“Amani Yangu Nawaachieni”
Bwana aliwaahidi amani wanafunzi Wake alipokuwa karibu kuwaacha. Yeye ametupa ahadi hiyo hiyo.
Kina dada zangu wapendwa, tumebarikiwa na Roho wa Bwana usiku wa leo. Jumbe zenye mwongozo kutoka kwa kinadada viongozi wenye nguvu, na muziki vimeimarisha imani yetu na kuzidisha hamu yetu ya kuweka maagano matakatifu ambayo tumefanya na Baba yetu wa Mbinguni mpendwa. Tumehisi kuongezeka kwa upendo wetu kwa Bwana Yesu Kristo na shukrani kwa zawadi yake ya ajabu ya dhabihu ya upatanisho Wake.
Ujumbe wangu jioni ya leo ni rahisi. Wote tumehisi amani jioni ya leo. Sisi wote tungependa kuhisi amani kama hiyo kila mara ndani yetu, katika familia zetu, na pamoja watu wanatuzunguka. Bwana aliwaahidi amani wanafunzi Wake alipokuwa karibu kuwaacha. Yeye ametupa ahadi hiyo hiyo. Lakini yeye alisema kwamba Yeye angetoa amani katika njia Yake, siyo katika njia ya ulimwengu. Yeye alielezea njia Yake ya kutuma amani.
“Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
“Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu wala msiwe na woga.” (Yohana 14:26–27).
Wana wa Mosia walihitaji hicho kipawa cha amani walipoanza misheni yao kwa Walamani. Na zaidi ya wasi wasi kidogo wakihisi ukubwa wa jukumu lao, walisali wapate uthibitisho. Na “Bwana aliwatembelea kwa Roho Wake, na kuwaambia: Pateni faraja. Na wakafarijika” (Alma 17:10; ona pia Alma 26:27).
Wakati mwingine unaweza kutamani amani unapokabiliana na utovu wa hakika na kile unachoweza kuona kama changamoto zinazotanda. Wana wa Mosia walijifunza somo ambalo Bwana alimfundisha Moroni. Ni mwongozo kwetu sisi wote. “Na ikiwa watu watakuja kwangu nitawaonyesha udhaifu wao. Ninawapatia watu udhaifu ili katika udhaifu wao wawe wanyenyekevu; na neema yangu inatosha watu wote ambao hujinyenyekeza mbele yangu; kwani wakijinyenyekeza mbele yangu, na kuwa na imani ndani yangu, ndipo nitafanya vitu dhaifu kuwa vya nguvu kwao” (Etheri 12:27).
Moroni alisema ya kwamba baada ya “kusikia maneno haya,” “alifarijika” (Etheri 12:29). Yanaweza kuwa faraja kwetu wote. Wale ambao hawatambui udhaifu wao hawawezi kusonga mbele. Utambuzi wako wa udhaifu wako ni baraka, kwa vile hukusaidia kusalia mnyenyekevu na hukufanya kumgeukia Mwokozi. Roho hakufariji tu bali Yeye pia ni chombo ambacho kwacho Upatanisho hufanya mabadiliko katika asili yako hasa. Kisha vitu vinyonge vinakuwa thabiti.
Mara kwa mara imani yako itatiwa changamoto na Shetani; hili huwafanyikia wanafunzi wote wa Yesu Kristo. Kinga yako dhidi ya mashambulizi haya ni kuwa na Roho Mtakatifu kama mwenzi wako. Roho atazungumza amani katika nafsi yako. Atakuhimiza usonge mbele kwa imani. Na atakukumbusha kuhusu zile nyakati ulizohisi nuru na upendo wa Yesu Kristo.
Kukumbuka kunaweza kuwa mojawapo ya zawadi ya thamani kubwa sana ambayo Roho anaweza kukupa wewe. Yeye “atakuwakumbusha yote [Bwana] aliyowaambia.” (Yohana 14:26). Kumbukumbu inaweza kuwa ya ombi lililojibiwa, agizo la ukuhani ulilopokea, uthibitisho wa ushuhuda wako, au wakati ambapo uliona mkono elekezi wa Bwana maishani mwako. Pengine katika siku za usoni wakati utakapohitaji nguvu, Roho anaweza kukuletea kwenye kumbukumbu yako hisia unazohisi katika mkutano huu. Ninaomba kwamba haya yawe hivyo.
