2010–2019
Yule Atakaye Vumilia hadi Mwisho, Huyo Ataokolewa.
Aprili 2018


2:3

Mwenye Kuvumilia hadi Mwisho, Ndiye Atakayeokoka.

Na tuwe waaminifu kwa kile tulichokiamini na kukijua.

Wapendwa akina kaka na akina dada, ninashukuru sana kwa fursa ya kuwaeleezeni baadhi ya hisia zangu.

Miaka kadhaa iliyopita, mke wangu na mimi tulikuwepo kwenye sherehe ya ufunguzi wa maadhimisho ya muingiliano ya watoto katika jumba la Makumbusho ya Historia ya Kanisa Jijini Salt Lake. Mwishoni mwa sherehe, Rais Thomas S. Monson alitusogelea, na alipokuwa akitusalimu kwa mikono, alisema, “Vumilia, nawe utashinda”— fundisho la maana na ambalo ukweli wake, ndiyo, sote tunaweza kuthibitisha.

Yesu Kristo ametuhakikishia kwamba “Mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.”1

Kuvumilia humaanisha “kubakia imara katika ahadi ya kuwa wakweli katika amri za Mungu licha ya majaribu, upinzani, au dhiki.”2

Hata wale ambao walikuwa na uzoefu mkubwa wa kiroho na wametoa huduma ya uaminifu wanaweza siku moja kupotoka au kuanguka katika kutoshiriki kikamilifu kama hawatavumilia hadi mwisho. Na tuweze daima na kwa bidii kukiweka akilini na mioyoni mwetu kirai hiki “Hii haitatokea kwangu.”

Wakati Yesu Kristo alipofundisha Kapernaumu, wengi wa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena.

“Kisha Yesu akawaambia wale Kumi na Wawili, Je, Ninyi nanyi mwataka kuondoka?”3

Ninaamini kwamba leo, Yesu Kristo hutuuliza sisi sote ambao tumefanya maagano matakatifu Naye, “Je, Ninyi nanyi mwataka kuondoka?”

Ninaomba kwamba sote, kwa tafakari ya kina juu ya kile kinachotusubiri milele, tuweze kujibu kama vile Simoni Petro: “Bwana, twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.”4

Na tuwe waaminifu kwa kile tulichokiamini na kukijua. Kama tumekua hatuishi kulingana na ufahamu wetu, na tubadilike. Watenda dhambi wanaoendelea katika dhambi zao, na hawatubu, huzama zaidi na zaidi katika uchafu, hadi Shetani anadai kuwamiliki, ikimaanisha kuhatarisha nafasi yao ya kutubu, ya kusamehewa, na ya kubarikiwa kwa baraka zote za milele.

Nimesikia uhalalishaji mwingi kutoka kwa wale ambao wameacha kushiriki kikamilifu Kanisani na wakapoteza ono sahihi la lengo la safari yetu ya hapa duniani. Ninawasihi kutafakari na kurudi, kwa sababu mimi ninaamini kwamba hakuna ye yote atakayeweza kutoa udhuru mbele ya Bwana wetu, Yesu Kristo.

Tulipobatizwa, tulifanya maagano—siyo na mtu ye yote bali na Mwokozi, tukikubali “kujichukulia juu [yetu wenyewe] jina la Yesu Kristo, tukiwa na dhamira ya kumtumikia hadi mwisho.”5

Mahudhurio katika mikutano ya sakramenti ni moja ya njia kuu tunayoweza kutathmini dhamira yetu ya kumtumikia Yeye, ustahimilivu wetu wa kiroho, na ukuaji wa imani yetu katika Yesu Kristo.

Kupokea sakramenti ni kitu muhimu sana tunachokifanya siku ya Sabato. Bwana aliielezea ibada hii kwa Mitume Wake kabla tu ya kufariki Kwake. Alifanya vivyo hivyo katika bara la Amerika. Anatuambia sisi kwamba kama tutashiriki katika ibada hii, itakuwa ni ushuhuda kwa Baba kwamba daima tutamkumbuka Yeye, na Yeye anaahidi kwamba, vile vile, Roho Wake atakuwa pamoja nasi.6

Katika mafundisho ya Alma Mdogo kwa mwanawe Shibloni, tunapata ushauri wa busara na maonyo ambayo yanatusaidia kubaki waaminifu kwenye maagano yetu:

“Hakikisha kwamba hujiinui kwa kiburi; ndio, angalia kwamba hujisifu kwa hekima yako mwenyewe, wala kwa nguvu yako nyingi.

“Tumia ujasiri, lakini usiwe mjeuri; na pia uone kwamba ujifunze kuzuia tamaa zako zote, ili uweze kujazwa na mapenzi; hakikisha kwamba uepuke kutokana na uvivu.”7

Miaka kadhaa iliyopita, tukiwa kwenye mapumziko, nilitaka kwenda kuendesha mtumbwi wa kieskimo kwa mara ya kwanza. Nilikodisha mtumbwi huo, na kwa shauku kubwa, nikautweka baharini.

