Walipo Wawili au Watatu Waliokusanyika Pamoja
Kama utasikiliza kwa Roho, utaona moyo wako umelainishwa, imani yako imeimarishwa, na uwezo wako wa kumpenda Bwana umeongezeka.
Wapendwa wangu ndugu na akina dada, ninawakaribisheni kwenye Mkutano Mkuu wa 186 wa Mwaka wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Mimi ninafurahia pamoja nanyi, na ninawakaribisheni kwa moyo mkujufu.
Ninashukuru kuwa mmekuja kwenye Mkutano Mkuu kuhisi mvuto kutoka mbinguni na kujisikia karibu zaidi na Baba yetu wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo.
Waliokusanyika katika mkutano huu, ulioenea ulimwenguni kote, ni mamilioni ya wafuasi wa Yesu Kristo ambao wako kwenye maagano ya daima kumkumbuka na kumtumikia. Kwa miujiza ya tekinolojia ya kisasa, utengano wa muda na umbali mkubwa unatoweka. Tunakutana kama kwamba sisi sote tupo pamoja katika ukumbi mmoja mkubwa.
Lakini hata hivyo cha muhimu zaidi kuliko kukutana kwetu pamoja ni katika jina la nani tunafanya hivyo. Bwana aliahidi kwamba hata pamoja na idadi kubwa ya wafuasi Wake duniani leo, atakuwa karibu na kila mmoja wetu. Alisema kwa kikosi Chake kidogo cha wafuasi mwaka 1829, “Amini, amini, ninawaambia, …Walipo wawili au watatu waliokusanyika pamoja katika lina langu, … tazama, mimi nitakuwa katikati yao—hata sasa nipo katikati yenu” (M&M 6:32).
Wakiwa na idadi zaidi ya moja au mbili, umati wa wafuasi Wake umekusanyika katika mkutano huu mkuu, na kama ilivyoahidiwa, Bwana yupo katikati yetu. Kwa sababu Yeye ni kiumbe aliyefufuka, na Yeye aliyetukuka hayupo kimwili kila sehemu ambapo Watakatifu wamekusanyika. Lakini, kwa uwezo wa Kiroho, tunaweza kuhisi kwamba yupo hapa pamoja nasi leo.
Wapi na lini tunahisi ukaribu wa Mwokozi inategemea na kila mmoja wetu. Alitoa maelekezo haya:
“Na tena, amini ninawaambia, marafiki zangu, ninayaacha maneno haya kwenu kwenu ili muyatafakari katika mioyo yenu, pamoja na amri hii ambayo ninatoa kwenu, kwamba mtanilingana maadamu Mimi nipo karibu—
“Sogeeni karibu nami na mimi nitasogea karibu na nyinyi, nitafuteni kwa bidii nanyi mtanipata; ombeni, nanyi mtapewa, bisheni, nanyi mtafunguliwa” (M&M 88:62–63).
Nawajua angalau watu wawili wanaosikiliza leo wanaotaka baraka hiyo kwa mioyo yao yote. Watajitahidi kwa dhati kuja karibu zaidi kwa Bwana wakati wa mkutano huu mkuu. Kila mmoja wao aliniandikia—barua zao zikifika ofisini kwangu wiki hiyo hiyo—wakisihi kwa msaada aina hiyo hiyo.
Wote wawili ni waongofu wa Kanisa na hivi majuzi walipokea ushuhuda wa wazi wa upendo wa Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo, Mwokozi wa ulimwengu. Walijua kwamba Nabii Joseph Smith aliasisi Kanisa kwa ufunuo wa moja kwa moja kutoka kwa Mungu na kwamba funguo za ukuhani mtakatifu zilirejeshwa. Kila mmoja alihisi ushahidi kwamba funguo zipo katika Kanisa leo. Walinitolea ushuhuda wao wa dhati katika maandishi.
Hata hivyo wote walisikitika kwamba hisia za upendo kwa Bwana na upendo Wake kwao ulikuwa unapungua. Wote wawili walitaka, kwa moyo wote, mimi niwasaidie kupata tena furaha na hisia ya kupendwa ambayo ilikuwa yao walipokuja kwenye ufalme wa Mungu. Wote wawili walionyesha woga kwamba kama wasingeweza kupata kikamilifu hisia hizo za upendo kwa Mwokozi na Kanisa Lake, majaribu na majaribio waliyokabiliana nayo hatimaye yatashinda imani yao.
Hawapo pekee yao katika shaka yao, wala majaribu sio mapya. Wakati wa huduma Yake duniani, Mwokozi alitupa mfano wa mbegu na mpanzi. Mbegu ilikuwa ni neno la Mungu. Mpanzi alikuwa Bwana. Kuokoka kwa mbegu na kukua kwake kulitegemea na hali ya udongo. Unakumbuka maneno Yake.
“Na alipokuwa akipanda, mbega nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila:
“Nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina:
“Na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka.
“Na nyingine zikaanguka penye miiba; na ile miiba ikamea, ikazisonga:
“Lakini nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini.
“Mwenye masikio na asikie” (Mathayo 13;4–9).
