Kuwa Mwanafunzi wa Bwana wetu Yesu Kristo
Mkusanyiko wa tabia zinazotokana na imani katika Kristo zote ni muhimu katika kusimama imara kwetu katika siku hizi za mwisho.
Inamaanisha nini kuwa mwanafunzi wa Bwana wetu Yesu Kristo? Mwanafunzi ni yule aliyebatizwa na yupo tayari kujichukulia juu yake jina la Mwokozi na kumfuata. Mwanafunzi anajitahidi kuwa kama Yeye kwa kutii amri Zake katika maisha haya, ni sawa na mwanafunzi anavyotafuta kuwa kama mwalimu wake.
Watu wengi husikia neno mwanafunzi na kudhani linamaanisha “mfuasi” tu. Lakini uanafunzi halisi ni hali ya kuwa. Hii inamaanisha ni zaidi ya kusoma na kufanya orodha ya sifa binafsi za mtu. Wanafunzi huishi ili kwamba tabia za Kristo zifumwe katika uzi wa utu wao, kama katika zulia la kiroho.
Sikiliza mwaliko wa Mtume Petro wa kuwa mwanafunzi wa Mwokozi:
“Mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema; na katika wema wenu maarifa;
“Na katika maarifa yenu kiasi; na katika kiasi chenu saburi; na katika saburi yenu utauwa;
“Na katika utauwa wenu upendano wa ndugu; na katika upendano wa ndugu, upendo.”1
Kama unavyoweza kuona, kufuma zulia la kiroho la uanafunzi binafsi kunahitaji zaidi ya uzi mmoja. Katika siku ya Mwokozi, kulikuwa na wengi waliodai kuwa wenye haki katika jambo moja au lingine la maisha yao. Walifanya kile nilichoita utii wa kuchagua. Kwa mfano, walitii amri ya kutokufanya kazi katika Sabato lakini walimkosoa Mwokozi kwa kuponya katika siku hiyo takatifu.2 Walitoa msaada kwa maskini lakini walitoa kilichozidi—wasichokihitaji wao binafsi.3 Walifunga lakini kwa uso wa kukunjamana.4 Walisali ili tu waonekane kwa watu.5 Yesu alisema, “Husogea karibu nami kwa midomo yao, ila mioyo yao iko mbali nami.”6 Watu hao wanaweza zingatia tabia fulani au kitendo lakini hawawi kama Yeye katika mioyo yao.
Kwa hawa, Yesu alitangaza:
“Wengi watasema kwangu siku ile: Bwana, Bwana, si tulifanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako si tumetoa pepo chafu, na katika jina lako kufanya miujiza mingi?
“Ndipo nitawaambia dhahiri, sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”7
Sifa za Mwokozi, kama tunavyodhani, sio mswada wa kufuata au orodha ya kukaguliwa. Ni tabia zilizofumwa, zimeongezwa moja kwa nyingine, zinazoongezeka ndani yetu katika njia shirikishi. Kwa maneno mengine, hatuwezi pata tabia moja kama ya Kristo pasipo pia kupata na kuhamasisha zingine. Kadiri tabia moja inavyokuwa imara, ndivyo zingine pia.
Katika 2 Petro na Mafundisho na Maagano sehemu ya 4, tunajifunza kwamba imani katika Bwana Yesu Kristo ndiyo msingi. Tunapima imani yetu kwa kile kinatupelekea sisi kufanya—kwa utii wetu. “Ikiwa mtakuwa na imani ndani yangu,” Bwana ameahidi, “mtakuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote ambacho ni cha kufaa kwangu.”8 Imani ni kichocheo. Pasipo kazi, pasipo kuishi maisha mema, imani yetu haitakuwa na uwezo kuamsha uanafunzi. Kweli, imani imekufa.9
Na hivyo Petro alieleza, “katika imani yenu tieni wema.” Huu wema ni zaidi ya usafi wa kimwili. Ni usafi na utakatifu katika akili na mwili. Wema pia ni uwezo. Tunapoishi injili kikamilifu, tutakuwa na uwezo wa kuwa wema katika kila wazo, hisia, na tendo. Akili zetu zinakuwa sikivu zaidi katika ushawishi wa Roho Mtakatifu na Mwanga wa Kristo.10 Tunamfanana Kristo sio tu katika kile tunachokisema na kufanya lakini katika utu wetu.
Petro aliendelea, “Tieni katika wema [wenu] maarifa.” Tunapoishi maisha mema, tunakuja kumjua Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye katika njia maalum. “Mtu akipenda kuyatenda mapenzi ya [Baba], atajua habari ya yale mafunzo.”11 Maarifa haya ni ushuhuda binafsi, utokanao na uzoefu binafsi. Ni maarifa yanayotubadilisha, ili kwamba “mwanga wetu uambatane na mwanga [Wake] na wema wetu uupende wema [Wake].”12 Kwa kuishi kwetu kwa wema, tunasafiri kutoka “Naamini” kuelekea kwenye mwisho wa utukufu wa ”Najua.”