Baada ya dakika chache, wimbi likaupindua mtumbwi ule. Kwa jitihada kubwa, nikishikilia kasia mkono mmoja na mtumbwi mkono mwingine, niliweza kusimama tena.

Nilijaribu tena kupiga kasia kuendesha mtumbwi wangu, lakini dakika chache tu baadae, mtumbwi ukapinduka tena. Kwa ushupavu niliendelea kujaribu, pasipo mafanikio, hadi pale mtu mmoja mwenye kufahamu kuendesha mtumbwi aliponiambia kwamba lazima kutakuwa na ufa katika kuta na ule mtumbwi lazima uliingiza maji yakajaa, yakaufanya ushindwe kutulia na kutoweza kuudhibiti. Niliuburuza mtumbwi mpaka ufukweni na kuondoa kifuniko, na kwa uhakika, nje kikatoka kiasi kikubwa cha maji.

Ninafikiria kwamba wakati mwingine tunatembea maishani tukiwa na dhambi ambazo, kama vile kuvuja katika mtumbwi wangu, zinazuia maendeleo yetu ya kiroho.

Kama tukiendelea katika dhambi zetu, tunasahau maagano tuliyofanya na Bwana, ingawa tunazidi kuzama kwa sababu ya kukosa kutulia ambako dhambi hizo huleta katika maisha yetu.

Kama vile nyufa katika mtumbwi wangu, nyufa katika maisha yetu huhitaji kushughulikiwa. Baadhi ya dhambi zitahitaji jitihada zaidi kuliko nyingine ili kutubu.

Tunapaswa basi kujiuliza wenyewe: Je, tuko wapi kuhusu msimamo wetu juu ya Mwokozi na kazi Yake? Je, tuko katika hali ile ya Petro alipomkana Yesu Kristo? Au tumesonga mbele hadi kufikia mahali ambapo tuna msimamo na azimio ambalo alikuwa nalo baada ya mamlaka makubwa aliyopokea kutoka kwa Mwokozi?8

Lazima tujitahidi kutii amri zote na kuwa makini na zile ambazo ni vigumu kwetu sisi kuzishika. Bwana atakuwa upande wetu, akitusaidia nyakati za shida na udhaifu, na tukionyesha nia ya dhati na utendaji sahihi, Yeye atafanya “vitu dhaifu kuwa vya nguvu.”9

Utii utatupatia uwezo wa kushinda dhambi. Lazima pia tuelewe kwamba jaribu la imani yetu linatutaka sisi tutii, mara nyingi pasipo kufahamu matokeo yake.

Napendekeza kanuni ambazo zitatusaidia kuvumilia hadi mwisho:

  1. Kila siku, sali na kusoma maandiko.

  2. Kila wiki, pokea sakramenti ukiwa na moyo uliovunjika na roho iliyopondeka.

  3. Tulipe zaka zetu na matoleo yetu ya mfungo kila mwezi.

  4. Kila miaka miwili—kila mwaka kwa vijana—- pata kibali kipya cha kuingia hekaluni.

  5. Maisha yetu yote, tutumikie katika kazi ya Bwana.

Na ukweli mkuu wa injili uimarishe akili zetu, na tuyaweke maisha yetu huru dhidi ya nyufa ambazo zinaweza kuikwamisha safari yetu salama ya kuvuka bahari ya maisha haya.

Mafanikio kwa njia ya Bwana yana gharama, na njia pekee ya kuyapata ni kulipa hiyo gharama.

Ninashukuru sana kwamba Mwokozi wetu alivumilia hadi mwisho, akikamilisha dhabihu Yake kuu ya kulipia dhambi.

Aliteseka kwa ajili ya dhambi zetu, maumivu, huzuni, uchungu, udhaifu, na hofu, na hivyo anajua jinsi ya kutusaidia, jinsi ya kutupa mwongozo wa kiungu, jinsi ya kutufariji, na jinsi ya kutuimarisha ili tuweze kuvumilia na kupata taji ambalo limewekwa kwa ajili ya wale ambao hawakushindwa.

Maisha ni tofauti kwa kila mmoja wetu. Sisi sote tunao wakati wa majaribu, wakati wa furaha, wakati wa kufanya maamuzi, wakati wa kushinda vizuizi, na wakati wa kutumia fursa.

Vyovyote hali yetu binafsi iwavyo, ninashuhudia kwamba Baba Yetu wa Mbinguni daima husema, “Ninakupenda. Nitakuhimi. Nitakuwa nawe. Usife moyo. Tubu na vumilia katika njia ambayo nimekuonyesha. Na ninakuhakikishieni kwamba tutaonana tena katika nyumba yetu ya selestia.” Katika jina la Yesu Kristo, amina.