2010–2019
Simama Ndani na Kuwa Ndani
Aprili 2017


11:59

Simama Ndani na Uwe Ndani

Naomba tufanye upya mpangilio wa njia yetu kama inahitajika  na kuangalia mbele kwa matumaini na imani kubwa. Na “tusimame imara ndani” kwa kuwa jasiri na “ndani pamoja.”

Miaka kadhaa iliyopita binti mjukuu wetu mdogo alinikimbilia na kwa furaha alitamka, “Babu, babu, nimefunga magoli yote matatu katika mchezo wangu wa soka leo!”

Kwa shauku nikajibu, “Vizuri sana, Sarah!”

Mama yake alinitazama kwa jicho la kukonyeza na akasema, “Magoli yalikuwa mawili kwa moja.”

Sikuthubutu kuuliza nani alishinda!

Mkutano mkuu ni muda wa kutafakari, ufunuo, na wakati mwingine mwelekeo mpya.

Kuna kampuni ya kukodisha magari yakiwa na GPS iitwayo NeverLost. Kama unakata kona isiyo sahihi kuelekea uendako, sauti inayoongoza haisemi, “Wee mpumbavu!” Lakini badala yake, kwa sauti ya kufurahisha, inasema, “Tunafanya upya mpangilio wa njia—ikiwezekana geuza kurudi utokako sheria.”

Katika Ezekieli tunasoma ahadi hii nzuri:

“Kama mtu mwovu akiachana na dhambi zake alizotenda, kama atashika kanuni zangu zote, na akatenda yaliyo ya haki na sawa, huyo hakika ataishi, hatakufa.

“Uvunjaji sheria wake wote aliofanya, hautakumbukwa.”1

Ni ahadi nzuri kiasi gani, lakini huhitaji mbili zote ili kupokea ile ahadi ya tatu. Achana na yote; shika yote; kisha yote yamesamehewa. Hii inahitaji kuwa “ndani pamoja”!

Hatupaswi kuwa kama yule mtu ambaye, kama Wall Street Journal ilivyotoa taarifa, alituma bahasha iliyojaa fedha pamoja na barua iliyopelekwa kwenye Idara ya Huduma ya Mapato ambayo ilisema, “Mpendwa IRS, Kilichomo ndani tafadhali pokea pesa ya kodi ninayodaiwa kwenye kodi zilizopita. Kama baada ya hili dhamira yangu bado itanisumbua, nitawatumieni iliyobaki.”2

Hivi sivyo tunavyofanya! Hatuachi kulipa kodi sahihi ili kuona ni kima gani cha chini tunachoweza kukwepa. Bwana anahitaji moyo na akili yenye kukubali.3 Kwa moyo wetu wote! Tunapobatizwa, tunazamishwa kabisa kama ishara ya ahadi yetu ya kumfuata Mwokozi kikamilifu, na siyo kwa nusu moyo. Wakati tunapojizatiti kikamilifu na “ndani pamoja,” mbingu hutikisika kwa mazuri yetu.4 Wakati tunapokuwa vuguvugu au kujizatiti nusu nusu, tunapoteza baadhi ya baraka nono za mbinguni.5

Miaka mingi iliyopita, niliwapeleka Maskauti kupiga kambi jangwani. Wavulana walilala karibu na moto mkubwa walioukoka, na kama ilivyo kwa kila kiongozi mzuri wa Skauti, nililala nyuma ya gari langu. Asubuhi nilipoamka na kuangalia pale kambini, nilimwona Skauti mmoja, ambaye nitamwita Paul, ambaye alionekana mchafu amekaa pembeni. Nilimwuliza jinsi alivyolala, na akajibu, “Sikulala vizuri.”

Nilipomwuliza kwa nini, alisema, “Nilijisikia baridi; moto ulizima.”

Nikamjibu, “Sawa, moto huwa hufanya hivyo. Je, mfuko wako wa kulalia haukuwa na joto la kutosha?”

Hakuna jibu.

Kisha mmoja wa vijana wa Skauti kwa sauti akajitolea kuongea, “Hakutumia mfuko wake wa kulalia.”

Nikauliza kwa mshangao, “Kwa nini, Paul?”

