Andaa Njia
Japokuwa wamekabidhiwa misheni na mamlaka tofauti, Ukuhani wa Haruni na wa Melkizedeki ni wenzi wasiotenganishwa katika kazi ya wokovu.
Nilipokuwa na umri wa miaka 30, nilianza kufanya kazi kwenye kampuni ya rejareja huko Ufaransa. Siku moja rais wa kampuni, mtu mzuri wa imani nyingine, aliniita ofisini kwake. Swali lake lilinishtusha: “Nimegundua kwamba wewe ni kuhani katika kanisa lako. Je, ni kweli?”
Nikajibu, “Ndio, hiyo ni sahihi. Nina ukuhani.”
Alionekana kushangazwa na jibu langu, alidadisi, “Ulisomea kwenye chuo cha dini cha umisionari?”
“Ndio,” Nikamjibu, “kati ya umri wa miaka 14 na 18, na nilijifunza masomo ya seminari karibu kila siku asubuhi!” Karibu apigwe na butwaa.
Kwa mshangao wangu mkubwa, wiki kadhaa baadaye aliniita tena ofisini kwake na kutoa pendekezo la nafasi ya ukurugenzi katika mojawapo ya makampuni. Nilishangazwa na kuelezea wasiwasi wangu kuwa nilikuwa mdogo na nisiye na uzoefu wa kushika wadhifa muhimu. Akiwa na tabasamu la ukarimu, alisema, “Hiyo yaweza kuwa kweli, lakini haijalishi. Ninajua kanuni zako, na nimejua kile ulichojifunza kanisani kwako. Ninakuhitaji.”
Alikuwa sahihi kuhusu kile nilichojifunza Kanisa kwangu. Miaka iliyofuata ilikuwa ya changamoto, na sijui kama ningeweza kuwa na mafanikio bila ya uzoefu nilioupata kwa kuhudumu Kanisani toka nikiwa mdogo.
Nilikuwa na baraka ya kukua katika tawi dogo la Kanisa. Kwa sababu idadi yetu ilikuwa ndogo, vijana waliitwa kushiriki kikamilifu katika mambo yote ya tawi. Nilikuwa na kazi nyingi na nilifurahi kutumika. Jumapili niliongoza kwenye meza ya sakramenti, nilihudumu kwenye akidi nyingi za ukuhani, na kufanya kazi katika miito mingine. Katikati ya wiki mara nyingi niliambatana na baba yangu na wakubwa wengine wenye ukuhani tukiwa tunafundisha waumini, kuwafariji wagonjwa na wenye kusumbuka, na kuwasaidia wenye shida. Hakuna aliyejiona alikuwa mdogo kuhudumu au hata kuongoza. Kwangu mimi, yote yalionekana ya kawaida na asili.
Huduma niliyoitoa wakati wa hiyo miaka ya udogo wangu ilinisaidia kujenga ushuhuda wangu na kutia nanga maisha yangu kwenye injili. Nilizungukwa na watu wazuri na wenye huruma ambao walijitoa kuutumia ukuhani wao kubariki maisha ya wengine. Nilitaka kuwa kama wao. Katika kutumika pamoja nao, zaidi ya nilivyogundua wakati huo, nilijifunza kuwa kiongozi katika Kanisa na pia katika ulimwengu.
Tuna vijana wengi wanaohudhuria au kutizama mkutano huu jioni hii ambao wana Ukuhani wa Haruni. Ninapoutazama umati huu, ninawaona wengi wenu mmekaa na watu wazima, huenda baba zenu, babu zenu, kaka zenu wakubwa, au viongozi wenu wa ukuhani—wote wakiwa na Ukuhani wa Melkizedeki. Wanawapendwa, na kwa sehemu kubwa, wamekuja hapa jioni hii kuwa pamoja nanyi.
Mkusanyiko huu wa vizazi unatoa maono ya ajabu ya umoja na undugu ambao unadumu kati ya kuhani mbili za Mungu. Japokuwa wamekabidhiwa misheni na mamlaka tofauti, Ukuhani wa Haruni na wa Melkizedeki ni wenzi wasiotenganishwa katika kazi ya wokovu. Unakwenda pamoja bega kwa bega na una haja kubwa ya kila moja.
