2010–2019
Zi Wapi Funguo na Mamlaka ya Ukuhani?
Aprili 2016


14:6

Zi Wapi Funguo na Mamlaka ya Ukuhani?

Mamlaka na funguo za ukuhani huwasha injini, hufungua milango ya mbinguni, na kutayarisha njia ya maagano ya kurudi kwa Baba wa Mbinguni.

Wakati jua la alasiri ya majira ya baridi lilipotelea nyuma ya kilima kikubwa cha kuteleza kilichofunikwa na theluji, hewa ya mlima ya kugandisha ilitupiga vikali mashavuni na mapuani, ikionekana kama bawabu mkali kwetu akituelekeza twende kwenye magari yetu katika maegeshoni ya hoteli ya watelezaji. Pale kwenye faraja ndani ya magari yetu vikanza vya joto punde vingepasha joto vidole vyetu vya mikono na miguu vilivyokuwa baridi. Sauti ya theluji iliyoganda iliyosikika na kila hatua tuliyochukua ilidhibitisha kwamba hii ilikuwa baridi iliyokithiri.

Familia yetu ilikuwa imestarehe siku iliyojawa na furaha kwenye vilima vya kuteleza, na sasa ilikuwa inafikia tamati yenye baridi mno. Tulipofika kwenye gari, nilitafuta funguo mfukoni mwa koti langu na kisha katika mfuko mwingine na mwingine. Zi wapi funguo? Kila mtu alikuwa akisubiri funguo kwa hamu! Betri ilikuwa na moto, na kila mfumo—pamoja na vikanza—vilikuwa tayari, lakini bila funguo, milango iliyofungwa haingeturuhusu kuingia; bila funguo injini haingetoa nguvu kwa gari.

Kwa wakati huo, lengo letu la kimsingi lilikuwa ni namna ambayo tungeweza kuingia garini na kupata joto, lakini singeweza kujizuia kufikiria—hata hivyo—kunaweza kuwa na somo hapa. Bila funguo, muujiza huu wa ajabu wa uhandisi ulikuwa ni kama plastiki na chuma tu. Hata kama gari lilikuwa na uwezo mkubwa, bila funguo, halingeweza kutekeleza kazi ya lengo lake.

Ninavyozidi kutafakari tukio hili, ndivyo mlinganisho huu umekuwa wa kina sana kwangu. Ninastaajabia upendo wa Baba wa Mbinguni kwa watoto Wake. Ninashangazwa na ziara ya mbinguni na maono makuu ya milele ambayo Mungu alimpatia Joseph Smith. Na hasa, moyo wangu umejazwa na shukrani nyingi kwa urejesho wa mamlaka ya ukuhani na funguo za ukuhani. Bila urejesho huu, tungefungiwa nje ya gari ambalo lingeweza kutusafirisha katika safari yetu kuelekea nyumbani kwa wazazi wetu wapendwa wa mbinguni. Utendaji wa kila agizo la wokovu ambayo ni njia yetu ya agano kurudi katika uwepo wa Baba wa Mbinguni huhitaji uongozi unaofaa kupitia funguo za ukuhani.

Mnamo Mei 1829, Yohanna Mbatizaji aliwatokea Joseph Smith na Oliver Cowdery, akatawaza juu yao Ukuhani wa Haruni na kuwapa funguo zinazohusika na ukuhani huo. Na muda mfupi baadaye, Petro Yakobo, na Yohana walitawaza juu yao Ukuhani wa Melkizedeki na funguo zinazohusika nao.1

Karibu miaka saba baadaye Jumapili katika Hekalu la Kirtland, wiki moja tu baada ya kuwekwa wakfu, “Bwana Yehova atokea katika utukufu” kwake Joseph na Oliver, tukio likifuatiwa na kutokea kwa Musa, Elia, na Eliya, ambao walikabidhi “funguo za nyakati zao.”2 Mamlaka ya ukuhani na hizi funguo zilizorejeshwa zilikuwa zimepotea kwa karne nyingi. Katika njia sawa ambavyo familia yangu ilifungiwa nje ya gari kutokana na funguo zilizopotea, hivyo pia ndivyo watoto wote wa Baba wa Mbinguni walikuwa wamefungiwa nje kutokana na maagizo ya wokozi ya injili ya Yesu Kristo—hadi wakati ambapo urejesho mtakatifu ulifanyika na hawa wajumbe kutoka mbinguni. Kamwe, tena hatuhitaji kuuliza, “Zi wapi funguo?”

