Viongozi Wakuu Ni Wafuasi Wakuu
Kutakuwa na wakati ambapo njia iliyoko mbele yako itakuwa na giza, lakini endelea kumfuata Mwokozi. Yeye anajua njia; hakika, Yeye ndiye njia.
Nilipokuwa na umri wa miaka 12, baba yangu alinichukua kwenda kuwinda milimani. Tuliamka saa 9:00 alfajiri, tukaweka matandiko migongoni mwa farasi wetu, na tukaanza safari yetu kuelekea mlimani palipokuwa na msitu na katika giza totoro. Hata jinsi nilivyopenda kuwinda na baba yangu, kwa wakati huo nilijihisi kidogo nikiwa na wasiwasi. Sijawahi kufika katika milimani hii mbeleni, na sikuweza kuona njia—au kwa kweli chochote kinginecho! Kitu pekee nilichoweza kuona ilikuwa ni mwangaza wa tochi ndogo ambayo baba yangu alikuwa ameibeba ilipokuwa ikimulika mwangaza hafifu kwenye misonobari iliyokuwa mbele yetu. Kama farasi wangu angeteleza na kuanguka—angeweza hata kuona alipokuwa akielekea? Lakini wazo hili lilinifariji: “Baba anajua anapokwenda. Nikimfuata, kila kitu kitakuwa sawa.”
Na kila kitu kilikuwa sawa. Hatimaye jua lilichomoza, na tukawa na wakati mzuri pamoja. Tulipoanza kuelekea nyumbani, baba yangu alinionyesha kilele kikuu, chenye mwinuko mkali ambacho kilijitokeza miongoni mwa vingine. “Ile ni Windy Ridge,” alisema. “Pale ndipo pana uwindaji mzuri.” Mara moja nilijua kwamba nilitaka kurudi na kakwea Windy Ridge siku moja.
Katika miaka iliyofuata, mara nyingi nilimsikia baba akizungumza kuhusu Windy Ridge, lakini hatukuwahi rudi—hadi siku moja, miaka 20 baadaye, nilimpigia simu baba yangu na nikasema, “Twende Windy.” Kwa mara nyingine tena tulitandika tandiko juu ya farasi wetu na tukaanza kukwea pande za mlimani. Sasa nilikuwa mpanda farasi mwenye uzoefu nikiwa katika miaka yangu ya 30, lakini bado nilishangaa kuona kuwa nina wasiwasi ule ule jinsi nilivyohisi nilipokuwa mvulana wa miaka 12. Lakini baba yangu alijua njia, na mimi nilimfuata.
Hatimaye tulifika kileleni mwa Windy. Mandhari yalikuwa ya kupendeza mno, na hisia niliyokuwa nayo zaidi ilikuwa kwamba nilitaka kurudi tena—sio tu kwa manufaa yangu safari hii, bali kwa manufaa ya mke wangu na watoto. Nilitaka wao pia wapate kujionea kile nilichokuwa nimejionea.
Kwa miaka mingi, nimekuwa na nafasi nyingi za kuwaongoza wanangu na wavulana wengine hadi kwenye vilele vya milima, kama vile tu baba yangu alivyoniongoza mimi. Matukio haya yalinisababisha kutafakari maana ya kuongoza—na maana ya kuwa mfuasi.
Yesu Kristo, Kiongozi Mkuu na Mfuasi Mkuu
Ikiwa ningekuuliza, “Ni nani kiongozi mkuu aliyewahi kuishi duniani?” Je ungesema nini? Jibu, bila shaka, ni Yesu Kristo. Yeye anatupa mfano kamili wa kila aina ya ubora tunaoweza kufikiria.
Lakini ikiwa ningekuuliza, “Ni nani mfuasi mkuu aliyewahi kuishi?” —si jibu lingekuwa tena ni Yesu Kristo? Yeye ni kiongozi mkuu kwa sababu Yeye ni mfuasi mkuu—Yeye humfuata Baba Yake kwa ukamilifu, katika kila jambo.
Dunia inafundisha kwamba viongozi ni lazima wawe wenye nguvu; Bwana anatufundisha kwamba ni lazima wawe wanyenyekevu. Viongozi wa dunia hupata nguvu na ushawishi kupitia vipaji vyao, ujuzi na mali. Viongozi walio kama Kristo hupata nguvu na ushawishi “kwa njia ya ushawishi, kwa uvumilivu, kwa upole na unyenyekevu, na kwa upendo usio unafiki.”1
Machoni pa Mungu, viongozi wakuu siku zote wamekuwa wafuasi wakuu.