Tena, mbegu ni neno la Mungu. Udongo ni moyo wa mtu anayepokea mbegu.
Sisi sote tuna mengi yaliyo sawa na hawa watu wa ajabu walioniandikia wakiomba msaada na hakikisho. Sisi sote tulikuwa na mbegu, au neno la Mungu, lililopandwa katika mioyo yetu wakati fulani. Kwa baadhi, ilikuwa utotoni wakati wazazi wetu walituita tubatizwe na kuthibitishwa na wale wenye mamlaka. Wengine kati yetu walifundishwa na watumishi walioitwa wa Mungu. Kila mmoja alihisi kwamba mbegu ilikuwa nzuri, hata kuhisi uvimbe katika mioyo yetu, na tukapata furaha wakati mioyo yetu na akili ilionekena kupanuka.
Sisi sote tumekuwa na imani zilizojaribiwa na baraka zilizocheleweshwa za thamani kuu, mashambulizi makali ya wale waliotaka kuharibu imani yetu, majaribu ya kufanya dhambi, na uchoyo wa kibinafsi ambao unapunguza juhudi zetu za kukuza na kulainisha vina vya kiroho vya mioyo yetu.
Wale ambao wamehuzunishwa na kupotelewa na furaha waliyokuwa nayo wakati mmoja ndio wabarikiwa. Wengine hawaoni kunyauka kwa imani ndani yao wenyewe. Shetani ni mjanja. Anawaambia wale anaotaka wawe na dhiki kwamba furaha waliohisi mwanzo ilikuwa ni kujidanganya.
Leo ujumbe wangu kwetu sote ni kwamba kutakuwa na nafasi ya thamani katika siku chache zijazo kuchagua kuwa na mioyo iliyolainishwa na kupokea na kurutubisha mbegu. Mbegu ni neno la Mungu, na itamwagwa juu yetu sote tunaosikia, kutazama na kusoma mchakato wa mkutano mkuu huu. Muziki, hotuba, na shuhuda zimeandaliwa na watumishi wa Mungu waliomtafuta kwa bidii Roho Mtakatifu kuwaongoza katika maandalizi yao. Wamesali kwa muda mrefu na kwa unyenyekevu mwingi wakati siku za mkutano mkuu zimekaribia.
Wamesali kuwa na uwezo wa kukushawishi wewe kufanya chaguzi ambazo zitajenga katika moyo wako udongo wenye rotuba kwa ajili ya neno zuri la Mungu kukua na kuzaa matunda. Kama utasikiliza kwa Roho, utaona moyo wako umelainishwa, imani yako imeimarishwa, na uwezo wako wa kumpenda Bwana umeongezeka.
Uchaguzi wako wa kuomba kwa nia kamilifu ya moyoni utageuza uzoefu wako katika vikao vya mkutano mkuu na katika siku na miezi inayofuata.
Wengi wenu tayari wameshaanza. Mwanzoni mwa kikao hiki, hamkusikiliza tu sala; bali mliongeza imani yenu kuomba kwamba tutafurahia baraka za Roho Mtakatifu kumwagwa juu yetu. Wakati mlipoongeza kusihi kwenu kimya kimya katika jina la Yesu Kristo, mlimkaribia Yeye zaidi. Huu ni mkutano Wake mkuu. Ni Roho Mtakatifu pekee anayeweza kuleta baraka ambazo Bwana anatamani kwa ajili yetu. Katika upendo Wake kwetu sisi, Ameahidi tunaweza kuhisi hivyo:
“Na lolote watakalolisema wakati wanaongozwa na Roho Mtakatifu litakuwa andiko, litakuwa ni mapenzi ya Bwana, litakuwa nia ya Bwana, litakuwa ni neno la Bwana, litakuwa ni sauti ya Bwana, na ni uweza wa Mungu hata kwa wokovu.
“Tazama, hii ni ahadi ya Bwana kwenu, Enyi watumishi wangu.
“Kwa hiyo, changamkeni, na msiogope kwani mimi Bwana nipo pamoja nanyi, na nitasimama karibu yenu; nanyi mtanishuhudia, hata Yesu kristo, kuwa mimi ndimi Mwana wa Mungu aliye hai, kwamba nilikuwepo, kwamba nipo, na kwamba nitakuja”(M&M 68:4–6).
Mnaweza kuomba na kuongeza imani yenu kila wakati mtumishi wa Mungu anapokaribia mimbari ili ahadi ya Bwana katika mafundisho na maagano sehemu ya 50 itimizwe.
“Amini ninawaambia, yule aliyetawazwa na mimi na kutumwa kwenda kilihubiri neno la kweli kwa njia ya Mfariji, katika Roho wa kweli, je, afundisha kwa Roho wa kweli au kwa njia nyingine?
“Na kama itakuwa kwa njia nyingine hatokani na Mungu.
“Na tena yule apokeaye neno la kweli, je, hulipokea kwa Roho wa kweli au kwa njia nyingine?
“Na kama itakuwa kwa njia ingine hatokani na mungu.
“Kwa hiyo, kwa nini kwamba hamwezi kuelewa na kujua, kwamba yule ambaye hulipokea neno kwa njia ya Roho wa kweli hulipokea kama vile lifundishwavyo na Roho wa kweli?
