Zawadi za Thamani kutoka kwa Mungu
Maisha yanaweza yakajawa na imani, shangwe, furaha, tumaini, na upendo wakati tunapokuwa na kiasi kidogo kabisa cha imani ndani ya Kristo.
Kaka zangu na dada zangu, tumetoka kushiriki hivi punde katika kusanyiko takatifu, zoezi ambalo linaweza kufuatiliwa kwa kurudi nyuma hadi kwenye Biblia wakati Israeli wa kale walipokusanyika kuona uwepo wa Bwana na kusherehekea baraka Zake.1 Tuna bahati kuishi katika wakati ambapo zoezi hili la kale limerejeshwa kupitia Nabii Joseph Smith.2 Ninawasihi muandike katika shajara zenu binafsi kile ulichokihisi kuhusu tukio hili takatifu ambapo wewe umehusika.
Hivi majuzi, tulimpa mkono wa buriani rafiki yetu mpendwa na nabii, Rais Thomas S. Monson. Ingawa sisi wote tunamkosa, tunazo shukrani za dhati kwa maana Bwana amemuita nabii mpya, Rais Russell M. Nelson, ili kuliongoza Kanisa Lake. Katika njia ya utaratibu sasa tumeanza enzi mpya katika historia ya Kanisa letu. Ni zawadi ya thamani kutoka kwa Mungu.
Wakati kila mmoja wetu alipomkubali Rais Nelson kwa mikono yetu iliyoinuliwa juu, tulisimama kama mashahidi mbele ya Mungu na kumtambua kama mrithi halali wa Rais Monson. Kwa mikono yetu iliyoinuliwa, tuliahidi kutii sauti yake anapopokea maelekezo kutoka kwa Bwana.
Bwana amesema:
“Nawe utayaangalia maneno yake [akimaanisha Rais wa Kanisa] yote na amri ambazo atazitoa kwenu kadiri anakavyozipokea … ;
“Kwani neno lake mtalipokea, kama vile linatoka kinywani mwangu, katika uvumilivu na imani yote.”3
Nimemfahamu nabii-rais wetu mpya kwa zaidi ya miaka 60. Nimehudumu pamoja naye katika Akidi ya Kumi na Wawili kwa miaka 33, na mimi ni shahidi kwamba mkono wa Bwana umekuwa ukimtayarisha ili awe mtume kiongozi na nabii ili kusimamia funguo zote za ukuhani hapa duniani. Na kila mmoja wetu amkubali kikamilifu pamoja na washauri wake na kufuata ushauri wao. Pia tunawakaribisha kwa moyo mkunjufu Mzee Gong na Mzee Soares kama washiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili.
Baada ya ufufuko wa Yesu, tukio ambalo tunalisherehekea wikendi hii tukufu ya Pasaka, Aliwatokea wanafunzi Wake na kusema, “Amani iwe kwenu: kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi.”4 Tazama tendo hili la pande mbili—Mungu anamtuma Mwanawe. Mwana anawatuma watumishi Wake—wanaume na wanawake—kumalizia kazi Yao.
Tusishangae kujua ya kwamba wale watu waliopewa wito kufanya kazi ya Bwana sio wakamilifu katika hali ya kibinadamu. Hadithi katika maandiko zinaeleza matukio kuhusu wanaume na wanawake ambao wamepewa wito na Mungu kufanikisha kazi muhimu—wana na mabinti wazuri wa Baba yetu wa Mbinguni walioitwa kuhudumu katika majukumu yao Kanisani, wanaojitahidi kufanya vyema, lakini hakuna ye yote ambaye ni mkamilifu. Hilo pia ni kweli kwetu sisi leo.
Kwa sababu ya hali halisi ya udhaifu wetu wa kibinadamu na kasoro zetu, ni jinsi gani tunaweza kusonga mbele katika kutoa msaada na kumkubali kila mmoja? Inaanza na imani—ya kweli, imani ya dhati katika Bwana Yesu Kristo. Imani katika Mwokozi ni kanuni ya kwanza ya mafundisho na injili ya Kristo.
Miaka kadhaa iliyopita nilitembelea, Nchi Takatifu. Tulipopita kando ya mmea wa mharadali, mkurugenzi wa Kituo cha Yerusalemu cha BYU aliniuliza kama nilikuwa nimewahi kuona punje ya haradali. Sikuwahi kuiona kwa hiyo tulisimama. Alinionyesha mbegu kutoka kwenye mmea wa mharadali. Kwa ajabu zilikuwa ndogo mno.
