“Tembea Nami”
Kutawazwa kwetu katika ukuhani ni mwaliko kutoka kwa Bwana wa kutembea Naye, tufanye kama vile afanyavyo yeye, na kuhudumu vile anavyohudumu
Wapendwa ndugu zangu wa ukuhani, lengo langu leo ni kuwahakikishia na kuwatia nguvu ninyi, katika huduma zenu za ukuhani. Katika njia fulani, ni sawa na lengo ninalodhani Mwokozi alikuwa nalo pindi alipomkuta kijana tajiri ambaye aliuliza, “Ni jema lipi napaswa kufanya ili niwe na uzima wa milele?” (Mathayo 19:16). Yawezekana umefika katika mkutano huu, kama huyu kijana alivyoenda kwa Mwokozi, ukijiuliza kama huduma yako inakubalika. Na kwa wakati huo huo, unaweza dhani kuwa kuna zaidi ya kufanya—labda zaidi kabisa! Naomba kwamba niweze kuwasilisha kukubaliwa katika upendo wa Bwana kwa kile ulichokwisha kufanya, wakati pia natoa mtazamo wa hamasa kwa kile uwezacho, kwa msaada Wake, lakini pia kama mwenye ukuhani Wake mtakatifu.
Kijana tajiri aliombwa kuuza vyote alivyo navyo ili kumfuata Mwokozi, maendeleo yako yanaweza yasihitaji hivyo, lakini yanaweza kuhitaji kiasi fulani cha dhabihu. Vyovyote vile, Natumaini ujumbe wangu hautakusababisha “[kuondoka] na huzuni,” kama kijana alivyofanya. (Ona Mathayo 19:20–22.) Badala yake, naamini “utaondoka njiani ukifurahi” (M&M 84:105) kwa sababu unahitaji kufanya vizuri zaidi.
Hata hivyo, ni kawaida kuhisi mapungufu fulani wakati tunapofikiria kitu gani Bwana ametuita kufanya. Kwa kweli, kama ungeniambia unahisi unawezatimiza kiukamilifu majukumu yako ya ukuhani, naweza kuwa hofu kwamba haujayaelewa. Kwa upande mwingine, kama utaniambia unahisi kukata tamaa kwa sababu jukumu ni kubwa kuliko uwezo wako, hapo ningetaka kukusaidia uelewe jinsi gani Bwana anavyowakuza na kuwaimarisha wenye ukuhani wake ili kufanya vitu wasivyoweza kuvifanya wao pekee yao.
Hili ni kweli kabisa katika wito wangu kama ilivyo kwako katika wito wako. Hakuna kati yetu awezaye kufanya kazi ya ukuhani, na kufanya ipasavyo, kwa kutegemea tu hekima na vipaji vyetu. Hilo ni kwa sababu hii sio kazi yetu—ni kazi ya Bwana. Hivyo njia pekee ya kufanikiwa ni kumtegemea Yeye, Hata kama wewe ni shemasi mpya uliyeitwa na kuaminiwa kwa kazi ya kuleta kiasi cha nguvu za kiroho katika ibada ya sakramenti; au mwalimu wa nyumbani uliyetumwa na Bwana kuwapenda na kusaidia familia usiyoifahamu na wanaoonekana hawahitaji upendo au msaada wako; au baba ajuaye unapaswa kuongoza nyumba yako katika haki, lakini hauna uhakika jinsi ya kufanya hivyo, na muda unaonekana unaisha, kwa sababu wale watoto wanakua kwa haraka na dunia inaonekana kuwa katili na yenye uhasama.
Hivyo basi kama unahisi umelemewa kiasi, chukulia hilo kama ishara nzuri. Inaashiria kuwa unaweza kuhisi kiasi fulani cha imani Mungu ameweka kwako. Inamaanisha kuwa una uelewa kidogo kuhusu ukuhani ni nini hasa.
Kuna watu wachache duniani wenye uelewa huo. Hata wale wanaoweza kukariri maana yenye mantiki hawatoweza kuuelewa vyema. Kuna baadhi ya maandiko ambayo, kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu yanabeba, yanaweza kukuza hisia zetu za kustahajabisha kuhusu ukuhani mtakatifu. Hizi ni baadhi yake:
“Ile nguvu na mamlaka ya juu zaidi, au Ukuhani wa Melkizedeki, ni kushikilia funguo za baraka zote za kiroho za kanisa—
Kuwa na haki ya kupokea siri za ufalme wa mbinguni, mbingu kufunuliwa kwao, kuwasiliana na baraza kuu na kanisa la Mzaliwa wa Kwanza, na kufurahia ushirikiano wao na uwepo wa Mungu Baba, na Yesu aliye mpatanishi wa agano jipya.
“Nguvu na mamlaka ya … Ukuhani wa Haruni, ni kushikilia funguo za huduma ya malaika (M&M 107:18–20).
