Kung’ara na Kung’ara hata Mchana Mkamilifu.
Hata katika nyakati ngumu zaidi na zenye giza, kuna nuru na wema kote kutuzunguka sisi.
Paulo alielezea ujumbe wa kupendeza wa matumaini kwa Wakorintho:
“Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa;
“Twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi.”1
Nini kilikuwa chanzo cha matumaini ya Paulo? Sikiliza majibu yake: “Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang’aa toka gizani, ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo.”2
Hata katika nyakati ngumu zaidi na zenye giza, kuna nuru na wema kote kutuzunguka sisi. Oktoba iliyopita Rais Dieter F. Uchtdorf alitukumbusha, “Tumezungukwa na utajiri wa nuru na ukweli wa ajabu hata kwamba nashangaa kama kwa kweli tunathamini kile tulichonacho.3
Hata hivyo, adui angetaka atufanye tuzingatie “ukungu wa giza … wenye kupofusha macho, … kushupaza, mioyo … , na … kuelekeza … mbali.”4
“Na kile kilicho cha Mungu ni nuru; na yule ambaye huipokea nuru, na kukaa ndani ya Mungu, hupokea nuru zaidi; na nuru hiyo huzidi kung’ara hata mchana mkamilifu.”5
Sisi ni watoto wa Mungu. Kupokea nuru, kuendelea katika Mungu, na kupokea nuru zaidi ndio tumeumbwa kufanya. Tokea mwanzo kabisa, tulifuata nuru; tulimfuata Baba yetu wa Mbinguni na mpango Wake. Kutafuta nuru kuko katika DNA yetu ya kiroho.
Nilisikia ukweli huu wa milele ukifundishwa vizuri zaidi katika sehemu nyingine isiyotarajiwa Nilipokuwa nikifanya kazi katika benki kubwa, nilialikwa kuhudhuria programu ya utendaji katika Chuo Kikuu cha Michigan. Wakati wa programu, Profesa Kim Cameron alifundisha dhana ya uongozi mwema na athari zake kiheliotropiki. Alieleza: “Hii ina maana ya tabia katika mifumo yote hai kuegemea nishati chanya [mwanga] mbali na nishati hasi [giza]. Kutoka kwenye kiini chenye chembehai kimoja hadi kwa mifumo tata wa binadamu, kila kitu hai kina asili ya kuelekea upande chanya mbali na hasi.”6
Kwa usaidizi wa utajiri wa masomo, pia alilenga vipengele vitatu muhimu vya utamaduni bora wa sehemu ya kazi: huruma, msamaha, na shukrani.7 Ni jambo linalofaa kikamilifu kwamba watu wanapogeuka kuelekea kwa yale chanya [nuru], sifa zilizodhihirishwa kikamilifu na Nuru ya Ulimwengu, Yesu Kristo, zipo!
Kaka zangu na na dada zangu, tafadhali mfurahie kwamba kuna nuru inayopatikana kwetu sisi. Naomba nipendekeze maeneo matatu ambapo daima tutaweza kupata nuru:
1. Nuru ya Kanisa
Kanisa ni nguzo ya nuru kwa ulimwengu wenye giza. Huu ni wakati wa kupendeza wa kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho! Kanisa ni imara zaidi kuliko lilivyowahi kuwa8 na kwa uhalisia linaimarika kila siku kadiri waumini wapya wanavyojiunga nasi, mikusanyiko mipya inaundwa, wamisionari wapya wanaitwa, na maeneo mapya yanafunguliwa kwa ajili ya injili. Tunaona wale ambao wameteleza kutoka kwenye shughuli za Kanisa kwa muda wakirudi kama uokoaji uliotabiriwa na Rais Thomas S. Monson ukileta miujiza wa kila siku.
Hivi karibuni niliwatembelea vijana huko Paraguay, Uruguay, Chile, na Argentina wakati wao wa mikutano yao ya For the Strength of Youth (Kwa Uimara wa Vijana). Maelfu ya wavulana na wasichana walikaa wiki nzima wakiimarisha upendo wao wa Mwokozi, kisha wakarudi nyumbani kwenye familia zao na marafiki wakiakisi nuru na upendo wa Kristo.
Angalia, daima Kanisa litakuwa na wakosoaji wake. Imekuwa hivyo tangu mwanzo na itaendelea hadi mwisho. Hatuwezi kuruhusu upinzani kama huo kupoozesha hisia zetu kwa nuru ambayo inapatikana kwetu Kwa kutambua mwanga na kuufuata utatupasisha sisi kupata hata nuru zaidi.
Katika dunia inayotiwa giza, nuru ya Kanisa itang’ara na kung’ara hata mchana mkamilifu.
2. Nuru ya Injili
Nuru ya injili ni njia ambayo “inazidi kung’ara na kung’ara hata mchana mkamilifu,”9 na inazidi kung’ara zaidi katika familia zetu na katika mahekalu duniani kote.
