Upendo Msafi: Ni ishara ya Kweli ya Mfuasi Halisi wa Yesu Kristo.
Injili ya Yesu Kristo imejikita kwenye upendo wa Baba na Mwokozi na upendo wetu Kwao na kwa kila mmoja kwa mwingine.
Tunampenda na kumkosa Rais Monson, na tunampenda na kumwidhinisha Rais Nelson. Rais Nelson ana sehemu maalum moyoni mwangu.
Nilipokuwa baba kijana, mwana wetu mdogo aliyekuwa na umri wa miaka mitano alikuja nyumbani kutoka shuleni siku moja na kumwuliza mama yake “Baba hufanya kazi ya aina gani?” Kisha akaeleza kuwa wenzake darasani walianza kujadili kuhusu kazi za baba zao. Mmoja alisema kuwa baba yake alikuwa mkuu wa polisi jijini, huku mwingine akisema kwa kujigamba kuwa baba yake alikuwa mkuu wa kampuni kubwa.
Kwa hivyo alipoulizwa kuhusu baba yake, mwana wangu alisema kwa urahisi, “Baba yangu hufanya kazi kwenye ofisi kwa kompyuta.” Alipoona kuwa jibu lake halikuwavutia sana marafiki zake wadogo, aliongeza, “na, je mnajua baba yangu ni mkuu wa Ulimwengu.”
Ninadhani hiyo ilikuwa mwisho wa mazungumzo hayo.
Nilimwambia mke wangu, “Ni wakati wa kumfundisha maelezo zaidi kuhusu mpango wa wokovu na nani aliye msimamizi halisi.
Lakini tulipowafundisha watoto wetu mpango wa wokovu, upendo wao kwa Baba wa Mbinguni na kwa Mwokozi ulikua walipojifunza kuwa ni mpango wa upendo. Injili ya Yesu Kristo imejikita kwenye upendo wa Baba na Mwokozi na upendo wetu Kwao na kwa kila mmoja kwa mwingine.
Mzee Jeffrey R. Holland alisema, “amri kuu ya kwanza zaidi ya zote za milele ni kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote, uwezo, akili, na nguvu—hiyo ndiyo amri kuu ya kwanza. Lakini ukweli mkuu wa kwanza wa milele yote ni kwamba Mungu anatupenda sisi kwa moyo Wake wote, nguvu, akili na uwezo. Upendo huo ni jiwe la msingi wa milele, na linapaswa kuwa jiwe la msingi wa maisha ya kila siku.1
Ukiwa jiwe la msingi la maisha yetu ya kila siku, upendo msafi ni sharti kwa kila mfuasi wa Yesu Kristo.
Nabii Mormoni alifundisha: “Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, ombeni kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba mjazwe, na upendo huu, ambao ametoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwana wake, Yesu Kristo” (2).
Kwa kweli upendo ni ishara ya kila mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo.
Wafuasi wa kweli wanapenda kuhudumu. Wanafahamu kuwa kuhudumu ni maonyesho ya upendo wa kweli na maagano waliyofanya wakati wa ubatizo.3 Licha ya miito yao kanisani au majukumu yao katika jamii, wanahisi ongezeko la hamu ya kumpenda na kumhudumia Bwana na mmoja kwa mwingine.
Wafuasi wa kweli hupenda kusamehe. Wanafahamu kuwa Upatanisho wa Mwokozi hushughulikia dhambi na makosa ya kila mmoja wetu. Wanajua kuwa gharama Aliyolipa ni “gharama inayojumuisha yote” Kodi za kiroho, karo, ujira na malipo yanayohusiana na dhambi, makosa na maovu yameshughulikiwa. Wanafunzi wa kweli husamehe haraka na wanaomba msamaha kwa haraka.
Akina kaka na dada wapendwa, ikiwa unapambana kupata nguvu ya kusamehe, usifikirie yale wengine wanekufanyia, lakini fikiria yale Mwokozi amekufanyia, utapata amani kwenye baraka yenye ukombozi ya Upatanisho Wake.
Wafuasi wa kweli wanapenda kumtii Bwana wakiwa na amani mioyoni mwao. Ni wanyenyekevu na watiifu kwa sababu wanampenda Yeye. Wana imani kukubali kwa ukamilifu mapenzi Yake, si tu kwa kile anachofanya bali pia namna na lini anapofanya. Wafuasi wa kweli wanafahamu kuwa baraka halisi si kila mara kile wanachotaka bali ni kile ambacho Bwana anawatakia.
Wafuasi wa kweli wanampenda Bwana kuliko wanavyoupenda ulimwengu na ni imara na wasiotikisika katika imani yao. Wanasalia kuwa wenye nguvu na imara katika ulimwengu unaobadilika na unaokanganya. Wafuasi wa kweli wanapenda kusikiliza sauti ya Roho na ya manabii na hawakanganywi na sauti za ulimwengu. Wafuasi wa kweli wanapenda “kusimama pahali patakatifu”4 na hupenda kufanya sehemu takatifu mahali ambapo watakaa. Popote waendapo, wanapeleka upendo wa Bwana na amani katika mioyo ya wengine. Wafuasi wa kweli hupenda kufuata amri za Bwana na kutii kwa sababu wanampenda Bwana. Kwa kuwa wanapenda na kuweka maagano yao, mioyo yao na asili yao hubadilika.