“Katika ibada [za ukuhani], nguvu za uchamungu zinajidhihirisha. …
“Kwani pasipo hizi hakuna mwanadamu anayeweza kuuona uso wa Mungu, hata Baba, na kuishi” (M&M 84:20, 22).
“Ukuhani huu mkuu ukiwa kwa ule mpango wa Mwana [wa Mungu], mpango ambao ulikuwa tangu msingi wa ulimwengu; au kwa maneno mengine, haukuwa na mwanzo wa siku au mwisho wa miaka, ukiwa ulitayarishwa tangu milele hadi milele, kulingana na ufahamu wake wa mbele wa vitu vyote”(Alma 13:7).
“Kila mmoja atakayekuwa ametawazwa kwa mfano na wito huu awe na nguvu, kwa imani, kuivunja milima, kuzigawanya bahari, kuyakausha maji, kuzibadilisha njia zake;
“Kuyazuia kwa mafanikio majeshi ya mataifa, kuigawa dunia, kuvunja kila kamba, kusimama katika uwepo wa Mungu; kufanya mambo yote kulingana na mapenzi yake, kulingana na amri yake, kuzitiisha himaya na mamlaka; na hii ni kwa mapenzi ya mwana wa Mungu ambaye alikuwepo kabla ya kuweko kwa msingi wa ulimwengu” (Tafsiri ya Joseph Smith, Mwanzo 14:30–31 [katika kiambatisho cha Biblia]).
Njia moja ya kujibu maelezo hayo yenye mvuto ya uwezo wa ukuhani ni kuchukulia kuwa hayatuhusu. Njia nyingine ya kujibu ni kwa maswali ya kujichunguza kiroho, tukijiuliza katika mioyo yetu, kama haya: Je, nilishawahi kuhisi kwamba mbingu zimenifungukia? Je, kuna mtu yeyote anayetumia neno “msaada wa malaika” kuelezea huduma yangu ya ukuhani? Je, ninaleta “nguvu ya uchamungu” katika maisha ya wale ninaowatumikia? Je, nilishawahi kuvunja mlima, kulishinda jeshi, kukata kamba za mtu fulani, kushinda nguvu za dunia—hata kama ni kwa kufikirika tu—ili kukamilisha nia ya Mungu?
Kujichunguza kwa namna hii huleta hisia kwamba tungeliweza fanya zaidi katika huduma ya Bwana. Natumaini inakuletea pia hisia kwamba unahitaji kufanya zaidi—haja ya kushiriki zaidi katika kazi ya kimiujiza ya Bwana. Hisia hizo ni hatua za awali kuelekea kuwa aina ya watu ambao huduma ya ukuhani imelengwa kuwazalisha.
Hatua inayofuata imeelezwa katika kukutana kati ya Yehova na Henoko. Tunajua Henoko kama Nabii hodari ambaye alianzisha Sayuni katikati ya uovu mkubwa. Lakini kabla hajawa Nabii hodari, Henoko alijiona binafsi “kama kijana, … si mwepesi wa kusema,” na alichukiwa na watu wote (Musa 6:31). Sikiliza maneno ambayo Bwana aliyatumia katika kumhamasisha Henoko. Pia ni maneno Yake kwenu mlioitwa ili kusaidia wengine kama wenye ukuhani:
“Naye Bwana akamwambia Henoko: Enenda zako na ukafanye kama nilivyokuamuru, na hakuna mtu atakayekurarua wewe. Fumbua kinywa chako, nacho kitajazwa, nami nitakupa maneno, kwa maana wenye mwili wote wako mikononi mwangu, nami nitafanya kama nionavyo kuwa vyema. …
Tazama Roho yangu i juu yako, kwa sababu hiyo maneno yako yote nitayahesabia kuwa haki; na milima itakukimbia mbele yako, na mito itageuka kutoka uelekeo wake; nawe utakaa ndani yangu, nami ndani yako; kwa hiyo tembea pamoja nami.(Musa 6:32, 34).
Ndugu, kutawazwa kwetu katika ukuhani ni mwaliko kutoka kwa Bwana wa kutembea Naye. Na ina maana gani kutembea na Bwana? Inamaanisha kufanya kile afanyacho, kuhudumu kama Anavyohudumu. Alitoa dhabihu faraja Zake ili kuwabariki wenye shida, hicho ndicho tunachojaribu kufanya. Alionekana kuwatambua watu ambao walidharauliwa na hata kutengwa na jamii, basi tunajaribu kufanya hivyo pia. Alishuhudia kwa ujasiri pia kwa upendo mafundisho ya kweli Aliyopokea kutoka kwa Baba Yake, hata kama haikupendelewa, na hivyo ndivyo tunavyopaswa pia. Alisema kwa wote, “Njooni kwangu” (Mathayo 11:28), na tunasema kwa wote, “Njooni Kwake.” Kama wenye ukuhani, sisi ni wawakilishi Wake. Hatufanyi kwa ajili yetu lakini kwa ajili Yake. Hatuongei maneno yetu lakini Yake. Watu tunaowahudumia watakuja kumjua Yeye vyema kwa sababu ya huduma zetu.