Eneo la Urejesho wa Ukuhani
Mto Susquehanna

Kwenye siku njema majira ya majani kupukutika mwaka jana, niliutembelea msitu mzuri mtulivu ulio kaskazini mashariki mwa Pennsylvania, ijulikanayo katika maandiko kama Harmony, ambapo Yohana Mbatizaji aliwatokea Joseph Smith na Oliver Cowdery na kurejesha Ukuhani wa Haruni. Pia nilisimama kwenye kingo za Mto Susquehanna ambapo Joseph na Oliver, wakiwa wamepewa mamlaka na funguo, walibatizwa. Karibu na mto huu, Petro Yakobo, na Yohana walitokea na kurejesha Ukuhani wa Melkizedeki na funguo zinazohusika nao.3

Nyumba ya Joseph and Emma Smith
Ndani ya kituo cha wageni cha eneo la urejesho wa Ukuhani
Nje ya kituo cha wageni cha eneo la urejesho wa Ukuhani

Maeneo haya, pamoja na nyumba kwanza ya Joseph na Emma iliyojengwa upya, ambapo sehemu kubwa ya Kitabu cha Mormoni kilitafsiriwa; nyumba iliyoko karibu ya wazazi wake Emma; na kituo cha wageni, kilichounganishwa kuwa jumba jipya la mikutano; ndiyo Eneo jipya la Urejesho wa Ukuhani, lililowekwa wakfu na Rais Russell M. Nelson mnamo Septemba mwaka uliopita. Pale, nilihisi nguvu na ukweli wa matukio ya mbinguni ambayo yalifanyika kwenye ardhi hiyo takatifu. Tukio hilo lilinisababisha kutafakari, kusoma, na kusali kuhusu mamlaka ya ukuhani na funguo za ukuhani, ambapo ilinipa hisia ya kutaka kushiriki na wavulana na wasichana wa Kanisa jinsi mamlaka ya ukuhani na funguo zilizorejeshwa zinaweza kuwabariki.

Kwanza, kuelewa kwa istilahi hizi kunaweza kuwa kwa manufaa. Ukuhani au mamlaka ya ukuhani imefafanuliwa kama “uwezo na mamlaka ya Mungu”4 na “nguvu kamilifu duniani humu.”5 Funguo za ukuhani zimefafanuliwa kwa kuelewa kwetu pia: “Funguo za ukuhani ni mamlaka ambayo Mungu amewapa viongozi wa ukuhani kuongoza, kudhibiti, na kutawala matumizi ya ukuhani wake duniani.”6 Funguo za ukuhani hudhibiti matumizi ya mamlaka ya ukuhani. Maagizo ambayo husababisha kuwepo kwa rekodi Kanisani yanahitaji funguo na hayawezi kufanyika bila idhini. Mzee Dallin H. Oaks alifundisha kwamba “hatimaye, funguo zote za ukuhani zinashikiliwa na Bwana Yesu Kristo, ambaye ndiye mwenye ukuhani. Ni yeye aamuaye funguo gani zitatolewa kwa wanadamu na jinsi gani funguo hizo zitatumika.”7

Na sasa kwenu nyinyi wavulana na wasichana, nimezingatia njia tatu ambazo mwaweza “kupata funguo” au kutumia funguo za ukuhani na mamlaka kubariki maisha yenu na maisha ya wengine.

Ya kwanza ni Kujiandaa kwa Huduma ya Umisionari

Ndugu na dada zangu vijana, mnaweza kukosa kugundua, lakini funguo za kukusanyika kwa Israeli zilizorejeshwa na Musa zinawezesha utendaji wa kazi ya umisionari katika kipindi chetu. Hebu fikiria, mwishoni wa mwaka wa 2015, wamisionari 74,000 walikuwa wakifanya kazi chini ya uongozi wa funguo hizi. Na haya akilini, kumbuka kwamba si mapema sana kujitayarisha kwa huduma ya umisionari. Katika Kwa Nguvu ya Vijana, tunasoma, Wavulana wa Ukuhani wa Haruni, … fanyeni bidii mjiandae kumwakilisha Bwana kama mmisionari.”8 Wasichana waweza pia kujiandaa, lakini nyinyi, “hamko chini ya jukumu sawa la kuhudumu.”9 Maandalizi yenu yote, hata hivyo, ikiwa mtahudumu kama wamisionari au la, yatakupa faida katika maisha yako yote kama mshiriki mmisionari.

