Atakubeba Mabegani Mwake na Kukupeleka Nyumbani
Lakini kama vile Mchungaji Mwema anavyomtafuta kondoo aliyepotea, kama tu utainua moyo wako kwa Mwokozi wa ulimwengu, Atakupata.
Moja ya kumbukumbu za utotoni mwangu zinaanza na mlio wa mbali wa king’ora cha mashambulizi ya hewani ulioniamsha toka usingizini. Muda mfupi baadaye, mlio mwingine, ukigongagonga na sauti za propella, ziliongezeka kidogo kidogo hadi zikatetemesha hewa. Kama vile mama yetu alivyotufundisha kufanya, sisi watoto kila mmoja alichukua mkoba ulioandaliwa na kukimbia juu ya kilima kwenye makao ya kijikinga na bomu. Tukiharakisha kwenda kwenye uwanja wenye giza, mwanga wa kijani na mweupe ulianguka toka angani kutimiza malengo ya mpiga mabomu. Cha ajabu, kila mtu aliuita mwanga huu mti wa Mkrismasi.
Nina umri wa miaka minne, na ninashuhudia vita katika ulimwengu.
Dresden
Si mbali kutoka pale familia yangu ilipoishi kulikuwa jiji la Dresden. Wale walioishi kule walishuhudia huenda mara elfu yale ambayo mimi niliyaona. Mioto mikubwa, iliyosababishwa na maelfu ya tani za vilipuzi, ilifagia Dresden, na kuharibu zaidi ya asilimia 90 ya jiji na kuacha kidogo isipokuwa tu vifusi na majivu walipoamka.
Kwa muda mfupi, jiji lililoitwa kwa jina la utani “Sanduku la Kito” halikuwepo tena. Erich Kästner, mwandishi wa Kijerumani, aliandika kuhusu uharibifu, “Katika miaka elfu uzuri wake ulijengwa, katika usiku mmoja ulibomolewa.”1 Wakati wa utoto wangu sikuweza kufikiria jinsi uharibifu wa vita ambao watu wetu wenyewe walianzisha ungeweza kushindwa. Ulimwengu uliotuzunguka ulionekana kuwa bila matumaini, bila ya mwelekeo.
Mwaka jana, nilipata nafasi ya kurudi Dresden. Miaka sabini baada ya vita, na, mara nyingine tena, jiji la “Sanduku la Kito.” Uharibifu umeondolewa, na jiji limerejeshwa na hata kuendelezwa.
Wakati wa ziara yangu nililiona kanisa zuri la Lutheran, Frauenkirche, Church of Our Lady. Kwanza lilijengwa miaka 1700, lilikuwa ni moja ya tunu ya kung’aa ya Dresden, lakini vita vikalisababisha kuwa rundo la vifusi. Kwa miaka mingi lilibaki hivyo, hadi pale ilipoamuliwa kwamba Frauenkirche litajengwa tena.
Bado kuna mawe kutoka kwenye kanisa lililoharibiwa yaliyohifadhiwa na kutunzwa, ilipowezekana, yalitumika tena kwenye ujenzi upya. Leo unaweza kuona nawe haya yaliyoungua moto yakioneka kwenye kuta za nje. Haya “makovu” siyo tu kumbusho la historia ya jengo hili bali pia kumbukumbu ya matumaini—ishara kubwa ya uwezo wa mtu wa kujenga maisha mapya kutoka kwenye majivu.
Nilipokuwa nikifakari historia ya Dresden na kushangaa ustadi na uamuzi wa wale waliorejesha jengo ambalo lilikuwa limeharibiwa, nilihisi uwepo mzuri wa Roho Mtakatifu. Hakika, nikafikiria, kama mtu anaweza kuchukua mabaki, vumbi, uharibifu wa jiji lililobomoka na kujenga upya jengo zuri ambalo linasimama kuelekea mbinguni, ni uwezo kiasi gani wa Baba Mwenyezi kuwarejesha watoto Wake walioanguka, wanaoangaika, au waliopotea?
