Mfanye Roho Mtakatifu kama Kiongozi Wako
Ni zawadi iliyoje isiyo na kifani inayowajia wale ambao wanaweka imani yao katika Yesu Kristo. Kipawa hicho ni Roho Mtakatifu.
Jumapili hii ya Pasaka, mawazo yetu yanageukia Ufufuko wa Bwana Yesu Kristo na kwenye kaburi lililo tupu ambavyo vinampa kila muumini tumaini katika ushindi wa Kristo dhidi ya kile ambacho vinginevyo kingekuwa kushindwa bila shaka. Ninaamini, pamoja na Mtume Paulo, kwamba jinsi tu Mungu “aliyemfufua Kristo Yesu katika Wafu [hivyo] itakuwa [Yeye] ataihuisha miili [yetu] iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani [yetu].”1
Kuhuisha inamaanisha kufanya kuwa hai. Kama vile Kristo anavyorudisha miili yetu katika uhai baada ya kifo cha mwili kupitia nguvu za Ufufuko Wake, hivyo anaweza kutuhuisha, au kutufanya tuwe hai, kutoka katika kifo cha kiroho.2 Katika kitabu cha Musa, tunasoma kuhusu Adamu akipitia aina hii ya kuhuishwa: “[Adamu] akawa amebatizwa, na Roho wa Mungu akamshukia juu yake, na hivyo akawa amezaliwa kwa Roho, na akawa amehuishwa katika utu wa ndani.”3
Ni zawadi iliyoje isiyo na kifani inayowajia wale ambao wanaweka imani yao katika Yesu Kristo. Zawadi hiyo ni Roho Mtakatifu akitupa kile ambacho Agano Jipya linakiita “uzima ule ulio katika Kristo.”4 Lakini je, inawezekana kuwa mara nyingine tunakichukulia kuwa kawaida kipawa kama hiki?
Wakina kaka na wakina dada, ni heshima isiyo ya kawaida “kumchukua … Roho Mtakatifu kuwa kiongozi [wetu”5 kama inavyoonyeshwa katika hadithi ifuatayo.
Wakati wa Vita vya Korea, Ensign Frank Blair alihudumu kwenye meli ya kusafirisha wanajeshi iliyotumika kule Japani.6 Meli hiyo haikuwa kubwa vya kutosha ili kuwa na kasisi rasmi, kwa hivyo nahodha alimwomba Ndugu Blair awe kasisi wa meli asiye rasmi, akiwa amemchunguza kijana na kuona kwamba alikuwa mtu wa imani na maadili, anayeheshimika na wafanyakazi wote melini.
Ensign Blair aliandika: “Meli yetu ilinaswa katika kimbunga kikubwa. Mawimbi yalikuwa takribani futi 45 [14m] urefu. Nilikuwa katika ulinzi … Wakati ambapo mojawapo ya injini zetu tatu iliacha kufanya kazi na ufa katika mstari wa katikati ya meli uliripotiwa. Tulikuwa tumesalia na injini mbili, moja kati ya hizo ilikuwa inafanya kazi kwa nusu ya uwezo wake. Tulikuwa katika matatizo makubwa.”
Ensign Blair alimaliza ulinzi wake na alikuwa akielekea kitandani wakati nahodha alibisha mlangoni kwake. Aliuliza, “Ninakuomba uombe kwa ajili ya meli hii?” Bila shaka, Ensign Blair alikubali kufanya hivyo.
Wakati huo, Ensign Blair angeliweza tu kuomba kwa kawaida, “Baba wa Mbinguni, tafadhali ibariki meli yetu na utuweke salama,” na kisha arudi kulala. Badala yake, alisali ili kujua ikiwa kulikuwa na kitu ambacho angeweza kufanya ili kusaidia kuhakikisha usalama wa meli ile. Katika kujibu sala ya Ndugu Blair, Roho Mtakatifu alimshawishi kwenda kwenye jukwaa, azungumze na nahodha, na ajifunze zaidi. Aligundua kwamba nahodha alikuwa akijaribu kuamua ni kwa kasi gani angeweza kuendesha injini za meli zilizosalia. Ensign Blair alirudi katika kibanda chake ili asali.
Alisali, “Je, naweza kufanya nini ili kusaidia kutatua matatizo ya hizi injini?”
