2010–2019
Kukusanya Familia ya Mungu
Aprili 2017


18:1

Kukusanya Familia ya Mungu

Ninashuhudia kuwa Mungu Baba anawataka watoto Wake tena nyumbani katika familia na utukufu.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, nina furaha kwa nafasi hii ya kujumuika nanyi katika mwanzo wa kikao hiki cha mkutano mkuu. Ninawakaribisha kwa moyo mkunjufu.

Mkutano mkuu daima umekuwa ni muda wa kukusanyika kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho Kwa muda mrefu wingi wetu umezidi uwezo kukusanyika sehemu moja, lakini Bwana ametoa njia ambazo kwazo baraka za mkutano mkuu zinawafikia bila kujali mahali mnapoishi. Wakati inavutia kuona mkusanyiko wa Watakatifu katika hiki Kituo kikubwa cha Mikutano, sisi ambao tunasimama katika mimbari hii daima katika macho yetu ya kimawazo tunawaona mamilioni ya watu waliokusanyika nasi kote duniani wakiangalia na kusikiliza mkutano. Wengi wenu mmekusanyika na familia zenu; baadhi wanaweza kukusanyika pamoja na marafiki au waumini wenza wa kanisa.

Kokote mlipo, na kwa vyovyote mnavyoisikia sauti yangu, tafadhali jueni kwamba ingawa hamko nasi kimwili, tunahisi kuwa mko nasi kiroho. Tunatumaini ninyi nyote mtajihisi kuwa pamoja nasi—kwamba mtahisi nguvu ya kiroho ambayo huja kila mara mkusanyiko wa waaminio hukusanyikapo katika jina Yesu Kristo.

Nimehisi kuvutiwa kuzungumza nanyi leo kuhusu mkusanyiko wa aina nyingine. Aina hii haitokei kila baada ya miezi sita pekee, kama mkutano mkuu unavyofanyika. Badala yake, umekuwa ukiendelea bila kikomo tangu siku za kale za Urejesho wa Kanisa, na umekuwa ukishika kasi miaka ya hivi karibuni. Ninazungumzia mkusanyiko wa familia ya Mungu.

Kuelezea mkusanyiko huu, itakuwa vizuri zaidi kuanza kabla hatujazaliwa, kabla ya kile Biblia huita “mwanzo” (Mwanzo1:1). Kipindi hicho tuliishi na Baba wa Mbinguni kama watoto Wake wa kiroho. Hii ni kweli kwa kila mtu ambaye amewahi kuishi duniani.

Unaona, majina “kaka” na “dada” sio tu salamu za kirafiki au usemi wa kuonyesha upendo kwetu. Ni ya kuonyesha ukweli wa milele: Mungu ni Baba halisi wa watu wote; sisi sote ni sehemu ya familia Yake ya milele. Kwa sababu anatupenda kwa upendo wa Baba mkamilifu, Yeye anataka tukue na kuendelee na kuwa kama Yeye. Alitawaza mpango ambao tungekuja duniani, katika familia, na kupata uzoefu ambao ungetuandaa kurudi Kwake na kuishi kama aishivyo.

Kitovu cha mpango huu kilikuwa ni ahadi kuwa Yesu Kristo atateseka kama dhabihu, kutuokoa kutoka kwa dhambi na mauti. Kazi yetu katika mpango huo ni kukubali dhabihu ya Kristo kwa kutii sheria na ibada za injili. Mimi na wewe tulikubali mpango huu. Ukweli, tuliufurahia, japokuwa ilimaanisha kwamba tungeondoka katika uwepo wa Baba yetu na hata kusahau yale tuliyoyapitia huko pamoja Naye.

Lakini hatukutumwa hapa tukiwa gizani. Kila mmoja wetu alipewa sehemu ya nuru ya Mungu iitwao “Nuru ya Kristo” ili kutusaidia kutofautisha kati ya mema na mabaya, sahihi na yasiyo sahihi. Hii ndio maana wale wanaoishi na kidogo au bila maarifa ya mpango wa Baba bado wanahisi, mioyoni mwao, kwamba matendo fulani ni ya haki na mema wakati mengine sivyo.