“Kwa sababu hiyo, yule ambaye huhubiri na yule apokeaye, huelewana, na wote hujengana na kufurahi kwa pamoja” (M&M 50:17–22).
Unaweza kuomba wakati kwaya inakaribia kuimba. Mkurugenzi wa kwaya, mpiga kinanda, na wana kwaya wameomba na kufanya mazoezi pamoja na sala katika mioyo yao na kwa imani kwamba muziki na maneno vitalainisha mioyo na kutukuza uwezo wao wa kujenga imani za wengine. Wataimba kwa ajili ya Bwana kama vile walikuwa mbele Yake, na watajua kwamba Baba wa Mbinguni anawasikiliza kwa uhakika kama anavyosikiliza sala zao binafsi. Pamoja wamefanya kazi kwa upendo kufanya ahadi ya mwokozi kwa Emma Smith iwe kweli: “Kwani nafsi yangu hufurahia katika nyimbo za moyoni; ndiyo, wimbo wa mwenye haki ni sala kwangu Mimi, nayo itajibiwa kwa baraka juu ya vichwa vyao” (M&M 25:12).
Kama husikilizi tu lakini pia unasali wanapoimba, sala yako na sala zao zitajibiwa na baraka juu ya vichwa vyenu na vyao vile vile. Utahisi baraka ya upendo wa Mwokozi na kukubalika. Wote wanaojiunga katika kusifu huku watahisi upendo wao Kwake unakua.
Unaweza kuchagua kusali wakati mzungumzaji anaonekana kukaribia kufikia mwisho wa ujumbe wake. Yeye atakuwa akisali kimoyomoyo kwa Baba ili Roho Mtakatifu ampe maneno ya ushuhuda ambayo yatainua mioyo ya wasikilizaji, matumaini, na matamanio ya daima kumkumbuka Mwokozi na kutii amri ambazo ametupa.
Ushuhuda hautakuwa ujumbe wa kurudiwarudiwa. Utakuwa ni uthibitisho wa sehemu ya ukweli kwamba Roho anaweza kupeleka kwenye mioyo ya wale watakaokuwa wanasali kuomba msaada, kwa maelekezo matakatifu, na kupokea upendo halisi wa Kristo.
Ushuhuda wa kweli utatolewa kwa wazungumzaji. Maneno yao yanaweza kuwa machache, lakini yatachukuliwa ndani ya mioyo ya wasikilizaji wanyenyekevu waliokuja kwenye mkutano mkuu wakiwa na njaa ya neno zuri la Mungu.
Ninajua kutoka kwa uzoefu kile imani ya watu wazuri inaweza kufanya kuleta maneno kutoka kwa Roho mwishoni mwa mahubiri. Zaidi ya mara moja, mtu fulani amesema kwangu baada ya ushuhuda wangu, “Ulijuaje nini nillihitaji sana kusikia?” Nimejifunza kutokushangazwa wakati siwezi kukumbuka kusema maneno hayo. Nilisema maneno ya ushuhuda, lakini Bwana alikuwa pale, akinipa mimi wakati ule ule. Ahadi kwamba Bwana atatupa sisi maneno wakati ule ule tunapoyahitaji kuyatumia hususani kushuhudia (ona M&M 24:6). Sikiliza kwa makini shuhuda zinazotolewa katika mkutano huu mkuu—utajihisi karibu sana na Bwana.
Unaweza kuhisi kwamba ninakuja kwenye wakati ambao nitafunga ujumbe niliojaribu kuuleta pamoja na ushuhuda wa ukweli. Sala zenu zitanisaidia mimi kupewa maneno ya ushuhuda ambao unaweza kusaidia mtu fulani anayetamani jibu kwa maswali yake.
Nawaachia ushahidi wangu wa hakika kwamba Baba yetu wa Mbinguni, Elohim mkuu, anatupenda na anatujua, kila mmoja. Chini ya maelekezo Yake, Mwanawe, Yehova, alikuwa Muumbaji. Ninashuhudia kwamba Yesu wa Nazareti alizaliwa Mwana wa Mungu. Aliponya wagonjwa, vipofu waliona, na alifufua wafu. Alilipa gharama ya dhambi zote za kila mmoja wa watoto wa Baba wa Mbinguni waliozaliwa duniani. Alivunja minyororo ya kifo kwa wote wakati alipoinuka kutoka kaburini Jumapili ile ya kwanza ya Pasaka. Yu hai leo, Mungu—aliyefufuka na kutukuka.
Hili ni Kanisa la kweli pekee, na Yeye ni jiwe kuu la pembeni. Thomas S. Monson ni nabii Wake kwa ulimwengu mzima. Manabii na mitume mtakaowasikia katika mkutano huu mkuu wananena kwa niaba ya Mungu. Wao ni watumishi Wake, walioruhusiwa kufanya kazi kwa ajili Yake. Anatangulia mbele yao watumishi Wake ulimwenguni. Haya mimi ninajua. Na hivyo ninatoa ushahidi katika jina Lake, hata jina Lake takatifu Yesu Kristo, amina.