Katika kujibu, Roho Mtakatifu alinong’ona kwamba alihitaji kutembea kuzunguka melini na kuchunguza aweze kukusanya taarifa zaidi. Kisha akarudi tena kwa nahodha na kuomba ruhusa ya kutembea kuzunguka kwenye jukwaa. Kisha, akiwa na kambaokozi ikiwa imefungwa kiunoni, alienda nje kwenye dhoruba.
Akiwa amesimama kwenye shetri, alichunguza zile propela kubwa zikiinuka nje ya maji wakati meli ilipofika kileleni mwa wimbi. Ni moja tu ilikuwa ikifanya kazi kikamilifu, na ilikuwa ikizunguka kwa kasi mno. Baada ya uchunguzi huu, Ensign Blair alisali tena. Jibu la wazi alilopata ilikuwa ya kwamba injini nzuri iliyokuwa imebaki ilikuwa imekazwa mno na ilihitaji kupunguzwa mwendo. Kwa hivyo alirudi kwake nahodha na kufanya mapendekezo hayo. Nahodha alishangazwa, na kumwambia kwamba mhandisi wa meli alikuwa tu amependekeza kinyume—kwamba waongeze kasi ya injini nzuri ili waweze kuikimbia dhoruba. Hata hivyo, nahodha alichagua kufuata pendekezo la Ensign Blair na kupunguza mwendo wa injini. Kufikia alfajiri, meli ile ilikuwa salama katika maji yaliyotulia.
Masaa mawili tu baadaye, ile injini nzuri ilisita kufanya kazi kabisa. Ikiwa na nusu ya uwezo wake katika injini iliyobaki, meli ile iliweza kuchechemea hadi bandarini.
Nahodha alimwambia Ensign Blair, “Kama tusingepunguza mwendo wa ile injini wakati tulipofanya hivyo, tungeliipoteza katikati ya dhoruba ile.”
Bila injini ile hakungekuwepo na njia ya kuendesha. Meli ingelipinduka, na ingelizama. Nahodha alimshukuru yule afisa kijana MSM na kusema kwamba aliamini kwa kufuata ushawishi wa kiroho wa Ensign Blair kulikuwa kumeiokoa ili meli na wafanyikazi wake.
Sasa hadithi hii ni ya kusisimua. Wakati yawezekana kuiwa vigumu kwetu sisi kukabiliwa na hali ngumu kama hii, hadithi hii inajumuisha mwongozo muhimu kuhusu jinsi tunavyoweza kupokea mwongozo wa Roho mara kwa mara.
Moja, inapokuja kwenye ufunuo, ni lazima tutegee sawa sawa redio yetu kwa masafa ya mbinguni. Ensign Blair alikuwa akiishi maisha safi na ya uaminifu. Asingelikuwa mtiifu, hangelikuwa na uwezo wa kujiamini kiroho uliohitajika kusali kama alivyofanya kwa ajili ya usalama wa meli yake na kupokea mwongozo ulio maalum. Ni lazima kila mmoja wetu ajitahidi kulinganisha maisha yetu na amri za Mungu ili tuweze kuongozwa Naye.
Wakati mwingine hatuwezi kusikia ishara ya mbinguni kwa sababu sisi sio wenye kustahiki. Toba na utiifu ni njia ya kufanikisha mawasiliano dhahiri tena. Neno la Agano la Kale la kutubu linamaanisha “kurudi” or “kugeuka”7 Wakati unapohisi kuwa mbali na Mungu, unahitaji tu kufanya uamuzi kurudi kutoka dhambini na kumtazama Mwokozi, utamkuta akikusubiri, mikono Yake ikiwa imenyooshwa. Yeye ana hamu ya kukuongoza, na wewe upo umbali wa hatua moja tu ya sala ili kupokea mwongozo huo tena.8
Pili, Ensign Blair hakumwomba tu Bwana atatue shida yake. Aliuliza kile ambacho angeweza kufanya ili awe sehemu ya suluhisho. Kadhalika tunaweza tukauliza, “Bwana, ni kipi ninahitaji kufanya ili niwe sehemu ya suluhisho?” Badala ya kuorodhesha tu shida zetu katika maombi na kumuuliza Bwana azisuluhishe, tunapaswa kuwa tunatafuta njia thabiti zaidi za kupokea msaada wa Bwana na kuahidi kutenda kulingana na mwongozo wa Roho.