Kisha nikakumbuka mafundisho ya Yesu: “Kwa maana, amini, nawaambia, mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.”5
Ikiwa tutakuwa na imani ndogo kama punje ya haradali, Bwana anaweza kutusaidia kuondoa milima ya kukata tamaa na shaka katika majukumu yaliyo mbele yetu huku tukihudumu na watoto wa Mungu, ikiwa ni pamoja na wanafamilia, washiriki wa Kanisa, na wale ambao bado hawajajiunga na Kanisa.
Akina kaka na akina dada, maisha yanaweza yakajawa na imani, shangwe, furaha, tumaini, na upendo wakati tunapokuwa na kiasi kidogo kabisa cha imani ndani ya Kristo—hata punje ya haradali ya imani.
Mzee George A. Smith alikumbuka mawaidha ambayo Nabii Joseph Smith alimpa yeye: “Aliniambia kuwa kamwe nisije kata tamaa, licha ya shida zo zote zinazoweza kunizingira. Ikiwa nitazamishwa katika shimo la kina zaidi la Nova Scotia na Milima yote ya Rocky kushindiliwa juu yangu, sipaswi kukata tamaa bali nivumilie, na niwe na imani, na niendelee kuwa jasiri na nitaibuka juu ya rundo hilo mwishowe.”6
Tunapaswa kukumbuka tamko la Paulo: “Nayaweza mambo yote katika Kristo anitiaye nguvu.”7 Kufahamu hili ni kipawa kingine cha thamani kutoka kwa Mungu.
Kuongezea kwenye zawadi nilizotaja, ziko nyingine nyingi, nyingi mno. Kwa sasa nitazungumzia tu baadhi yake—zawadi ya siku ya Sabato, sakramenti, kuwatumikia wengine, na zawadi isiyo na kifani kutoka kwa Mungu wa Mwokozi wetu.
Nguvu ya siku ya Sabato ni kuwa na uzoefu kanisani na nyumbani wa furaha, shangwe, na joto la kuhisi Roho wa Bwana bila kuzuiliwa na kitu chochote.
Wengi wanajiruhusu karibia kuishi katika mtandao kwenye vifaa vyao vya kisasa—skrini zikimulika nyuso zao mchana na usiku na vyombo vya kusikilizia masikioni mwao vikizuia sauti tulivu, ndogo ya Roho. Ikiwa hatutapata muda wa kupumzika, tunaweza tukakosa nafasi za kusikia sauti ya Yule aliyesema, “Tulieni, na jueni kuwa Mimi ni Mungu.”8 Sasa hakuna ubaya katika kutumia kwa manufaa yetu hatua za technolojia zilizotiwa mwongozo wa kiungu na Bwana, lakini ni lazima tuwe na hekima katika matumizi yake. Kumbuka zawadi ya Siku ya Sabato.
Baraka ya kupokea sakramenti katika mkutano wa sakramenti sharti usiwe jambo la kawaida au kitu tunachofanya tu. Ni dakika tu 70 katika wiki mzima ambapo tunaweza kupumzika na kupata amani zaidi, shangwe, na furaha katika maisha yetu.
Kupokea sakramenti na kufanya upya maagano yetu ni ishara yetu kwa Bwana kwamba daima tunamkumbuka. Upatanisho Wake ni zawadi ya neema kutoka kwa Mungu.
Heshima ya kuwatumikia watoto wa Baba wa Mbinguni ni nafasi nyingine ya kumfuata Mwanawe Mpendwa kwa kutumikiana.
Baadhi ya nafasi za huduma ni rasmi—katika familia, wito wetu wa Kanisa, na kushiriki kwetu katika taasisi za huduma za jamii.
Waumini wa Kanisa—wanaume na wanawake—wasisite, ikiwa wana hamu, kugombea viti vya utumishi wa umma katika nyanja zo zote serikalini popote wanapoishi. Sauti zetu ni muhimu leo na ni muhimu katika shule zetu, miji yetu, na mataifa yetu. Pale ambapo demokrasia ipo, ni jukumu letu kama washiriki kuwapigia kura wanaume na wanawake wenye maadili mema ambao wako radhi kuhudumu.
