Yesu Akamkazia Macho na Akampenda
Wakati wowote unapohisi umeombwa kufanya kitu kigumu, fikiria kuhusu Bwana akikukazia macho akikupenda na akikualika kumfuata Yeye.
Miaka kadhaa iliyopita niliitwa pamoja na mke wangu Jacqui, kusimamia misheni ya Washington Spokane. Tulifika katika eneo la misheni tukiwa na hisia mchanganyiko za woga na kusisimuka juu ya majukumu ya kufanya kazi pamoja na wamisionari wengi wadogo wa ajabu. Walitoka katika matabaka mengi tofauti na mara wakawa kama wana na mabinti zetu.
Ingawa wengi walikuwa wakifanya vizuri, wachache walihangaika na matarajio ya juu ya miito yao. Nakumbuka mmisionari mmoja akiniambia “Rais, siwapendi watu tu.” Baadhi waliniambia walikosa hamu ya kufuata sheria ngumu za umisionari Nilikuwa na wasiwasi na nikashangaa nini tungefanya kubadili mioyo ya wamisionari hao wachache ambao bado hawakuwa wamejifunza furaha ya kuwa watiifu.
Siku moja wakati nikiendesha gari kupita mashamba mazuri ya ngano kwenye mpaka wa Washington–Idaho, nilikuwa nasikiliza rekodi ya Agano la Jipya. Nilisikiliza maelezo yayojulikana ya kijana tajiri akija kwa Mwokozi kuuliza nini angefanya kupata uzima wa milele, nilipokea ufunuo binafsi usiotarajika lakini muhimu ambao sasa ni kumbukumbu takatifu.
Baada ya kumsikia Yesu akinukuu amri na kijana akijibu amekuwa akishika amri hizo tangu ujana wake, nilimsikiliza masahihisho ya Mwokozi ya upole: “Unapungukiwa na kitu kimoja: … uza vyote ulivyonavyo, na … njoo, … unifuate.”1 Lakini kwa mshanagao wangu, badala yake nilisikia maneno sita kabla ya mistari hiyo, ambayo niloyaona kama sijawahi kuyasikia au kuyasoma. Yalikuwa kama vile yaliongezwa kwenye maandiko matakatifu. Nilishangaa kwa uelewa wa kuvutia ambao ulifunguliwa.
Ni maneno sita yapi ambayo yalikuwa na matokeo ya kina? Sikiliza uone kama utaweza kuyatambua maneno haya ambayo yanonekana ya kawaida, ambayo hayapatikani katika maelezo ya injili yoyote isipokuwa injili ya Marko.
“Mtu mmoja akaja mbio, … akamwuliza, Mwalimu Mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?
“Na Yesu akamwambia, …
“Wazijua amri, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako.
Akamwambia … , Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu.
“Ndipo Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja: Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha beba msalaba na unifuate.”2
“Ndipo Yesu akamkazia macho akampenda.”
Niliposikia maneno haya, taswira kamilifu ikajaza mawazo yangu ya Bwana akisubiri na kumkazia machokijana huyu. Kumkazia macho—kumwangalia kwa undani na kwa kipenyo katika nafsi yake akitambua uzuri wake na pia umuhimu wake pia akitambua mahitaji yake makuu.
Ndipo kwa maneno rahisi—Yesu akampenda. Alihisi upendo wa ajabu na huruma kwa kijana huyu mzuri, na kwa sababu ya upendo huu, na kwa upendo huu, Yesu aliuliza hata zaidi kutoka kwake. Nikapiga twasira ni jinsi gani kijana huyu tajiri angehisi kufunikwa na upendo huo hata pale ambapo aliulizwa kufanya kitu kigumu sana kama kuuza vyote alivyonavyo na kuwapa maskini.
Wakati huo, nilijua haikuwa ni mioyo tu ya baadhi ya wamisionari wetu ambayo ilihitaji kubadilika. Ulikuwa ni moyo wangu pia. Swali si tena “Ni jinsi gani rais wa misheni aliyevunjika moyo anaweza kumsaidia mmsionari anayehangaika aweze kuwa bora? Badala yake, swali lilikuwa “Ninaweza kujazwa vipi na upendo wa Kristo ili mmisionari aweze kuhisi upendo wa Mungu kupitia mimi na apate hamu ya kubadilika?” Nawezaje kuwakazia macho kwa namna ile Bwana alimkazia macho kijana tajiri, kuwaona kwa uhalisia walivyo na jinsi watavyokuwa, kuliko tu kile ambacho wanafanya au hawafanyi? Ninawezaje kuwa zaidi kama Mwokozi?
