2010–2019
Histioria ya familia na Kazi ya Hekalu: Kuunganishwa na Uponyaji
Aprili 2018


2:3

Historia ya Familia na Kazi ya Hekalu: Kuunganishwa na Uponyaji

Tunapokusanya historia za familia zetu na kwenda hekaluni kwa niaba ya wahenga wetu, Mungu anatimiza ahadi zake zilizoahidiwa kwa wakati mmoja pande zote mbili za pazia.

Uhusiano wa kifamilia unaweza kuwa baadhi ya matukio yenye thawabu na huko yakiwa na changamoto tunazokabiliana nayo. Wengi wetu tumekutana na mvunjiko wa aina fulani ndani ya familia zetu. Mvunjiko wa jinsi hiyo ulionekana kati ya mashujaa wawili wa Urejesho wa Kanisa la Yesu Kristo katika siku hizi za mwisho. Parley na Orson Pratt walikuwa mtu na kaka yake, waongofu wa mwanzo, na Mitume waliotawazwa. Kila mmoja alikabiliwa na jaribu la imani lakini walivuka kwa ushuhuda usiotingishika. Wote walitoa dhabihu na walichangia sana kwa kazi hii ya ukweli.

ParleyPratt

Katika zama za Nauvoo, uhusiano wao ulitetereka, kwa kiwango cha juu katika ugomvi mkali, mbele ya kadamnasi mwaka 1846. Ufa wa kina na wa muda mrefu ukaibuka. Parley alianza kumwandikia Orson ili wasuluhishe ule ufa, lakini Orson hakujibu. Parley akakata tamaa, akijisikia kuwa mawasiliano yalikuwa yamekatika milele, labda yaanzishwe na Orson.1

Orson Pratt

Miaka kadhaa baadae, mnamo Machi 1853, Orson akajua kuwa kuna mradi wa kuchapisha kitabu cha wazao wa William Pratt, wahenga wa Kimarekani wa wakina kaka hawa. Orson akaanza kulia “kama mtoto mdogo” wakati alipokuwa akiangalia tunu hii ya historia ya familia. Moyo wake ukayeyuka, akaazimia kutengeneza ufa pamoja na kaka yake.

Orson akamwandikia Parley, “Sasa kaka yangu mpendwa, hakuna yeyote miongoni mwa wazao wa babu yetu Lu [teni] William Pratt, ambaye anahamu kubwa ya kutafuta wazao wake kama sisi wenyewe.” Orson alikuwa mmoja kati ya watu wa kwanza kuelewa kwamba Watakatifu wa Siku za Mwisho wanao wajibu wa kutafuta na kukusanya kwa kuandika historia za familia ili tuweze kufanya ibada kwa niaba ya mababu zetu. Barua yake iliendelea: “Sisi tunajua kwamba Mungu wa mababu zetu amekuwa na mkono katika hili. … Nitaomba msamaha kwa kuwa nyuma sana katika kukuandikia wewe. … Natumaini utanisamehe.”2 Licha ya shuhuda zao zisizotingishika, upendo wao kwa wahenga wao ulikuwa kichocheo cha kuponyesha ufa, kurekebisha maumivu, na kutafuta na kutoa msamaha.3

Bwana anapotuelekeza kufanya kitu kimoja, Yeye mara nyingi anakuwa na makusudi mengi akilini. Historia ya familia na kazi ya hekalu si tu kwa ajili ya wafu bali huwabariki na walio hai vile vile. Kwa Orson na Parley, ilifanya mioyo yao igeukiane. Historia ya familia na kazi ya hekalu ilileta nguvu ya kuponya kile ambacho kilihitajika uponyaji

Kama waumini wa Kanisa, tunao wajibu mtakatifu wa kuwatafuta wahenga wetu na kukusanya historia za familia. Hii ni zaidi sana kuliko jambo alipendalo mtu kwa kuhimizwa kwa sababu ibada za wokovu ni muhimu kwa wokovu wa watoto wote wa Mungu.4 Tunapaswa kuwatambua wahenga wetu wenyewe ambao wamekufa pasipo kupokea ibada za wokovu. Sisi tunaweza kufanya ibada hizo kwa niaba yao hekaluni, na wahenga wetu wanaweza kuchagua kuzikubali ibada hizo.5 Tunahimizwa pia kuwasaidia waumini katika kata au vigingi katika kupata majina ya familia zao. Inapendeza sana kwamba, kupitia historia ya familia na kazi ya hekalu, sisi tunaweza kusaidia kuwakomboa wafu.

