Kama Kristo Anavyowasamehe Ninyi, Vivyo na Ninyi
Sisi sote twaweza kupokea amani isiyo na kifani na kushirikiana na Mwokozi wetu tunapojifunza kuwasamehe bila vikwazo wale ambao wametukosea.
“Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari, na wengine wakiwa pamoja nao.
“Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi.
“Wakaingia, wasiuone mwili wa Bwana Yesu.
“Ikawa walipokuwa wakifadhaika kwa ajili ya neno hilo, tazama, watu wawili walisimama karibu nao, wamevaa nguo za kumetameta:
“Nao walipoingiwa na hofu na kuinama kifudifudi hata nchi, hao waliwaambia, Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu?
“Hayupo hapa, amefufuka.”1
Kesho, Sabato ya Pasaka, tutakumbuka kwa njia maalum kile ambacho Yesu Kristo ametutendea: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”2 Hatimaye tutafufuliwa kama alivyofufuka, ili tuishi milele.
Kupitia muujiza wa Upatanisho mtakatifu wa Yesu Kristo, tunaweza pia kupokea zawadi ya msamaha wa dhambi zetu na makosa yetu, ikiwa tutakubali nafasi na jukumu la toba. Na kwa kupokea ibada muhimu, kuyashika maagano na kutii amri, tunaweza kupokea uzima wa milele na kuinuliwa.
Leo hii, ningependa kulenga kwenye msamaha, zawadi muhimu na yenye thamani iliyotolewa kwetu kutoka kwa Mwokozi na Mkombozi wetu, Yesu Kristo.
Usiku mmoja wa Disemba ya mwaka wa 1982, mke wangu, Terry, pamoja nami tuliamshwa na mlio wa simu nyumbani kwetu kule Pocatello, Idaho. Nilipokuwa nikijibu simu, nilisikia tu kilio. Hatimaye, sauti dhaifu ya dada yangu ilisema, “Tommy amefariki.”
Dereva mlevi mwenye umri wa miaka 20, akienda kwa kasi ya zaidi ya maili 85 (135 km) kwa saa, bila ya kujali alivuka taa nyekundu katika kiunga cha mji wa Denver, Colorado. Aliligonga kwa nguvu sana gari lililokuwa likiendeshwa na ndugu yangu mdogo, Tommy, na kumuua papo hapo pamoja na mkewe, Joan. Walikuwa wakirejea nyumbani kwa binti mdogo baada ya sherehe ya Krismasi.
Mke wangu pamoja nami mara moja tulipanda ndege kwenda Denver na kuelekea katika chumba cha kuhifadhia maiti. Tulikutana na wazazi wangu na ndugu zangu na kuomboleza kuwapoteza wapendwa wetu Tommy na Joan. Tulikuwa tumewapoteza kupitia kitendo cha kipuuzi na cha kihalifu. Mioyo yetu ilivunjwa, na hasira kwa kijana huyo mkosaji ilianza kukua ndani yangu.
Tommy alikuwa amehudumu kama mwanasheria katika Idara ya Haki ya Marekani na alikuwa akielekea kuwa mtetezi mkubwa wa kulinda maeneo ya Kiasili ya Amerika na maliasili kwa miaka mingi ijayo.
Baada ya muda kiasi kupita, kikao cha kutoa hukumu kortini kilifanyika kwa ajili ya mvulana aliyepatikana na hatia ya kuua kwa gari bila kukusudia. Katika huzuni na masikitiko yao yaliyokuwa yakiendelea, wazazi wangu na dada yangu mkubwa, Katy, walihudhuria kikao hicho. Wazazi wa yule dereva mlevi pia walikuwepo, na baada ya kikao hicho kukamilika, waliketi kwenye benchi na kulia. Wazazi wangu na dada yangu walikuwa wameketi karibu walipokuwa wakijaribu kuthibiti hisia zao. Baada ya muda, wazazi wangu na dada yangu walisimama na kwenda kwa wazazi wa yule dereva mlevi na kuwapa maneno ya kufariji na msamaha. Wanaume walisalimiana; wanawake walishikana mikono; kulikuwepo na huzuni kubwa na machozi kutoka kwa wote na kutambua kwamba familia zote mbili zilikuwa zimeteseka mno. Mama, Baba, na Katy waliongoza nija kwa nguvu zao za kimya na ujasiri na kuoyesha familia yetu jinsi msamaha unavyofanana.