Upendo msafi ni ishara kweli ya mfuasi halisi wa Yesu Kristo.
Nilijifunza kuhusu upendo msafi kutoka kwa mama yangu. Hakuwa mshiriki wa Kanisa.
Siku moja, miaka mingi iliyopita, nilimtembelea mama yangu ambaye alikuwa akipambana na ugonjwa wa saratani. Nilijua kuwa angekufa lakini nilikuwa na wasiwasi kwamba alikuwa anateseka. Sikusema chochote, lakini kwa kunifahamu vilivyo, alisema “Naona una wasiwasi.”
Kwa mshangao wangu, aliniuliza kwa sauti hafifu, “unaweza kunifundisha kuomba?” Ninataka kukuombea. Ninajua unaanza kwa kusema ‘Baba Mpendwa wa Mbinguni,’ lakini kisha ninapaswa niseme nini?
Nilipopiga magoti karibu na kitanda chake na aliponiombea, nilisikia upendo nisiosikia tena hapo awali. Ilikuwa upendo rahisi, wa kweli, msafi. Ingawa hakujua kuhusu mpango wa wokovu, alikuwa moyoni mwake na mpango binafsi wa upendo, mpango wa upendo wa mama kwa mwanawe. Alikuwa na uchungu, akipambana hata kupata nguvu ya kusali. Ilikuwa vigumu kwangu kumsikia.
Ninakumbuka nikifikiria, “Mtu anawezaje akiwa kwenye uchungu mkuu hivi kumwombea mtu mwingine? Yeye ndiye mwenye hitaji”
Kila jibu likaja dhahiri akilini mwangu: upendo msafi Alinipenda sana hata akajisahau mwenyewe. Katika wakati wake wa haja, alinipenda kuliko alivyojipenda.
Na sasa, wapendwa kaka na dada zangu, si haya ndiyo Mwokozi aliyafanya? Bila shaka kwa mtazamo mpana zaidi na wa milele. Lakini kati ya uchungu Wake mkuu zaidi, kwenye bustani usiku huo, alikuwa mwenye kuhitaji usaidizi, akiumia kwa njia ambayo hata hatuwezi kufikiria wala kuelewa. Lakini hatimaye, alijisahau na kutuombea hadi alipolipa dhamana yote. Aliwezaje kutimiza hilo? Kwa sababu ya upendo msafi kwa Baba, Aliyemtuma, na kwetu. Alimpenda Baba kuliko jinsi alivyojipenda.
Alilipa kitu ambacho hakuwa amefanya. Alilipia dhambi ambazo hakutenda. Kwa nini? Upendo msafi Baada ya kulipa dhamana kamili alikuwa kwenye sehemu ambapo angetupa baraka ya kile alicholipia, kama tungetubu. Kwa nini alitupa hayo? Tena, na daima, upendo msafi.
Upendo msafi ni ishara kweli ya mfuasi halisi wa Yesu Kristo.
Rais Thomas S. Monson alisema, “Na tuanze sasa, siku ya leo, kuonyesha upendo kwa watoto wote wa Mungu, iwe wao ni wanafamilia wetu, marafiki zetu, watu tunaowafahamu, au hata wageni tu. Tunapoamka kila asubuhi, acha sisi tuamue kujibu kwa upendo na ukarimu kwa kile chochote kinachoweza kuja njia yetu.5
Akina kaka na dada, injili ya Yesu Kristo ni injili ya upendo. Amri iliyo kuu inahusu upendo. Kwangu mimi yote ni kuhusu upendo Upendo wa Baba, aliyetoa dhabihu mwanawe Upendo wa Mwokozi aliyejitoa dhabihu kwa ajili yetu sote . Upendo wa mama au baba ambaye angetoa chochote kwa ajili ya watoto wake. Upendo wa wale wanaohudumu kimya kimya na wasiojulikana kwa wengi wetu lakini wanajulikana kwa Bwana. Upendo wa wale wanaosamehe yote na kila wakati. Upendo wa wale wanaotoa zaidi ya wanayopokea.
Nampenda Baba yangu wa Mbinguni. Ninampenda Yesu. Mimi naipenda injili. Ninalipenda Kanisa hili. Mimi naipenda familia yangu. Nayapenda maisha haya ya ajabu. Kwangu mimi, yote ni kuhusu upendo.
Na siku hii ya ukumbusho wa ufufuo wa Mwokozi iwe siku ya kutengenezwa upya kwa kila mmoja wetu. Na siku hii iwe mwanzo wa maisha yaliyojaa upendo, jiwe la msingi wa misha yetu ya kila siku.
Na mioyo yetu ijazwe na upendo msafi wa Kristo, ishara halisi ya kila mfuasi wa Yesu Kristo. Haya ndiyo maombi yangu katika jina la Yesu Kristo, amina.