Misingi ya Imani
Ombi langu ni kwamba tutafanya dhabihu na kuwa na unyenyekevu unaohitajika ili kuimarisha misingi ya imani yetu katika Bwana Yesu Kristo.
Huu umekuwa mkutano mkubwa wa kupendeza. Kwa kweli tumejengwa. Kuna lengo moja kuu la mkutano mkuu linaloshinda mengine yote, nalo ni kujenga imani katika Mungu Baba na Mwokozi wetu, Bwana Yesu Kristo.
Hotuba yangu inahusu misingi ya imani hiyo.
Misingi binafsi, kama vile shughuli nyingi za kufaa, kwa kawaida hujengwa pole pole safu moja, uzoefu mmoja, changamoto moja, kipingamizi kimoja, na fanikio moja kwa wakati mmoja. Tukio la kufurahisha kabisa la kimwili ni hatua za kwanza za mtoto. Na inapendeza kutazama. Sura nzuri usoni—mchanganyiko wa dhamira, furaha, mshangao, na mafanikio—ama kweli ni jambo la kipekee.
Katika familia yetu, kuna tukio moja lenye asili sawa hukumbukwa daima. Wakati mwana wetu mdogo alipokuwa na umri wa miaka minne, aliingia ndani ya nyumba na kuitangazia familia kwa ufahari mkubwa: “Naweza kufanya kila kitu sasa. Naweza kufunga na naweza kuendesha baiskeli na naweza kufunga zipu.” Tulidhani alikuwa akituambia kwamba angeweza kufunga kama za viatu vyake, angeweza kuendesha baiskeli yake ya miguu mitatu mkikubwa, na angefunga zipu ya koti lake. Sote tulicheka lakini tulitambua kwamba kwake ilikuwa ni mafanikio makubwa. Alidhani alikuwa amefika na amekuwa mtu mzima.
Ukuaji wa kimwili, kiakili, na kiroho una mambo mengi yanayofanana. Ukuaji wa kimwili ni rahisi kuona. Tunaanza na hatua za mtoto na kukua siku baada ya siku, mwaka baada mwaka, kukua na kuendelea ili kufikia kimo cha mwili wetu. Ni tofauti kwa kila mtu.
Tunapotazama mahodari katika riadha au upigaji muziki, mara nyingi tunasema kwamba mtu huyo ana kipaji sana, ambayo kwa kawaida ni kweli. Lakini ustadi msingi wake ni miaka ya matayarisho na mazoezi. Mwandishi maarufu, Malcolm Gladwel, aliita hili sheria ya masaa 10,000. Watafiti wamethibitisha kwamba kiasi hiki cha mazoezi ni muhimu katika riadha, upigaji muziki, ustadi wa kitaaluma, ujuzi maalumu wa kikazi, utaalamu wa kitabibu au kisheria, na kadhalika. Mmoja wa wataalamu hawa watafiti anadai “kwamba masaa elfu kumi ya mazoezi yanahitajika ili kufikia kiwango cha ushupavu kinachohusishwa na ubingwa wa ulimwengu—katika kitu chochote.”1
Watu wengi hutambua kwamba ili kufikia kilele cha ustadi wa kimwili na kiakili maandalizi kama hayo na mazoezi ni muhimu.
Kwa bahati mbaya, katika dunia inayokua kilimwengu zaidi, mkazo kidogo umewekwa kwenye kiwango cha ukuaji wa kiroho muhimu ili kufanana zaidi kama Kristo na kuimarisha misingi ambayo inatuelekeza kwenye imani yenye kustahmili. Tunajaribu kusisitiza nyakati za uelewa wa ufahari wa kiroho. Haya ni matukio ya thamani tunapojua kuwa Roho Mtakatifu ameshuhudia ufahamu maalum wa kiroho katika mioyo na akili zetu. Tunafurahi katika matukio haya; hayapaswi kutharauliwa kwa njia yoyote. Lakini kwa imani yenye kustahmili na ili kuwa na wenza wa Roho Mtakatifu kila mara , hakuna mbadala kwa utiifu binafsi wa kidini ambao unalingana na ukuaji wa kimwili na kiakili. Tunapaswa kujenga uzoefu huu ambao wakati mwingine hufanana na hatua za mwanzoni za mtoto. Tunafanya hivyo kwa kujiwekea wakfu dhamira yetu ya kuhudhuria mikutano mitakatifu ya sakramenti, kujifunza maandiko, maombi, na kuhudumu kama tulivyoitwa. Katika mojawapo ya hutoba ya tanzia ya baba wa watoto 13, iliripotiwa kuwa“uaminifu wake kwa maombi na kujifunza maandiko kila siku umewavutia sana watoto wake, na kuwawekea msingi imara wa imani katika Bwana Yesu Kristo.”2
Tukio lililonipata nilipokuwa na umri wa miaka 15 lilikuwa la msingi sana kwangu. Mama yangu mwaminifu alikuwa amejaribu sana kunisaidia kuanzisha misingi ya imani katika maisha yangu. Nilihudhuria mkutano wa sakramenti, Msingi, kisha ya darasa la Wavulana na seminari. Nilikuwa nimekisoma Kitabu cha Mormoni na daima nilikuwa nikiomba binafsi. Wakati huo tukio kubwa lilitokea katika familia yetu wakati kaka yangu mpendwa alipokuwa akitarajia wito wa kwenda misheni. Baba yangu mpendwa, muumini wa Kanisa alisiyehudhuria ipasavyo, alimtaka kuendelea na elimu yake na asitumikie misheni. Hii ikawa chanzo cha ugomvi.