Kielelezo kizuri cha uhusiano wa karibu uliopo kati ya kuhani mbili hupatikana katika mahusiano kati ya Yesu na Yohana Mbatizaji. Je, mtu anaweza kufikiria Yohana Mbatizaji bila Yesu? Je, misheni ya Mwokozi ingekuwa vipi bila kazi ya maandalizi iliyofanywa na Yohana?
Yohana Mbatizaji alipewa kazi kubwa ambayo haijapata kuweko: “kuandaa mapito ya Bwana,”1 kumbatiza Yeye kwa maji, na kuwaandaa watu kumpokea Yeye. Huyu “[mtu] wa haki… na … mtakatifu,”2 ambaye alikuwa ametawazwa katika ukuhani wa chini, alikuwa anaelewa kikamilifu yote umuhimu na uwezo wa misheni na mamlaka yake.
Watu walijaa kwa Yohana ili kumsikiliza na kubatizwa. Aliheshimika na kuthaminiwa katika haki zake mwenyewe kama mtu wa Mungu. Lakini Yesu alipojidhihirisha, Yohana kwa unyenyekevu aliridhia kwa Mtu mkubwa kuliko yeye na alitangaza, “Mimi nabatiza kwa maji: katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi, … yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake.”3
Kwa upande Wake, Yesu Kristo, Mwana Pekee wa Baba, aliye na ukuhani wa juu, kwa unyenyekevu alitambua mamlaka ya Yohana. Kwake yeye, Mwokozi alisema, “Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji.”4
Hebu fikiria kile ambacho kingetokea katika akidi zetu za ukuhani kama mahusiano kati ya watu wenye kuhani mbili wangehuishwa na mpangilio ulioanzishwa na Yesu na Yohana Mbatizaji. Ndugu zangu wadogo wa Ukuhani wa Haruni, kama Yohana, kazi yenu ni “kuandaa njia”5 kwa ajili ya kazi kuu ya Ukuhani wa Melkizedeki. Mnafanya hivi kwa njia nyingi tofauti. Mnasimamia ibada za ubatizo na sakramenti. Mnasaidia kuwaandaa watu kwa Bwana kwa kuhubiri injili, kwa [kutembelea] nyumba ya kila muumini,”6 na “kwa [kulinda] kanisa.”7 Mnatoa msaada kwa maskini na wenye mahitaji kwa kuokota matoleo ya mfungo, na mnashiriki katika kutunza majumba ya mikutano ya kanisa na raslimali zingine. Jukumu lenu ni muhimu, linahitajika, na ni takatifu.
Ndugu zangu watu wazima, iwe ni kina baba, maaskofu, washauri wa Vijana, au watu wenye Ukuhani wa Melkizedeki, mnaweza kufuata mfano wa Mwokozi kwa kuwageukia kaka zenu wenye ukuhani mdogo na kuwaalika kufanya kazi pamoja nanyi. Kwa kweli, mwaliko huu unakuja kutoka kwa Bwana Mwenyewe. Alisema, “Kwa hiyo, wachukueni pamoja nanyi wale waliotawazwa katika ukuhani mdogo, na kuwatuma mbele yenu kuweka ahadi, na kuitengeneza njia, na kutimiza miadi ambayo ninyi wenyewe hamwezi kuitimiza.”8
Mnapowaalika kina kaka wadogo “kuandaa njia,”9 mnawasaidia kugundua na kuheshimu mamlaka takatifu waliyonayo. Kwa kufanya hivyo, mnawasaidia kuandaa njia yao wenyewe wakiwa wanasubiri siku ambayo watapokea na kutenda kazi ukuhani wa juu.
Naomba mniruhusu nishiriki nanyi hadithi ya kweli ya Alex, kuhani kijana, mkimya, makini, na mwerevu. Jumapili moja askofu wa Alex alimkuta akiwa peke yake darasani akiwa na hali ya kukatatamaa. Kijana alielezea ni jinsi ilivyokuwa vigumu kwake kuhudhuria kanisa bila baba yake, ambaye hakuwa muumini. Kisha kwa machozi alisema huenda ingekuwa vyema kwake kuacha Kanisa.
Akiwa na wasiwasi kwa ajili ya kijana huyu, askofu mara moja alilihamasisha baraza la kata ili kumsaidia Alex. Mpango wake ulikuwa rahisi: ili kumfanya Alex awe imara na kumsaidia kukuza ushuhuda wa injili kutoka moyoni, walihitaji “kumzunguka na watu wazuri na kumpa kazi muhimu za kufanya.”
