Maneno ya Utangulizi
Usiku wa leo, tunatangaza mpango mpya muhimu katika akidi zetu za Ukuhani wa Melkizedeki ili kufanikisha kazi ya Bwana kwa ufanisi zaidi.
Asante, Kaka Holmes, kwa ujumbe wako muhimu.
Ndugu wapendwa, tunamkosa kwa dhati Rais Thomas S. Monson na Mzee Robert D. Hales. Bado sote “tunasonga mbele katika kazi ya Bwana.”1
Nina shukrani nyingi kwa kila mwanaume aliye na ukuhani mtakatifu. Nyinyi ni tumaini la Mkombozi wetu, ambaye anataka “kwamba kila mwanadamu aweze kuongea katika jina la Mungu Bwana, hata Mwokozi wa ulimwengu.”2 Anawataka wanawe wote waliotawazwa kumuwakilisha Yeye, kuzungumza kwa niaba Yake, kutenda kwa niaba Yake, na kubariki maisha ya watoto wa Mungu kote ulimwenguni ili kwamba mwisho wa yote “imani pia ipate kuongezeka kote duniani.”3
Baadhi kati yenu mnahudumu mahali Kanisa limeanzishwa kwa vizazi vingi. Wengine wanahudumu mahali ambapo Kanisa kiasi fulani ni geni. Kwa baadhi, kata zenu ni kubwa. Kwa wengine, matawi yenu ni madogo na masafa ni marefu. Bila kujali hali zenu binafsi, kila mmoja wenu ni mshiriki wa akidi ya ukuhani uliye na majukumu matakatifu ya kujifunza na kufundisha, na kuwapenda na kuwahudumia wengine.
Usiku wa leo, tunatangaza mpango mpya muhimu katika akidi zetu za Ukuhani wa Melkizedeki ili kufanikisha kazi ya Bwana kwa ufanisi zaidi. Katika kila kata, makuhani wakuu na wazee watajumuishwa katika akidi moja ya wazee. Marekebisho haya yataboresha sana ukubwa na uwezo wa wanaume wenye ukuhani katika kuwahudumia wengine. Wazee watarajiwa watakaribishwa na kushirikishwa katika akidi hiyo. Katika kila kigingi, rais wa kigingi ataendelea kuongoza akidi ya makuhani wakuu katika kigingi. Lakini muundo wa akidi hiyo utategemea miito ya sasa hivi ya ukuhani, kama itakavyoelezwa hapo baadaye.
Mzee D. Todd Christofferson na Mzee Ronald A. Rasband wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili sasa watatufundisha zaidi kuhusu marekebisho haya muhimu.
Mabadiliko haya yamekuwa yakichunguzwa kwa muda wa miezi mingi. Tumehisi mahitaji ya dharura ya kuboresha jinsi tunavyowajali washiriki wetu na tunavyoripoti mikutano yetu na wao. Ili kuweza kufanya hivyo vyema zaidi, tunahitaji kuimarisha akidi zetu za ukuhani ili kutoa mwelekeo mkubwa kwa huduma ya upendo na usaidizi ambao Bwana anautaka kwa Watakatifu Wake.
Marekebisho haya yana mwongozo wa kiungu kutoka kwa Bwana. Tukiyatekeleza, tutakuwa na ufanisi zaidi kuliko hapo awali.
Tumejiingiza katika kazi ya Mwenyezi Mungu. Yesu ndiye Kristo! Sisi ni watumishi Wake wanyenyekevu! Mungu awabariki ninyi ndugu tunapojifunzana kutekeleza majukumu yetu, naomba haya katika jina la Yesu Kristo, amina.