Lakini, tunaposhiriki katika historia ya familia na kazi ya hekalu leo, pia tunajiwekea madai ya “kuponywa” baraka iliyoahidiwa na manabii na mitume.6 Baraka hizi pia ni baraka za kupendeza sana kwa sababu ya upana wake, umaalumu wake na matokeo yake hapa duniani. Orodha hii ndefu inajumuisha baraka hizi:

  • Ongezeko la uelewa juu ya Mwokozi na dhabihu Yake ya kulipia dhambi;

  • Ongezeko la ushawishi wa Roho Mtakatifu7 kujisikia na nguvu na mwongozo kwa ajili ya maisha yetu wenyewe;

  • Ongezeko la imani, ili wongofu kwa Mwokozi uwe wa kina na kwa kudumu;

  • Ongezeko la uwezo na hamasa ya kujifunza na kutubu8 kwa sababu ya kuelewa sisi ni nani, tumetoka wapi, na ono dhahiri la kule tunakoenda;

  • Ongezeko la uwezo wa kujiboresha, kujitakasa na nguvu ya kujisimamia katika mioyo yetu,

  • Ongezeko la furaha kupitia ongezeko la uwezo wa kuhisi upendo wa Bwana,

  • Ongezeko la baraka za familia, bila kujali hali ya familia yetu kwa sasa, hapo nyuma au ya baadaye au namna mti wetu wa familia usivyo mkamilifu,

  • Ongezeko la upendo na shukrani kwa wahenga wetu na ndugu walio hai, ili tusijisikie tena upweke;

  • Ongezo la nguvu za utambuzi wa kile kinachohitaji uponyaji na hivyo, kwa msaada wa Bwana, kuwatumikia wengine;

  • Ongezeko la ulinzi kutokana na majaribu na ushawishi wa nguvu za mwovu; na

  • Ongezeko la usaidizi wa kurekebisha mioyo iliyotatizwa, iliyovunjika, iliyo na wasiwasi na kuponya majeruhi.9

Kama umesali kwa ajili ya yo yote kati ya baraka hizi, shiriki katika historia ya familia na kazi ya hekalu. Ufanyapo hayo, maombi yako yatajibiwa. Ibada zinapofanyika kwa niaba ya waliofariki dunia, watoto wa Mungu duniani wanapona. Si ajabu Rais Russell M. Nelson, katika ujumbe wake wa kwanza kama Rais wa Kanisa, alitamka, “Kuabudu kwako hekaluni na huduma yako huko kwa niaba ya mababu zako vitakubariki kwa ongezeko la ufunuo binafsi na amani na vitaimarisha ahadi yako ya kubakia katika njia ya agano.”10

Nabii wa mwanzo zaidi pia aliona kabla baraka za wote walio hai na wafu.11 Mjumbe wa mbinguni alimwonyesha Ezekieli ono la hekalu na maji yakibubujika kutoka ndani yake. Ezekiali alielezwa:

“Maji haya yanatoka … na kwenda chini jangwani, na kwenda ndani ya bahari [ya mauti] … , na maji haya yataponywa.

“Na itakuja kuwa, kwamba kila kitu kilcho hai, kitembeacho, ko kote mito itakakotokea, kitaishi: … kwani kitaponywa; na kila kitu kitaishi ko kote mto utokako.”12

Sifa mbili za maji zinazostahili kukumbukwa. Kwanza, ingawa mto mdogo haukuwa na kijito, ulikua na kuwa mto mkubwa, ukawa mpana na wenye kina kirefu kadiri ulivyotiririka. Kitu kama hicho hutokea kwa baraka ambazo hutiririka kutoka hekaluni wakati watu binafsi wanapounganishwa kama familia. Makuzi ya maana hutokea kwenda nyuma na mbele kupitia vizazi wakati ibada za kuunganisha zinapounganisha familia pamoja.

