. Hinckley alitufundisha “Ni jambo moja kutubu. Ni jambo lingine kupata ondoleo la dhambi au kusamehewa. Nguvu ya kufanikisha hili inapatikana katika Ukuhani wa Haruni.”21 Ibada za Ukuhani wa Haruni za ubatizo na sakramenti hushuhudia na kukamilisha toba yetu kwa ondoleo la dhambi.22 Rais Dallin H. Oaks alielezea hili hivi: “Tumeamriwa kutubu dhambi zetu na kuja kwa Bwana na moyo uliovunjika na roho iliyopondeka na kupokea sakramenti. Tunapofanya upya maagano yetu ya ubatizo kwa njia hii, Bwana hufanya upya uwezo wa ubatizo wetu kutusafisha.23
Ndugu, ni heshima takatifu kusimamia ibada zinazosaidia kuleta ondoleo la dhambi kwenye mioyo iliyo na toba kupitia kuwa uwezo wa Mwokozi wa upatanisho.24
Hivi majuzi niliambiwa kuhusu kuhani, aliye na changamoto ya kujieleza mwenyewe, ambaye alikuwa akibariki sakramenti kwa mara ya kwanza. Alipofanya hivyo, roho mwenye nguvu alimjia yeye pamoja na umati ule. Baadaye kwenye mkutano, alitoa ushuhuda rahisi na dhahiri juu ya uwezo wa Mungu aliouona wakati wa ibada hiyo.
Huko Sydney, Australia waumini wanne wa akidi ya makuhani waliibatiza familia ya Mbuelongo. Mama wa mmoja wa makuhani hawa alinielezea jinsi uzoefu huu ulivyomwathiri mwanawe kwa nguvu. Makuhani hawa walikuja kuelewa maana ya “kutumwa na Yesu Kristo”25
Kama mnavyojua, makuhani sasa wanaweza kusimamia ubatizo mbadala hekaluni. Mwanangu mwenye umri wa miaka 17 hivi majuzi alinibatiza kwa niaba ya baadhi ya wahenga wetu. Sote tulihisi shukrani ya kina kwa Ukuhani wa Haruni na fursa ya kuweza kutenda kwa ajili ya wokovu wa watoto wa Mungu.
Vijana mnapojishughulisha kwa bidii katika majukumu yenu ya ukuhani, mnashirikiana na Mungu katika kazi Yake ya “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.”26 Uzoefu kama huu unaongeza hamu yenu kufundisha toba na kuwabatiza wanaoongoka kama wamisionari. Pia unawatayarisha kwa huduma ya maishani mwote kwenye Ukuhani wa Melkizediki.
Yohana Mbatizaji Mfano Wetu
Wenye wa Ukuhani wa Haruni, tunayo heshima na wajibu wa kuwa wahudumu wenza wa Yohana Mbatizaji. Yohana alitumwa kama mjumbe aliyepewa mamlaka kushuhudia kuhusu Kristo na kuwaalika wote kutubu na kubatizwa—yaani, alitumia funguo za Ukuhani wa Haruni ambazo tumejadili. Yohana alitangaza, “Mimi nawabatiza kwa maji kama ishara kwamba mmetubu dhambi zenu. Lakini baada yangu anakuja aliye mkuu kuliko mimi, … : Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.27
Hivyo Ukuhani wa Haruni husimamia injili ya matayarisho, huandaa njia kwa watoto wa Mungu kupokea kwa kupitia Ukuhani wa Melkizedeki kipawa cha Roho Mtakatifu, kipawa kilicho kikuu kuu tunachoweza kupokea katika maisha haya.28
Ni jukumu kuu lilioje ambalo Mungu amewapa wenye Ukuhani wa Haruni!
Mwaliko na Ahadi
Wazazi na viongozi wa ukuhani, mnaweza kuona umuhimu wa ushauri wa Rais Monson wa kuwasaidia vijana kuelewa “kinachomaanisha … kuwa wenye ukuhani wa Mungu”?29 Kuelewa na kupanua Ukuhani wa Haruni ni matayarisho bora zaidi tunayoweza kuwapa ili waweze kuwa makuhani waaminifu wa Melkizedeki, wamisionari waliojawa na nguvu na wakina baba na waume wenye haki. Kupitia huduma yao, hawataelewa tu bali watahisi ukweli na uhalisi wa uwezo wa ukuhani, na uwezo wa kutenda katika jina la Kristo kwa ajili ya wokovu wa watoto wa Mungu.
Wavulana, Mungu ana kazi kwa ajilii yenu.30 Kutawazwa kwenu katika Ukuhani wa Haruni ni muhimu katika kuwasaidia watoto wa Mungu kupokea nguvu za Kristo za kulipia dhambi. Ninaahidi kuwa mnapoweka majukumu haya matakatifu katikati ya maisha yenu, mtahisi nguvu za Mungu kwa njia ambayo hamjawahi kuona hapo awali. Mtaelewa utambulisho wenu kama mwana wa Mungu, aliyeitwa katika wito mtakatifu ili kufanya kazi Yake. Nanyi, kama Yohana Mbatizaji, mtasaidia kutayarisha njia kwa ajili ya kurudi kwa Mwana Wake. Juu ya ukweli huu mimi nashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.