Naomba mnikubalie nishiriki nanyi matukio mawili kutokana na maongezi na wavulana wa Kanisa ambayo yamenifundisha kuhusu kuongoza na kuwa mfuasi.
Sisi Sote Ni Viongozi
Hivi karibuni, mke wangu pamoja nami tulihudhuria mkutano wa sakramenti mbali na kata ya nyumbani. Kabla ya mkutano kuanza, mvulana mmoja alinijia na kuuliza ikiwa ningesaidia kupitisha sakramenti. Nilisema, “Itakuwa furaha yangu kufanya hivyo.”
Niliketi pamoja na mashemasi wengine na nikamuuliza yule ambaye alikuwa ameketi karibu nami, “Kazi yangu ni ipi?” Alinielezea kuwa nilipaswa kuanza kupitisha kutoka nyuma ya sehemu ya katikati ya chumba cha ibada na kuwa yeye angelikuwa katika sehemu hiyo hiyo kwa upande mwingine, na pamoja tungetekeleza kazi yetu hadi mbele.
Nilisema, “Sijafanya hivi kwa muda mrefu.”
Alijibu, “Ni sawa. Utaweza tu. Nilijisikia hivyo wakati nilipoanza.”
Baadaye, shemasi mwenye umri mdogo zaidi katika akidi, aliyetawazwa wiki chache tu zilizopita, alihutubia mkutano wa sakramenti. Baada ya mkutano wale mashemasi wengine walikusanyika kando yake ili kumwambia kwamba waliona fahari kwa ajili ya mshiriki wa akidi mwenzao.
Niligundua kwamba kila wiki washiriki wa akidi zote za Ukuhani wa Haruni katika kata ile waliwaendea wavulana wengine na kuwaalika kushiriki katika akidi zao.
Hawa wavulana wote walikuwa viongozi wakuu. Na ni wazi kwamba nyuma yao kulikuwa na usaidizi wa ajabu kutoka kwa wenye Ukuhani wa Melkizediki, wazazi, na wengine ambao waliwanasihi katika wajibu wao. Watu wazima wanaojali kama hawa huona wavulana sio tu jinsi walivyo sasa, bali pia jinsi wanavyoweza kuwa. Wakati wanapozungumza na wavulana au wanapozungumza juu yao, hawasisitizi kuhusu upungufu wao. Badala yake, wao husisitiza sifa za ubora mkuu wa uongozi wanaoonyesha.
Wavulana, hivi ndivyo Bwana anavyowaona. Ninawaalika ninyi mjione katika njia hii. Kutakuwa na wakati maishani mwenu ambapo mtapewa miito ya kuongoza. Wakati mwingine, mtategemewa kufuata. Lakini ujumbe wangu kwenu leo hii ni kwamba bila ya kujali mwito wako, wewe siku zote ni kiongozi, na wewe daima ni mfuasi. Uongozi ni onyesho la ufuasi—kiurahisi ni jambo la kuwasaidia wengine kwenda kwa Kristo, ambavyo ndiyo wafuasi wa kweli hufanya. Kama unajitahidi kuwa mfuasi wa Kristo, basi unaweza kusaidia wengine kumfuata Yeye na unaweza kuwa kiongozi.
Uwezo wako wa kuongoza hautokani na utu wako kijamii maumbile, ujuzi wa kuhamasisha, au hata kipaji cha kuzungumza hadharani. Unatokana na kujitoa kwako kuwa mfuasi wa Yesu Kristo. Unatokana na hamu yako kuwa, katika maneno ya Ibrahimu, “mfuasi mkubwa wa haki.”2 Ikiwa unaweza kufanya hivyo—basi wewe ni kiongozi
Huduma ya Ukuhani ni Uongozi
Wakati mwingine, nilikuwa kule New Zealand nikitembelea nyumbani kwa mama aliyekuwa mzazi pekee na vijana watatu. Mwana mkubwa alikuwa na miaka 18 na alikuwa amepokea Ukuhani wa Melkizediki Jumapili iliyokuwa imepita tu. Nilimwuliza ikiwa alikuwa ameweza kutumia ukuhani wake tayari. Alisema, “Sina uhakika hiyo inamaanisha nini.”