Kumbukumbu moja ambayo Roho mara kwa mara huleta akilini mwangu ni ya mkutano wa sakramenti jioni fulani miaka mingi iliyopita katika banda la mabati kule Innsbruck, Austria. Banda lilikuwa chini ya mtambo wa reli. Kulikuwepo tu na watu takriban watu dazeni moja, wakiwa wameketi kwenye viti vya mbao. Wengi wao walikuwa wanawake, wengine wadogo na wengine wakubwa. Niliona machozi ya shukrani wakati sakramenti ilikuwa ikipitishwa katika mkutano huu. Nilihisi upendo wa Mwokozi kwa Watakatifu hao, nao pia. Lakini muujiza ambao ninaokumbuka ni nuru niliyoiona katika lile banda la mabati, huleta hisia za amani. Ilikuwa ni usiku na hapakuwepo na madirisha, na bado chumba kile kilikuwa na mwangaza kana kwamba kwa mwangaza wa jua saa sita mchana.
Nuru ya Roho Mtakatifu ilikuwa angavu na tele jioni ile. Na madirisha ambayo yaliingiza nuru ilikuwa ni mioyo iliyonyenyekea ya wale Watakatifu, waliokuwa wamekuja mbele za Bwana wakitafuta msamaha kwa dhambi zao na wakiahidi kumkumbuka Yeye siku zote. Ilikuwa si vigumu kumkumbukaYeye wakati huo, na kumbukumbu yangu ya uzoefu huo mtakatifu imefanya iwe rahisi kwangu kumkumbuka Yeye na Upatanisho Wake katika miaka iliyofuata. Siku ile ahadi katika sala za sakramenti ni kwamba Roho atakuwa pamoja nasi ilitimizwa na basi kuleta hisia za nuru na amani.
Kama nyinyi, nimekuwa na shukrani kwa njia nyingi ambazo Bwana amenitembelea kupitia Msaidizi wakati nilipohitaji amani. Hali Baba yetu wa Mbinguni hajali tu faraja yetu bali hata zaidi kuhusu maendeleo yetu kwenda mbinguni. “Msaidizi” ni njia moja tu kati ya nyinginezo ambazo Roho Mtakatifu anavyoelezwa katika maandiko. Nyingine ndio hii: “Na sasa, amini, amini, ninakuambia wewe, weka imani yako katika yule Roho ambaye huongoza kufanya mema” (M&M 11:12). Mara nyingi, mema ambayo atakuongoza kufanya yatahusu kumsaidia mtu mwingine kupokea faraja kutoka kwa Mungu.
Katika hekima Yake, Bwana amewaleta pamoja katika makundi na madarasa katika Kanisa Lake. Amefanya hivi ili kuzidisha uwezo wako wa kutenda mema. Katika makundi haya, unayo majukumu maalum kuwahudumia wengine kwa niaba Yake. Kwa mfano, ikiwa wewe ni msichana, unaweza kuombwa na askofu wako au kiongozi wa Wasichana kumtafuta msichana wa Laureli ambaye amekuwa kile mara nyingine sisi huita “asiyeshiriki kikamilifu.” Unaweza kuwa unamjua vizuri zaidi kuliko askofu au kiongozi wa Wasichana. Unaweza kuwa unajua ya kwamba anahisi yuko na shida nyumbani au shuleni au pengine kote. Viongozi wako wanaweza kukosa kujua ni kwa nini walihisi wamesukumwa kukuuliza umtafute, lakini Bwana anajua, na anaongoza kazi yake kupitia msukumo wa Roho Wake.
Mafanikio katika juhudi zenu yatahitaji muujiza wa mabadiliko ufanyike katika moyo wako na katika moyo wa msichana uliyetumwa kumuokoa—na hilo linahitaji uenzi wa Roho Mtakatifu. Roho anaweza kukuruhusu umuone msichana wa Laureli asiyeshiriki kikamilifu jinsi Bwana anavyomuona. Bwana anajua moyo wake na moyo wako, na anajua uwezekano wa mioyo kubadilishwa. Anaweza kuwatembeleeni kwa Roho Wake kuwatia msukumo muwe wanyenyekevu, wenye kusamehe, na wenye upendo.
Roho huyo anaweza kutia msukumo maneno, vitendo, na subira inayohitajika kwenu kumwalika mwanakondoo arudi katika kundi. Na anaweza kugusa mioyo ya kundi katika darasa la Laureli limpende na limkaribishe kondoo aliyepotea, ili wakati anaporudi, aweze kuhisi amerudi nyumbani.
Uwezo wenu kufanya mema kama kikundi cha mabinti wa Mungu utategemea, kwa kiwango kikubwa, juu ya umoja na upendo uliopo kati ya kundi lenu. Hii ni zawadi ya amani nyingine inayotoka kwa Roho Mtakatifu
Alma alielewa haya. Hiyo ndiyo sababu aliwasihi watu wake “wasiwe na ubishi wao kwa wao, lakini kwamba watazame kwa jicho moja, kwa imani moja na ubatizo mmoja, na mioyo yao ikiwa imeunganishwa pamoja kwa umoja na kwa kupendana wao kwa wao” (Mosia 18:21).