Ufikiaji huo wa msamaha katika nyakati hizo ulisababisha moyo wangu kuwa mwepesi na kufungua njia ya uponyaji. Baada ya muda nilijifunza namna ya kuwa na moyo wenye kusamehe. Ni kupitia tu msaada wa Mfalme wa Amani mzigo wangu wa uchungu uliinuliwa. Moyo wangu daima utamkosa Tommy na Joan, lakini msamaha sasa unaniruhusu kuwakumbuka kwa furaha isiyo na vikwazo. Na ninajua tutakuwa pamoja tena kama familia.
Sipendekezi kwamba tupuuze vitendo visivyo halali. Tunajua kabisa kwamba watu wanapaswa kuwajibika binafsi kwa vitendo vyao vya uhalifu na makosa ya kiraia. Hata hivyo, pia tunajua ya kwamba, kama wana na mabinti wa Mungu ambao wanafuata mafundisho ya Yesu Kristo. Tunapaswa kuwa wenye kutoa msamaha hata inapoonekana kuwa wengine pengine hawastahili msamaha wetu.
Mwokozi alifundisha:
“Maana mkiwasamehe watu makosa yao, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi pia:
“Lakini kama hamtawasamehe watu makosa yao Baba yenu hatawasamehe makosa yenu.”3
Sisi sote twaweza kupokea amani isiyo na kifani na kushirikiana na Mwokozi wetu tunapojifunza kuwasamehe bila vikwazo wale ambao wametukosea. Kushirikiana huku kunaleta nguvu za Mwokozi maishani mwetu katika njia dhahiri, na kamwe isiyoweza kusahaulika.
Mtume Paulo alishauri:
“Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, … jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole; uvumilivu;
“Mkichukuliana, na kusameheana, … : kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.”4
Bwana Mwenyewe ametamka:
“Kwa hiyo, ninawaambia, kwamba mnapaswa kusameheana ninyi kwa ninyi; kwani yule asiyemsamehe ndugu yake makosa yake husimama na hatia mbele za Bwana; kwa kuwa ndani yake imebaki dhambi kubwa.
“Mimi, Bwana, nitamsamehe yule nitakaye kumsamehe, lakini ninyi mnatakiwa kuwasamehe watu wote.”5
Mafundisho ya Mwokozi na Mkombozi wetu, Yesu Kristo, yako wazi; mwenye dhambi ni lazima awe radhi kuwasamehe wengine ikiwa yeye anatumai kusamehewa.6
Akina kaka na akina dada, je kuna watu maishani mwetu ambao wametuumiza? Je, tunahifadhi kile kinachoonekana kama hisia zilizohalalishwa kikamailifu za chuki na hasira? Je, tunaruhusu kiburi kutuzuia kutokana na kusamehe na kusahau? Nawaalika sisi sote kusamehe kikamilifu na kuruhusu uponyaji kufanyika kutoka ndani. Na hata kama msamaha hautakuja leo, jua ya kwamba tunapoutamani na kuushughulikia, utakuja—jinsi tu ulivyonijia mimi baada ya kifo cha ndugu yangu.
Tafadhali pia mkumbuke ya kwamba sehemu muhimu ya msamaha ni pamoja na kujisamehe sisi wenyewe.
“Tazama, yule ambaye ametubu dhambi zake, Bwana alisema “huyu anasamehewa, na Mimi, Bwana, sizikumbuki tena.”7
Ninaomba kwa niaba yetu sisi sote siku ya leo tukumbuke kufuata mfano wa Yesu Kristo. Msalabani Goligotha, katika maumivu Yake, Alisema maneno haya: “Baba, uwasamehe; kwa kuwa hawajui watendalo.”8
Kwa kuwa na roho ya kusamehe na kutenda, kama wazazi wangu na dada yangu mkubwa tunaweza kutambua ahadi ya Mwokozi: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msiwe na wasiwasi moyoni mwenu, wala msifadhaike.”9
Ninashuhudia amani hii itakuja maishani mwetu tunapotii mafundisho ya Yesu Kristo na kufuata mfano Wake kwa kuwasamehe wengine. Tunaposamehe, ninaahidi ya kwamba Mwokozi atatuimarisha, na nguvu Zake na furaha yake vitatiririka maishani mwetu.
Kaburi li tupu. Kristo yu hai. Ninamjua. Ninampenda. Ninashukuru kwa ajili ya neema Yake, ambayo ni nguvu ya kuimarisha ambayo ina uwezo wa kuponya vitu vyote. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.