Pili, mto ulihuisha kila kitu ambacho ulikigusa. Baraka za hekaluni vile vile zina nguvu za kushangaza za kuponya. Baraka za hekalu zinaweza kuponya mioyo na maisha na familia.

Todd mwana wa Betty

Wacha niwaonyeshe. Katika mwaka 1999, kijana aliyeitwa Todd alizimia kutokana na mpasuko wa mshipa wa damu katika ubongo wake. Ingawa Todd na familia yake walikuwa waumini wa Kanisa, lakini ushiriki wao haukuwa imara, na hakuna aliyewahi kupata baraka za hekalu. Usiku wa mwisho wa maisha ya Todd, mama yake, Betty, aliketi pembeni mwa kitanda chake akisugua mkono wake na kusema, “Todd, kama hakika ni lazima uende, ninakuahidi nitahakikisha kazi yako ya hekaluni inafanyika.” Asubuhi iliyofuata, Todd alitangazwa kuwa ubongo wake umekufa. Madaktari wa upasuaji walipandikiza moyo wa Todd kwa mgonjwa wangu, mtu wa kusifika aliyeitwa Rod.

Miezi michache baada ya upandikizaji ule, Rod alijua utambulisho wa familia ya mtu aliyejitolea kumpa moyo wake na akaanza kuwasiliana nao. Karibia miaka miwili baadae, mama yake Todd, Betty, alimwalika Rod awepo wakati yeye alipokwenda hekaluni kwa mara ya kwanza. Rod na Betty kwanza walikutana uso kwa uso katika chumba cha selestia cha Hekalu la St. George Utah.

Wakati fulani baada ya hapo, baba yake Todd—mumewe Betty—akafariki. Miaka miwili baadae, Betty alimwalika Rod kumwakilisha mwanaye marehemu katika kupokea ibada za hekaluni kwa niaba yake. Rod kwa shukrani kubwa alifanya hivyo, na kazi hii ya uwakilishi ilikamilika katika chumba cha kuunganishwa katika Hekalu la St. George Utah. Betty aliunganishwa na mumewe marehemu, akipiga magoti upande mwingine wa madhabahu alikuwa mjukuu wake, ambaye alihudumu kama mwakilishi. Kisha, na machozi yakitirika mashavuni, akamwashiria Rod kuungana nao madhabahuni Rod alipiga magoti pembeni yao, akifanya kama kumwakilisha mwanawe, Todd, ambaye moyo wake ulikuwa bado ukidunda ndani ya kifua cha Rod. Aliyemtolea moyo Rod, Todd, alikuwa sasa ameunganishwa kwa wazazi wake kwa milele yote. Mama yake Todd alitimiza ahadi aliyoifanya kwa mwanawe aliyekuwa mahututi mwaka mmoja kabla.

Rod na Kim katika siku ya harusi yao

Lakini hadithi hii haikomei hapo. Miaka kumi na tano baada ya upandikizaji wa moyo Rod akawa ameingia katika uchumba ili aoe na akaniomba mimi kufanya ibada ya kuunganishwa kwao katika Hekalu la Provo Utah. Siku ya harusi, nilikutana na Rod na bibi harusi wake kipenzi Kim, katika chumba kinachopakana na chumba cha kuunganishia, ambamo familia zao na marafiki wa karibu sana walikuwa wakisubiria. Baada ya mazungumzo mafupi na Rod na Kim, niliwauliza kama wana swali lolote.

Rod alisema, “Ndiyo. Familia ya aliyenitolea moyo wake iko hapa na wangependa kuonana nawe.”

Nilishitukizwa na nikauliza, “Una maana wako hapa? Sasa hivi?”

Rod alijibu, “Ndiyo.”

Nilipiga hatua hadi kwenye kona na nikawaita familia ile kutoka katika chumba cha kuunganishwa. Betty, binti yake, na mkwewe wa kiume wakaungana nasi. Rod alimsalimu Betty kwa kumkumbatia, akamshukuru kwa kuja, na kisha akanitambulisha kwake. Rod alisema, “Betty, huyu ni Mzee Renlund. Yeye ndiye daktari aliyeuangalia moyo wa mwanao kwa miaka mingi sana.” Alivuka chumba na kunikumbatia. Na kwa dakika kadhaa zilizofuata, kulikuwa na kukumbatiana na machozi ya furaha kote.

