Aliye Mkubwa Miongoni Mwenu
Zawadi kuu sana ya Mungu inawaendea wale wanaohudumu bila kutarajia zawadi.
Kaka zangu wapendwa, marafiki zangu wapendwa, nina shukrani jinsi gani kuwa pamoja nanyi katika huu mkutano wa ukuhani wenye mwongozo wa ulimwengu kote. Rais Monson, tunakushukuru kwa ajili ya ujumbe wako na baraka zako. Sisi daima tutayatia moyoni maneno yako ya maelekezo, ushauri, na hekima. Sisi tunakupenda na tunakukubali, daima tunakuombea. Wewe hakika ni nabii wa Mungu. Wewe ni Rais wetu. Sisi tunakukubali, tunakupenda.
Karibu miongo miwili iliyopita, Hekalu la Madrid Uhispania liliwekwa wakfu na likaanza huduma yake kama nyumba tukufu ya Bwana. Harriet nami tunakumbuka vyema kwa sababu nilikuwa nikihudumu katika Urais wa Eneo la Uropa wakati huo. Pamoja na wengine wengi, tulitumia muda mwingi mno tukishughulikia utondoti wa kupanga na kuandaa matukio yaliyotangulia kuweka wakfu.
Tarehe ya kuweka wakfu ilipokuwa ikikaribia, niligundua ya kwamba sikuwa nimepokea mwaliko wa kuhudhuria. Hili halikuwa limetazamiwa. Baada ya yote, katika majukumu yangu kama Rais wa Eneo, nilikuwa nimehusika pakubwa katika mradi huu wa hekalu na nilihisi kiasi kidogo cha umiliki wake.
Nilimwuliza Harriet ikiwa alikuwa ameona mwaliko. Hakuwa ameuona.
Siku zilipita na wasiwasi wangu ukazidi. Niliwaza ikiwa mwaliko wetu ulikuwa umepotea—pengine ulikuwa katikati ya mito ya sofa. Pengine ulikuwa umechanganyika na barua taka na kutupwa. Majirani walikuwa na paka mdadisi, na hata nikaanza kumtazama kwa nikimshuku.
Hatimaye nililazimika kukubali ukweli kwamba: Sikuwa nimealikwa.
Lakini hili liliwezekanaaje? Je, nilikuwa nimetenda kosa lolote? Je, kunaye mtu yeyote aliyedhania kwamba ilikuwa mbali mno kwetu kusafiri? Je, nilikuwa nimesahaulika?
Hatimaye, niligundua ya kwamba mfululizo huu wa mawazo ulielekea hadi mahali ambapo sikuwa nataka kufanya makao.
Harriet nami tulijikumbusha ya kwamba kuwekwa wakfu kwa hekalu haikuwa juu yetu. Haikuwa juu ya yule aliyestahili kualikwa au yule asiyestahili. Na haikuwa inahusu hisia zetu au hisia zetu za kuwa na haki.
Ilihusu kuweka wakfu kwa jengo takatifu, hekalu la Mungu Aliye Juu Sana. Ilikuwa ni siku ya kufurahi kwa waumini wa Kanisa kule Uhispania.
Ikiwa ningealikwa kuhudhuria, ningelifanya hivyo kwa furaha. Lakini ikiwa sikuwa nimealikwa, furaha yangu haingepunguka vyovyote. Harriet nami tungefurahia pamoja na marafiki zetu, kina ndugu na dada zetu wapendwa, kutoka mbali. Tungemsifu Mungu kwa baraka hii ya ajabu kwa shauku kutoka nyumbani kwetu Frankfurt jinsi tungefanya kule Madrid.
Wana wa Ngurumo
Miongoni mwa wale Kumi na Wawili ambao Yesu aliita na kutawaza kulikuwepo na ndugu wawili, Yakobo na Yohana. Je mnakumbuka jina la utani alilowapa?