Hisi zetu za mema na mabaya huonekana hasa wa umakini pale tunapowalea watoto wetu. Hulka ya karibu kila mzazi ni hamu ya kuwafundisha watoto wao maadili mema. Hii ni sehemu ya muujiza wa mpango wa Baba wa Mbinguni. Anataka watoto Wake waje duniani, wakifuata mfumo wa milele wa familia uliopo mbinguni. Familia ni vikundi vya msingi katika ufalme wa milele, na hivyo Yeye ananuia kuwa viwe vikundi vya msingi pia katika dunia. Ingawa familia za kidunia ziko mbali sana na ukamilifu, huwapa watoto wa Mungu nafasi nzuri sana ya kukaribishwa katika ulimwengu kwa upendo pekee duniani ambao hukaribia ule ambao tuliuona mbinguni—pendo la wazazi. Familia pia ni njia nzuri sana ya kutunza na kurithisha maadili mema na kanuni za kweli ambazo zaidi zinaweza kutuongoza kurudi katika uwepo wa Mungu.

Ni sehemu ndogo tu ya watoto wa Mungu hupata, katika maisha haya, uelewa kamili wa mpango wa Mungu, pamoja na njia ya kufikia ibada na maagano ukuhani ambayo hufanya nguvu ya upatanisho wa Mwokozi kufanya kazi kikamilifu maishani mwetu. Hata wale wenye wazazi bora sana wanaweza kuishi kiuaminifu kulingana na nuru walionayo lakini kamwe wasisikie kuhusu Yesu Kristo na upatanisho Wake au kualikwa kubatizwa katika jina Lake. Hii imekuwa kweli kwa mamilioni yasiyohesabika ya kaka na dada zetu katika historia nzima ya ulimwengu.

Baadhi wanaweza kuchukulia kuwa hii si haki. Wanaweza hata kuchukulia hili kama ushahidi kuwa hakuna mpango, hakuna vigezo maalum kwa ajili ya wokovu—kuhisi kuwa Mungu wa haki na upendo asingeunda mpango ambao unapatikana kwa sehemu ndogo ya watoto Wake. Wengine wanaweza kuhitimisha kwamba Mungu lazima alinuia mapema kuwa nani kati ya watoto Wake ambaye angemwokoa na kufanya injili ipatkane kwao, wakati wale ambao kamwe hawakuwahi kusikia injili ni kwamba tu hawakuwa “wamechaguliwa.”

Lakini mimi na wewe tunajua, kwa sababu ya kweli zilizorejeshwa na Nabii Joseph Smith, kwamba mpango wa Mungu ni wa upendo na haki kuliko inavyofikiriwa. Baba Yetu wa Mbinguni anatamani kuwakusanya na kubariki familia Yake yote. Wakati anajua kwamba si wote kati yao watachagua kukusanyika, mpango Wake hutoa nafasi kwa kila mtoto Wake kukubali au kukataa mwaliko Wake. Na familia ni moyo wa mpango Wake.

Karne kadhaa zilizopita, nabii Malaki alisema kwamba katika siku ijayo, Mungu angemtuma Eliya “kugeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao” (Malaki 4:6).

Unabii huu ulikuwa muhimu sana, Mwokozi aliunukuu alipotembelea mabara ya Amerika baada ya kufufuka kwake (ona 3 Nefi 25:5–6). Na wakati malaika Moroni alipomtembelea Nabii Joseph Smith, pia alinukuu unabii kuhusu Eliya na mioyo, baba na watoto (ona Historia ya–Joseph Smith 1:36–39).

Leo ni Aprili 1. Siku mbili kutoka sasa, Aprili 3, itatimia miaka 181 toka siku unabii wa Malaki ulipotimizwa. Siku hiyo Eliya alikuja na akampa Joseph Smith nguvu ya ukuhani kuunganisha familia milele (ona M&M 110:13–16).

Tangu siku hiyo mpaka leo, shauku ya kutafiti historia ya familia ya mtu imekuwa kwa kipeo. Kwa kiwango kikubwa, watu wameonekana kusogea karibu na mababu zao zaidi ya shauku tu ya kawaida. Maktaba za elimu ya nasaba, mashirika na teknolojia vimetokeza kote ulimwenguni kusaidia hili. Nguvu ya intanenti ili kusaidia katika mawasiliano imewezesha familia kufanya kazi pamoja kutafiti historia ya familia kwa kasi na kwa undani zaidi kuliko ilivyowezekana zamani.

Kwa nini haya yote yanatokea? Kwa kukosa neno sahihi zaidi, tunaita hili “Roho ya Eliya.” Tunaweza kuita pia utimizajiwa unabii. Ninashuhudia kuwa Eliya alikuja. Mioyo ya watoto—wangu na wako imegeuzwa kwa baba zetu, mababu zetu. Upendo unaouhisi kwa mababu zako ni sehemu ya utimizaji wa unabii huo. Umekaa ndani kwa kina katika fikira za wewe ni nani. Lakini inahusu zaidi ya DNA ya kurithi.

