Uzuri wa Utakatifu
Baba yetu wa Mbinguni ametupa kila tunachohitaji ili tuweze kuwa watakatifu jinsi alivyo mtakatifu.
Nilipokuwa nikijitayarisha kwa mkutano huu, moyo wangu umewageukia kina dada wengi waaminifu ambao nilikutana nao, hapa karibu na mbali. Kwangu mimi, wanaelezewa bora zaidi kupitia zaburi ya kutoa shukrani ya Mfalme Daudi. “Mpeni Bwana utukufu wa jina lake; Leteni sadaka, mje mbele zake; Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.”1
Ninaona uzuri wa utakatifu katika kina dada ambao mioyo yao inazingatia yale yote ambayo ni mazuri, ambao wanataka kuwa zaidi kama Mwokozi. Wanatoa nafsi yao yote, moyo, uwezo, akili, na nguvu kwake Bwana kupitia jinsi wanavyoishi kila siku.2 Utukufu upo katika kujitahidi na kupambana kutii amri na kuheshimu maagano ambayo tumefanya na Mungu. Utukufu ni kufanya uchaguzi ambao utamuweka Roho Mtakatifu kama kiongozi wetu.3 Utukufu ni kutupilia mbali tabia zetu za kiasilia na kuwa mtakatifu kupitia upatanisho wa Kristo aliye Bwana.4 “Kila dakika ya [maisha yetu] ni lazima iwe utakatifu kwa Bwana.”5
Mungu wa mbinguni aliwaamuru wana wa Israeli, “Kwa kuwa mimi ni Bwana, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu.”6
Mzee D. Todd Christofferson amefundisha ya kwamba: Baba yetu wa Mbinguni ni Mungu wa matarajio makubwa. … Anapendekeza kutufanya watakatifu ili tuweze ‘kustahimili katika utukufu wa selestia’ (M&M 88:22) na ‘kukaa mbele zake’ (Musa 6:57).”7 Hotuba juu ya Imani inaeleza, “Hakuna kiumbe kinachoweza kufurahia utukufu wake bila kumiliki ukamilifu na utakatifu wake.”8 Baba yetu wa Mbinguni anatujua. Anatupenda, na ametupa kila tunachohitaji ili tuweze kuwa watakatifu jinsi alivyo mtakatifu.
Sisi ni mabinti wa Baba wa Mbinguni, na kila mmoja wetu ana urithi mtakatifu. Baba yetu wa Mbinguni ametangaza, “Tazama, Mimi ndimi Mungu; Mtu wa Utakatifu ndilo jina langu.”9 Katika maisha yetu kabla ya dunia, tulimpenda Baba yetu na tulimwabudu. Tulitamani kuwa kama yeye. Kutokana na upendo mkamilifu wa baba, Yeye alimtoa Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo, awe Mwokozi na Mkombozi wetu. Yeye ni Mwana wa Mtu wa Utakatifu.10 Jina lake ni Takatifu,11 Mtakatifu wa Israeli.12
Tumaini letu la utakatifu liko ndani ya Kristo, katika huruma Yake na neema Yake. Kwa imani katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake, tunaweza kuwa wasafi, bila dosari, wakati tunapojinyima ubaya13 na kutubu kwa kweli. Tunabatizwa majini kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Nafsi zetu zinatakaswa wakati tunapopokea Roho Mtakatifu kwa mioyo iliyo wazi. Kila wiki, tunashiriki katika ibada ya sakramenti. Katika roho ya kutubu kwa hamu za kweli za kutaka kuwa waadilifu, tunaagana ya kwamba tuko radhi kujichukulia juu yetu jina la Kristo, kumkumbuka, na kushika amri zake ili siku zote tuwe na Roho Wake kuwa nasi. Baada ya muda, tunapojitahidi kila mara kuwa kitu kimoja na Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, tunakuwa washiriki wa tabia yao ya uungu.14
Utakatifu ni Kutii Maagano Yetu
Tunatambua wingi wa majaribu, na dhiki ambayo inaweza kutuvuta mbali na yote yaliyo mema, na yenye kustahili sifa mbele ya Mungu. Lakini tunayopitia maishani yanatupa nafasi ya kuchagua utakatifu. Mara nyingi ni dhabihu tunazofanya ili kutii maagano yetu ambayo inatutakasa na kutufanya watakatifu.