Wana wa Ngurumo (Boanerge).1
Huwezi kupata jina la utani kama hilo bila historia ya kuvutia hapo awali. Kwa bahati mbaya maandiko hayaelezi kwa undani kuhusu chanzo cha jina hilo la utani. Hata hivyo, tunapata kuona tu kidogo tabia ya Yakobo na Yohana. Hawa ni wale wale kaka wawili ambao walipendekeza waagize moto kutoka juu mbinguni katika kijiji cha Samaria kwa sababu ya kutoalikwa mjini.2
Yakobo na Yohana walikuwa wavuvi—labda wakali—lakini nadhania walifahamu sana kuhusu nguvu za asili. Hakika, walikuwa wanaume wa vitendo.
Katika tukio moja, Mwokozi alipokuwa akijitayarisha kufanya safari yake ya mwisho kuingia Yerusalemu, Yakobo na Yohana walimkaribia na ombi maalum—moja pengine lililostahiki jina lao la utani.
“Twataka utufanyie lo lote tutakalokuomba. ,” walisema.
Ninaweza kufikiria Yesu akitabasamu alipowajibu, “Mwataka niwafanyie nini?”
“Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako.”
Mwokozi sasa aliwachochea wafikiria kwa kina kidogo kuhusu walichokuwa wakitaka na akasema, “Lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari.”3
Kwa njia nyingine, hauwezi kupata heshima katika ufalme wa mbinguni kupitia kampeni. Wala “kula chakula na watu maarufu” kwa madhumuni ya kuingia katika utukufu wa milele.
Wakati wale Mitume wengine kumi walisikia kuhusu ombi hili kutoka kwa Wana wa Ngurumo, wakakasirikia. Yesu alijua ya kwamba muda Wake ulikuwa kidogo, na akiona ubishi miongoni mwa wale ambao wangeendeleza kazi Yake ni lazima ilimpa wasiwasi.
Alisema na wale Kumi na Wawili kuhusu asili ya nguvu na jinsi inavyoathiri wale wanaoitafuta na kuipata. “Wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa,” Alisema, “huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha.”
Karibu naweza kumuona Mwokozi, akitazama kwa upendo usio na mwisho katika nyuso za wale wanafunzi waaminifu wenye imani. Karibu naweza kusikia sauti Yake ya kusihi. “Lakini haitakuwa hivyo kwenu. Bali, mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu: Na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote.”4
Katika ufalme wa Mungu, ukubwa na uongozi humaanisha kuwaona wengine jinsi walivyo kweli—jinsi Mungu anavyowaona—na kisha kuwafikia na kuwatumikia. Humaanisha kufurahia na wale walio na furaha, kulia na wale walio na huzuni, kuwainua wale walio katika shida, na kumpenda jirani yetu jinsi Yesu anavyotupenda. Mwokozi anawapenda wana wa Mungu wote bila kujali hali yao ya kijamii na uchumi, mbari, lugha, mtazamo wa kisiasa, au utaifa, au makundi yoyote mengine. Na sisi tunafaa kuwa hivyo!
Zawadi kuu sana ya Mungu inawaendea wale wanaohudumu bila kutarajia zawadi. Inawaendea wale wanaohudumu bila ya kutangaza: wale ambao kimya kimya hutafuta njia za kuwasaidia wengine: wale ambao huwatumikia wengine kwa sababu tu wanampenda Mungu na wana wa Mungu.5
Usikubali Haya Yaingie Kichwani Mwako
Muda mfupi baada ya mwito wangu kama Kiongozi Mwenye Mamlaka, nilipewa heshima ya kuandamana na Rais James E. Faust kwa upangaji mpya wa kigingi. Nilipokuwa nikiendesha gari kuelekea kwenye jukumu letu kule Kusini mwa Utah, Rais Faust alikuwa mkarimu kutumia wakati huo kunifundisha. Somo moja ambalo sitawahi sahau. Alisema, “Waumini wa Kanisa wana na heshima sana kwa Viongozi wakuu wenye Mamlaka. Watakutendea kwa ukarimu na kusema maneno mazuri juu yako.” Kisha akatua na kusema, “Dieter, siku zote kuwa mwenye shukrani kwa haya, lakini usikubali haya yaingie kichwani mwako.”
