2010–2019
Nabii wa Mungu.
Aprili 2018


Nabii wa Mungu.

Nabii hasimami kati yetu na Mwokozi. Badala, yeye husimama pembeni mwetu na kuonyesha njia inayoelekea kwa Mwokozi.

Nami naongeza makaribisho yangu kwa Mzee Gerrit Gong na Mzee Ulisses Soares kwenye undugu usiyo na kifani wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili.

Katika kumuidhinisha Rais Russell M. Nelson kama nabii wa Bwana na Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tulikuwa sehemu ya kusanyiko la kiroho na la kiungu lililoamrishwa—kiroho kwa sababu matukio ya saa lililopita yametarajiwa mbinguni tangu kabla ya ulimwengu kuwepo. Bwana Yesu Kristo, anayeongoza Kazi Yake, leo hii, kupitia Rais Eyring, amemuwasilisha nabii Wake, kiongozi wake aliyepakwa mafuta, kwetu sisi, watu Wake wa agano, kuturuhusu sisi kuonyesha hadharani utayari wetu kumuidhinisha na kufuata ushauri wake.

Kwa yale mamilioni ya waumini ambao hawako hapa pamoja nasi katika Kituo cha Mikutano, mimi nataka mjue kwamba Roho wa Bwana katika jengo hili wakati kuidhinishwa kwa Rais Nelson alikuwa hasa kama vile mngelitarajia—wingi wa nguvu za kiroho. Kusanyiko letu lililoongozwa kutoka mbinguni sio tu katika hiki Kituo cha Mikutano pekee lakini kote duniani: katika majumba ya mikutano kule Asia, Afrika, na Amerika Kaskazini; majumbani, katika Amerika ya Kati na Kusini na Uropa; katika mabaraza kule Pasifiki na visiwa vya baharini. Kusanyiko hili liko katika sehemu yoyote ile ya dunia pale mnapoweza kuwa, hata ikiwa miunganisho yenu si zaidi ya sauti ya simu ya mkono ya kisasa. Mikono yetu iliyonyooshwa haikuhesabiwa na maaskofu wetu, lakini hakika ilitambuliwa, kama agano letu na Mungu, na vitendo vyetu vilirekodiwa katika kitabu cha uzima.

Bwana Humteua Nabii Wake

Kuchaguliwa kwa nabii kunafanywa na Bwana Mwenyewe. Hakuna kampeni, hakuna mijadala kwa sauti kubwa, hakuna kujipendekeza, hakuna kutokubaliana, kutoaminiana, mkanganyiko, au vurugu. Mimi, pia nathibitisha kwamba nguvu za mabinguni zilikuwa pamoja nasi katika chumba cha juu cha hekalu tulipokuwa kwa maombi tumemzunguka Rais Nelson na kuhisi idhinisho wazi la Bwana juu yake.

Uteuzi wa Rais Nelson kutumikia kama nabii wa Mungu ulifanywa kitambo sana. Maneno ya Bwana kwaYeremia pia yanatumika kwa Rais Nelson: “Kabla sijakuumba katika tumbo nilikujua, na kabla hujatoka tumboni, nilikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.”1 Miaka mitatu tu iliyopita, Mzee Nelson, akiwa na umri wa miaka 90, alikuwa wa nne katika ukuu, na wawili kati ya wale Mitume wakuu wakiwa na umri mdogo kumliko. Bwana aliye na uwezo juu ya uhai na kifo, humteua nabii Wake. Rais Nelson, akiwa na umri wa miaka 93 yuko na afya ya ajabu. Tunatumai atakuwa nasi kwa muongo mmoja zaidi au miwili, lakini kwa sasa tunajaribu kumshawishi akae mbali na miteremko ya kutelezea ya Utah.

Huku tukimkubali nabii kama mpakwa mafuta wa Bwana, na iwe wazi kwamba tunamwabudu tu Mungu, Baba yetu wa Mbinguni, na Mwana Wake mtakatifu. Ni kupitia ustahili, rehema, na neema, ya Mwokozi wetu, Yesu Kristo, ambayo siku moja tunaweza tukaingia tena katika uwepo Wao.2

Kwa Sisi Tumfuate Nabii?

Hata hivyo, Yesu amefunza ukweli muhimu kuhusu watumishi ambao Yeye uwatuma kwetu. “Awapokeaye ninyi,” Alisema “anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma.”3

Wajibu muhimu zaidi wa nabii wa Bwana ni kutufundisha juu ya Mwokozi na kutuongoza hadi Kwake.

Kunazo sababu nyingi za kimantiki za kumfuata Rais Russell M. Nelson. Hata wale wa ulimwengu wanaweza kumwita mwerevu. Alikuwa daktari wa kimatibabu akiwa na umri wa miaka 22, mpasuaji wa moyo aliyeenziwa, na mtangulizi aliyesifika katika usitawi wa upasuaji wa moyo wazi.