Umoja ni muhimu kwetu kuwa na Roho katika darasa letu na familia yetu. Lakini mnajua kama ninavyojua kutokana na uzoefu kama ninavyojua kwamba umoja wa upendo kama huu ni vigumu kudumisha. Inahitaji kuwa na Roho Mtakatifu kama mwenzi ili kufungua macho yetu na kupoza mioyo yetu.
Nakumbuka wakati mmoja mwana wetu wa miaka saba au minane alirukaruka sana kitandani kwake hata kwamba niliona kama kingevunjika. Nilihisi mwako wa kuhudhika, na nikaamua upesi kurekebisha nyumba yangu. Nilimnyakua kwa mabega yake madogo na kumuinua hadi kiwango ambapo macho yetu yalikutana.
Roho aliweka maneno akilini mwangu. Ilionekana kama sauti tulivu ambayo ilichoma moyo wangu. “Wewe umemuinua mtu mkuu sana. Nilimuwekewa juu ya kitanda kwa upole na nikamuomba msamaha.
Sasa ameshakuwa yule mwanaume mkuu ambaye Roho Mtakatifu aliniruhusu nimwone miaka 40 iliyopita. Nina shukrani za milele kwa kuwa Bwana aliniokoa kutokana na hisia zangu mbaya kwa kunitumia Roho Mtakatifu aniruhusu nimuone mwana wa Mungu jinsi Mungu alivyomuona.
Umoja tunaotafuta katika familia zetu na katika Kanisa utakuja tunapomruhusu Roho Mtakatifu kuathiri kile tunachoona na wakati tunapotazamana—na hata tunapofikiriana. Roho huona upendo msafi wa Kristo. Sikilizeni maneno ya Mormoni yaliyotumika kufafanua hisani. Fikiria juu ya nyakati umehisi.
“Hisani huvumilia, na ni karimu, na haina wivu, na haijivuni, haitafuti mambo yake, haifutuki kwa upesi, haifikirii mabaya, na haifurahii uovu lakini hufurahi katika ukweli, huvumilia vitu vyote, huamini vitu vyote, hutumaini vitu vyote, hustahamili vitu vyote.
“Kwa hivyo, ndugu [na naongezea dada] zangu wapendwa, kama hamna hisani, nyinyi si kitu, kwani hisani haikosi kufaulu kamwe. Kwa hivyo, ambatana na hisani, ambayo ni kubwa kuliko yote, kwani vitu vyote lazima vishindwe—
“Lakini hisani ni upendo msafi wa Kristo, na inavumilia milele; na yeyote atakayepatikana nayo katika siku ya mwisho, itakuwa vyema kwake.
“Kwa hivyo, ndugu zangu [na dada] zangu wapendwa, ombeni kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba mjazwe na upendo huu, ambao ametoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwana Wake, Yesu Kristo; ili muwe wana na [mabinti] wa Mungu; kwamba wakati atakapoonekana tutakuwa kama yeye, kwani tutamwona vile alivyo; ili tuwe na tumaini hili; ili tutakaswe hata vile alivyo mtakatifu” (Moroni 7:45–48).
Hili ndilo lengo ambalo Baba yako wa Mbinguni yuko nalo kwenu ninyi, mabinti Zake wenye thamani. Inaweza kuonekana kwenu kama lengo la mbali sana, lakini kutoka kwa mtazamo Wake, hamko mbali sana. Kwa hivyo anawatembelea kwa Roho Wake kuwafariji, kuwahimiza, na kuwatia msukumo wa kusonga mbele.
Ninawaachieni ushuhuda wangu hakika kwamba Baba anawajua—anajua mahitaji yenu na majina yenu—anawapenda, na husikia maombi yenu. Mwana Wake Mpendwa anawaalika mje Kwake., Na Wao watamtuma Roho Mtakatifu kuwasaidia katika juhudi zenu za kuwahudumia wengine kwa niaba Yao.
Kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo, uenzi wa kila mara wa Roho Mtakatifu utakuwa na athari ya kutakasa na kusafisha katika roho yako. Kisha utahisi amani ambayo Mwokozi aliahidi kuwaachia wanafunzi Wake. Kwa amani hiyo litakuja tumaini angavu na hisia za nuru na upendo kutoka kwa Baba na Mwanawe Mpendwa, ambaye huongoza ufalme Wake hapa ulimwenguni kupitia mafunuo hata kwa nabii Wake aishiye. Mimi nashuhuudia hivyo katika jina la Bwana Yesu Kristo, amina.