Somo hili muhimu kuhusu huduma ya Kanisa linafaa kila mmoja ya wenye ukuhani katika kila jamii ya Kanisa. Linatufaa sisi sote katika Kanisa hili.
Wakati Rais J. Reuben Clark aliwashauri wale walioitwa katika nafasi zenye mamlaka Kanisani, aliwaambia wasisahau sheria ya sita.
Bila ya kuepuka, mtu huyo aliuliza, “Sheria ya sita ni ipi?”
“Usijichukulie kwa uzito kabisa,” alisema.
Bila shaka, hili lilielekeza kwa swali la kufuatilia: “Ni zipi sheria zingine tano?”
Na uangavu machoni, Rais Clark angelisema, “Hamna zingine.”6
Ili tuwe viongozi wa Kanisa wanaofaa, ni lazima tujifunze somo hili muhimu: Uongozi Kanisani hauhusiki sana na kuwaelekeza wengine kama unavyohusika na sisi kuwa radhi kuelekezwa na Mungu.
Miito kama Nafasi za Huduma.
Kama Watakatifu wa Mungu Aliye Juu Sana, tunafaa “kuwakumbukeni katika mambo yote maskini na wenye shida, wagonjwa na walioteseka, kwani yule asiyefanya mambo haya, huyu siyo mwanafunzi wangu.”7 Nafasi za kuwahudumia wengine ni nyingi mno. Tunaweza kuzipata katika jumuia yetu, katika kata zetu na matawi, na bila shaka nyumbani kwetu.
Na juu ya hayo, kila muumini wa Kanisa anapewa nafasi maalum ya kuhudumu. Tunaziita nafasi hizi “miito”—neno ambalo linafaa kutukumbusha kuhusu ni nani ambaye anatuita tuhudumu. Tukipokea miito yetu kama nafasi za kumtumikia Mungu na kuwatumikia wengine kwa imani na unyenyekevu, kila kitendo cha huduma kitakuwa ni hatua katika njia ya uanafunzi. Katika njia hii, Mungu hajengi tu Kanisa Lake bali pia anajenga watumishi Wake. Kanisa limeundwa kwa ajili ya kutusaidia kuwa wanafunzi wakweli na waaminifu wa Kristo, wana na mabinti wa Mungu wazuri na waadilifu. Hili halifanyiki tu wakati tunapohudhuria mikutano na kusikiliza hotuba, bali pia tunapotoka nje na kuhudumu. Hivi ndivyo tunakuwa “wakubwa” katika ufalme wa Mungu.
Tunakubali miito kwa neema, unyenyekevu na shukrani. Wakati tunapopumzishwa kutoka miito hii, tunakubali mabadiliko haya kwa neema ile ile, unyenyekevu, na shukrani.
Mbele ya Mungu hamna mwito katika ufalme ulio muhimu kuliko mwingine. Huduma yetu—iwe kubwa au ndogo—inasafisha roho zetu, inafungua madirisha ya mbinguni, na kuachilia baraka za Mungu sio tu juu ya wale tunaohudumu bali juu yetu pia. Wakati tunapowafikia wengine, tunaweza kujua hakika kwa unyenyekevu kwamba Mungu anatambua huduma yetu kwa idhinisho na sifa. Anatabasamu juu yetu wakati tunapofanya vitendo hivi vya huruma, hasa vile vitendo visivyoonekana na kutambuliwa na wengine.8
Kila wakati tunapojitolea kwa wengine, tunachukua hatua karibu na kuwa wanafunzi wazuri na wa kweli wa yule aliyejitolea kikamilifu kwa kila mmoja wetu.
Kutoka Kusimamia hadi kwa Gwaride
Wakati wa maadhimisho ya miaka 150 ya kuwasili kwa watangulizi katika Bonde la Salt Lake, Ndugu Myron Richins alikuwa akihudumu kama rais wa kigingi kule Henefer, Utah. Maadhimisho hayo yalijumuisha kuigiza kwa safari ya watangulizi wakipitia mjini mwake.
Rais Richins alihusika pakubwa sana na mipango ya maadhimisho hayo, na alihudhuria mikutano mingi mno na Viongozi wenye Mamlaka pamoja na wengine kujadili matukio. Yeye alikuwa ameshikamana.