Kimya—kisha hatimaye kwa aibu alijibu: “Sawa, nilidhani kama nisingeukunjua mfuko wangu wa kulalia, nisingetakiwa kuukunja tena.”

Hadithi ya kweli: alipigwa na baridi kwa sababu ya kujaribu kuokoa dakika tano za kufanya kazi. Tunaweza kudhania, “Ni ujinga vipi! Ni nani angeweza kufanya hivyo? Hakika, tunafanya hivi kila wakati katika njia za hatari zaidi. Sisi, kwa kweli, tunakataa kuanua mifuko yetu ya kulalia ya kiroho wakati tunaposhindwa kuchukua muda kwa ajili ya kuomba kwa dhati, kujifunza, na kwa umakini kuishi injili kila siku; siyo tu moto utazima, bali hatutalindwa na kupatwa na baridi kiroho.

Wakati tunapokuwa tumeridhika mno na maagano yetu, tunakula njama na matokeo yake. Bwana ametushauri “kuwa waangalifu juu yenu wenyewe, ili kufanya bidii ya usikivu kwa maneno ya uzima wa milele.”6 Na kisha akatangaza, “Damu yangu haitawatakasa kama hawatanisikiliza.”7

Katika uhalisia, ni rahisi sana kuwa “ndani kabisa” kuliko kuwa ndani nusu au kutokuwa ndani kabisa, kuna, katika lugha ya Star Wars , “usumbufu katika jeshi.” Tumeenda kinyume cha asili ya mapenzi ya Mungu na kwa hivyo kinyume cha asili ya furaha.8 Isaya alisema:

“Bali wabaya wanafanana na bahari iliyochafuka; maana haiwezi kutulia, na maji yake hutoa tope na takataka.

“Hapana amani kwa wabaya; asema Mungu wangu.”9

Kwa bahati, bila kujali tupo ni wapi au tulikuwa wapi, hatupo mbali na uwepo wa Mwokozi, aliyesema: “Kwa hivyo, yeyote anayetubu na kuja kwangu kama mtoto mdogo, yeye nitampokea, kwani hivyo ndivyo ulivyo ufalme wa Mungu. Tazama, kwa ajili ya kama hawa nimetoa maisha yangu, na nimeyachukua tena.”10

Tunapoendelea kutubu na kumtumaini Bwana, tunapata nguvu tunapozungukwa na kuwa na uvumilivu na imani kama ya mtoto mchanga,11 tukistawishwa na hekima inayozaliwa kutokana na uzoefu wa maisha. Ayubu alisema, “ Lakini mwenye haki ataishika njia yake, Naye mwenye mikono safi atazidi kupata nguvu.”12 Alikuwa ni Tennyson ambaye aliandika, “nguvu zangu ni sawa na nguvu za watu kumi, kwa sababu moyo wangu ni msafi.”13 Bwana ameshauri, “Simameni katika mahali pa takatifu, na wala msiondoshwe.”14

Mwana wetu Justin alifariki akiwa na miaka 19 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Katika kipindi cha maongezi ya sakramenti aliongea kabla hajatuacha, alishiriki nasi hadhithi ambayo lazima ilivuma pamoja naye kuhusu baba na mwanawe mdogo ambao walikwenda kwenye duka la wanasesere ambako kulikuwa na begi ya kujazwa na upepo yenye umbile la mtu. Mvulana alipiga konde yule mtu hewa ambaye alianguka na mara akasimama tena kila baada ya konde. Baba akamwuliza mwanawe mdogo kwa nini yule mtu alikuwa akisimama tena. Kijana alifikiria kwa muda na kisha akasema, “Sijui. Nahisi ni kwa sababu anasimama kwa ndani.” Ili kuwa “ndani pamoja,” tunatakiwa “kusimama ndani,” “lolote liwalo.”15

Tunasimama ndani wakati tunaposubiri kwa uvumilivu hadi Bwana atuondoe au atupe nguvu za kuvumilia miiba yetu katika mwili.16 Miiba ya aina hiyo yaweza kuwa ugonjwa, ulemavu, utindio wa akili, kifo cha tuwapendao, na mambo mengi mengi.