Njia ya pili ya “Kupata funguo” Ni Kuhudhuria Hekalu

Funguo za kuunganisha zilizorejeshwa na nabii wa Agano la Kale zinawezesha utendaji wa maagizo katika mahekalu matakatifu. Maagizo yanayofanyika katika mahekalu haya yanawezesha watu binafsi na familia kurudi katika uwepo wa wazazi wa mbinguni.

Tunawahimiza nyinyi wavulana na wasichana kufanya utafiti na kupata majina ya mababu zenu na kufanya ubatizo kwa niaba yao hekaluni. Tunaona kwamba haya yanafanyika kwa idadi kubwa na ambayo haijawahi kufanyika kote ulimwenguni! Mahali pa kubatizia katika mahekalu mengi huwa pamefurika na wavulana na wasichana mapema asubuhi na hadi usiku. Funguo zimegeuzwa ambazo zinawezesha familia kuunganishwa wakati maagizo matakatifu yanafanyika mahekaluni.

Mnaweza kuona uhusiano kati ya funguo na baraka za ukuhani? Wakati mnapohusika katika kazi hii, ninafikiri mtapata kwamba Bwana yuko ndani yake. Kuna tukio linaloonyesha hili. Hivi majuzi nilikuja kujua kumhusu mama ambaye mara kwa mara husindikiza watoto wake hekaluni kufanya ubatizo wa niaba. Siku hii hasa, wakati hii familia ilikamilisha ubatizo wao na walikuwa wakiondoka hekaluni, mwanaume aliingia mahali pa ubatizo na orodha ndefu ya majina ya familia yake. Ilipogunduliwa kuwa hapakuwepo na mtu yeyote mahala pa ubatizo kutoa usaidizi na majina haya, mfanyikazi wa hekalu aliifikia familia iliyokuwa ikiondoka na kuwauliza watoto ikiwa wangeweza kurudi na kubadilisha mavazi tena ili kutoa usaidizi kwa ubatizo huu. Kwa hiari yao walikubali na kurudi ndani. Wakati watoto walipofanyiwa ubatizo, mama yao, akisikiliza, alianza kutambua majina na punde, kwa mshangao wa wote, aligundua kwamba orodha ya majina ya mwanaume huyu ilikuwa ni mababu walioaga wa familia yake pia. Rehema tamu na ororo kwao.

Wiki mbili zilizopita Hekalu la Provo City Center liliwekwa wakfu kama hekalu la 150 la Kanisa linalofanya kazi duniani kote. Tunakumbuka kuwa wakati Rais Thomas S. Monson aliidhinishwa kama Mtume mwaka wa 1963, kulikuwepo na mahekalu 12 yaliyokuwa yakifanya kazi Kanisani. Mahekalu yanasongea karibu na karibu zaidi pale mlipo. Hata hivyo, kwa wale wenu ambao mnaishi mahali ambapo umbali au hali hairuhusu kuhudhuria hekalu kila mara, mnafaa kuwa wastahiki wa kuhudhuria siku zote. Mnaweza kufanya kazi muhimu nje ya mahekalu mnapofanya utafiti na kuwasilisha majina ya wanafamilia.

Hatimaye, Nambari Tatu: Songa Mbele kwa Imani

Nabii wa Agano la Kale Ibrahimu alipokea baraka kuu kutoka kwa Bwana katika kipindi chake, mara nyingine huitwa Agano la Ibrahimu. Maelfu ya miaka baadaye, baraka za maongozi ya Mungu ya injili kwake Ibrahimu zilirejeshwa. Hili lilifanyika wakati ambapo nabii Elia alimtokea Joseph Smith na Oliver Cowdery katika Hekalu la Kirtland.

Kupitia urejesho huu, kila mmoja wetu ana fursa ya kupokea baraka kuu alizoahidiwa Ibrahimu. Baraka Hizi zinaweza kuwa zako ikiwa utasalia kuwa mwaminifu na kuishi kwa ustahiki. Katika kijitabu Kwa Nguvu za Vijana, Mnapatiwa mafundisho yanayowawezesha “kusonga mbele kwa imani.” Ninatoa muhtasari wa baadhi ya ushauri huo: “Ili kukusaidia kuwa kila kitu ambacho Bwana angependa uwe, piga magoti kila asubuhi na usiku kwa maombi kwa Baba yako wa Mbinguni. … Soma maandiko kila siku na kutumia unayosoma maishani mwako. … Jitahidi kila siku kuwa mtiifu. … Katika hali zote, fuata mafundisho ya manabii. … Kuwa mnyenyekevu na tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu.”