Wengine wangeweza kutambua hekima na maamuzi yake: miongo kenda ya kujifunza kuhusu uzima na kifo, akiishi kwa kujinyima, kuwapenda na kuwafundisha watoto wa Mungu katika pembe ya ulimwengu, na uzoefu wa kulea watoto 10, wajukuu 57, na vitukuu 118 ( idadi hii ya mwisho inabadilika kila mara; wa 118 unatarajiwa leo)

Picha
Rais Russell M. Nelson akiwa na kituu wa kiume mpya

Wale ambao wanamjua vyema wangeogea juu ya Rais Nelson akikumbana na magumu ya maisha kwa imani na ujasiri. Wakati saratani ilichukuwa maisha ya bintiye wa miaka 37, Emily, na kumwacha mume mpendwa na watoto tano wadogo, nilimsikia akisema, “Nilikuwa baba yake, daktari wa kimatibabu, na Mtume wa Bwana Yesu Kristo, lakini ilinibidi niinamishe kichwa na kutambua, ‘walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.’”4

Walinzi Juu ya Mnara

Ingawa tunapenda hizi sifa zote za ungwana, je, kwa nini tumfuate Rais Nelson? Kwa nini ni tumfuate nabii? Kwa sababu Bwana Yesu Kristo amemtawaza kama mlinzi wake juu ya mnara.

Picha
Carcassonne, France

Carcassonne ni mji wa ajabu uliozingirwa na ukuta kule Ufaransa ambao umestawi toka enzi za kati. Minara mirefu inainuka juu kutoka kwenye kuta zake zilizolindwa, ulijengwa kwa ajili ya walinzi waliosimama katika minara ile mchana na usiku, wakitazama kwa makini kabisa katika upeo wa macho ili wamuone adui. Wakati mlinzi alipomuona adui akikaribia, sauti yake ya kuonya iliwalinda watu wa Carcassonne dhidi ya hatari iliyokuwa ikikaribia ambayo hawangeweza kuona.

Nabii ni mlinzi juu ya mnara, anatulinda dhidi ya hatari za kiroho tusizoweza kuziona.

Bwana alimwambia Ezekieli “Nimekuweka kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli; basi, sikia neno hili [litokalo] katika kinywa changu, ukawape maonyo haya yatokayo kwangu.”5

Mara nyingi sisi huzungumza kuhusu umuhimu wetu sisi kumfuata nabii, lakini zingatia mzigo mzito ambao Bwana anamtwika nabii Wake: “Nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo… mtu mbaya huyo … atakufa katika uovu wake; … damu yake nitaitaka mkononi mwako.”6

Ushuhuda Mkuu wa Kibinafsi

Tunamkubali Rais Nelson jinsi ambavyo tungemkubali Petro au Musa ikiwa tungeishi katika siku zao. Mungu alimwambia Musa, “Nitakiongoza kinywa chako, na kukufundisha nini cha kusema.”7 Tunamsikiliza nabii wa Bwana kwa imani kwamba maneno yake “yanatoka kwenye kinywa cha Bwana.”8

Je, hii ni imani pofu? Hapana, si kweli. Kila mmoja wetu ana ushuhuda wa kiroho juu ya ukweli wa Urejesho wa injili ya Yesu Kristo. Kwa hiari na uchaguzi wetu wenyewe, tulinyoosha mikono yetu asubuhi ya leo, kutangaza azimio letu la kumuunga mkono nabii wa Bwana kwa “ujasiri [wetu], imani [yetu], na sala [zetu]”9 na kufuata ushauri wake. Tunayo heshima kama Watakatifu wa Siku za Mwisho kupokea ushahidi binafsi kwamba wito wa Rais Nelson unatoka kwa Mungu. Huku mke wangu, Kathy, akiwa anamfahamu Rais Nelson kibinafsi kwa karibu miungo tatu na hana swali lolote kuhusu wito wake mtakatifu, baada ya kusimikwa kwake, alianza kuzisoma hotuba zake mkutano mkuu za miaka 34 iliyopita, akisali ili apate uhakika wa kina zaidi kuhusu jukumu lake la unabii. Ninawaahidi ya kwamba ushahidi huu mkubwa utakuja kwenu mtakapoutafuta kwa unyenyekevu kwa ustahiki.

Ni kwa nini tuko radhi sana kufuata sauti ya nabii wetu? Kwa wale wanaotafuta uzima wa milele kwa dhati, sauti ya nabii huleta usalama wa kiroho katika dunia iliyojaa msukosuko.