Petro anatuhimiza kuongeza “katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi.” Kama wanafunzi wenye kiasi, tunaishi injili katika njia ya kiasi na thabiti. Sisi “hatukimbii kwa haraka kupita uwezo wetu.”13 Siku hadi siku tunasonga mbele, hatuzuiliwi na changamoto za kututakasa za maisha haya.
Kuwa wa kiasi kwa njia hii, tunaongezeka katika uvumilivu na tumaini kwa Bwana. Tunaweza kutegemea usanifu Wake kwa maisha yetu, hata kama hatuwezi kuona kwa macho yetu ya kimwili.14 Kwa hiyo tunaweza “kutulia, na kujua kuwa [Yeye] ni Mungu.”15 Tukikumbwa na dhoruba za dhiki, tunauliza, “Ni kitu gani Unahitaji nijifunze katika uzoefu huu?” Kwa mpango na malengo Yake katika mioyo yetu, tunasonga mbele sio tu kuvumilia vitu vyote lakini kuvumilia yote vizuri16
Uvumilivu huu, Petro anafundisha, hutupeleka kwenye utauwa. Kama Baba alivyo mvumilivu kwetu, watoto Wake, tunakuwa wavumilivu na kila mmoja wetu na kwetu binafsi. Tunafurahi katika uhuru wa wengine na fursa wanayopata kukua “mstari juu ya mstari, “17 “nuru zaidi na zaidi hata mchana mkamilifu.”18
Kutoka kiasi hata saburi, na kutoka saburi hata utauwa, asili yetu inabadilika. Tunapata upendano wa undugu ambao ni fadhila mahususi ya wanafunzi wote wa kweli. Kama Msamaria Mwema, tunavuka barabara kuhudumia yeyote mwenye uhitaji, hata kama hawapo katika mzunguko wa marafiki zetu.19 Tunawabariki wale wanaotulaani. Tunatenda mema kwa wale wanaotutumia vibaya.20 Kuna sifa yeyote ya kitauwa au Kikristo?
Nashuhudia kwamba jitihada tunazofanya kuwa wanafunzi wa Mwokozi, kiukweli zinaongezwa hadi “tunapopatwa” na upendo Wake.21 Upendo huu ni kiashiria cha tabia ya mwanafunzi wa Kristo:
“Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.
“Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.”22
Ni imani, matumaini, na upendo hutuwezesha kwa kazi ya Mungu.23 “Basi, sasa inadumu … haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.”24
Kaka na dada zangu, kwa sasa kuliko kipindi chochote, hatuwezi kuwa wanafunzi wa muda fulani tu”! Hatuwezi kuwa wanafunzi katika funzo moja au lingine tu. Mkusanyiko wa tabia ambazo zinatokana na imani katika Kristo—pamoja na ambazo tumekwisha zungumzia leo—zote ni muhimu kwa msimamo wetu imara katika siku hizi za mwisho.
Tunavyojitahidi kwa bidii kuwa wanafunzi halisi wa Yesu Kristo, hizi tabia zitakusanyika, na kuongezwa, na zitaimarishwa ndani yetu kwa kushirikiana. Hakutakuwa na utofauti kati ya wema tunaoonesha maadui zetu na wema tunaoonesha kwa marafiki zetu. Tutakuwa waaminifu pindi hakuna mtu anatazama kama tu tunavyokuwa wengine wanavyokuwa wakitutazama. Tutakuwa tunajitoa kwa Mungu katika umma kama tu tunapokuwa sehemu zetu za faragha.
Nashuhudia kuwa kila mtu anaweza kuwa mwanafunzi wa Mwokozi. Uanafunzi hauzuiliki kwa umri, jinsia, au asili ya ukabila au wito. Kupitia uanafunzi wetu binafsi, sisi kama watakatifu wa siku za mwisho, tunajenga uwezo wa pamoja kubariki kaka na dada zetu duniani kote. Sasa ni wakati wa kuamua tena kuwa wanafunzi Wake kwa bidii yote.
Kaka na dada zangu, wote tumeitwa kuwa wanafunzi wa Mwokozi. Fanya mkutano huu kuwa fursa kwako ya “kuanza kama wakati wa kale na kwenda [Kwake] kwa mioyo yenu yote.”25 Hili ni Kanisa Lake. Natoa ushahidi wangu maalum kuwa Yeye anaishi. Naomba atubariki wote katika haja yetu ya milele kuwa wanafunzi waliojitolea na jasiri. Katika jina la Yesu Kristo, amina.