Kabla tu ya maadhimisho, kigingi cha Rais Richins kilipangwa upya, na akapumzishwa kama Rais. Katika Jumapili iliyofuata, alikuwa akihudhuria mkutano wa ukuhani wa kata yake wakati viongozi waliuliza watu wajitolee ili watoe usaidizi wakati wa maadhimisho. Rais Richins, pamoja na wengine, aliinua mkono wake na akapewa maelekezo kwamba avae mavazi yake ya kazi na alete gari lake pamoja na koleo.
Hatimaye, asubuhi ya tukio hilo kubwa ikaja, na Rais Richins akaripoti kwa jukumu lake la kujitolea.
Wiki chache tu hapo mbeleni, alikuwa mchangiaji mwenye ushawishi katika kupanga na kusimamia tukio hili kubwa. Siku hiyo, hata hivyo, kazi yake ilikuwa kuwafuata farasi katika gwaride na kusafisha walipochafua.
Rais Richins alifanya hivyo kwa shukrani na furaha.
Alielewa kwamba aina moja ya huduma sio muhimu kuliko nyingine.
Alijua na aliyaweka maneno ya Mwokozi katika vitendo: “Atakaye kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu.”9
Kushiriki Uanafunzi kwa Njia Sahihi
Mara nyingine, kama wana wa ngurumo tunatamani nafasi za umaarufu. Tunajitahidi ili tutambuliwe. Tunatafuta kuwa viongozi na kuchangia katika njia za kukumbukwa.
Hakuna jambo baya na kutaka kumhudumia Bwana, lakini tunapotafuta kupata ushawishi Kanisani kwa ajili yetu—ili tupokee sifa na pongezi za wanadamu—tumepata zawadi yetu. Wakati sifa za wengine “zinapotuingia kichwani”, sifa hizo zitakuwa fidia yetu.
Ni mwito gani ndiyo muhimu zaidi Kanisani? Ni ule ulionao sasa hivi. Haijalishi jinsi ulivyo wa kunyenyekeza au unavyoonekana maarufu, mwito ulio nao sasa hivi ndio utakaokuwezesha sio tu kuinua wengine lakini pia kuwa mwana wa Mungu uliyeumbwa kuwa.
Marafiki zangu wapendwa na ndugu zangu katika ukuhani, inua mahali uliposimama!
Paulo aliwafundisha Wafilipi, “Badala ya kutiwa motisha na ubinafsi au ubatili, kila mmoja wenu anapaswa, kwa unyenyekevu, kuwa na msukumo wa kumtendea mwenzake kama ambaye ni muhimu kukuliko.”10
Kuhudumu kwa Heshima
Kutafuta heshima na umaarufu Kanisani badala ya huduma ya kweli na yenye unyenyekevu kwa wengine ndiyo biashara aliyofanya Esau.11 Tunaweza kupokea zawadi ya hapa duniani, lakini itakuja kwa bei ghali mno—kupoteza kukubalika mbinguni.
Na tufuate mfano wa Mwokozi wetu, ambaye alikuwa mpole na mnyenyekevu, ambaye hakutafuta sifa za wanadamu lakini kutenda mapenzi ya Baba Yake.12
Na tuwahudumie wengine kwa unyenyekevu—kwa nguvu, shukrani, na heshima. Hata kama matendo yetu ya ukarimu yanaweza kuonekana kama dhaifu, madogo, au ya thamani ndogo, wale ambao hutafuta kuhudumu kutokana na ukarimu na huruma kwa wengine siku moja watajua thamani ya huduma yao kupitia neema ya milele ya Mwenyezi Mungu.13
Ndugu zangu wapendwa, marafiki zangu wapendwa, acheni tutafakari, tuelewe, na kuishi hili somo kuu la uongozi wa Kanisa na utawala wa ukuhani: “Mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu:” Haya ni maombi na baraka zangu katika jina takatifu la Bwana wetu, Mkombozi wetu, katika jina la Yesu Kristo, amina.