Baada ya kurudia hali zetu, tulienda katika chumba cha kuunganishwa, ambamo Rod na Kim waliunganishwa kwa maisha ya duniani na ya milele yote. Rod, Kim, Betty, na mimi tunaweza kushuhudia kuwa mbingu ilikuwa karibu sana, kwamba palikuwako na wengine pamoja nasi siku ile ambao walishavuka pazia la maisha katika mwili wenye kufa.

Mungu, katika uwezo wake usio na mwisho, huunganisha na kuponya watu na familia licha ya majanga, vifo na magumu. Wakati mwingine tunalinganisha hisia tunazopata katika mahekalu kama kupata kuiona mbingu.13 Lakini siku ile katika Hekalu la Provo Utah, kauli hii ya C.S. Lewis ilibaki ikiniletea mwangwi: “[Wenye mwili] husema juu ya baadhi ya mateso ya kimwili, ‘hakuna upeo wa furaha mbeleni unaoweza kufidia,’ pasipokujua kwamba Mbingu, mara ukiipata, itafanya kazi kwa kurudi nyuma na kugeuza hata ule uchungu kuwa utukufu. … Wenye heri watasema, ‘Katu hatujaishi po pote isipokuwa Mbinguni.’”14

Mungu atatuimarisha, atatusaidia na kututetea;15 na atatutakasia dhiki zetu.16 Tunapokusanya historia za familia zetu na kwenda hekaluni kwa niaba ya wahenga wetu, Mungu anatimiza nyingi za ahadi zake kwa wakati mmoja pande zote mbili za pazia. Vile vile, tunabarikiwa tunapowasaidia wengine katika kata na vigingi vyetu kufanya vivyo hivyo. Waumini ambao hawakai karibu na hekaluni pia hupokea baraka hizi kwa kushiriki katika kazi za historia za familia, wakikusanya majina ya wahenga wao kwa ajili ya kufanyiwa ibada za hekaluni.

Hata hivyo, Rais Russell M. Nelson alitahadharisha: “Tunaweza tukapewa mwongozo wa kiungu siku nzima juu ya matukio ya hekaluni na historia ya familia ambayo wengine wamepata. Lakini tunatakiwa kufanya kitu fulani ili tuweze kuipata furaha hiyo sisi wenyewe.” Ameendelea, “Ninakualikeni ninyi kwa sala mfikirie ni dhabihu gani—hususani dhabihu ya muda—ambayo mnaweza kutoa [ili ] kufanya kazi zaidi ya hekalu na historia ya familia.”17 Unapoukubali mwaliko wa Rais Nelson, mtagundua, mtakusanya na kuunganisha familia yako. Kama nyongeza, baraka zitamiminika kwako na kwa familia yako kama mto ulionenwa na Ezekieli. Utaona uponyaji kwa kile kinachohitaji kuponywa.

Orson na Parley Pratt walikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuonja matokeo ya uponyaji na matokeo chanya ya historia ya familia na kazi za hekalu katika kipindi hiki. Betty, familia yake, na Rod walijionea hili. Na wewe unaweza pia. Kupitia dhabihu Yake ya kulipia dhambi, Yesu Kristo anatoa baraka hizi kwa wote, wafu na walio hai. Kwa sababu ya baraka hizi, tutajikuta kuwa, kiistiari, “hatujawahi kuishi popote isipokuwa … Mbinguni.”18 Mimi nashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Parley P. Pratt to Orson Pratt, May 25, 1853, Orson Pratt Family Collection, Church History Library; in Terryl L. Givens and Matthew J. Grow, Parley P. Pratt: The Apostle Paul of Mormonism (2011), 319.

  2. Orson Pratt to Parley P. Pratt, Mar. 10, 1853, Parley P. Pratt Collection, Church History Library; in Givens and Grow, Parley P. Pratt, 319.

  3. Tukumbuke, Orson Pratt si tu alisaidia kuchapisha kitabu cha uzao wa William Pratt, bali miaka kadhaa baadae, mnamo 1870, Orson Pratt na familia yake walifanya zaidi ya ubatizo kwa ajili ya wafu 2, 600 walioko katika kitabu katika Nyumba ya Endaumenti huko Jijini Salt Lake. (ona Breck England, The Life and Thought of Orson Pratt [1985], 247).

