2010–2019
Tazama! Jeshi la Kifalme
Aprili 2018


2:3

Tazama! Jeshi la Kifalme

Itakuwa shangwe iliyoje kwa wote wanaoshikilia Ukuhani wa Melkizedeki kuwa na baraka ya kufundisha, kujifunza, na kutumikia bega kwa bega.

Wapendwa ndugu zangu wa ukuhani, ni kwa unyenyekevu mkuu ninasimama mbele yenu katika tukio hili la kihistoria, chini uteuzi wa nabii na rais wetu mpendwa, Russel M. Nelson. Jinsi gani ninampenda na kumkubali mtu huyu mwema wa Mungu na Urais wetu wa Kwanza mpya. Ninaongeza ushahidi wangu kwenye ule wa Mzee D. Todd Christofferson na Ndugu zangu wengine wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili kwamba mabadiliko yaliyotangazwa jioni hii ni mapenzi ya Mungu.

Kama ilivyoelezwa na Rais Nelson, hili ni jambo ambalo kwa sala limejadiliwa na kufikiriwa na Ndugu waandamizi wa Kanisa kwa muda mrefu. Hamu ilikuwa ni kutafuta mapenzi ya Bwana na kuimarisha akidi za Ukuhani wa Melkizedeki. Mwongozo wa kiungu ulipokelewa, na jioni hii nabii wetu amefanya yajulikane mapenzi ya Bwana. “Hakika Bwana Mungu hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake”!1 Ni baraka iliyoje kwetu sisi kuwa na nabii anayeishi leo!

Katika maisha yetu yote, Mimi na Dada Rasband tumezuru ulimwengu katika majukumu mbalimbali ya Kanisa na ya kitaaluma. Nimeona karibu kila aina ya umbo la kikundi katika Kanisa: tawi dogo huko Urusi ambapo idadi ya wenye Ukuhani wa Melkizedeki iliweza kuhesabika katika mkono mmoja, kata mpya inayokuwa huko Afrika ambapo wote makuhani wakuu na wazee walikutana kama kundi moja kwa sababu idadi ya jumla ya wenye Ukuhani wa Melkizedeki ilikuwa ndogo; na kata-zenye mafanikio ambapo idadi ya wazee ilihitaji kugawanywa kwa akidi yao katika akidi mbili!

Kila mahali tulipokwenda, tumeshuhudia mkono wa Bwana ukitangulia mbele ya watumishi Wake, kuwaandaa watu na njia mbele ili kwamba watoto Wake wote waweze kubarikiwa kulingana na kila hitaji lao. Kwani, Yeye hajaahidi kwamba “Atakwenda mbele ya uso [wetu]” na kuwa katika “mkono [wetu] wa kuume na wa kushoto” na kwamba “Roho Wake atakuwa mioyoni mwenu, na malaika [Wake] watatuzingira”?2

Nikiwafikirieni ninyi nyote, Ninakumbushwa juu ya wimbo “Tazama” Jeshi la Kifalme.”

Tazama! Jeshi la kifalme,

Likiwa na bendera, upanga, na ngao,

Linasonga mbele kushinda

Kwenye uwanja mkuu wa vita vya maisha

Safu zake zimejazwa na wanajeshi,

Wamoja, wakakamavu na wenye nguvu,

Wanaomfuata Kamanda wao

Na kuimba wimbo wao wa shangwe.3

Mzee Christofferson amejibu maswali kadhaa ambayo ni hakika kuibuka kutokana na tangazo hili kwamba kundi la makuhani wakuu na akidi za wazee, katika ngazi ya kata, zimeunganishwa katika muungano mmoja, jeshi kuu la ndugu wa Ukuhani wa Melkizedeki.

Mabadiliko haya yatasaidia akidi za wazee na Muungano wa Usaidizi wa Wakina Mama kulinganisha kazi yao. Yatarahisisha pia uratibu wa akidi na uaskofu na baraza la kata. Na yanaruhusu askofu kunaibisha majukumu zaidi kwa marais wa akidi ya wazee na Muungano wa Usaidizi wa Wakina Mama ili kwamba askofu na washauri wake waweze kujikita katika majukumu yao ya msingi—hususani kuongoza wasichana, na wavulana ambao wana Ukuhani wa Haruni.