Ushauri huu unafuatiwa na ahadi inayoelekeza kwa ahadi zinazokuja kupitia baraka za Ibrahimu. “Unapofanya vitu hivi, Bwana atatimiza mengi katika maisha yako kuliko unavyoweza peke yako. Ataongeza nafasi zako, kupanua maono yako, na kukuimarisha. Atakupa usaidizi unaohitaji kukabiliana na majaribio na changamoto zako. Utapata ushuhuda wa nguvu zaidi na furaha ya kweli unapokuja kumjua Baba yako wa Mbinguni na Mwana Wake, Yesu Kristo, na kuhisi upendo wao kwako.”10

Nikifanya muhtasari: jiandaeni kwa huduma ya umisionari, hudhurieni hekalu, na msonge mbele kwa imani.

Hitimisho

Acheni sasa tumalizie tulipoanzia, tukiwa tumekwama katika maegesho yenye baridi kali, “Zi wapi funguo?” Ijapokuwa, baadaye jioni hiyo kimiujiza nilipata funguo ambazo zilikuwa zimeanguka kutoka mfukoni huko mlima. Bwana ametuonyesha kwamba hatatuacha tukiwa tumesimama kwenye baridi iliyokithiri bila funguo au mamlaka kutuelekeza salama Kwake nyumbani.

Ikiwa wewe ni kama mimi, waweza kujipata katika maisha yako ya kila siku ukijiuliza, “ Zi wapi funguo za gari, ofisini, nyumbani au fleti? Wakati haya yananitendekea, siwezi kujizuia kutabasamu kwa undani, kwa vile ninavyotafuta funguo, ninajikuta nikitafakari kuhusu funguo za ukuhani za urejesho na kumhusu Rais Thomas S. Monson, ambaye tunamuidhinisha “kama nabii, mwonaji, na mfunuzi” na “kama mtu wa pekee juu ya dunia aliye na mwenye mamlaka ya kutumia funguo zote za ukuhani.”11 Ndio, funguo ziko salama, mikononi mwa manabii, waonaji, na wafunuzi. Zinatolewa, kuwakilishwa, na kupeanwa kwa wengine, kulingana na mapenzi ya Bwana, chini ya uongozi wa Rais wa Kanisa.

Ninashuhudia ya kwamba mamlaka ya ukuhani na funguo za ukuhani huwasha injini, hufungua milango ya mbinguni, zinawezesha nguvu za mbinguni, na kuandaa njia ya maagano ya kurudi kwa Baba wa Mbinguni mwenye upendo.

Ninaomba kwamba nyinyi, kizazi chipukizi cha wavulana na wasichana, “msonge mbele mkiwa na imani imara katika Kristo,”12 kwamba muweze kuelewa ni nafasi yenu takatifu kutenda chini ya uongozi wa wale wenye funguo za ukuhani ambazo zitawafungulia baraka, karama na nguvu za mbinguni.

Ninatoa ushuhuda kuhusu Mungu Baba, Mwokozi wetu na Mkombozi, Yesu Kristo, Roho Mtakatifu, na Urejesho wa injili katika hizi siku za mwisho, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Joseph Smith—History 1:68–72.

  2. Mafundisho na Maagano 110 sehemu ya muhtasari.

  3. Ona Mafundisho na Maagano 128:20.

  4. Kitabu cha Maelezo cha 2: Usimamizi wa Kanisa (2010), sura ya 8.

  5. Boyd K. Packer, “Priesthood Power in the Home” (worldwide leadership training meeting, Feb. 2012), lds.org/broadcasts; see also James E. Faust, “Power of the Priesthood,” Ensign, May 1997, 41–43.

  6. Kitabu cha Maelezo 2, 2.1.1.

  7. Dallin H. Oaks, “Funguo na Mamlaka ya Ukuhani,” Liahona, Mei 2014, 50.

  8. Kwa Nguvu za Vijana, (kijitabu, 2011), 43.

  9. Thomas S. Monson, “Karibuni Mkutanoni,” Liahona, Nov. 2012, 5.

  10. Kwa Nguvu za Vijana, 42–43.

  11. Ona fomu za Maafisa Walioidhinishwa zinazosomwa katika mikutano ya kata na kigingi inayofanyika kila mwaka.

  12. 2 Nefi 31:20.