Hubiri Injili Yangu inasema: “Kupitia nuru ya injili, familia zinaweza kutatua kutoelewana, ugomvi na changamoto. Familia zilizogawanyika kwa ajili ya kutoelewana zinaweza kuponywa kwa njia ya toba, msamaha, na imani katika uwezo wa Upatanisho wa Yesu Kristo.”10 Sasa kuliko wakati mwingine wowote, familia zetu lazima ziwe vyanzo vya nuru kuu kwa kila mtu anayetuzunguka. Familia zinaongezeka kwa nuru kadri zinavyokua katika upendo na wema. Tunapoanzisha familia za “imani, … toba, msamaha, heshima, upendo, [na] huruma,”11 tutahisi ongezeko la upendo kwa Mwokozi na kwetu wenyewe. Familia zitaimarika, na nuru katika kila mmoja wetu itang’ara
Tunasoma katika Kamusi ya Biblia, “Ni nyumbani pekee ndiko tunaweza kulinganisha na hekalu katika utakatifu.”12 Kwa sasa tuna mahekalu 155 yanayofanya kazi na mengine zaidi yana kuja hivi karibuni. Familia zaidi na zaidi zinaunganishwa kwa muda na milele yote. Waumini wanawasilisha majina zaidi ya mababu hekaluni ili kufanyiwa ibada zao zenye kuokoa. Tunaona furaha kubwa na sherehe katika pande zote za pazia!
Katika dunia inayotiwa giza, nuru ya Injili itang’ara na kung’ara hadi mchana mkamilifu.
3. Nuru ya Kristo
Huwezi kuongea juu ya nuru katika ulimwengu bila kuzungumzia juu ya Nuru ya Ulimwengu, Yesu Kristo. Dhihirisho la Baba mwenye upendo wa Mbinguni ni kwamba kila mtu ambaye anakuja katika maisha haya amebarikiwa kwa kuwa na Nuru ya Kristo ili kuwasaidia kurudi nyumbani. Mzee Boyd K. Packer alifundisha: “Roho wa Kristo yupo wakati wote. … Nuru ya Kristo ni ya ulimwengu wote kama jua lenyewe. Popote ambapo kuna maisha ya binadamu, kuna Roho wa Kristo.”13 Nuru ya Kristo “hukaribisha na hushawishi kufanya mema siku zote”14 na huandaa wote wanaotafuta mema na ukweli ili kumpokea Roho Mtakatifu.
Mwokozi anafundisha kwamba Yeye ndiye nuru ambayo “inaangaza macho yako,” “kuhuisha ufahamu wako,” na “kutoa uhai kwa vitu vyote.”15 Nuru ya Kristo itatusaidia kuona watu wengine kupitia macho ya Mwokozi. Tutapenda na kuelewa zaidi mapambano ya watu wengine. Itatusaidia kuwa na subira zaidi na wale ambao hawawezi kuabudu au kutumika kama sisi. Itatusaidia kuelewa mpango mkuu wa furaha kikamilifu zaidi na kuona jinsi sisi sote tutakavyoingia katika mpango huo mkuu wenye upendo. Hutupa maisha, maana, na kusudi kwa yote ambayo tunafanya. Kwa furaha yote ambayo itakuja kwetu tunapoelewa kikamilifu zaidi Nuru ya Kristo, haitalingana na furaha ambayo tunahisi tunapoona Nuru ya Kristo ikifanya kazi kwa wengine: familia, marafiki, na hata wageni.
Nilihisi furaha hiyo niliposikia kuhusu juhudi za kundi shujaa la kuzima moto ambao walipigana ili kuokoa kituo cha kigingi kilichokuwa kikiteketea katika Kusini mwa California mwezi Julai 2015 Moto ilipokuwa ikiendelea, kamanda wa kikosi alimwita rafikiye wa WSW ili kuuliza mahali ambapo sanduku takatifu na vikombe vya sakramenti vilipohifadhiwa ili waweze kuviokoa. Rafiki yake alimhakikishia kwamba hapakuwa na sanduku takatifu na kwamba vikombe vya sakramenti vitaweza kupatikana kwa urahisi sana. Lakini kamanda aliona kwamba anapaswa kufanya zaidi, hivyo akawatuma wazima moto wake kurejea ndani ya jengo lililokuwa likiteketea ili kuondoa kila mchoro wa Kristo kwenye ukuta ili iweze kuhifadhiwa. Hata waliweka moja ya picha hizo ndani ya gari ya kuzima moto kwa matumaini kwamba wazima moto waweze kulindwa. Hakika niliguswa na ukarimu, wema, kiwango cha kuhisi Nuru cha kamanda huyo, hasa katika wakati wa hatari na mgumu.
Katika dunia inayotiwa giza, Nuru ya Kristo itang’ara na kung’ara hata mchana mkamilifu.
Narudia tena maneno ya Paulo: “Basi tuzivae silaha za nuru.”16 Nashuhudia juu ya Kristo.Petro Anashuhudia juu ya Kristo. Yeye ndiye Nuru ya ulimwengu. Tuweze kuimarishwa na nuru ambayo inapatikana kwetu kwa njia ya ushiriki mkubwa kanisani na matumizi zaidi ya kanuni za injili katika familia zetu. Tuweze kuona Nuru ya Kristo kwa wengine mara kwa mara na kuwasaidia kuiona ndani yao wenyewe. Tunapopokea nuru hiyo, tutabarikiwa kuwa na nuru zaidi, hata mpaka siku kamili tutakapomwona tena “Baba wa mianga,”17 Baba yetu wa Mbinguni. Hivyo nashuhudia katika jina takatifu la Nuru wa Ulimwengu, hata Yesu Kristo, amina.