Mabadiliko katika muundo na utendaji wa Kanisa siyo kitu kigeni. Mnamo 1833, Bwana alisema kwa Rais John Taylor: “[Kuhusiana] na uongozi na muundo wa Kanisa langu na Ukuhani … Nitafunua kwako, muda baada muda, kupitia njia ambazo nimezichagua, kila kitu ambacho kitakuwa muhimu kwa maendeleo ya baadaye na kutakaswa kwa Kanisa langu, kwa mabadiliko na kusonga mbele kwa ufalme wangu.”4

Sasa, maneno machache kwenu ninyi ndugu ambao ni makuhani wakuu—jueni kwamba tunawapenda! Baba yetu wa Mbinguni anawapenda! Ninyi ni sehemu kuu ya jeshi la kifalme la ukuhani, na hatuwezi kuipeleka mbele kazi hii bila wema wenu, huduma, uzoefu, na haki. Alma alifundisha kwamba watu huitwa kuwa makuhani wakuu kwa sababu ya imani yao kubwa na kazi nzuri za kufundisha na kuwatumikia wengine.5 Uzoefu huo unahitajika sasa pengine zaidi ya wakati wowote.

Katika kata nyingi, tunaweza kuwa na makuhani wakuu ambao sasa watapata nafasi ya kuongozwa na mzee kama rais wa akidi yao. Tunao mfano wa wazee kuwaongoza makuhani wakuu: wazee kwa sasa wanatumikia kama marais wa matawi katika baadhi ya maeneo ya ulimwengu ambapo makuhani wakuu wanaishi katika tawi hilo, na kuna matawi ambapo akidi ya wazee tu ndiyo imeundwa na makuhani wakuu wapo.

Itakuwa shangwe iliyoje kwa wote wanaoshikilia Ukuhani wa Melkizedeki kuwa na baraka ya kufundisha, kujifunza, na kutumikia bega kwa bega na waumini wote katika kata yao. Popote mlipo na bila kujali hali zenu, tunakualikeni kwa sala, kwa uaminifu, na kwa furaha kukubali fursa mpya za kuongoza au kuongozwa na kutumikia kwa umoja kama kundi la ndugu wa ukuhani.

Sasa nitaongelea mambo ya mengine ambayo yanaweza kuhitaji ufafanuzi, tunaposonga mbele kutekeleza mapenzi ya Bwana kuhusiana na muundo wa akidi Zake za ukuhani mtakatifu.

Kuna mabadiliko yapi kwa akidi ya makuhani wakuu wa kigingi? Akidi za makuhani wakuu wa kigingi zitaendelea kufanya kazi. Urais wa vigingi utaendelea kutumikia kama urais wa akidi ya makuhani wakuu katika kigingi. Hata hivyo, kama ilivyoelezwa na Mzee Christofferson, washiriki wa akidi ya makuhani wakuu katika kigingi sasa itaundwa na makuhani wakuu ambao kwa sasa wanatumikia katika urais wa kigingi, kama washiriki wa uaskofu wa kata, kama washiriki wa baraza kuu katika kigingi, na patriaki anayefanya kazi. Makarani wa kata na vigingi na makatibu watendaji siyo washiriki akidi ya makuhani wakuu wa kigingi. Wakati mtu ambaye anatumikia kwa sasa kama kuhani mkuu, patriaki, Sabini, au Mtume anatembelea kata na kutamani kuhudhuria mkutano wa ukuhani, atakwenda kwenye akidi ya wazee.

Pale ndugu katika miito hii wanapopumzishwa kwa wakati upasao, watarudi kwenye vitengo vyao vya nyumbani kama washiriki wa akidi ya wazee.

Je, nafasi ya akidi ya makuhani wakuu ni ipi? Urais wa kigingi hukutana na washiriki wa akidi ya makuhani wakuu ili kushauriana pamoja, kushuhudia, na kutoa mafunzo. Mikutano ya vigingi kama ilivyoonyeshwa katika vitabu vyetu vya mwongozo itaendelea kwa mabadiliko mawili:

Moja, kata na vigingi havitafanya tena mikutano ya kamati ya utendaji ya Ukuhani. Kama jambo maalumu la kata limetokea, kama vile mambo nyeti ya kifamilia au changamoto ya ustawi isiyo ya kawaida, itaweza kuongelewa katika mkutano uliopanuliwa wa uaskofu. Mambo mengine yasiyohitaji umakini-mkubwa yanaweza kuongelewa katika baraza la kata. Kile ambacho kimekuwa kikijulikana kama mkutano wa kamati ya utendaji ya ukuhani ya kigingi sasa kitaitwa “mkutano wa baraza kuu.”

Pili, mkutano wa mwaka wa makuhani wakuu wote waliotawazwa katika kigingi hautafanyika tena. Isipokuwa, urais wa kigingi utaendelea kufanya mkutano wa mwaka wa akidi ya makuhani wakuu wa kigingi kama ilivyotangazwa leo.