Haraka ndugu wa ukuhani na waumini wote wa kata walimuendea Alex na kumwonyesha mapenzi yao na kutoa msaada. Kiongozi wa kundi la makuhani wakuu, mtu mwenye imani na upendo mkubwa, alichaguliwa kuwa mwenza wake wa ualimu wa nyumbani. Washiriki wa uaskofu walimchukua kwenye mabawa yao na kumfanya rafiki yao wa karibu.
Askofu alisema: “Tulimpa Alex kazi nyingi. Alikaribisha kwenye harusi, alikaribisha katika misiba, alinisaidia kuweka wakfu makaburi, kubatiza waumini kadhaa wapya, kuwatawaza vijana katika ofisi za ukuhani wa haruni, alifundisha masomo ya vijana, alifundisha pamoja na wamisionari, alifungua milango kwa ajili ya mikutano, na kufunga milango nyakati za jioni baada ya mikutano mikuu. Alifanya miradi ya huduma, aliungana nami katika kutembelea waumini wazee hospitalini, kutoa maongezi katika mkutano wa sakramenti, kuhudumia sakramenti kwa wagonjwa mahospitalini au katika nyumba zao, na akawa ni miongoni mwa watu wachache ambao niliwategemea kama askofu.”
Kidogo kidogo, Alex alibadilika. Imani yake kwa Bwana iliongezeka. Alipata kujiamini yeye mwenyewe na katika nguvu za ukuhani aliokuwa nao. Askofu alimalizia: “Alex amekuwa na ataendelea kuwa mojawapo ya msaada wangu mkubwa wakati wa kipindi changu cha uaskofu. Ni nafasi nzuri kiasi gani kuhusiana naye. Ninaamini kwa dhati kwamba hakuna kijana aliyekwenda Misheni akiwa amejiandaa vilivyo kwa huduma yake ya ukuhani.”9
Maaskofu wangu wapendwa, katika kutawazwa na kusimikwa kama askofu wa kata yako, una wito mtakatifu wa kuhudumu kama rais wa Ukuhani wa Haruni na akidi za makuhani. Ninajua mizigo mizito mnayobeba, lakini mnatakiwa kuzifanya kazi zenu kwa ajili ya vijana hawa kuwa mojawapo ya majukumu yenu ya juu. Humwezi kukwepa au kumpa mtu mwingine jukumu lenu katika wajibu huu.
Nawaalikeni kutafakari juu ya kila kijana wa Ukuhani wa Haruni katika kata yenu. Hata mmoja wao kamwe asihisi ameachwa nyuma au hafai. Je, kuna kijana yeyote ambaye ninyi na ndugu wengine mnaweza kumsaidia? Mualike ahudumu pamoja nanyi. Mara nyingi tunajaribu kuwafurahisha vijana wetu na kuwaacha wawe mashabiki, wakati imani zao na upendo katika injili unaweza kuendelezwa kwa kuufanyia kazi ukuhani. Kwa kushiriki kwa dhati katika kazi ya wokovu, wataunganishwa na mbingu na watatambua umuhimu wao mtakatifu.
Ukuhani wa Haruni ni zaidi ya kundi la umri, kazi ya programu ya kufundisha, au neno la kuonyesha vijana wa Kanisa. Ni nguvu na mamlaka ya kushiriki katika kazi kubwa ya kuokoa nafsi—nafsi zote za wale vijana wenye ukuhani na wale wanao watumikia. Acha tuuweke Ukuhani wa Haruni katika sehemu nzuri, sehemu iliyochaguliwa, na sehemu ya huduma, maandalizi, na utimilifu kwa ajili ya vijana wa Kanisa.
Wapendwa ndugu zangu wa Ukuhani wa Haruni, ninawaalika kuimarisha kiungo muhimu ambacho kinaunganisha kuhani mbili za Mungu. Wapeni mamlaka vijana wa Ukuhani wa Haruni kuandaa njia mbele yenu. Waambie kwa kujiamini, “Ninakuhitaji.” Kwenu ninyi wenye Ukuhani wa Haruni, ninaomba kwamba mnapohudumu na ndugu wakubwa, mtasikia sauti ya Bwana ikiwaambia: “Umebarikiwa wewe, kwani utafanya mambo makubwa. Tazama wewe umetumwa, kama vile Yohana, kuitengeneza njia mbele yangu.”10 Katika jina la Yesu Kristo, amina.