Niliona utakatifu katika uso wa Evangeline, msichana wa miaka 13 kule Ghana. Njia moja ambayo anatii maagano yake ni kupitia kutukuza mwito wake kama rais wa darasa lake la Bihaivu. Alieleza kwa unyenyekevu kwamba yeye huenda nyumbani kwa marafiki zake, wasichana wasioshiriki kikamilifu, kuzungumza na wazazi wao kuwaruhusu waje Kanisani. Wazazi humwambia kwamba ni vigumu kwa sababu Jumapili ni lazima watoto wafanye kazi za nyumbani. Kwa hivyo Evangeline huenda kuwasaidia na kazi hizo, na kwa sababu ya juhudi zake marafiki zake mara nyingi huruhusiwa kwenda kanisani.
Ikiwa tutatii maagano husika, maagizo yatatubadilisha, kututakasa, na kututayarisha kuingia katika uwepo wa Bwana.15 Kwa hiyo, tunabeba mizigo ya mmoja na ya mwingine; tunaimarisha mmoja na mwingine. Tunahifadhi msamaha wa dhambi wakati tunapotoa usaidizi wa muda na wa kiroho kwa maskini, walio njaa, walio uchi, na wagonjwa.16 Tunajilinda ili kuwa bila mawaa kutoka ulimwenguni tunapoishika siku ya Sabato na kwa ustahili kupokea sakramenti katika siku takatifu ya Bwana.17
Tunabariki familia zetu na kufanya nyumba zetu kuwa sehemu takatifu. Tunatawala hisia zetu ili tuweze kujazwa na upendo msafi na unaodumu.18 Tunawasaidia wengine kwa ukarimu, na huruma, na kusimama kama mashahidi wa Mungu. Tunakuwa watu wa Sayuni, wa moyo mmoja na wazo moja, watu wasafi wanaoishi pamoja kwa umoja na haki.19 “Kwani Sayuni lazima iongezeke katika uzuri, na katika utakatifu.”20
Kina dada , njooni hekaluni. Ikiwa tunaweza kuwa watu watakatifu walio tayari kumpokea Mwokozi wakati wa ujio Wake, ni lazima tuinuke na tuvae mavazi yetu mazuri.21 Kwa nguvu na heshima, tunawacha njia za dunia na kutii maagano yetu ili tuweze “[ku]vishwa usafi, ndio, hata kwa joho la utakatifu.”22
Utakatifu Ni Kumkubali Roho Mtakatifu Kuwa Kiongozi Wetu
Utakatifu ni zawadi ya Roho. Tunakubali zawadi hii wakati tunapochagua kufanya yale mambo ambayo yataongeza uwezo wa kutakasa wa Roho Mtakatifu maishani mwetu.
Wakati ambapo Martha alimpokea Yesu Kristo nyumbani kwake, alihisi hamu kubwa sana ya kumhudumia Bwana kwa uwezo wake wote. Dada yake, Mariamu, alichagua “[ku]keti miguuni pake Yesu” na kusikiliza maneno Yake. Wakati Martha alipohisi amezidiwa kwa utumishi bila ya usaidizi, alimlalamikia, “Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu?”