Haijalishi ni kiasi gani maisha yetu yameharibiwa. Haijalishi dhambi zetu ni nyekundu kiasi gani, uchungu mkubwa kiasi gani, wapweke kiasi gani, kutelekezwa, au kuvunjika kwa mioyo yetu. Hata wale wasio na tumaini, waliokata tamaa, ambao walisaliti uaminifu, waliosalimisha heshima zao, au kumkufuru Mungu wanaweza kujengwa upya. Isipokuwa kwa wale wana wa mwovu, hakuna maisha ambayo yaliyobomolewa ambayo hayawezi kurejeshwa.
Habari njema za injili ni hizi: kwa sababu ya mpango wa furaha wa milele uliotolewa na Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo na kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo, hatuwezi tu kukombolewa toka kwenye anguko na kurejeshwa kwenye usafi, bali tunaweza pia kuvuka mawazo ya maisha ya kufa na kuwa warithi wa uzima wa milele na washiriki wa utukufu wa Mungu.
Fumbo la Kondoo Aliyepotea.
Kipindi cha utumishi wa Mwokozi, viongozi wa dini wa nyakati Zake hawakukubali Yesu kutumia muda na watu walioitwa “watenda dhambi.”
Huenda kwao ilionekana kama alikuwa anakubali au hata kuruhusu tabia ya dhambi. Huenda waliamini kwamba njia nzuri ya kuwasaidia watenda dhambi watubu ilikuwa ni kuwatuhumu, kuwacheka, na kuwaaibisha.
Wakati Mwokozi alipogundua nini Mafarisayo na waandishi wanafikiria, Alitoa historia fupi:
“Ni mtu wa namna gani, akiwa na kondoo mia, akigundua kwamba mmoja wao amepotea, hatawaacha wale tisini na tisa mbugani, na kwenda kumtafuta yule aliyepotea hadi ampate?
“Akimpata atambeba begani kwa furaha.”2
Kwa karne nyingi, fumbo hili limetafsiriwa kama wito wa matendo kwa ajili ya sisi kumrudisha kondoo aliyepotea na kuwafikia wale waliopotea. Huku hili likiwa sahihi na jema, nashangaa kama kuna la zaidi ya hapo.
Inawezekana kwamba malengo ya Yesu, kwanza na zaidi, ni kufundisha kuhusu kazi ya Mchungaji Mwema?
Inawezekana kwamba Alikuwa anashuhudia upendo wa Mungu kwa watoto Wake?
Inawezekana kwamba ujumbe wa Mwokozi ulikuwa kwamba Mungu anawajua wale waliopotea—na kwamba Atawatafuta, kwamba Yeye atawafikia, na kuwaokoa?
Na kondoo wanahitaji kufanya nini ili kuweza kupata msaada huu mtakatifu?
Je, kondoo wanahitaji kujua jinsi ya kutumia sextanti changamani ya kuhesabu vituo vya uratibu? Je, anahitaji kujua kutumia GPS kufafanua mahali alipo? Je, anahitaji kuwa na utaalamu wa kujenga programu ambayo itaomba msaada? Je, kondoo anahitaji idhinisho la mdhamini kabla ya Mchungaji Mwema kuja kumwokoa??
La, Hasha kabisa! Kondoo anastahili kuokolewa kwa sababu anapendwa na Mchungaji Mwema.
Kwangu mimi, fumbo la kondoo aliyepotea ni mojawapo ya vifungu vya matumaini katika maandiko yote.
Mwokozi wetu, Mchungaji Mwema, anatujua na anatupenda. Yeye anakujua na anakupenda.
Anajua wakati umepotea, na anajua mahali ulipo. Anaujua huzuni wako. Maombi yako ya kimya kimya. Woga wako. Majonzi yako.