“Ndipo Yesu akamkazia macho akampenda.”
Kuanzia wakati huo na kuendelea, ninapopiga magoti pamoja na kijana mmisionari anayesumbuka na baadhi ya kipengele cha utiifu, ndani ya moyo wangu sasa niliona msichana au mvulana mwaminifu ambaye alifuata hamu ya kuja misheni. Halafu niliweza kusema kwa hisia zote kama zile za mzazi mpole:3 “Mzee au Dada, kama nisingekupenda nisingejali nini kinatokea katika misheni yako. Lakini nakupenda, na kwa sababu nakupenda, najali kile utakachokuwa. Kwa hiyo nakualika kubadili vile vitu ambavyo ni vigumu kwako na kuwa vile Bwana anataka uwe.
Kila muda nilipokwenda kuwasahili wamisionari, nilisali kwanza kwa zawadi ya hisani na kwamba niweze kumuona kila mzee na dada kama Bwana awaonavyo.
Kabla ya mkutano wa kanda, pale dada Palmer na mimi tulipomsalimia kila mmisionari mmoja mmoja, nilisubiri na kuwaangilia kwa kina katika macho yao, kuwakazia macho wao—usahili bila maneno—na bila kufeli, nilijazwa na upendo mkuu kwa hawa wana na mabinti wa thamani wa Mungu.
Nimejifunza mafunzo mengi ya kubadili maisha kupitia uzoefu huu wa kibinafsi wa kina kupitia Marko sura ya 10. Hapa kuna mafunzo manne naamini yatatumsaidia kila mmoja wetu:
-
Tunapojifunza kuwaona wengine kama vile Bwana awaonavyo kuliko kwa macho yetu tu, upendo wetu kwao utakua na pia hamu yetu ya kuwasaidia. Tutaona uwezo ndani ya wengine ambao hawauoni ndani yao wenyewe. Kwa upendo wa Kristo hatutaogopa kuongea kwa ujasiri, kwani “upendo mkamilifu huondoa hofu.”4 Na hatutakata tamaa, tukikumbuka kuwa wale ambao ni vigumu kuwapenda wanahitaji upendo zaidi.
-
Hakuna ufundishaji wala kujifunza kutaweza kutokea kukifanywa katika kuvunjika moyo au hasira, na mioyo haitabadilika ambapo upendo haupo. Iwe ni katika kufanya majukumu yetu kama wazazi, walimu, au viongozi, mafunzo ya kweli yatatokea katika hali ya uaminifu kuliko kushutumu. Nyumba zetu kila mara lazima ziwe kimbilio salama kwa watoto wetu—si mazingira kandamizi.
-
Upendo usikosekane pale mtoto, rafiki au mwanafamilia anapofeli kuishi kufikia matarajio yetu. Hatujui nini kilitokea kwa kijana tajiri baada ya kuondoka kwa huzuni, lakini nina ujasiri Yesu bado alimpenda kikamilifu ingawa alichagua njia rahisi. Labda baadae katika maisha, baada ya kukuta utajiri wake mkuu hauna kina, alikumbuka na akafuata uzoefu wa Bwana Wake akimkazia macho, kumpenda na kumwalika amfuate Yeye.
-
Kwa sababu anatupenda, Bwana hutegemea mengi kutoka kwetu. Kama tu wanyenyekevu, tutakubali mwaliko wa Bwana wa kutubu, kutoa dhabihu na kutumikia kama ushahidi wa pendo Lake kamilifu kwetu. Hata hivyo, mwaliko wa kutubu pia ni mwaliko wa kupokea zawadi nzuri ya msamaha na amani. Kwa hivyo, “usiyadharau … marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye: Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi.”5
Kaka zangu na dada zangu wapendwa wakati wowote unapohisi umeombwa kufanya jambo gumu—kuacha tabia mbovu au uraibu, kuweka pembeni vitu vya kidunia kwa sababu ni Sabato, kumsamehe mtu ambaye amekukosea—fikiria kuhusu Bwana akikukazia macho , akikupenda na kukualika kuacha na kumfuata Yeye. Na mshukuru Yeye kwa kukupenda vya kutosha kukualika kufanya zaidi.
Ninashuhudia kuhusu Mwokozi, Yesu Kristo, na ninatazamia siku ile atakayoweka mikono kumkumbatia kila mmoja wetu, akitukazia macho na kutuzunguka na upendo Wake kamili. Katika jina la Yesu Kristo, amina.