Je, kata inaweza kuwa na akidi ya wazee zaidi ya moja? Jibu ni ndiyo. Katika roho ya Mafundisho na Maagano 107, mstari wa 89, wakati kata inapokuwa na idadi kubwa isiyo ya kawaida ya wenye Ukuhani wa Melkizedeki wanaoshiriki kikamilifu, viongozi wanaweza kuunda akidi ya wazee zaidi ya moja. Katika hali kama hizo, kila akidi inapaswa kuwa na uwiano sawa katika masuala ya umri, uzoefu, na ofisi na uimara.

Ninashuhudia kwamba tunaposonga mbele na muundo huu mpya wenye mwongozo wa kiungu katika kata zetu na vigingi, tutaona baraka tele. Wacha nitaje mifano michache tu.

Chini ya maelekezo ya askofu, nyenzo nyingi za ukuhani zinaweza kusaidia kwenye kazi ya wokovu. Hii itajumuisha kukusanywa kwa Israeli kupitia kazi ya hekalu na historia ya familia, kufanya kazi na familia na watu binafsi wenye shida, na kuwasaidia wamisionari kuleta roho kwa Yesu Kristo.

Viongozi waliopita wakirudi kushiriki uzoefu wao na akidi ya wazee, ushiriki imara zaidi wa akidi utazaliwa.

Kutakuwa na tofauti kubwa ya talanta na uwezo ndani ya akidi.

Kutakuwa na kunyumbulika zaidi na upatikanaji ili kutatua shida za sasa na za haraka ndani ya kata na akidi na katika kutimiza majukumu yetu mbalimbali ya utumishi.

Kutakuwa na ongezeko katika ushauri na umoja pale mzee mpya na kuhani mkuu mwenye uzoefu wanaposhiriki uzoefu, bega kwa bega, katika mikutano na kazi za akidi.

Maaskofu na marais wa matawi watakuwa kwa tumaini wameachwa huru ili kukuza miito yao kuchunga kundi lao na kuhudumia wale wenye shida.

Tunafahamu kwamba kila kata na kigingi ni tofauti. Tukiwa tunafahamu tofauti hizi, tunatumaini kwamba mtafuata mabadiliko haya mara tu baada ya mkutano huu mkuu. Tumepewa maelekezo na nabii wa Mungu! Ni baraka na wajibu mkubwa ulioje. Acha tuutimize kwa haki na bidii yote!

Ninawakumbusha kwamba mamlaka ya ukuhani huja kwa njia ya kusimikwa na kutawazwa, lakini nguvu halisi ya ukuhani, nguvu ya kutenda katika jina la Bwana Yesu Kristo, inaweza kuja tu kwa njia ya kuishi kwa haki.

Bwana alitangaza kwa Joseph Smith, nabii wa Urejesho:

“Tazama na lo, nitalichunga kundi lenu, na kuwainua wazee na kuwatuma kwao.

“Tazama, nitaiharakisha kazi yangu katika wakati wake.”6

Kweli, huu ni wakati ambapo Bwana ana harakisha kazi Yake.

Acha tutumie nafasi hii kutafakari na kuboresha maisha yetu ili yafungamane zaidi na mapenzi Yake ili kwamba tustahili baraka nyingi Alizoahidi kwa wa kweli na walio waaminifu.

Ndugu zangu wa ukuhani, asanteni kwa yote mnayofanya kuwa sehemu ya kazi hii kuu. Na tusonge mbele katika kusudi hili kuu na lenye heshima.

Ee, vita itakapokuwa imekwisha,

Wakati vurugu na mapambano vikikoma,

Wakati wote wamekusanywa salama

Ndani ya bonde la amani,

Mbele ya Mfalme milele,

Ule mkusanyiko mkubwa na mkuu

Utasifu jina lake milele,

Na huu utakuwa wimbo wao:

Ushindi, ushindi,

Kupitia yeye aliyetukomboa!

Ushindi, ushindi,

Kupitia Yesu Kristo, Bwana wetu!

Ushindi, ushindi, ushindi,

Kupitia Yesu Kristo, Bwana wetu!7

Leo sote tunasimama kama mashahidi wa Bwana kufunua mapenzi Yake kupitia nabii Wake, Rais Russell M. Nelson. Ninashuhudia kwamba yeye ndiye nabii wa Mungu hapa duniani. Ninatoa ushahidi wangu juu ya Bwana Yesu Kristo, ambaye ni Mkombozi wetu mkuu na Mwokozi. Hii ni kazi Yake; haya ni mapenzi Yake, ambayo kwayo Natoa ushuhuda wangu wa dhati katika jina la Yesu Kristo, amina.