Mkono Wake wa Kuongoza Kila Siku
Baba wa Mbinguni anajua vyema zaidi kile wewe na mimi tunahitaji kuliko mtu mwingine yeyote.
Mojawapo ya zana zipendwazo sana za Baba wa Mbinguni katika kuelekeza watoto Wake ni mababu na mabibi wema. Mama ya baba yangu alikuwa mwanamke wa namna hiyo. Katika hafla ambayo ilifanyika nilipokuwa mdogo sana kukumbuka, baba yangu alikuwa akiniadhibu. Kuona marekebisho haya, bibi yangu alisema, “Monte, naamini unamrekebisha kwa ukali sana.”
Baba yangu akajibu, “Mama, nitawarekebisha watoto wangu ninavyotaka.”
Na bibi yangu mwenye busara akasema, “Nami nitafanya vivyo hivyo.”
Nina uhakika baba yangu alisikia ushauri wa hekima wa mama yake siku hiyo.
Ninapofikiria kuhusu mwongozo, tunaweza fikiria juu ya wimbo tunaoujua na kuupenda sote- “Mimi Ni Mtoto wa Mungu.” Katika kibwagizo tunapata maneno “Niongoze, kaa nami, unifundishe, unionyeshe njia.”1
Hadi hivi karibuni, nilielewa kwamba kibwagizo hicho ni mwongozo mtakatifu kwa wazazi. Nilipokuwa nikitafakari maneno haya, niligundua kwamba ingawa haya mwongozo huo, kuna maana kubwa zaidi. Kibinafsi, kila mmoja wetu anasihi kila siku kwamba Baba wa Mbinguni atatuongoza, kutuelekeza, na kutembea kando yetu.
Rais Dieter F. Uchtdorf alifafanua: “Baba yetu wa Mbinguni anajua mahitaji ya watoto Wake vizuri kuliko mtu mwingine ye yote. Ni kazi na utukufu Wake kutusaidia katika kila kona, kutupatia rasilimali nzuri za kimwili na za kiroho ili kutusaidia katika njia yetu ya kurejea Kwake.”2
Sikilizeni Maneno Hayo: Baba wa Mbinguni anajua vyema zaidi kile wewe na mimi tunahitaji kuliko mtu mwingine yeyote. Matokeo yake, ametengeneza kifurushi cha huduma binafsi inayofaa kwa kila mmoja wetu. Kina vitu vingi. Hujumuisha Mwanawe na Upatanisho, Roho Mtakatifu, amri, maandiko, maombi, manabii, mitume, wazazi, babu na bibi, viongozi wa Kanisa wa eneo lako, na wengine wengi—wote ili kutusaidia kurudi kuishi pamoja naye siku moja.
Naomba nishiriki nanyi leo vitu vichache tu vya kifurushi cha huduma ambavyo vimenifanya mimi kutambua kwamba Baba mwenye upendo anaongoza, anaelekeza, na kutembea kando yangu mimi na familia yangu? Ombi langu ni kwamba kila mmoja wenu atatambua katika uzoefu wake kwamba Baba wa Mbinguni anaongoza, anaelekeza, na kutembea kando yake na, kwa maarifa hayo, utaendelea kwa ujasiri, ukijua kamwe hauko peke yako.
Amri za Baba wa Mbinguni ni vitu muhimu katika hicho kifurshi cha huduma. Alma alitangaza kwamba “uovu haujapata kuwa furaha.”3 Kuvumilia tabia mbaya bila kupenda marekebisho ni huruma potovu na huimarisha dhana ya kawaida ya kuwa maovu kwa kweli yanaweza kuwa furaha. Samweli Mlamani alijibu wazo hili wazi wazi: “Na mmetafuta furaha kwa kufanya uovu, kitu ambacho ni kinyume cha asili ya haki ambayo huja kutoka kwa mkuu na Kiongozi wetu wa Milele.”4
Kupitia kwa manabii Wake, Baba wa Mbinguni anatukumbusha daima kwamba haki ndiyo furaha. Mfalme Benjamini, kwa mfano, alifundisha kwamba Baba wa Mbinguni “anahitaji kwamba nyinyi mtende yale ambayo amewaamuru; kwani kama mtatenda hivyo, atawabariki papo hapo”5 Kutoka katika wimbo mwingine huja ukumbusho wa aina hiyo hiyo:
Karibia siku yangu ya mwaka wa 14 wa kuzaliwa , niligundua kuhusu baadhi ya baraka hizi. Niliona tabia tofauti kwa upande wa wazazi wangu. Kwa kuzingatia kile nilichokiona, Niliuliza, “Je, tunaenda misheni?” Mshtuko kwenye uso wa mama yangu ulithibitisha wasi wasi wangu. Baadaye, katika baraza la familia, ndugu zangu na mimi tuligundua kwamba wazazi wetu walikuwa wameitwa kuongoza misheni.