Tunasimama ndani wakati tunapoinua juu mikono ambayo imelegea. Tunasimama ndani tunapoutetea ukweli dhidi ya uovu na ulimwengu ambao unaongezeka zaidi kutokuwa na raha kwa ajili ya nuru, wakiita uovu wema na wema ni uovu17 na “kuhukumu wale wenye haki kwa sababu ya haki yao.”18

Kusimama ndani bila kujali ugumu inawezekana kwa sababu ya dhamira wazi, uimarisho na uhakika wa ufariji kutoka kwa Roho Mtakatifu na matarajio ya milele ambayo yanashinda uelewa wa kimwili.19 Katika maisha yetu kabla ya kuzaliwa tulipiga kelele kwa shangwe kwa fursa ya kupata uzoefu katika mwili wenye kufa.20 Wote tulikuwa “ndani pamoja” tukiwa na furaha tulifanya maamuzi ya kuwa wateteaji jasiri wa mpango wa Baba yetu wa Mbinguni. Ni wakati wa kusimama na kuutetea mpango Wake!

Baba yangu wa miaka 97 amefariki hivi karibuni. Wakati mtu alipomuuliza alikuwa anaendeleaje, jibu lake la wakati wote lilikuwa, “Katika kipimo cha 1–10, nipo karibu 25!” Japokuwa mtu huyu mpendwa hakuweza tena kusimama au hata kukaa, na kupata wakati mgumu kuongea, jibu lake lilikuwa lile lile. Wakati wote kwa ndani alisimama.

Wakati baba yangu alipokuwa na miaka 90, tulikuwa uwanja wa ndege na nikamwomba nimletee kitimwendo. Alisema, “Hapana, Gary—labda nitakapokuwa mzee.” Na kisha akaongeza, “Pamoja na hivyo, nikichoka kutembea, ninaweza wakati wote kukimbia.” Kama hatuwezi kuwa “ndani pamoja” jinsi tunavyotembea sasa, hapo ndipo huenda tunahitaji kukimbia; ndipo huenda tunatakiwa kufanya upya mpangilio wa njia yetu. Inawezekana tukahitaji kupinda kona ya kurudi tutokako. Yawezekana tunahitaji kusoma kwa makini zaidi, kuomba kwa dhati zaidi, au kuacha vitu vingine vipite ili tuweze kushikilia vitu ambavyo vina maana. Yawezekana tunahitaji kuyaacha mambo ya kidunia ili tuweze kuyashika ya milele. Baba yangu alilielewa hili.

Baba ya Mzee Sain katika jeshi la mwanamaji

Wakati alipokuwa katika jeshi la wana maji kipindi cha Vita Kuu ya Pili ya Dunia, palikuwepo na wale waliokuwa kwenye jumba kubwana pana21 ambao walifanya mzaha wa kanuni zake; rafiki zake wawili kwenye meli, Dale Maddox na Don Davidson, walifanya muhtasari na hawakumtania. Walimwuliza, “Sabin, kwa nini u tofauti na watu wengine? Una uadilifu mkubwa na hunywi, huvuti, au huapi, lakini unaonekana mpole na mwenye furaha.”

Mwonekano chanya wa baba yangu hakufanana na jinsi walivyofundishwa kuhusu Wamormoni, na baba yangu aliweza kufundisha na kuwabatiza mabaharia wenzake wote wawili. Wazazi wa Dale wakasirika sana na wakamuonya kwamba kama akijiunga na Kanisa atampoteza kipenzi chake, Maryolive, lakini alikutana na wamisionari kwa maombi yake na pia yeye alibatizwa.

Karibu na mwisho wa vita, Rais Heber J. Grant aliwaita wamisionari ikijumuisha baadhi ya wanaume waliooa. Mwaka wa 1946, Dale na mke wake, Mary Olive, waliamua Dale akatumikie japokuwa walikuwa wanatarajia mtoto wao wa kwanza. Hatimaye walikuwa na watoto tisa, wavulana watatu na wasichana sita. Wote tisa walihudumu misheni, wakifuatiwa na Dale na Mary Olive ambao walihudumu misheni zao tatu. Majozi ya wajukuu wao wamehudumu pia. Wana wao wawili, John na Matthew Maddox, ni washiriki wa Kwaya ya Tabernacle, na pia Ryan , mkwe wake wa Matthew. Familia ya Maddox sana ina idadi ya 144 na ni mifano ya ajabu ya “kuwa ndani pamoja.”