Kwa mfano, unapofuata msukumo wa kujifunza kuhusu historia ya familia yako, unaweza kugundua kuwa ndugu wa mbali anashiriki baadhi ya sifa za mwonekano wako wa vitu upendavyo katika vitabu au kipaji chako katika kuimba. Hii inaweza kuwa ya kuvutia sana na ni umaizi. Lakini kama kazi yako itaishia hapo, utahisi kuwa kuna kitu kinakosekana. Hii ni kwa sababu kukusanya na kuunganisha familia ya Mungu kunahitaji zaidi ya hisia kali pekee. Inahitaji maagano matakatifu yaliyofanywa kulingana na ibada za ukuhani.

Wengi wa mababu zetu hawakupokea ibada hizo. Lakini kwa majaliwa ya Mungu wewe ulipokea. Na Mungu alijua kuwa ungehisi kuvutwa karibu na mababu zako katika upendo na kwamba ungekuwa na teknolojia ipasayo ya kuwatambua. Pia alijua kwamba ungeishi katika wakati ambao kuyafikia mahekalu matakatifu, ambapo ibada huweza kufanywa, uwezekano ungekuwa mkubwa zaidi kuliko wakati wowote katika historia. Na alijua kuwa angeweza kukuamini kutimiza kazi hii kwa niaba ya mababu zako.

Bila shaka, sisi sote tuna wajibu muhimu na wa lazima ambao unahitaji umakini na muda wetu. Sisi sote tutafute sehemu ambayo Bwana anategemea tuifanye zaidi ya uwezo wetu. Bahati nzuri Bwana hutoa njia kwa kila mmoja wetu kupata ujasiri na kuridhika katika huduma zetu zote, ikiwemo huduma ya historia ya familia. Tunapata nguvu kufanya kile Yeye anachotuomba kupitia imani yetu kuwa Bwana hatoi amri “Isipokuwa ataandaa njia [kwetu] kwamba [sisi] tuweze kutimiza kile ambacho ameamuru” (1 Nefi 3:7).

Ninajua hii ni kweli kutokana na uzoefu. Miaka mingi iliyopita, kama mwanafunzi wa chuo kikuu, nilikutana na mtu ambaye aliifanyia kazi kampuni kubwa ya talakilishi. Hii ilikuwa ni mapema katika siku za mwanzo wa talakilishi na ilitokea tu kwamba kampuni yake ilimtuma kuuza talakilishi kwa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Kadri nilivyojua, muuzaji huyu hakuwa na imani ya kidini. Lakini alisema kwa mshangao na msisimko “Katika kanisa hili walikuwa wanafanya kile wanachoita ‘elimu ya nasaba,’ wakiyatafuta majina ya watu waliokufa , wakijaribu kutambua mababu zao. Watu, sana sana wanawake walikuwa wakikimbia makabatini, wakitafuta taarifa kupitia kadi ndogondogo.” Kama nakumbuka vyema, alisema wanawake walikuwa wamevalia viatu vya tenisi ili waweze kukibia kasi kidogo. Yule mtu aliendelea, “Nilivyoona umati ukijaribu kufanya hivyo, nilijua kwamba nimegundua sababu ya uvumbuzi wa talakilishi.”

Vema, alikuwa sahihi kiasi fulani. Talakilishi zingeweza kuwa sehemu muhimu ya kazi ya historia ya familia—sio tu talakilishi alizokuwa akiuza. Kiongozi wa kanisa mwenye mwongozo wa kiungu alichagua kutonunua talakilishi zake. Kanisa lilitakiwa kusubiria teknolojia ambayo kwa wakati huo ilikuwa hata haijafikiriwa. Lakini nimejifunza kwa miaka mingi tangu wakati huo hata teknolojia nzuri sana haiwezi kuchukua nafasi ya ufunuo kutoka mbinguni, kama ule aliopokea kiongozi wa kanisa. Hii ni kazi ya kiroho, na Bwana anaiongoza kupitia Roho Mtakatifu.

Wiki chache tu zilizopita, nilikuwa nafanyia kazi historia yangu ya familia na mshauri pembeni mwangu na msaidizi mwingine kwenye simu. Kwenye skrini ya talakilishi mbele yangu kulikuwa na tatizo lizidilo uwezo wangu kutatua. Niliona majina mawili, yametumwa na maajabu ya teknolojia, ya watu ambao kuna uwezekano walikuwa wakisubiri ibada ya hekaluni. Majina yalikuwa tofauti, lakini kulikuwa na sababu ya kuamini yangeweza kuwa mtu mmoja. Kazi yangu ilikuwa kutambua ukweli ni nini.