Katika mjadala mkali na kaka yangu, ambaye alikuwa mkubwa kwangu kwa umri wa miaka mitano na kuongoza mjadala, tulihitimisha kuwa uamuzi wake kuhusu iwapo kutumikia misheni au la unategemea masuala matatu: (1) Je, Yesu Kristo alikuwa Mungu? (2) Je, Kitabu cha Mormoni ni cha kweli? (3) Je, Joseph Smith alikuwa nabii wa Urejesho?
Nilipokuwa nikiomba kwa dhati usiku huo, Roho alithibitisha kwangu ukweli wa maswali yote matatu. Pia nilikuja kuelewa kwamba karibu kila uamuzi ambao ningefanya kwa maisha yangu yote utategemea majibu ya maswali hayo matatu. Nilitambua hasa kwamba imani katika Bwana Yesu Kristo ilikuwa muhimu. Katika kutazama nyuma, nilitambua kwamba, kimsingi kwa sababu ya mama yangu, misingi ilikuwepo mahali pale kwa ajili yangu ili nipokee uthibitisho wa kiroho jioni hiyo. Kaka yangu, ambaye tayari alikuwa na ushuhuda, alifanya uamuzi wa kutumikia misheni na hatimaye kupata idhini ya baba yetu.
Mwongozo wa kiroho hupokelewa wakati unapohitajika, katika muda wa Bwana na kulingana na mapenzi Yake.3 Kitabu cha Mormoni: Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo ni mfano bora. Hivi karibuni niliangalia toleo la kwanza la Kitabu cha Mormoni. Joseph Smith alikamilisha tafsiri yake alipokuwa na umri wa miaka 23. Tunajua jambo kuhusu mchakato huo na vifaa alivyotumia katika tafsiri hiyo. Katika uchapishaji huo wa kwanza wa 1830, Joseph aliongezea dibaji fupi na kwa urahisi na kwa uwazi alitangaza kilitafsiriwa “kwa kipawa na uwezo wa Mungu.”4 Na Je, kuhusu vifaa saidizi vya tafsiri—Urimu na Thuminu, mawe ya mwonaji? Je, vilikuwa muhimu, au vilikuwa kama magurudumu ya kujifunzia kwenye baiskeli mpaka Joseph alipoweza kuonyesha imani muhimu ili kupokea ufunuo zaidi wa moja kwa moja?5
Kama vile tu marudio na juhudi thabiti zinavyotakiwa ili kupata uwezo wa kimwili au kiakili, hiyo ni kweli hata katika mambo ya kiroho. Kumbuka Nabii Joseph alimpokea mgeni huyohuyo, Moroni, akiwa na ujumbe ule ule mara nne katika maandalizi kwa ajili ya kupokea mabamba. Naamini ushiriki wa kila wiki katika mikutano mitakatifu ya sakramenti ina maana ya kiroho ambayo hatuwezi kuelewa kikamilifu. Kutafakari maandiko kila mara—badala ya kuyasoma kwa wakati tu—inaweza kubadilisha uelewa wa juu juu kwa uimarishaji wa kuvutia wa mabadiliko ya maisha ya imani yetu.
