Roho Wake Atakuwa Pamoja Nanyi
Ninasali kwa moyo wangu wote kwamba mtasikia sauti ya Roho, ambayo inatumwa kwenu kwa ukarimu.
Akina kaka na akina dada zangu, nashukuru kwa nafasi kuzungumza nanyi katika siku ya Sabato, katika mkutano mkuu wa Kanisa Lake, katika kipindi hiki cha Pasaka. Nina mshukuru Mungu kwa Zawadi ya Mwanawe Mpendwa, ambaye alikuja kwa hiari duniani kuwa Mkombozi wetu. Ninashukuru kujua kwamba alifilia dhambi zangu na kufufuka katika ufufuko. Kila siku ninabarikwa kujua kwamba, kwa sababu ya Upatanisho Wake, siku moja ninaweza kufufuka na kuishi milele katika familia yenye upendo.
Ninajua vitu hivyo kwa njia pekee ambayo kila mmoja wetu anaweza kujua. Roho Mtakatifu amezungumza akilini mwangu na moyoni mwangu kwamba ni vya kweli—si mara moja tu lakini mara kadhaa. Nimehitaji faraja hiyo endelevu. Sote tunapitia magumu ambapo tunahitaji uthibitisho wa Roho. Nilihisi hivyo siku moja wakati niliposimama na baba yangu hospitalini. Tulimwangalia mama yangu akihema kwa tabu—na kisha akaacha. Wakati tulipomwanagalia usoni, alikuwa akitabasamu wakati maumivu yalipokuwa yakiondoka. Muda mfupi wa ukimya, baba yangu akongea kwanza. Alisema, “msichana mdogo amerudi nyumbani.”
Alisema hayo kwa upole. Alionekana kuwa mwenye amani. Alikuwa akisema kitu alichojua kuwa ni cha kweli. Taratibu alianza kukusanya vitu binafsi vya mama. Alikwenda nje kwenye ukumbi wa hospitali kumshukuru kila muuguzi na daktari ambaye alimhudumia mama kwa siku nyingi.
Baba yangu alikuwa na wenza wa Roho Mtakatifu katika wakati huo kuhisi, kujua, na kufanya kile alichofanya siku ile. Alipokea ahadi kama wengi walivyopokea: “Ili daima Roho wake apate kuwa pamoja nao” (M&M 20:79).
Tumaini langu leo ni kuongeza hamu na uwezo wenu wa kumpokea Roho Mtakatifu. Kumbuka, Yeye ni mshiriki wa tatu wa Uungu. Baba na Mwana ni wanadamu waliofufuka. Roho Mtakatifu ni mtu wa kiroho. (Ona M&M 130:22.) Ni uchaguzi wako kama utampokea Yeye na kumkaribisha Yeye katika moyo na akili yako.
Masharti ambayo kwayo tunaweza kupokea baraka hiyo ya kiungu yamewekwa wazi katika maneno ambayo husemwa kila wiki lakini labda hayazami kwa kina katika mioyo na akili zetu. Ili Roho aweze kutumwa kwetu lazima mara zote “tumkumbuke” Mwokozi na “kushika amri zake” (M&M 20:77).
Kipindi hiki cha mwaka hutusaidia kukumbuka dhabihu ya Mwokozi na ufufuko Wake kutoka kaburini kama mwanadamu aliyefufuka. Wengi wetu tuna taswira ya matukio hayo katika kumbukumbu zetu. Niliwahi kusimama na mke wangu nje ya kaburi huko Yerusalemu. Wengi huamini kwamba hilo ndilo kaburi ambalo Mwokozi aliyesulubiwa alitoka kama Mungu aliyefufuka na aishiye.
Mwongozi wenye heshima siku ile iliashiria na mkono wake na kutwambia sisi, “Njoo, ona kaburi li wazi.”
Tuliinama kuingia. Tuliona benchi la jiwe kwenye ukuta. Lakini akilini mwangu ikaja picha nyingine, halisi kama ile tuliyoona siku ile. Ilikuwa ni ya Mariamu, ambaye aliachwa na Mitume kaburini. Hicho ndicho Roho aliniruhusu nione na hata kusikia katika akili yangu, waziwazi kama vile niliwahi kuwa mahali pale:
“Lakini Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia: Basi akilia hivi, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi,
“Akaona malaika wawili wenye mavazi meupe wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu.
“Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka.
“Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu.
“Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhani ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa.
“Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia, Raboni; yaani, Mwalimu wangu.”
“Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu” (Yohana 20:11–17).
Nimeomba ili kuweza kuhisi kile ambacho Mariamu alihisi katika kaburi na kile wanafunzi wawili walihisi wakiwa njiani kwenda Emau wakati wakitembea na Mwokozi aliyefufuka, wakidhani ni mgeni Yerusalemu.
“Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao.
“Na ikatokea kwamba, alipoketi kula chakula pamoja nao, akachukua mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.
“Mara macho yao yakafumbuliwa, na wakamtambua ni yeye; naye akatoweka kati yao.
“Basi wakaambiana, je mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu, wakati alipokuwa anatufafanulia maandiko matakatifu kule njiani?” (Luka 24:29–32).
Baadhi ya hayo maneno yalirudiwa katika mkutano wa sakramenti niliohudhuria zaidi ya miaka 70 iliyopita Katika siku hizo mikutano ya Sakramenti ilikuwa ikifanyika jioni. Nje kulikuwa na kiza. Mkusanyiko uliimba maneno haya yanayotambulika. Niliyasikia mara nyingi. Lakini kukumbukumbu yangu inayodumu ni ya hisia katika usiku mmoja. Hunisogeza karibu na Mwokozi. Labda kama nitanukuu maneno yatajirudia kwetu tena:
Kaa nami; usiku unaingia.
Siku imepita na kwisha;
Giza la usiku linaingia;
Usiku unakuja.
Ndani ya moyo wangu karibu mgeni
Kaa katika nyumba yangu.
Kaa nami; usiku unaingia.
Kutembea kwako leo nami
Kumesababisha moyo wangu kuhisi mwako.
Nilipokuwa nikizungumza nawe.
Maneno ya dhati yameijaza nafsi yangu
Na kuniweka karibu nawe.
Ee Mwokozi, kaa nami usiku huu;
Tazama, ni usiku.
Ee Mwokozi, kaa nami usiku huu;
Tazama, ni usiku.1
Ya thamani zaidi kuliko kumbukumbu ya matukio ni kumbukumbu ya Roho Mtakatifu akigusa mioyo yetu na uthibitisho Wake endelevu wa ukweli. Ya thamani zaidi kuliko kuona kwa macho yetu, au kukumbuka maneno yaliyozungumzwa au kusomwa, ni kukumbuka hisia ambazo ziliambatana na sauti tulivu ya Roho. Mara chache, nimehisi sawa na wale wasafiri walivyohisi katika njia ya kuelekea Emau—kama mwako laini katika moyo. Mara nyingi ni hisia ya mwangaza na uthibitisho dhahiri.
Tuna ahadi ya thamani sana ya Roho Mtakatifu kama mwenzi wakati tukiwa na mwelekeo wa kweli wa jinsi gani ya kupata hiyo zawadi. Maneno haya yanasemwa na mtumishi wa Bwana mwenye mamlaka mikono yake ikiwa juu ya kichwa chetu: “Pokea Roho Mtakatifu.” Katika wakati huo, wewe na mimi tumepata uthibitisho kuwa Yeye atatumwa. Lakini jukumu letu ni kuchagua kufungua mioyo yetu kupokea uhudumu wa Roho, katika maisha yote.
Uzoefu wa Nabii Joseph Smith unatoa mwongozo. Alianza na kuendelea huduma yake akiwa na uamuzi kwamba hekima yake pekee haikutosha kujua njia ipi angefuata. Aliamua kuwa mnyenyekevu mbele za Mungu.
Kilichofuata, Joseph alichagua kumuuliza Mungu. Alisali kwa imani kwamba Mungu angemjibu. Jibu lilikuja wakati akiwa bado ni mvulana mdogo. Ujumbe huo ulikuja wakati alihitaji kujua ni kwa namna gani Mungu angetaka Kanisa Lake lianzishwe. Roho Mtakatifu alimfariji na kumuongoza katika maisha yake yote.
Alitii msukumo wakati ilipokuwa vigumu. Kwa mfano, alipokea mwongozo kuwatuma Kumi na Wawili Uingereza wakati alikuwa akiwahitaji sana. Aliwatuma.
Alikubali masahihisho na faraja kutoka kwa Roho wakati alipokuwa gerezani na Watakatifu walikuwa wakiteswa vibaya. Na alikubali alipokwenda katika njia kuelekea Carthage japokuwa alijua alikabiliwa na hatari.
Nabii Joseph aliweka mfano kwetu sote wa jinsi ya kupokea mwongozo endelevu wa kiroho na faraja kupitia Roho Mtakatifu
Uchaguzi wa kwanza alioufanya ni wa kuwa mnyenyekevu mbele za Mungu.
Wa pili ulikuwa ni kusali kwa imani katika Bwana Yesu Kristo.
Wa tatu ulikuwa ni kutii kwa usahihi. Utiifu unaweza kumaanisha kwenda haraka. Unaweza kumaanisha kujiandaa Au unaweza kumaanisha kusubiri kwa uvumilivu kwa ajili ya mwongozo zaidi.