Ninapenda maneno ya karipio la upole zaidi ambalo naweza kufikiria. Kwa upendo kamili na huruma usio na kikomo, Mwokozi alimkaripia:
Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi;
“Lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”23
Kina dada, ili tuwe watakatifu, ni lazima tujifunze kuketi miguuni pake Mtakatifu wa Israeli na tutenge wakati kwa ajili ya utakatifu. Je, tunaiweka simu kando, orodha ya majukumu yasiyo na kikomo, na shida za dunia? Sala, kujifunza, na kushika neno la Mungu huleta upendo Wake wa utakasaji na uponyaji katika nafsi zetu. Acha tutenga muda wa kuwa watakatifu, ili tuweze kujazwa na roho Wake mtakatifu na Roho wa kutakasa. Na Roho Mtakatifu kama kiongozi wetu, tutakuwa tayari kumpokea Mwokozi katika uzuri wa utakatifu.24
Utakatifu ni kuwa mtakatifu kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.
Kulingana na maneno yenye msukumo ya Mfalme Benjamin, wale ambao wamekuwa watakatifu kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo ni wale ambao ni watiifu, wapole, wanyenyekevu, wenye subira, na waliojawa na upendo, kama Mwokozi alivyo.25 Alitoa unabii ya kwamba Yesu Kristo, “Bwana Mwenyezi ambaye anatawala, ambaye alikuwa, na yuko kutoka milele yote hadi milele yote, atashuka chini kutoka mbinguni miongoni mwa watoto wa watu, na ataishi katika hekalu la udongo.” Alikuja kuwabariki wagonjwa, walemavu, viziwi, vipofu, na kuwafufua wale waliokuwa wamekufa kuwa hai. Na bado aliteseka “hata zaidi ya vile mtu anaweza kuteseka, ila tu hadi kifo.”26 Na ijapokuwa ni yeye pekee ambaye kupitia kwake wokovu unapatikana, alifanyiwa mzaha, akapigwa, na akamsulubishwa. Lakini Mwana wa Mungu alifufuka kutoka kaburini, ili sote tuweze kushinda kifo. Ni yeye atakayesimama kuhukumu dunia katika haki. Ni yeye atakayetukomboa sisi wote. Yeye ndiye Mtakatifu wa Israeli. Yesu Kristo ndiye Uzuri wa Utakatifu.
Wakati watu wa Mfalme Benjamin walisikia maneno yake, walianguka ardhini, unyenyekevu wao na heshima yao kwa neema na utukufu wa Mungu wetu ulikuwa mkubwa mno. Walitambua hali yao ya kimwili. Je, tunatambua kutegemea kwetu kabisa kwa neema na huruma ya Kristo, Bwana wetu? Je, tunatambua ya kwamba kila zawadi njema, ya muda au kiroho, inatujia kupitia Kristo? Je, tunakumbuka ya kwamba kulingana na mpango wa Baba wa milele, amani katika maisha haya na utukufu wa milele ni wetu tu katika na kupitia kwa Mwanawe Mtakatifu?
Natuungane na watu wa Mfalme Benjamin walipolia kwa sauti moja kubwa, “Ewe tuhurumie, na utumie damu ya upatanisho wa Kristo kwamba tupokee msamaha wa dhambi zetu, na mioyo yetu isafishwe; kwani tunamwamini Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, aliyeumba mbingu na dunia, na vitu vyote.”27
Ninashuhudia ya kwamba ikiwa tutakuja kwa Mtakatifu wa Israeli, Roho Yake itakuja juu yetu ili tujazwe na furaha, na tupokee ondoleo la dhambi zetu na amani ya dhamira.
Baba wa Mbinguni amempatia kila mmoja wetu uwezo wa kuwa mtakatifu. Ninajua ya kwamba tunapoweka maagano yetu, kumfanya Roho kiongozi wetu. Kwa imani katika Yesu Kristo, tuwe watakatifu kupitia Upatanisho Wake, ili tuweze kupokea kutokufa na maisha ya milele na kutampa Mungu Baba yetu utukufu unaostahili jina Lake. Acha Maisha yetu yawe sadaka takatifu, ili tuweze kusimama mbele za Bwana katika uzuri wa utakatifu. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.