Imani ni kanuni ya uwezo. Acha nieleze: Kama misionari kijana, rais mzuri wa misheni6 alinijulisha kwa njia ya kipekee kwenye hadithi ya maandiko inayopatikana katika Luka 8 ya mwanamke ambaye alikuwa ametokwa na damu kwa muda wa miaka 12 na alikuwa amegharimika mali zake zote kwa kuwapa waganga ambao hawakuweza kumponya. Imebakia mpaka leo mojawapo wa maandiko yangu niyapendayo.
Utakumbuka kwamba alikuwa na imani kwamba kama angeweza angalau kugusa upindo wa vazi la Mwokozi, angeweza kuponywa. Alipofanya hivyo, aliponywa mara moja. Mwokozi, ambaye alikuwa akitembea pamoja na wanafunzi wake, alisema, “Ni nani aliyenigusa?”
Jibu la Petro lilikuwa kwamba wote, wakitembea pamoja, walikuwa wakisukumana dhidi Yake.
“Yesu akasema, Mtu alinigusa, maana naona ya kuwa nguvu zimenitoka.”
Mzizi wa neno wema inaweza kwa urahisi kutafsiriwa kama “nguvu.” Kihispania na Kireno, inatafsiriwa kama “nguvu.” Lakini bila kujali, Mwokozi hakumwona; Hakuwa amelenga kwenye haja yake. Lakini imani yake ilikuwa kama kwamba kugusa upindo wa vazi kulimletea nguvu ya uponyaji ya Mwana wa Mungu.
Kama vile Mwokozi alivyomwambia, “Binti, imani yako imekuponya; enenda zako kwa amani.”7
Nimewaza kuhusu maelezo haya maisha yangu yote ya utu uzima. Natambua kwamba sala zetu binafsi na dua kwa Baba wa Mbinguni mwenye upendo katika jina la Yesu Kristo zinaweza kuleta baraka katika maisha yetu zaidi ya uwezo wetu wa kuelewa. Misingi ya imani, aina ya imani ambayo mwanamke huyu alionyesha, inapaswa kuwa hamu kubwa ya mioyo yetu.
Hata hivyo, misingi ya awali ya imani, hata pamoja na uthibitisho wa kiroho, haimaanishi kwamba hatutakabiliwa na changamoto. Kuongoka katika injili haimaanishi matatizo yetu yote yatatatuliwa.
Historia ya mwanzoni ya Kanisa na mafunuo yaliyoandikwa katika Mafundisho na Maagano yana mifano bora ya kujenga misingi ya imani na kushughulikia mabadiliko na changamoto ambazo kila mtu anapitia.
Kukamilika kwa Hekalu la Kirtland ilikuwa jambo la kimsingi kwa Kanisa zima. Ilifuatiwa na mwagiko la kiroho, mafunuo ya kimafundisho, na urejesho wa funguo muhimu kwa ajili ya mwendelezo wa uimarishwaji wa Kanisa. Mitume wa kale mnamo siku ya Pentekoste, waumini wengi waliona matukio mengi ya ajabu ya kiroho kwa uhusiano na kuwekwa wakfu kwa Hekalu la Kirtland.8 Lakini, kama vile katika maisha yetu wenyewe, hii haikumaanisha kuwa hawangeona changamoto au matatizo siku nyingine. Waumini hawa wa mwanzoni hawakujua mapema kuwa wangeweza kukabiliwa na mgogoro wa kifedha wa Marekani—hofu ya 1837—ambayo ingejaribu hata nafsi zao.9
Mfano mmoja unaohusiana na changamoto hizi za kifedha ilimpata Mzee Parley P. Pratt, mmoja wa viongozi wakuu wa Urejesho. Alikuwa mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili asili. Sehemu ya mapema ya mwaka 1837, mke wangu mpendwa, Thankful, alifariki baada ya kupata mtoto wao wa kwanza. Parley na Thankful walikuwa wameoana karibu miaka 10, na kifo chake kilibananga.
