Kwa Moyo Mmoja
Ili tuweze kufikia hatima yetu ya milele, tunahitajiana, na tunahitaji kuungana.
Mmoja wa viumbe wa ajabu duniani ni kipepeo monaki. Katika safari moja ya Mexico kwenda kusherehekea Krismasi na familia ya mume wangu, tulitembelea mahali ambapo vipepeo hufugwa, ambapo mamilioni ya vipepeo wakubwa hukaa wakati wa kipindi cha baridi. Lilikuwa jambo la kusisimua kuona sehemu hiyo nzuri na sisi kufikiria mfano wa umoja na utiifu wa sheria takatifu ambao viumbe wa Mungu wanadhihirisha.1
Vipepeo monaki ni waongozaji wazuri. Wanatumia muelekeo wa jua ili kutafuta njia wanayohitaji kwenda. Kila majira ya kuchipua, wanasafiri maelfu ya maili kutoka Mexico kwenda Canada, na kila majira ya majani kupukutika, wanarudi sehemu ileile ya Mexico.2 Wanafanya hivi mwaka hadi mwaka, wakipeperusha kibawa kimoja baada ya kingine. Wakati wa safari yao, wanakusanyika pamoja usiku kwenye miti kujizuia na baridi na maadui.3
Kundi la vipepeo linaitwa nelibini.4 Hiyo picha si ni nzuri? Kila kipepeo katika nelibini ni wakipekee na tofauti, hata hivyo viumbe hawa dhaifu wametengenezwa na Muumba mwenye upendo wakiwa na uwezo kuendelea kuishi, kusafiri, kuzaana, na kusambaza uhai wakiwa wanakwenda kutoka ua moja hadi lingine wakisambaza chavua. Na ijapokuwa kila kipepeo yupo tofauti, wanafanya kazi pamoja kuufanya ulimwengu upendeze zaidi na wenye mazao ya kupendeza.
Kama ilivyo kwa vipepeo wakubwa, tupo safarini kurejea katika makao ya mbinguni ambako tutaungana na Wazazi wetu wa Mbinguni.5 Kama vipepeo, tumepewa tabia takatifu ambayo inaturuhusu kusafiri katika maisha, ili “kujaza … kipimo cha uumbaji [wetu].”6 Kama wao, tukifunganisha mioyo yetu pamoja,7 Bwana atatulinda “kama kuku [akusanyavyo] vifaranga vyake kwenye mbawa zake”8 na atatufanya sisi kuwa nelibini maridadi.
Wasichana na wavulana, vijana wa kike na wakiume, kaka na dada, tupo katika safari hii pamoja. Ili tuweze kufikia hatima yetu ya milele, tunahitajiana, na tunahitaji kuungana. Bwana ametuamuru sisi, “Kuweni na umoja; na kama hamna umoja ninyi siyo wangu.”9
Yesu Kristo ni mfano mzuri wa umoja na Baba Yake. Ni wamoja katika malengo, upendo, na matendo, “nia ya Mwana ikimezwa na nia ya Baba.”10
Tunawezaje kuufuata mfano kamili wa Bwana wa umoja na Baba Yake na kuungana Nao zaidi na kila mmoja wetu?
Mfano wa kuvutia unapatikana katika Matendo ya Mitume 1:14 Tunasoma, “[Hawa] wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali na kuomba, pamoja na wanawake.”11
Ninafikiri ni muhimu kwamba kishazi “kwa moyo mmoja” kinajitokeza mara kadhaa katika kitabu cha Matendo ya Mitume, ambako tunasoma ni nini wafuasi wa Yesu Kristo walifanya mara baada ya kupaa mbinguni akiwa kiumbe mfufuka, na pia baraka walizopata kwa sababu ya juhudi zao. Pia ni wazi kwamba tunaona mpangilio kama huo miongoni mwa waaminifu katika bara la Amerika wakati Bwana alipowatembelea na kuwahudumia. “Kwa moyo mmoja” ina maana katika makubaliano, katika umoja, na wote kwa pamoja.
Baadhi ya vitu ambavyo Watakatifu waaminifu walifanya katika sehemu zote mbili ilikuwa kwamba walishuhudia juu ya Yesu Kristo, walijufunza neno la Mungu pamoja, na kuhudumiana wao kwa wao kwa upendo.12
Wafuasi wa Bwana walikuwa na lengo moja, katika upendo, na katika matendo. Walijitambua wao ni kina nani, walitambua nini walitakiwa kufanya, na walifanya kwa kumpenda Mungu na kwa kila mmoja wao. Walikuwa sehemu ya nelibini nzuri wakisonga kwa moyo mmoja.
