2010–2019
Wema, Hisani, na Upendo
Aprili 2017


4:4

Wema, Hisani, na Upendo

Ndugu zangu wa ukuhani, acha tuchunguze maisha yetu na kuamua kufuata mfano wa Mwokozi kwa kuwa wema, wenye upendo, na hisani.

Ndugu zangu wapendwa, ninayo heshima kwa fursa hii ya kuwahutubia katika mkusanyaniko huu wa ulimwengu wa wenye ukuhani wa Mungu walio waaminifu. Jioni hii ninarejea mada ambayo nimeshaizungumzia hapo awali.

Nabii Mormoni alielezea mojawapo ya sifa muhimu za Mwokozi na ambayo inapaswa kuigwa na wanafunzi Wake. Alisema:

“Na mtu akiwa myenyekevu na mpole katika moyo, na kukiri kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwamba Yesu ni Kristo, lazima awe na hisani; kwani kama hana hisani yeye si kitu; kwa hivyo lazima awe na hisani.

“Na hisani huvumilia, na ni karimu, na haina wivu, na haijivuni, haitafuti mambo yake, haifutuki kwa upesi. …

“Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, kama hamna hisani, nyinyi si kitu, kwani hisani haikosi kufaulu kamwe. Kwa hivyo, ambatana na hisani, ambayo ni kubwa kuliko yote, kwani vitu vyote lazima vishindwe—

“Lakini hisani ni upendo msafi wa Kristo, na inavumilia milele; na yeyote atakayepatikana nayo katika siku ya mwisho, itakuwa vyema kwake.”1

Ndugu zangu, hatuheshimu ukuhani wa Mungu tusipokuwa wema kwa wengine.

Rafiki yangu mpendwa na mshirika Mzee Joseph  B. Wirthlin kweli alikuwa mtu mkarimu. Alisema:

“Wema ni kiini cha maisha ya selestia. Wema ndiyo namna ambayo mtu aliye kama Kristo huwatendea wengine. Wema lazima hupenyeze katika maneno yetu yote na matendo yetu kazini, shuleni, kanisani, na hasa majumbani mwetu.

“Yesu, Mwokozi wetu, alikuwa mfano wa wema na huruma.”2

Maandiko yanatufundisha kwamba matumizi ya haki ya ukuhani yanategemea kuishi kwetu kwa kanuni za wema, hisani, na upendo. Katika Mafundisho na Maagano tunasoma:

“Hakuna nguvu au uwezo unaoweza au upaswao kudumishwa kwa njia ya ukuhani, isipokuwa tu kwa njia ya ushawishi, … kwa uvumilivu, kwa upole na unyenyekevu, na kwa upendo usio unafiki;

“Kwa wema, na maarifa safi, ambayo yataikuza sana nafsi isiyo na unafiki, na isiyo na hila.”3

Ndugu zangu wa ukuhani, acha tuchunguze maisha yetu na kuamua kufuata mfano wa Mwokozi kwa kuwa wema, wenye upendo, na hisani. Tunapofanya hivyo, tutakuwa katika nafasi bora ya kuita nguvu za mbingu juu yetu wenyewe, familia zetu, na kwa wasafiri wenzetu katika safari hii ambayo wakati mwingine huwa ngumu kurudi nyumbani kwetu mbinguni. Mimi ninaomba hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.