Miezi michache baadaye, Mzee Pratt alijikuta katika moja ya nyakati ngumu sana ambayo Kanisa limewahi kuona. Katikati ya janga la kitaifa, masuala ya kawaida ya kiuchumi—ikiwemo ulanguzi wa ardhi na changamoto za taasisi ya kifedha iliyoanzishwa na Joseph Smith na waumini wengine wa Kanisa zilileta—kutokuelewana na ugomvi huko Kirtland. Viongozi wa kanisa daima hawakufanya maamuzi ya busara ya kidunia katika maisha yao wenyewe. Parley alipata hasara kubwa ya kifedha na kwa muda akakosa imani na Mtume Joseph.10 Aliandika ukosoaji mchafu kwake Joseph na kuongea dhidi yake juu ya mimbari. Kwa wakati huo huo, Parley alisema aliendelea kuamini katika Kitabu cha Mormoni na Mafundisho na Maagano.11
Mzee Pratt alikuwa amempoteza mkewe, ardhi yake, na nyumba yake. Parley, bila kumwambia Joseph, aliondoka kwenda Missouri. Njiani akielekea huko, bila kutarajia alikutana na Mitume wenzake Thomas B. Marsh na David Patten akirudi Kirtland. Walihisi haja kubwa ya kurejesha maelewano katika Akidi na hivyo wakamsihi Parley kurudi pamoja nao. Aligundua kwamba hakuna yeyote aliyepoteza zaidi kuliko Joseph Smith na familia yake.
Parley alimtafuta Nabii, alilia, na kukiri kwamba kile alichokifanya kilikuwa makosa. Katika miezi baada ya kifo cha mkewe, Thankful, Parley alikuwa “chini ya wingu la simanzi” na alikuwa amezidiwa na hofu na kuchanganyikiwa.12 Joseph, akiwa anajua jinsi ilivyo kupambana dhidi ya upinzani na majaribu, “kwa upendo akamsamehe” Parley, akimwombea na kumbariki.13 Parley na wengine ambao walisalia waaminifu walinufaika kutokana na changamoto za Kirtland. Waliongezeka katika hekima na wakawa wasikivu na waadilifu. Ikawa sehemu ya misingi yao ya imani.
Shida haipaswi kuonekana kama karaha kutoka kwa Bwana au uondoaji wa baraka Zake. Upinzani katika vitu vyote ni sehemu ya moto wa msafishaji ili kutuandaa kwa ajili ya hatima yetu ya milele ya kiselestia.14 Wakati Nabii Joseph alipokuwa katika Jela ya Liberty, maneno ya Bwana kwake yanaeleza namna zote za changamoto—ikiwa ni pamoja na mateso, shutuma za uongo—na inahitimisha:
“Kama mataya yale ya jahanamu yataachama kinywa wazi kwa ajili yako, fahamu wewe, mwanangu, kwamba mambo haya yote yatakupa wewe uzoefu, na yatakuwa kwa faida yako.
“Mwana wa Mtu ameshuka chini yao wote. Je, wewe u mkuu kuliko yeye?”15
Bwana, katika maelekezo haya kwa Joseph Smith, pia aliweka wazi kwamba siku zake zinafahamika, na miaka yake haitahesabika kuwa michache. Bwana alihitimisha, “Usiogope mwanadamu awezacho kukutenda, kwani Mungu atakuwa pamoja nawe milele na milele.”16
Ni nini basi baraka za imani? Je, imani hukamilisha nini? Orodha ni ndefu hata haina mwisho:
Dhambi zetu zinaweza kusamehewa kwa sababu ya imani katika Kristo.17
Kadiri wengi walivyo na imani wana ushirika na Roho Mtakatifu.18
Wokovu huja kupitia imani katika jina la Kristo.19
Tunapokea nguvu kulingana na imani yetu katika Kristo.20
Hakuna anayeweza kuingia katika pumziko la Bwana isipokuwa wale walioosha mavazi yao katika damu ya Kristo kwa sababu ya imani yao.21
Maombi hujibiwa kulingana na imani.22
Bila imani miongoni mwa watu, Mungu hawezi kufanya miujiza yoyote kati yao.23
Mwishowe, imani yetu katika Yesu Kristo ni msingi muhimu kwa wokovu wetu wa milele na kuinuliwa. Kama Helamani alivyofundisha wanawe “Kumbukeni kwamba ni juu ya mwamba wa Mkombozi wetu, ambaye ni Kristo, Mwana wa Mungu, kwamba lazima mjenge msingi wenu … ambao ni msingi imara, msingi ambako watu wote wakijenga hawataanguka.”24
Ninashukuru kwa uimarishwaji wa misingi ya imani ambayo umekuja kutokana na mkutano huu. Ombi langu ni kwamba tutafanya dhabihu na kuwa na unyenyekevu unaohitajika ili kuimarisha misingi ya imani yetu katika Bwana Yesu Kristo. Kwa ajili Yake natoa ushahidi wangu wa dhati katika jina la Yesu Kristo, amina.