Tuliishi kwenye ranchi nzuri huko Wyoming. Kutokana na mtazamo wangu, maisha yalikuwa sawa. Ningeweza kurudi nyumbani kutoka shuleni, kukamilisha kazi yangu, na kuelekea mawindoni, kuvua, au kutembea na mbwa wangu.
Muda mfupi baada ya kuelewa wito huu, niligundua kwamba itanibidi nimwaache mbwa wangu, Blue. Nilikabiliana na baba yangu, nikamuuliza kile ambacho nitafanya na Blue. Nilitaka kusisitiza ukosefu wa usawa katika kile ambacho Mungu alikuwa anahitaji. Kamwe sitasahau jibu hili. Alisema, “Sina uhakika. Pengine hawezi kwenda na sisi, hivyo ingekuwa bora umuulize Baba wa Mbinguni.” Hayo hayakuwa majibu niliyotarajia.
Nilianza kusoma Kitabu cha Mormoni. Niliomba kwa dhati ili kujua kama nitapaswa kumkabidhiana mbwa wangu. Jibu langu halikuja kwa dakika moja; badala yake, mawazo maalum yaliendelea kupenya katika akili yangu: “Usiwe mzigo kwa wazazi wako. Usiwe mzigo. Nimewaita wazazi wako.”.
Nilijua kile Baba wa Mbinguni alihitaji. Elimu hiyo hakukupunguza uchungu wa kumkabidhiana mbwa wangu. Hata hivyo, kupitia dhabihu hiyo ndogo, moyo wangu ulilainika na nikapata amani katika kutafuta mapenzi ya Baba wa Mbinguni.
Namshukuru Baba yangu wa Mbinguni kwa baraka na furaha nilizoona kupitia kwenye maandiko, maombi, Roho Mtakatifu, na baba wa dunia mwenye kustahili aliyekubali jukumu lake kama mwalimu mkuu wa injili kwa watoto Wake. Walikuwa wakiniongoza, kunielekeza, na hata kutembea kando yangu ili kunisaidia kupata njia—hasa iliponibidi nifanye kitu kigumu.
Mbali na kuwa na vitu kwenye kifurushi cha huduma nilivyovitaja, kila mmoja wetu amebarikiwa kuwa na kiongozi wa ukuhani ili kutuongoza na kutuelekeza.
Rais Boyd K. Packer alisema: “Maaskofu wana mwongozo wa kiungu! Kila mmoja wetu ana haki ya kujiamulia kukubali au kukataa ushauri kutoka kwa viongozi wetu, lakini kamwe usipuuze ushauri wa askofu wako, iwe umetolewa kwenye mimbari au kibinafsi.”7
Hawa watu hujitahidi kumwakilisha Bwana. Iwe sisi ni vijana au wazee, wakati Shetani anapotaka tufikirie kwamba tumepoteza kila kitu, maaskofu wako pale ili kutuongoza. Ninapozungumza na maaskofu, nimeona kauli mbiu ya kawaida kuhusu kukiri juu ya uasi au mateso ya wasiokuwa na hatia kutokana na makosa ya kutisha. Maaskofu kwa haraka hutaka kuonyesha upendo wa Baba wa Mbinguni kwa mtu huyo na hamu ya kutembea kando yake wakati anapotafuta njia ya kurudi nyumbani.
Labda kitu muhimu sana katika kifurushi cha huduma cha Baba wa Mbinguni kinaelezwa katika maneno haya: “Kwa maana Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanae wa pekee.”8
Ili kutufundisha yote ambayo tunapaswa kufanya, Yesu Kristo aliongoza njia kwa kutoa mfano kamili ambao ni lazima tujaribu kuiga. Anatusihi kwa mikono iliyonyoshwa ili tuje, tumfuate Yeye.9 Na wakati tunaposhindwa, hicho hufanyika kwetu sote, Anatukumbusha, “Kwani tazama, Mimi, Mungu nimeteseka mambo haya kwa ajili ya watu wote, ili kwamba wasiteseke kama watatubu.”10
Ni zawadi nzuri iliyoje! Toba si adhabu; ni fursa. Ni fursa ambayo inatuongoza na kutuelekeza. Si ajabu kuwa maandiko yanatangaza kwamba hatupaswi kufundisha chochote ila toba.11
Baba wa Mbinguni ana rasilimali nyingi, lakini mara nyingi anatumia mtu mwingine ili kumsaidia Yeye. Kila siku Yeye hutupatia nafasi ya kuongoza, kuelekeza, na kutembea kando ya mtu mwenye shida. Ni lazima tufuate mfano wa Mwokozi. Sisi pia lazima tuwe katika kazi ya Baba wa Mbinguni.