Mara tu tunapokubali mwaliko wa Bwana “Tembea Nami,” asili ya huduma za ukuhani wetu itabadilika. Inakuwa mara moja kubwa na yenye maadili lakini pia yenye kufanikiwa zaidi, kwa sababu tunafahamu hatupo peke yetu. Nilihisi hili kwa nguvu zaidi wakati Rais Thomas S. Monson alipoweka mikono yake katika kichwa changu miaka tisa iliyopita na kunibariki nilipokuwa nikianza huduma katika wito nilionao sasa. Katika baraka ile, alikariri maneno ya Mwokozi: “Na yeyote awapokeaye ninyi, hapo nitakuwepo pia, kwani nitakwenda mbele ya uso wenu. Nitakuwa mkononi mwenu wa kulia na wa kushoto, na Roho wangu atakuwa mioyoni mwenu, na malaika wangu watawazingira, ili kuwabeba juu (M&M 84:88).
Nimekuwa nikitegemea hiyo ahadi mara nyingi, na nimeona ikitimia katika njia nyingi kipindi chote cha miaka 72 ya huduma ya ukuhani. Ilitokea nilipokuwa mpya katika Ukuhani wa Haruni nikiwa na zoezi la kupitisha sakramenti. Nikihofu kuwa ningelifanya kosa, Nilitoka nje ya kanisa kabla ya mkutano kuanza na kusali kwa kukata tamaa kwamba Mungu angelinisaidia. Jawabu lilikuja. Nilihisi kwamba Bwana alikuwa nami. Nilihisi imani Yake kwangu mimi, na hivyo nikahisi imani katika sehemu yangu ya kazi Yake.
Ilitokea tena nilipokuwa nikitumika kama askofu. Nilipokea simu kutoka kwa mwanamke ambaye alifanya kosa kubwa na hapo nilikabiliwa na uamuzi mgumu. Nilipokutana naye, nilihisi nilijua jibu la tatizo lake, lakini pia nilihisi kwa dhati kwamba nisimpe jibu lile—ilihitajika alipate jibu yeye mwenyewe. Maneno yangu kwake yalikuwa “Naamini Mungu atakuambia kitu gani cha kufanya kama utamuomba.” Baadaye alinitaarifu kwamba alimuomba Bwana Naye akamwambia.
Katika tukio lingine, simu nyingine iliingia, wakati huu nilikuwa askofu—kutoka kwa askari. Niliambiwa kwamba, dereva mlevi aligonganisha gari lake katika ukumbi wa benki. Wakati dereva mwenye mkanganyiko alipoimwona mlinzi akiwa na silaha yake kwa tahabibu, alilia, Usipige! Mimi ni Mmormoni!”
Dereva huyu alijulikana kuwa ni mshiriki wa kata yangu, alibatizwa hivi karibuni tu. Nilipokuwa nikisubiri kuzungumza naye katika ofisi yangu ya askofu, Nilipanga kile nitakachosema ili kumfaya ajute kwa jinsi alivyovunja maagano yake na kuliaibisha Kanisa. Lakini nilipokaa nikimtazama, Nilisikia sauti akilini mwangu ikisema, “Nitakufanya umuone kama ninavyomuona.” Halafu, kwa muda mchache, muonekano wake wote ulibadilika. Sikuona kijana aliyebumbuwazwa lakini kijana msafi, mwenye akili, mtoto wa Mungu mwenye maadili. Ghafla nilihisi upendo wa Bwana kwake. Ono lile lilibadilisha mazungumzo yetu. Lilinibadilisha mimi pia.
Nilijifunza masomo muhimu katika katika tukio hili kutembea na Bwana katika kufanya kazi Yake. Ningelipenda kushiriki nanyi matatu kati ya hayo. Kwanza ni kwamba Mungu anatambua na kusaidia hata wapya na shemasi wadogo kabisa. Hauhitaji kabisa kujiona kuwa wewe ni mdogo sana au sio wa muhimu kabisa kwake Yeye kukugundua wewe na huduma unayotoa katika jina Lake.