Kuna somo la tatu muhimu katika hadithi ya Ensign Blair. Je, iliwezekana kwake yeye kusali kwa uhakika na utulivu wa aina hii ikiwa hakuwa amepokea mwongozo kutoka kwa Roho katika matukio kabla ya hili? Kuwasili kwa kimbunga sio wakati wa kupangusa vumbi kipawa cha Roho Mtakatifu na kufikiria jinsi ya kukitumia. Mwanaume huyu kijana ni dhahiri ya kwamba alikuwa akifuata mtindo ambao alikuwa ameutumia mara nyingi hapo awali, ikijumuisha wakati alikuwa mmisionari. Tunahitaji Roho Mtakatifu kama kiongozi wetu katika maji matulivu ndiposa sauti Yake itakuwa dhahiri kwetu sisi katika dhoruba kali.
Wengine wanaweza kufikiria kwamba hatupaswi kutarajia mwongozo wa kila siku kutoka kwa Roho kwa sababu “si vyema kwamba [Mungu] aniamuru katika mambo yote,” tusije tukawa watumishi wazembe.9 Andiko hili, hata hivyo, lilitolewa kwa wamisionari fulani wa kale ambao walimuuliza Joseph Smith kupokea ufunuo ambao walipaswa kuupokea wao wenyewe. Katika aya inayotangulia, Bwana aliwaambia waje katika misheni “kama vile watakavyoshauriana wenyewe na Mimi.” 10
Hawa wamisionari walitaka ufunuo maalum kuhusu mipango ya safari zao. Bado hawakuwa wamejifunza kutafuta mwongozo wao wenyewe katika maswala ya kibinafsi. Bwana aliuita mtazamo huu kama: ulegevu. Waumini wa Kanisa wa hapo awali yawezekana walikuwa na furaha tele kuwa na nabii wa kweli kiasi cha kuwa walikuwa katika hatari ya kukosa kujifunza jinsi ya kupokea ufunuo wenyewe. Kuwa mwenye kujitegemea kiroho ni kusikia sauti ya Bwana kupitia Roho Wake kwa ajili ya maisha mtu binafsi.
Alma alimshauri mwanawe “shauriana na Bwana kwenye matendo yako yote.”11 Kuishi katika njia hii—tunayoiita kwa kawaida “kuishi kwa Roho”—ni fadhila kuu. Huleta pamoja hisia ya utulivu na uhakika pamoja na matunda ya Roho, kama vile upendo, furaha, na amani.12
Uwezo wa Ensign Blair kupokea ufunuo kulimwokoa pamoja na mabaharia wenzake kutokana na dhoruba iliyosukasuka. Aina nyingine ya dhoruba inasukasuka leo Mfano wa mti wa uzima katika Kitabu cha Mormoni13 unatoa taswira yenye nguvu ya jinsi usalama wa kiroho unavyoweza kupatikana katika dunia kama hii. Ndoto hii inazungumzia kuhusu ukungu wa giza unaotokea kwa ghafla na kuleta maangamizo ya kiroho kwa waumini wa Kanisa wanaotembea katika njia kurudi kwake Mungu.14
Katika kutafakari taswira hii, ninaona katika jicho la akilini mwangu umati wa watu wakisafiri katika njia hiyo, baadhi mikono yao ikishikilia kwa nguvu fimbo ya chuma, lakini wengine wengi wakifuata tu nyayo za wale watu walio mbele yao. Njia hii ya mwisho inahusisha mawazo na jitihada kidogo. Unaweza tu kufanya na kufikiria kile ambacho wengine wanafanya na kufikiria. Hii hufanya kazi sawa sawa wakati jua linapowaka. Lakini dhoruba za udanganyifu na ukungu wa uwongo hutokea bila onyo. Katika hali hizi, kuwa na uzoefu wa sauti ya Roho Mtakatifu ni jambo la uzima wa kiroho na kifo cha kiroho.
Ahadi ya Nefi yenye nguvu ni kwamba “yeyote atakayesikiliza hilo neno la Mungu, na … alizingatie, … hataangamia; wala majaribu na mishale ya moto ya adui kuwalemea na kuwapofusha ili kuwaelekeza kwenye maangamio.”15“
Kufuata nyayo za watu walio mbele yako njiani haitoshi. Hatuwezi tu kufanya na kufikiria kile ambacho wengine wanafanya na kufikiria; ni lazima tuishi maisha yaliyo na mwelekeo. Ni lazima kila mmoja wetu ashikilie fimbo ya chuma. Kisha tunaweza kumwendea Bwana kwa unyenyekevu wa kujiamini, tukijua ya kwamba “ata[tu]ongoza kwa mkono, na kutupa [sisi] jibu la sala [zetu].”16 Katika jina la Yesu Kristo, amina.