Nafasi nyingi za kutoa huduma sio rasmi—bila ya kupangiwa—na huja tunapowaendea wengine na kukutana nao katika safari ya maisha. Kumbuka Yesu alimfundisha mwanasheria kwamba tunapaswa kumpenda Mungu na jirani yetu kama vile tunavyopenda nafsi zetu akitumia Msamaria mwema kama mfano.9
Huduma inafungua dirisha ambalo kupitia kwake tunaelewa maisha na misheni ya Kristo. Alikuja kutumikia, kama maandiko yanavyofundisha: “kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa; bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”10
Petro yawezekana kuwa alitoa maelezo yaliyo bora zaidi juu ya huduma ya Mwokozi duniani kwa maneno matano wakati aliposema kuhusu Yesu, “akazunguka huko na huko akitenda kazi njema.”11
Bwana Yesu Kristo ni zawadi ya thamani kubwa zaidi kati ya zawadi zote kutoka kwa Mungu. Yesu akamwambia, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”12
Nefi aligusia umuhimu wa Mwokozi wetu alipotamka, “Na tunazungumza kuhusu Kristo, tunafurahia katika Kristo, tunahubiri kuhusu Kristo, tunatoa unabii kumhusu Kristo, na tunaandika kulingana na unabii wetu, ili watoto wetu wajue asili ya kutegemea msamaha wa dhambi zao.”13 Ni lazima tumfanye Kristo awe kiini cha maisha yetu nyakati zote na kila mahali.
Tunapaswa kukumbuka ya kwamba ni jina Lake ambalo linaonekana katika sehemu zetu za kuabudu; tunabatizwa katika jina Lake; na tunathibitishwa, kutawazwa, kupokea endaumenti, na kuunganishwa kwenye ndoa katika jina Lake. Tupokea sakramenti na kuahidi ya kwamba tutajichukulia jina Lake juu yetu—na kuwa Wakristo kweli. Hatimaye, tunaombwa katika maombi ya sakramenti “daima kumkumbuka.”14
Tunapojitayarisha kwa ajili ya Jumapili ya Pasaka hapo kesho, natukumbuke kwamba Kristo ni mkuu. Yeye ni hakimu mwenye haki, Mwombezi wetu mwaminifu, Mkombozi wetu aliyebarikiwa, Mchungaji Mwema, Masiya mwahidiwa, Rafiki wa kweli, na zaidi, na zaidi. Kwa kweli Yeye ni zawadi ya thamani kwetu kutoka kwa Baba yetu.
Katika ufuasi wetu, tunayo mahitaji mengi, maswali, na majukumu. Hata hivyo, baadhi ya shughuli ni lazima daima ziwe kwenye kiini cha uumini wetu wa Kanisa. “Kwa hiyo,” Bwana anaamuru, “uwe mwaminifu; simama katika ofisi ambayo nimekuteua; uwasaidie wadhaifu, inyooshe mikono iliyolegea, na yaimarishe na magoti yaliyo dhaifu.”15
Hii ni Kanisa katika vitendo! Hii ni dini iliyo safi! Hii ni injili katika hali yake halisi tunapowasaidia, inua, na kuwaimarisha wale walio na mahitaji ya kiroho na ya kimwili! Kufanya hivyo kunatuhitaji sisi kuwatembelea na kuwasaidia,16 ili kwamba shuhuda zao za imani katika Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo na Upatanisho Wake ziweze kutia nanga mioyoni mwao.
Na Mungu atusaidie na atubariki tuweze kuthamini zawadi zetu nyizi zenye thamani ikijumuisha uumini wetu katika Kanisa Lake lililorejeshwa. Naomba tujawe na upendo kwa watoto wa Baba yetu wa Mbinguni na tuweze kuona mahitaji yao na tuwe tayari kujibu maswali yao na wasiwasi wao kuhusu injili katika njia zilizo wazi na karimu ambazo zitazidisha uelewa na kuthaminiana.
Ninatoa ushahidi wangu kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi wetu. Kile tutakachofundishwa katika huu mkutano mkuu kinatujia kwa mwongozo wa kiungu kutoka kwa mitume na manabii, kutoka kwa Viongozi Wakuu Wenye Mamlaka, na akina dada viongozi ambao ni Maafisa Wakuu wa Kanisa. Na furaha na amani ya Mungu iwe na kila mmoja ni maombi yangu katika jina la Bwana Yesu Kristo, amina.