  4. Ona pia Joseph Smith, katika History of the Church, 6:312-13.

  5. Ona “Names Submitted for Temple Ordinances,” First Presidency letter, Dec. 29, 2012. Wahenga ambao majina yao yanapelekwa kwa ajili ya ibada za uwakilishi yanapaswa yawe na uhusiano na mtumaji. Pasipo udhuru, waumini wa Kanisa wasipeleke majina ya makundi yasiyoruhusiwa kama vile ya watu maarufu, na waathiriwaa wa janga la Jewish Holocaust .

  6. Ona Dallin H. Oaks, “In Wisdom and Order,” Tambuli, Dec. 1989, 18–23; D. Todd Christofferson, “The Redemption of the Dead and the Testimony of Jesus,” Liahona, Jan. 2001, 10–13; Boyd K. Packer, “Your Family History: Getting Started,” Liahona, Aug. 2003, 12–17; Thomas S. Monson, “Constant Truths for Changing Times,” Liahona, May 2005, 19–22; Henry B. Eyring, “Hearts Bound Together,” Liahona, May 2005, 77–80; M. Russell Ballard, “Faith, Family, Facts, and Fruits,” Liahona, Nov. 2007, 25–27; Russell M. Nelson, “Salvation and Exaltation,” Liahona, May 2008, 7–10; Russell M. Nelson, “Generations Linked in Love,” Liahona, May 2010, 91–94; David A. Bednar, “The Hearts of the Children Shall Turn,” Liahona, Nov. 2011, 24–27; Richard G. Scott, “The Joy of Redeeming the Dead,” Liahona, Nov. 2012, 93–95; Quentin L. Cook, “Roots and Branches,” Liahona, May 2014, 44–48; Thomas S. Monson, “Hastening the Work,” Liahona, June 2014, 4–5; Henry B. Eyring, “The Promise of Hearts Turning,” Liahona, July 2014, 4–5; David A. Bednar, “Missionary, Family History, and Temple Work,” Liahona, Oct. 2014, 14–19; Neil L. Andersen, “‘My Days’ of Temples and Technology,” Liahona, Feb. 2015, 26–33; Neil L. Andersen, “Sharing the Temple Challenge,” Family Discovery Day, Feb. 2015, LDS.org; Quentin L. Cook, “The Joy of Family History Work,” Liahona, Feb. 2016, 22–27; Gary E. Stevenson, “Where Are the Keys and Authority of the Priesthood? Liahona, May 2016, 29–32; Dieter F. Uchtdorf, “In Praise of Those Who Save,” Liahona, May 2016, 77–80; Quentin L. Cook, “See Yourself in the Temple,” Liahona, May 2016, 97–101; Dale G. Renlund, Ruth L. Renlund, and Ashley R. Renlund, “Family History and Temple Blessings,” Liahona, Feb. 2017, 34–39; Dallin H. Oaks and Kristen M. Oaks, “Connected to Eternal Families,” Family Discovery Day, Mar. 2018, LDS.org.

  7. Ona Mafundisho na Maagano 109:15.

  8. Ona Mafundisho na Maagano 109:21.

  9. Ona Boyd K. Packer, “Balm of Gilead,” Ensign, Nov. 1987, 16–18; Jeremiah 8:22; 51:8.

  10. Russell M. Nelson, “As We Go Forward Together,” Liahona, Apr. 2018, 7.

  11. Ona Ezekieli 40–47; Bible Dictionary, “Ezekieli.”

  12. Ezekieli 47:8-9.

  13. Ona Spencer W. Kimball, “Glimpses of Heaven,” Ensign, Dec. 1971, 36–37.

  14. C. S. Lewis, The Great Divorce: A Dream (2001), 69.

  15. Ona Isaya 41:10.

  16. Ona “How Firm a Foundation,” Nyimbo, no.85

  17. Russell M. Nelson and Wendy W. Nelson, “Open the Heavens through Temple and Family History Work,” Liahona, Okt. 2017, 19.

  18. Lewis, The Great Divorce, 69.