Nilimwelezea kwamba sasa alikuwa na mamlaka ya kutoa baraka za ukuhani kwa ajili ya faraja na uponyaji. Nilimtazama mama yake, ambaye hajapata kuwa na mtu mwenye Ukuhani wa Melkizediki kando yake kwa muda wa miaka mingi. “Ninafikiri itakuwa vyema sana,” nilisema, “ikiwa ungeweza kumbariki mama yako.”
Alijibu, “Sijui namna ya kufanya hivyo.”
Nilimweleza kwamba angeweza kuweka mikono yake kichwani mwa mama yake, ataje jina la mama yake, aseme kwamba anampa baraka kwa mamlaka ya Ukuhani wa Melkizediki, na aseme chochote ambacho Roho ataweka akilini na moyoni mwake, na afunge katika jina la Yesu Kristo.
Siku iliyofuata, nilipokea barua pepe kutoka kwake. Ilisema, kwenye sehemu fulani: “Usiku wa leo nilimbariki mama yangu!. … Nilijisikia wasiwasi, mkubwa sana na upungufu, kwa hiyo niliomba mfululizo kuhakikisha kwamba nilikuwa naye Roho, kwa sababu nisingeliweza kutoa baraka pasipo Roho Mtakatifu kuwa pamoja nami. Nilipoanza, nilijisahau kabisa na mapungufu yangu. … [sikutarajia] nguvu nyingi za kiroho na mhemko nilizohisi. … Baaaye roho wa upendo alinijia kwa nguvu sana hata singejizuia mhemko wangu, kwa hivyo nikamkumbatia mama yangu na kulia kama mtoto. … Hata sasa ninapoandika haya, [mimi nahisi] Roho [kwa wingi sana] kamwe staki kutenda dhambi tena. … Mimi naipenda injili.”3
Je si haya yanaleta msukumo kuona jinsi mvulana anayeonekana kuwa wa kawaida anaweza kutekeleza mambo makuu kupitia huduma yake ya ukuhani, hata wakati anapojiona mpungufu? Hivi karibuni nilikuja kufahamu kwamba mzee huyu kijana amepokea mwito wake wa misheni na ataingia katika kituo cha mafunzo ya umisionari mwezi ujao. Nina imani kwamba ataongoza nafsi nyingi kwake Kristo kwa sababu ameshajifunza jinsi ya kuwa mfuasi wa Kristo katika huduma yake ya ukuhani—kuanzia nyumbani kwake, ambapo mfano wake una ushawishi mkubwa kwa ndugu yake aliye na umri wa miaka 14.
Ndugu zangu, ikiwa tunatambua au la, watu wanatutazama sisi—wanafamilia, marafiki, hata wageni. Haitoshi kwetu sisi kama wenye ukuhani, kuja kwa Kristo; wajibu wetu sasa ni “kuwaalika wote waje kwa Kristo.”4 Hatuwezi kutosheka tu na kupokea baraka za kiroho kwa manufaa yetu; ni lazima tuwaongoze wale tuwapendao kuja kwenye baraka hizo hizo—na kama wanafunzi wa Yesu Kristo, ni lazima tumpende kila mtu. Amri ya Mwokozi kwa Petro pia ni amri kwetu sisi: “Nawe utakapoongoka, waimarishe ndugu zako.”5
Mfuate Yule Bwana wa Galilaya
Kutakuwa na wakati ambapo njia iliyoko mbele yako itakuwa na giza, lakini endelea kumfuata Mwokozi. Anaifahamu njia; kwa kweli, Yeye ndiye njia.6 Jinsi unavyozidi kujitahidi kuja Kwake Kristo, ndivyo utakavyohisi hamu ya kweli ya kuwasaidia wengine kujua yale ambayo wewe umeyajua. Neno lingine la hisia hii ni hisani, “ambayo [Baba] ametoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwanawe, Yesu Kristo.”7 Kisha utaona kwamba katika kile kitendo cha kumfuata Kristo, ni kwamba wewe unawaongoza wengine pia Kwake, kwani katika maneno ya Rais Thomas S. Monson, “Kadiri tunavyomfuata yule Bwana wa Galilaya—hata Bwana Yesu Kristo—ushawishi wetu wa kibinafsi utaonekana kwa wema popote tulipo, bila kujali miito yetu.”8
Ninashuhudia ya kuwa hili ni Kanisa la kweli la Kristo. Tunaongozwa na nabii wa Mungu, Rais Monson—kiongozi mkuu ambaye pia ni mfuasi wa kweli wa Mwokozi. Katika jina la Yesu Kristo, amina.