Tunaishi kwenye sayari iliyojaa kelele ya sauti milioni. Mtandao, simu zetu za mkononi, masanduku yetu makubwa ya burudani yote yanasihi usikivu wetu na kurusha ushawishi wao juu yetu kwa matumaini tutanunua bidhaa zao na kukubali viwango vyao.

Kinachoonekana kama mfululizo wa habari na maoni hutukumbusha kuhusu tahadhari za kimaandiko juu ya “tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa,”10 “kuchukuliwa na kila upepo,”11 tukishawishiwa sana na “ kwa ujanja,” na kushindwa na wale “tukizifuata njia za udanganyifu.”12

Kutia nanga nafsi zetu kwa Bwana Yesu Kristo huhitaji kusikiliza wale ambao amewatuma. Kumfuata nabii katika ulimwengu wenye vurugu ni kama kufungwa kwenye blanketi ya kutuliza, yenye joto katika siku ya baridi ya kugandisha.

Tunaishi katika ulimwengu wa uwazaji, majadiliano, mabishano, mantiki, na maelezo. Kuuliza, “Kwa nini?” inasaidia katika sehemu nyingi sana za maisha yetu, kuruhusu uwezo wa akili zetu kutuongoza katika chaguzi na uamuzi wote tunaokabiliana nao kila siku.

Lakini sauti ya Bwana kila mara huja bila maelezo.13 Kitambo kabla ya wasomi kujifunza juu ya athari ya uzinzi juu ya wenzi waaminifu na watoto, Bwana alitangaza, “Usizini.”14 Zaidi ya akili pekee, sisi tunathamini kipawa cha Roho Mtakatifu.

Msishangae

Picha
Nuhu akihubiri

Sauti ya nabii, huku ikisema kwa ukarimu, mara nyingi itakuwa sauti inayotuomba tubadilike, tutubu na kurudi kwa Bwana. Wakati marekebisho yanahitajika, tusichelewe. Na usiwe na wasiwasi wakati sauti ya kuonya ya nabii inatofautiana na maoni maarufu ya siku. Mishale ya moto ya kejeli za wasioamini wenye ghadhabu daima itarushwa wakati nabii anapoanza kusema. Ukiwa mnyenyekevu katika kufuata ushauri wa nabii wa Bwana, ninakuahidi baraka zaidi ya usalama na amani.

Picha
Samweli Mlamani atoa unabii

Usishangae ikiwa maoni yako binafsi wakati mwingine hayalingani na mafundisho ya nabii wa Bwana. Nyakati hizi za mafunzo, za unyenyekevu, wakati tunapopiga magoti kusali. Tunasonga mbele katika imani, tukimwamini Mungu, tukijua kwamba baada ya muda tutapokea uwazi zaidi wa kiroho kutoka kwa Baba wa Mbinguni. Nabii mmoja alielezea kipawa cha Mwokozi kisichoweza kulinganishwa kama “nia ya Mwana ikimezwa na nia ya Baba.”15 Kusalimisha mapenzi yetu kwa yale ya Mungu, hakika, sio kusalimu amri kabisa lakini mwanzo wa ushindi mtukufu.

Wengine watajaribu kuyachambua kupita kiasi maneno ya nabii, wakiwa na wakati mgumu kuelewa ni ipi sauti yake ya kinabii na ipi ni maoni yake.

Katika mwaka wa 1982 miaka miwili kabla ya kuitwa kama Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka, Ndugu Russell M. Nelson alisema: “Huwa sijiulizi, ‘Ni wakati gani nabii anazungumza kama nabii na ni wakati gani hafanyi hivyo?’ Hamu yangu imekuwa, ‘Nawezaje kuwa zaidi kama yeye?’” Aliongezea, “[Falsafa yangu ni] kuwacha kuweka alama ya kiuliza baada ya kauli za nabii na badala yake kuweka alama za mshangao.”16 Hivi ndivyo mtu mnyenyekevu na wa kiroho alichagua kupanga maisha yake. Sasa, miaka 36 baadaye, yeye ni nabii wa Bwana.

Kuzidisha Imani Yako katika Mwokozi

Katika maisha yangu binafsi, nimegundua kwamba ninapojifunza maneno ya nabii wa Mungu kwa maombi na kwa uangalifu, kwa subira, na kulinganisha mapenzi yangu na mafundisho yake, imani yangu katika Bwana Yesu Kristo daima huzidi.17 Ikiwa tutachagua kutupilia mbali ushauri wake na kuamua kwamba tunajua bora zaidi, imani yetu itaathirika na mtazamo wetu kuzibika. Mimi ninaahidi kwamba mnapobakia na azimio la kumfuata nabii, imani yenu katika Mwokozi itaongezeka.