Na wa nne ni kusali kujua mahitaji na mioyo ya wengine na jinsi gani ya kuwasaidia kwa niaba ya Bwana. Joseph alisali kwa ajili ya watakatifu katika dhiki wakati alipokuwa gerezani. Imekuwa ni fursa kwangu ya kuwaona manabii wa Mungu wakisali, wakiuliza mwongozo, wakipokea mwongozo na kuufanyia kazi.
Nimeona kila mara jinsi gani sala zao ni kwa ajili ya watu ambao wanawapenda na kuwatumikia. Wasiwasi wao kwa ajili ya wengine huonekana kufungua mioyo yao ili kupokea msukumo wa kiungu. Hiyo inaweza kuwa kweli kwenu.
Msukumo wa kiungu unatatusaidia kuwahudumia wengine kwa ajili ya Bwana. Mmeona hivyo katika uzoefu wenu, kama vile nilivyoona. Askofu wangu wakati mmoja aliniambia—wakati mke wangu akiwa katika maumivu makali katika maisha yake—Kila mara niliposikia kuna mtu kwenye kata anahitaji msaada, nilipofika pale kusaidia, nilikuta kwamba mke wako alikuwa ameshafika kabla yangu. Anawezaje kufanya hivyo vipi?
Yeye ni kama wale wote ambao ni wahudumu wakuu katika ufalme wa Mungu. Inaoneka kuna vitu viwili wanafanya. Wahudumu wakuu wamestahiki ushirika wa Roho Mtakatifu kwa karibu kabisa kama mwenzi wa wa muda wote. Na wamestahiki zawadi ya hisani, ambayo ni upendo msafi wa Kristo. Zawadi hizi zimekuwa ndani yao walipokuwa wakizitumia katika kuhudumu kwa upendo kwa ajili ya Bwana.
Njia ambayo sala, msukumo wa kiungu, na upendo wa Bwana hufanya kazi kwa pamoja katika huduma zetu kwangu mimi imeelezwa kikamilifu katika maneno haya:
“Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.
“Kama wanipenda, shika amri zangu.
“Na nitamwomba Baba, naye atawapa Mfariji mwingine, ili aweze kuwa nayi daima;
“Hata Roho wa kweli, ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa sababu hawamwoni, wala kumjua: ila ninyi mnamjua; kwani anakaa ndani yenu, na atakuwa nanyi.”
“Sitawaacha ninyi yatima: Naja kwenu.”
“Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona: Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai.
“Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu.
“Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye: naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda, na kujidhirihisha kwake” (Yohana 14:14–21).
Ninatoa ushuhuda wangu binafsi kwamba Baba katika wakati huu anawajua, hisia zenu, na mahitaji ya kimwili na kiroho ya kila mtu anayewazunguka. Ninatoa ushuhuda kwamba Baba na Mwana wanamtuma Roho Mtakatifu kwa wote ambao wana hii zawadi, omba kwa ajili ya baraka hiyo, na tafuta kuwa mwenye kustahiki hilo. Si Baba, wala Mwana, wala Roho Mtakatifu hulazimisha kuwa katika maisha yetu. Tuko huru kuchagua. Bwana amesema kwa wote:
“Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; kama mtu yeyote ataisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
“Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.
“Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa” (Ufunuo 3:20–22).
Ninasali kwa moyo wangu wote kwamba mtasikia sauti ya Roho, ambayo inatumwa kwenu kwa ukarimu. Na ninasali kwamba daima mtafungua mioyo yenu Kumpokea. Kama mtauliza kwa nia ya dhati na kwa imani katika Yesu Kristo kwa ajili ya msukumo wa kiungo, mtaupokea katika njia ya Mwokozi na katika muda Wake. Mungu alifanya hivyo kwa kijana Joseph Smith. Anafanya hivyo hata leo nabii wetu anyeishi, Rais Russell M. Nelson. Amekuweka wewe katika njia ya watoto wengine wa Mungu kuwahudumia kwa niaba Yake. Najua kwamba si tu kwa kile ambacho nimeona kwa macho yangu lakini kwa nguvu zaidi ni kwa kile ambacho Roho amenong’oneza katika moyo wangu
Nimehisi upendo wa Baba na wa Mwanawe Mpendwa kwa ajili ya watoto wote wa Mungu katika dunia na watoto Wake katika ulimwengu wa kiroho. Nimehisi faraja na mwongozo wa Roho Mtakatifu. Ninasali kwamba muwe na shangwe ya kuwa na Roho pamoja nanyi kama mwenzi daima. Katika jina la Yesu Kristo, amina.