Somo la pili ni kwamba kazi ya Bwana sio tu kutatua matatizo; ni kuwajenga watu. Hivyo kadiri unavyotembea Naye katika huduma ya ukuhani, utaweza kuona kwamba wakati mwingine linaloweza kuonekana kuwa ni suluhisho sahihi sio suluhisho alilotaka Bwana kwa sababu halitaruhusu watu kukua. Kama utasikiliza, Atakufundisha njia Zake. Kumbuka kwamba kazi ya Mungu na utukufu Wake si tu kuongoza shirika fanisi; ni “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (Musa 1:39). Na hii, mbali ya yote, ndiyo sababu Anatoa mamlaka ya ukuhani kwa watu wenye mapungufu kama wewe na mimi na kutualika kushiriki katika kazi Yake. Maendeleo yetu ni kazi Yake
Sasa somo la tatu: Kutembea na Mwokozi katika huduma ya ukuhani kutabadilisha jinsi unavyowaona watu wengine. Atakufundisha kuwaona kwa kutumia macho Yake, ambayo inamaanisha kuwaona zaidi ya muonekano wa nje na hata ndani ya moyo (ona 1 Samuel 16:7) Hivi ndivyo Mwokozi aliweza kumwona Simoni sio kama mvuvi mwenye mhemko wa ghafla lakini kama Petro, kiongozi mwamba dhabiti wa siku zijazo wa Kanisa Lake (ona Luka 5:1–11). Hivi ndivyo Aliweza kumwona Zakayo sio kama mtoza ushuru mfisadi wengine walivyomwona lakini kama mwana mwaminifu wa Ibrahimu (ona Luka 19:1–9). Ukitembea na Mwokozi kwa muda mrefu, utajifunza kumwona kila mtu kama mtoto wa Mungu aliye na uwezo usio na mipaka, bila ya kujali siku zake za nyuma zilikuwa za namna gani. Na ukiendelea kutembea na Mwokozi, utakuza zawadi nyingine aliyo nayo—uwezo wa kuwasaidia watu kuona uwezo huo ndani yao na kutubu.
Ndugu zangu wapendwa katika ukuhani, katika njia nyingi, sisi ni kama wale wafuasi wawili waliokuwa wakitembea katika barabara ya Emau Jumapili ile ya kwanza ya Pasaka. Ilikuwa asubuhi ya Ufufuko, lakini bado hawakuwa na uhakika wa kuwepo kwa ufufuko au hata ufufuko ulikuwa na maana gani. Wao “waliamini kuwa [Yesu wa Nazareti] alipaswa kuwa ameikomboa Israeli,” lakini wao “walikuwa wazito moyoni kuamini” kila kitu ambacho maandiko yalifundisha juu ya ufufuko. Kadiri walivyo kuwa wakitembea, wakijaribu kuwaza na kuwazua kwa [pamoja, “Yesu mwenyewe akajisogeza, na kwenda pamoja nao. “Macho yao yakafumbwa wasimtambue.” (Ona Luka 24:13–32.)
Ninawashuhudia kwamba tunapotembea katika njia ya huduma ya ukuhani, Mwokozi Yesu Kristo hutembea pamoja nasi kwani hiyo ni njia Yake. Nuru Yake hututangulia, na malaika Wake wakituzingira. Tunaweza kupungukiwa uelewa kamili wa ukuhani ni kitu gani hasa au namna ya kuutumia kama Yeye afanyavyo. Lakini kama tutatoa usikivu wa karibu kwa nyakati zile mioyo yetu “inapowaka moto ndani yetu” (Luka 24:32), macho yetu yanaweza yakafunguliwa, nasi tukauona mkono Wake katika maisha na huduma yetu. Ninashuhudia kwamba tunakuja kumjua vyema kwa kufanya kazi pamoja Naye na kumtumikia Yeye katika kazi kuu ya kuleta wokovu kwa watoto wa Mungu. Kwani ni vipi mtu atamjua yule bwana ambaye hajamtumikia, na aliye mgeni kwake, na yuko mbali katika mawazo na nia za moyo wake? (Mosia 5:13). Yesu Kristo ni Mfano Wetu Hili ni Kanisa Lake. Ni ukuhani Wake huu tunaoshikilia. Na kila mmoja wetu na achague kutembea pamoja Naye na kutambua ni namna gani Yeye hutembea na sisi.
Ninakupeni ushahidi wangu wa dhati kwamba Yesu ndiye Kristo, Bwana wetu mfufuka. Ninakutoleeni ninyi ushuhuda wangu kwamba ukuhani huu ambao ameuaminisha kwetu sisi ni nguvu ya kuongea na kutenda katika jina Lake. Sisi tu watoto wa Baba mpendwa wa mbinguni ambaye hujibu maombi yetu na humtuma Roho Mtakatifu ili atuimarishe katika kila kazi ya ukuhani ambayo tumebarikiwa kuipata. Joseph Smith aliwaona Baba na Mwana. Alipokea funguo za ukuhani ambazo zimepitishwa kwa kupokezana hadi kwa Rais Thomas S. Monson ambaye huzitumia hii leo. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, Amina.