Haijalishi umepoteaje—iwe kwa chaguzi mbaya zako mwenyewe au kwa sababu ya hali iliyo nje ya uwezo wako.
Kinachojalisha ni kwamba wewe ni mtoto Wake. Na Yeye anakupenda. Anawapenda watoto Wake.
Kwa sababu Anawapenda, Atawatafuta. Atawabeba mabegani mwake kwa furaha. Na atakapowaleta nyumbani, Atasema kwa mmoja na wote, “Furahini nami; kwani nimempata kondoo wangu aliyepotea.”3
Je, Sharti Tufanye Nini?
Lakini, unaweza kuwa unafikiria, kuna nini basi? Hakika nahitaji kufanya zaidi na siyo kusubiri kuokolewa.
Hali Baba yetu mwenye upendo anatamani kwamba watoto Wake wote warudi Kwake, Hatamlazimisha mtu kwenda mbinguni.4 Mungu hatatuokoa kinyume na mapenzi yetu.
Hivyo sharti tufanye nini?
Mwaliko Wake ni rahisi:
“Nigeukie … mimi.”5
“Njoo kwangu.”6
“Njoo karibu yangu nami nitakuja karibu yako.”7
Hivi ndivyo tunavyomwonyesha Yeye kwamba tunahitaji kuokolewa.
Inahitaji imani kidogo. Lakini usikate tamaa. Kama huwezi kuwa na imani sasa, anza na kutumaini.
Kama huwezi kusema unajua Mungu yupo pale, unaweza kutumaini kwamba yupo. Unaweza ukapenda kuamini.8 Inatosha kuanza hivyo.
Kisha, kutenda katika imani hiyo, mwendee Baba wa Mbinguni. Mungu ataonyesha upendo Wake kwako, na kazi Yake ya wokovu na mabadiliko itaanza.
Baada ya muda, utagundua mkono Wake katika maisha yako. Utahisi upendo Wake. Na matamanio ya kutembea katika nuru Yake na kufuata njia Yake yatakua kwa kila hatua unayopiga.
Tunaita hatua hizi za imani ya “utiifu.”
Hilo siyo neno linalopendwa sana siku hizi. Lakini utiifu ni dhana bora kabisa katika injili ya Yesu Kristo, kwa sababu tunajua kwamba “kupitia Upatanisho wa Kristo, watu wote wanaweza kuokolewa, kwa njia ya utiifu katika sheria na ibada za Injili.”9
Tunapoongezeka katika imani, pia lazima tuongezeke katika uaminifu. Mwanzoni nilimnukuu mtunzi wa Kijerumani aliyelalamikia kuangamizwa kwa Dresden. Yeye pia alandika kishazi “Es gibt nichts Gutes, ausser: Man tut es.” Kwa wale wasioongea lugha ya selestia, hii inatafsiriwa hivi “Hakuna kitu kizuri isipokuwa ukifanye.”10
Wewe na mimi twaweza kuongea kwa ufasaha sana juu ya mambo ya kiroho. Tunaweza kuwafanya watu watuone tunajua kwa tafsiri yetu ya ustadi ya mada za dini. Tunaweza kujisifia kuhusu dini na “ndoto ya nyumba [yetu] juu.”11 Lakini kama imani yetu haibadilishi jinsi tunavyoishi—ikiwa imani yetu haishawishi maamuzi yetu ya kila siku—dini yetu ni bure, kama si mfu, hakika si njema na ipo katika hatari ya kutoweka.12
Utii ni damu ya maisha ya imani. Ni kwa njia ya utiifu ambapo tunakusanya nuru katika nafsi zetu.
Lakini wakati mwingine ninafikiri hatuelewi utiifu. Tunaweza kuona utiifu kama mwisho wake, badala ya njia ya kwenda mwisho. Au huenda tukabonda nyundo ya sitiari ya utii dhidi ya chuma cha amri katika jitihada za kuwarekebisha wale tunaowapenda, kwa njia ya joto kila mara na kupigwa kila mara, katika mambo ya utakatifu, ya mbinguni.