Kama Urais Mkuu wa Vijana, tunajua kwamba vijana wanabarikiwa wanapokuwa na wazazi na viongozi wanaomtumikia Baba wa Mbinguni katika kuongoza, kuelekeza, na kutembea kando yao. Kanuni tatu12 ambazo zitatusaidia sisi kuwa sehemu ya kifurushi cha huduma cha Baba wa Mbinguni kwa ajili ya wengine ni:
Kwanza, kuwa pamoja na vijana. Rais Henry B. Eyring alisisitiza hoja hii: “Kuna baadhi ya mambo tunaweza kufanya ambayo yanaweza kuwa muhimu zaidi. Hata yenye nguvu zaidi kuliko kutumia maneno katika kufundisha kwetu mafundisho itakuwa mifano yetu ya kuishi mafundisho hayo.”13 Kuongoza vijana inahitaji kuwa pamoja nao. Muda unaotolewa ni dhihirisho la upendo ambao unaturuhusu kufundisha kwa maneno na kwa mfano.
Pili, ili kuwaongoza vijana kikamilifu, ni lazima tuwasaidie kuungana na mbingu. Inafika wakati ambapo kila mmoja ni lazima asimame peke yake. Baba wa Mbinguni ndiye pekee anayeweza kuongoza wakati wote na katika maeneo yote. Vijana wetu lazima wajue jinsi ya kutafuta mwongozo wa Baba wa Mbinguni.
Tatu, ni lazima tuache vijana waongoze. Kama mzazi mwenye upendo anayeshika mkono wa mtoto mdogo anayejifunza kutembea, ni lazima tuachilie ili vijana waweze kuendelea. Kuruhusu vijana kuongoza inahitaji uvumilivu na upendo. Ni vigumu na inachukua muda zaidi kuliko kufanya sisi wenyewe. Wanaweza kujikwaa njiani, lakini tunatembea kando yao.
Kaka zangu na dada zangu, kutakuwa na nyakati katika maisha yetu ambapo baraka za uongozi zinaonekana kuwa mbali au hazipo. Kwa nyakati hizo za dhiki, Mzee D. Todd Christofferson aliahidi: “Acha maagano yako yawe muhimu na utii wako kamili. Kisha unaweza kuuliza kwa imani bila shaka yoyote, kulingana na mahitaji yako, na Mungu atajibu. Atakusaidia unapofanya kazi na kuangalia. Kwa wakati Wake na njia Yake Ataunyosha mkono Wake kwako, akisema, ‘Mimi hapa.”’14
Wakati mmoja kama huo, nilitafuta ushauri wa Baba wa Mbinguni kwa njia ya maombi ya dhati mara kwa mara kwa zaidi ya mwaka ili kupata suluhu juu ya hali ngumu. Nilijua vyema kwamba Baba wa Mbinguni hujibu sala zote za dhati. Hata hivyo nilifikia hali hiyo ya kutamausha siku moja kiasi ya kuhudhuria hekaluni nikiwa na swali moja: “Baba wa Mbinguni, kweli Wewe unajali?”
Nilikuwa nimeketi nyuma karibu na chumba cha kusubiri cha Hekalu la Logan Utah ambapo, kwa mshangao wangu, aliyekuwa akiingia katika chumba siku hiyo alikuwa ni rais wa hekalu Vaughn J. Featherstone, rafiki wa karibu wa familia. Alisimama mbele ya mkutano na kutukaribisha sisi sote. Aliponigundua kati ya wahudhuriaji wa hekalu, aliacha kuzungumza, akaniangalia machoni, na kisha akasema, “Ndugu Brough, ni vizuri kukuona hekaluni leo.”
Kamwe sitaweza kusahau hisia ya wakati huo mfupi. Ilikuwa ni kana kwamba—katika salamu hiyo—Baba wa Mbinguni alikuwa Akinyoosha mkono wake na kusema, “Mimi hapa.”
Baba wa Mbinguni kweli anajali na husikia na hujibu maombi ya kila mtoto.15 Kama mmoja wa watoto Wake, najua kwamba majibu kwa maombi yangu yalikuja kwa wakati wa Bwana. Na kupitia uzoefu huo, nilielewa zaidi kuliko hapo awali kwamba sisi ni watoto wa Mungu na kwamba Yeye ametutuma hapa ili tuweze kuuhisi uwepo Wake sasa na kurudi kuishi Naye siku moja.
Nashuhudia kwamba Baba wa Mbinguni anatuongoza, kutuelekeza, na kutembea kando yetu. Tunapomfuata Mwanawe na kutii watumishi Wake, mitume na manabii, tutapata njia ya kuelekea katika uzima wa milele. Katika jina la Yesu Kristo, Amina.