Mwokozi alisema, “Manabii wote … wamenishuhudia.”18

Nabii hasimami kati yetu na Mwokozi. Badala, yeye husimama pembeni mwetu na kuonyesha njia inayoelekea kwa Mwokozi. Majukumu na zawadi kubwa zaidi ya Mwokozi kwetu sisi ni ushahidi wake thabiti, ufahamu wake hakika, kwamba Yesu ndiye Kristo. Kama Petro wa kale, nabii wetu anatangaza “[Yeye ndiye] Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”19

Katika siku za usoni, tukitazama nyuma kuhusu maisha yetu duniani, tutafurahia kwamba tulitembea ulimwenguni wakati wa nabii aliye hai. Siku hiyo, ninaomba kwamba tutaweza kusema:

Sisi tulimsikiliza.

Tulimwamini yeye.

Tulijifunza maneno yake kwa subira na imani.

Tulisali kwa ajili yake.

Tulisimama pamoja naye.

Tulikuwa wanyenyekevu vya kutosha kumfuata yeye.

Tulimwamini yeye.

Ninawaachieni ushahidi wangu wa dhati kwamba Yesu ndiye Kristo, Mkombozi wetu na Mwokozi wetu na kwamba Rais Russell M. Nelson ni nabii Wake mpakwa mafuta ulimwenguni. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Yeremia 1:5

  2. Ona 2 Nefi 2:8.

  3. Mathayo 10:40

  4. Kwa utondoti zaidi, ona Spencer J. Condie, Russell M. Nelson: Father, Surgeon, Apostle (2003), 153235.

  5. Ezekieli 33:7.

  6. Ezekieli 33:8.

  7. Kutoka 4:12.

  8. Mafundisho na Maagano 21:5.

  9. Mafundisho na Maagano 107:22.

  10. Waefeso 4:14.

  11. Yakobo 1:6

  12. Waefeso 4:14.

  13. Rais Dallin H. Oaks aliwahi kusema:

    “Katika usahili wa mwaka wa 1988 … nilielezea msimamo wangu juu ya majaribio ya kusambaza mawazo ya binadamu kwenye ufunuo mtakatifu.

    “‘Kama ukisoma maandiko ukiwa na swali akinini, “Kwa nini Bwana anaamuru hili au kwa nini aliamuru vile,” utapata kwamba chini ya moja katika amri mia moja kulikuwa na sababu zilitolewa. Sio utaratibu wa Bwana kutoa sababu. Sisi [binadamu] wanaweza kutoa sababu za ufunuo. Tunaweza kutoa sababau za amri. Tunapofanya hivyo, tunabaki peke yetu. Baadhi ya watu huweka sababu za [ufunuo] … , na inatokea walikuwa wamekosea. Hapa kuna somo. … Mimi niliamua kitambo sana kwamba nilikuwa na imani na amri na sikuwa na imani na sababu ambazo zilikuwa zimependekezwa.’ …

    “‘… Mrundo wa sababu ulionekana kwangu kuwa hatari kujaribu. … Acha tusifanye kosa ambalo lishafanywa hapo awali, … tukijaribu kutoa sababu za ufunuo. Sababu hutokea kuwa dhana za watu kwa kiasi kikubwa. Mafunuo nsiyo kile tunakubali kama mapenzi ya Bwana na hapo ndipo usalama ulipo’” (Life’s Lessons Learned [2011], 68–69).

  14. Kutoka 8:14.

  15. Mosia 15:7.

  16. Russell M. Nelson, in Lane Johnson, “Russell M. Nelson: A Study in Obedience,” Tambuli, Jan. 1983.

  17. Rais Henry B. Eyring alisema: “Hoja ya uwongo ingine ni kuamini kwamba chaguo la kukubali au kutokubali ushauri wa manabii sio kitu zaidi ya kuamua kama kukubali ushauri mzuri na kupata manufaa au kukaa jinsi tulivyo. Uchaguzi wa kutokukubali ushauri wa kinabii hubadili mahali tuliposimamia. Inakuwa ni hatari sana. Kushindwa kukubali ushauri wa kinabii hupunguza nguvu zetu za kukubali ushauri zaidi baadae. Muda muafaka wa kuchagua kumsaidia Nuhu kujenga safina ulikuwa ni mara ya kwanza alipouliza. Kila muda alipouliza baada ya hapo, kila kushindwa kuitikia kungeweza kupunguza umakini katika Roho. Na ndio kila muda ombi lake lingeoneka la kipumbavu zaidi, mpaka mvua ilipokuja. Na kisha ilikuwa kuchelewa sana” (“Finding Safety in Counsel,” Ensign, May 1997, 25).

  18. 3 Nefi 20:24.

  19. Mathayo 16:16; ona pia Yohana 6:69.

Chapisha