Niliwauliza washauri wangu waniiambie. Walisema, “La, wewe sharti ufanye hivyo.” Na walikuwa na hakika kabisa ningegunudua ukweli. Talakilishi, na nguvu zake zote na taarifa, iliniachia baraka ya kukazia macho majina hayo kwenye skrini, kuchanganua taarifa iliyopatikana, kuangalia utafiti mwingine, kusali kimyakimya, na kugundua ukweli ni nini. Wakati nikisali, nilijua kwa uhakika nini cha kufanya—kama nilivyoweza katika hali zingine ambapo nilihitaji kutegemea msaada wa mbinguni kutatua tatizo.

Hatujui ni maajabu gani Mungu atawapa mwongozo watu kutengeneza msaada katika kazi Yake ya kukusanya familia Yake. Lakini uvumbuzi wowote ule wa ajabu unaweza kuja, matumizi yake yanahitaji Roho afanye kazi ndani ya watu kama mimi na wewe. Hii isitushangaze. Hata hivyo, wote hawa ni wana na mabinti wa Mungu. Atatuma mwongozo wowote unaohitajika ili kuwapa wao nafasi ya kurudi Kwake.

Miaka ya hivi karibuni, vijana wa kanisa wameitikia roho ya Eliya katika njia ya kutia moyo. Wengi wao sasa wana vibali vyao vya hekaluni vya muda na huvitumia kila mara. Visima vya ubatizo hekaluni vinafanya kazi sana kuliko kabla, na hata baadhi ya mahekalu wamebadili ratiba ili kutoa nafasi kwa ongezeko la idadi ya vijana wanohudhuria hekaluni.

Ilikuwa nadra lakini kwa mwaliko maalum kwa vijana kuleta majina ya mababu zao hekaluni. Sasa ni kawaida na mara zote ni vijana wao wenyewe ambao wamewapata hao mababu.

Kwa kuongezea, vijana wengi wamegundua kuwa kutoa muda wao kufanya utafiti wa historia ya familia huongeza ushuhuda wao juu ya mpango wa wokovu. Imeongeza ushawishi wa Roho katika maisha yao na kupunguza ushawishi wa mwovu. Imewasaidia kuhisi ukaribu na familia zao na ukaribu na Bwana. Wamejifunza kuwa kazi hii huokoa sio tu wafu; hutuokoa sote (ona M&M 128:18).

Kwa mshangao ijana wameshika ono; sasa wazazi wao wanahitaji pia kushika. Sasa kuna watu wengi ambao wamekubali ubatizo kwenye ulimwengu wa kiroho, kwa sababu ya kazi iliyofanywa na vijana, na wanasubiri ibada zingine ambazo watu wazima pekee wanaweza kuzifanya mahekalu katika ulimwengu huu. Kazi ya kukusanya familia ya Mungu sio tu ya vijana, na sio tu kwa ajili ya mababu. Ni ya kila mtu. Sisi sote ni wakusanyaji.

Hii ni kazi ya kizazi chetu, kile Mtume Paulo alikiita “kipindi cha utimilifu wa wakati” ambapo Mungu “atavikusanya vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia. Naam, katika yeye huyo” (Waefeso 1:10). Hii inawezeshwa kupitia kazi ya upatanisho wa Mwanae Mpendwa wa Mungu, Yesu Kristo Kwa sababu yake, wanafamila wetu “ambao wakati mwingine walikuwa mbali wanasogezwa karibu kupitia damu ya Kristo. Kwani yeye ni amani yetu, aliyefanya vyote pamoja, na amevunja ukuta wa kati uliotutenga kati yetu” (Waefeso 2:13–14)). Umehisi hivyo, kama nilivyohisi, wakati ulipopata ongezeko la upendo ulipoangalia picha ya mhenga wako. Umehisi hivyo ukiwa Hekaluni, wakati jina kwenye kadi lilionekana kuwa zaidi ya jina na hukuweza kusaidia isipokuwa kuhisi kuwa mtu huyu alikuwa anakujua na alihisi upendo wako.

Ninashuhudia kuwa Mungu Baba anawataka watoto Wake tena nyumbani katika familia na katika utukufu. Mwokozi yu Hai. Anaongoza kazi hii, na anatuangalia na kutuongoza. Anakushukuru kwa huduma yako ya uaminifu katika kukusanya familia ya Baba Yake, na nakuahidi msaada wa mwongozo unaoutafuta na kuhitaji. Katika jina la Yesu Kristo, amina.