Hakuna shaka katika hilo, kuna wakati tunahitaji mwito wa huruma kwenda kutubu. Hakika, kuna baadhi wale ambao wanaweza kufikiwa tu kwa njia hii.
Lakini pengine kuna njia nyingine ambayo inaweza kuelezea kwa nini tunatii amri za Mungu. Huenda utii siyo mchakato mkubwa wa kukunja, kugeuza, na kuziponda nafsi zetu katika kitu ambacho sisi siyo. Inawezekana, badala yake, ni mchakato ambao tunagundua sisi tumetengenezwa kwa kitu gani.
Tumeumbwa na Mungu Mwenyezi. Ni Baba yetu wa Mbinguni. Sisi ni watoto Wake wa kipekee wa kiroho. Tumetengenezwa kwa nyenzo kutoka juu ambazo ni za thamani na zilizosafishwa, na hivyo tunabeba vitu vya kiungu.
Hapa duniani, hata hivyo, fikra na matendo yetu yanajazwa na kile kilicho haribifu, kisicho kitakatifu, na kichafu. Vumbi na uchafu wa duniani hutia doa nafsi zetu, kufanya vigumu kutambua na kukumbuka haki yetu ya kuzaliwa na lengo letu.
Lakini haiwezi kubadilisha ukweli kuwa sisi ni kina nani. Msingi wa uungu wa asili yetu hubakia. Na wakati tunapochagua kuelekeza mioyo yetu kwa Mwokozi wetu mpendwa na kuweka miguu yetu juu ya njia ya ufuasi, kitu cha miujiza hutokea. Upendo wa Mungu hujaza mioyo yetu; nuru ya kweli hujaza fikra zetu; tunaanza kupoteza hamu ya kutenda dhambi; na hatutaki kutembea tena katika giza.13
Tunakuja kuona utii siyo kama adhabu bali njia ya ukombozi kwa hatima yetu ya uungu. Na hatua kwa hatua, uharibifu, vumbi, na mapungufu ya dunia hii huanza kuanguka. Hatimaye, ya thamani, roho ya milele ya kiumbe wa mbinguni ndani yetu inadhihirika, na mng’ao wa wema unakuwa asili yetu.
Unastahili Kuokolewa
Akina kaka na dada wapendwa, rafiki zangu wapendwa ninashuhudia kwamba Mungu anatuona kama kweli tulivyo—na Anatuona kuwa tunastahili kuokolewa.
Unaweza kuhisi kwamba maisha yako yameharibika. Unaweza kuwa umetenda dhambi. Unaweza ukawa una uoga, umekasirika, au kuteseka na una shaka. Lakini kama vile Mchungaji Mwema anavyomtafuta kondoo aliyepotea, kama utainua moyo wako kwa Bwana wa ulimwengu, Atakupata.
Atakuokoa.
Atakuinua juu na kukuweka kwenye mabega Yake.
Atakupeleka nyumbani.
Kama mikono inaweza kubadilisha vifusi na uharibifu kuwa nyumba nzuri ya kuabudu, basi tunaweza kuwa na uhakika na imani kwamba Mungu wetu mwenye upendo anaweza na atatujenga upya sisi. Mpango Wake ni kutujenga kuwa kitu kizuri kuliko kama tulivyokuwa awali—wazuri kuliko tunavyoweza kufikiria. Katika kila hatua ya imani tunayopiga kwenye njia ya ufuasi, tunakua kuwa viumbe wa ufalme wa milele na furaha ambayo tulipangiwa kuwa.
Huu ni ushuhuda wangu, baraka zangu na maombi yangu ya unyenyekevu katika jina takatifu la Bwana yetu, katika jina la Yesu Kristo, amina.