Wanafamilia wa Maddox katika Kwaya ya Tabernacle

Nikiwa napitia hati za baba yangu, tukakutana na barua kutoka kwa Jennifer Richards, mmoja kati ya mabinti watano wa baharia mwenzi, Don Davidson. Aliandika: “Uadilifu wako ulibadilisha maisha yetu. Ni vigumu kutambua jinsi maisha yetu yanavyoweza kuwa bila Kanisa. Baba yangu alikufa akiipenda injili na kujaribu kuiishi hadi mwisho.”22

Ni vigumu kupima matokeo mazuri ya kila mtu anayoweza kuwanayo kwa kusimama ndani. Baba yangu na mabaharia wenzake wawili walikataa kuwasikiliza wale waliokuwa kwenye jengo kubwa na pana ambao walikuwa wakiwanyoshea vidole vya dhihaka.23 Walijua kwamba ni vizuri kumfuata Muumba badala ya kufuata umati.

Mtume Paulo alikuwa anaelezea siku yetu wakati alipokuwa anamwambia Timotheo kwamba “watu wengine wamepotoka, wamegeukia majadiliano yasiyo na maana.”24 Kuna “majadiliano yasiyo na maana” mengi ambayo yanaendelea katika ulimwengu leo. Ni maongezi ya wale walio katika jengo lile kubwa na pana.25 Mara nyingi yanaonekana ni njia ya kurazini maovu au kujidhihirisha wenyewe wakati watu wanapopotea njia na kuharakisha. Wakati mwingine yanakuja toka kwa wale ambao hawajalipia bei ya kuwa “ndani pamoja” na kutaka kumfuata mtu wa kawaida kama ilivyopingwa na nabii.

Vizuri, tunajua mwisho wake kwa wale walio waaminifu. Wakati tukiwa “ndani pamoja,” tunakuwa na uhakika kwamba “vitu vyote hufanya kazi kwa pamoja vyema kwa wale wanaompenda Mungu.”26  Mzee Neal A. Maxwell alisema, “Usiogope, ishi kwa maadili tu.”27

Baba mkwe wangu alifundisha BYU na aliipenda timu ya mpira ya BYU lakini hakuweza kwenda kuangalia mechi zao kwa sababu alikuwa mwoga juu ya matokeo. Ndipo kitu kizuri kikatokea; VCR (deki) iligunduliwa, ambayo ilimwezesha kurekodi mechi. Kama BYU ilishinda, ataangalia mechi aliyoirekodi akiwa na uhakika mkubwa, akiwa na uhakika wa matokeo! Kama walipewa adhabu isiyostahili, kuumia, au kuwa nyuma katika robo ya nne, hakuwa na wasiwasi kwa sababu alijua watashinda! Unaweza kusema alikuwa “na maono mazuri ya matumaini”!28

Hivi ndivyo ilivyo kwetu pia. Tukiwa waaminifu, tunaweza kuwa na uhakika sawa sawa na huo kwamba mambo yataenda vizuri kwetu hapo mwishoni. Ahadi za Bwana ni za kweli. Hii haimaanishi hiki chuo cha mauti kitakuwa rahisi au bila ya machozi, bali kama Paulo alivyoandika, “Jicho halijapata kuona, wala sikio kuyasikia, mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao”29

Akina kaka na akina dada, hakuna aliyetenda dhambi kesho. Naomba tufanye upya mpangilio wa njia yetu kama inahitajika  na kuangalia mbele kwa matumaini na imani kubwa. Naomba “tusimame ndani” kwa kuwa hodari na “ndani pamoja.” Naomba tuwe wasafi na mashujaa katika kuulinda mpango wa Baba wa Mbinguni na misheni ya Mwana Wake, Mwokozi wetu. Natoa ushahidi wangu kwamba Baba yetu yu hai, kwamba Yesu ndiye Kristo, na juu ya uhalisia wa mpango mkuu wa furaha. Naomba baraka teule za Bwana ziwe nanyi, na ninafanya hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.