Baadhi ya baraka walizozipata ni kwamba walijawa na Roho Mtakatifu, miujiza ikatokea miongoni mwao, Kanisa lilikua, hapakuwa na ugomvi miongoni mwa watu, na Bwana aliwabariki kwa mambo yote.13
Tunaweza kufikiri kwamba sababu zilizowafanya waungane ni kwa sababu walimjua Bwana moja kwa moja. Walikuwa karibu Naye, na walishuhudia kazi yake takatifu, juu ya miujiza aliyoifanya, na Ufufuko Wake. Waliona na kugusa alama katika mikono na miguu Yake. Walijua bila shaka kwamba Alikuwa Masihi aliyetarajiwa, Mkombozi wa ulimwengu. Walijua kwamba “Yeye ndiye kiini cha uponyaji, amani na uendelevu wa milele.”14
Ijapokuwa hatuwezi kumwona Mwokozi wetu kwa macho yetu, tunaweza kujua kwamba Anaishi. Tunapomkaribia Yeye, tunapojaribu kupata ushahidi binafsi kupitia kwa Roho Mtakatifu juu ya utumishi Wake uliotukuka, tutaweza kuelewa zaidi malengo yetu; upendo wa Mungu utakaa ndani ya mioyo yetu;15 tutakuwa na ujasiri wa kuwa mmoja katika nelibini ya familia zetu, kata, na jamii; na tutahudumiana sisi kwa sisi “katika njia mpya na nzuri.”16
Miujiza inatokea wakati watoto wa Mungu wanapofanya kazi pamoja wakiongozwa na Roho ili kuwafikia wengine wenye dhiki.
Tunasikia habari nyingi za upendo wa ujirani mwema ukionyeshwa miongoni mwa watu wakati majanga yanapotokea. Kwa mfano, wakati jiji la Houston lilipokumbwa na mafuriko makubwa mwaka jana, watu walisahau mahitaji yao na kwenda kwenye uokozi. Rais wa akidi ya wazee alitoa wito wa kuisaidia jamii, na msafara wa boti 77 uliandaliwa haraka. Waokoaji walikwenda kwa majirani walioathirika na kuzisafirisha familia zote hadi kwenye mojawapo ya majengo yetu ya mikutano, ambako walipata uhifadhi na misaada mingine iliyohitajika. Waumini na wasio waumini walifanya kazi pamoja kwa lengo moja.
Huko Santiago, Chile, Rais wa Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama alikuwa ametamani kuwasaidia wakimbizi katika jumuiya yake kutoka Haiti. Kwa kushauriana pamoja na viongozi wa ukuhani, yeye na viongozi wengine walipata wazo la kufundisha Kihispania kwa wale wakimbizi, kuwasaidia kuunganika vizuri katika makazi yao mapya. Kila Jumamosi asubuhi, wamisionari walikuwasanyika na wanafunzi wao wenye shauku. Hali ya muungano katika jengo lile ni mfano wa kuvutia wa watu kutoka matabaka mbalimbali wakihudumu kwa moyo mmoja.
Huko Mexico, mamia ya waumini walisafiri kwa masaa kuwasaidia manusra wa mitetemeko mikubwa miwili ya ardhi. Walikuja na vifaa, mashine, na upendo kwa majirani zao. Wakati watu wa kujitolea walipokusanyika katika mojawapo ya nyumba zetu za mikutano kwa ajili ya maelekezo, meya wa mji wa Ixhuatan alitokwa na machozi alipoona udhihirisho wa “upendo msafi wa Kristo”17
Sasa Bwana anatupa nafasi ya kushauriana pamoja kila mwezi katika akidi zetu za ukuhani na Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, ili wote tuwe washiriki hai katika nelibini yetu ya kata na tawi —sehemu ambayo wote tunatosheleza na tunahitajika.
Kila mojawapo ya njia zetu ni tofauti, lakini tunatembea pamoja. Njia yetu haihusu tulichofanya au tulikuwa wapi; ni kuhusu wapi tunakwenda na tutakuwa nani, katika umoja. Tunaposhauriana pamoja tukiongozwa na Roho Mtakatifu, tunaweza kuona mahali tulipo na wapi tunahitajika kuwepo. Roho Mtakatifu anatupa ono kwamba macho yetu ya kawaida hayawezi kuona, kwa sababu “ufunuo umetapakaa miongoni mwetu,”18 na tunapoweka ufunuo huo pamoja, twaweza kuona zaidi.
Tunapofanya kazi kwa umoja, lengo letu linatakiwa kuwa kuangalia na kufanya matakwa ya Bwana; kichocheo chetu kiwe upendo tunaohisi kwa ajili ya Mungu na jirani zetu;19 na tamanio letu kubwa linatakiwa “kufanya kazi kwa bidii,”20 ili tuweze kuandaa njia nzuri ya kurudi kwa Mwokozi wetu. Kitu pekee tunachoweza kufanya ni kufanya hivyo “kwa moyo mmoja.”
Kama vipepeo wakubwa, acheni tuendelee na safari yetu kwa amani na malengo, kila mmoja wetu akiwa na tabia na mchango wake, tukiifanya dunia iwe sehemu nzuri na yenye mafanikio—hatua moja kwa wakati na katika uwiano na Mwokozi wetu.
Bwana wetu Yesu Kristo ametuahidi kwamba tunapokusanyika pamoja katika jina Lake, Anakuwa katikati yetu.21 Ninashuhudia kwamba Yeye yu hai na kwamba Alifufuka asubuhi moja ya majira ya kuchipua kama leo. Yeye ni Mtawala juu ya watawala wote, “Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.”22
Naomba tuwe wamoja kwa Baba na Mwana Wake wa Pekee, tukiwa tunaongozwa na Roho Mtakatifu, ni maombi yangu ya unyenyekevu katika jina la Yesu Kristo, amina.