Agano la Kale 2022
Septemba 11. Ni kwa Jinsi Gani Ninaweza Kuwa Msafi na Mwenye Furaha Tena Baada ya Kutenda Dhambi? Isaya 1–12


“Septemba 11. Ni kwa Jinsi Gani Ninaweza Kuwa Msafi na Mwenye Furaha Tena Baada ya Kutenda Dhambi? Isaya 1–12,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Akidi za Ukuhani wa Haruni na Madarasa ya Wasichana: Mada za Mafundisho 2022 (2021)

“Septemba 11. Ni kwa Jinsi Gani Ninaweza Kuwa Msafi na Mwenye Furaha Tena Baada ya Kutenda Dhambi? Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Akidi za Ukuhani wa Haruni na Madarasa ya Wasichana: Mada za Mafundisho 2022

Picha
mvulana akitabasamu

Septemba 11

Ni kwa Jinsi Gani Ninaweza Kuwa Msafi na Mwenye Furaha Tena Baada ya Kutenda Dhambi?

Isaya 1–12

Picha
ikoni ya kushauriana kwa pamoja

Shaurianeni kwa Pamoja

Ikiongozwa na mshiriki wa urais wa akidi au wa darasa; dakika 10–20

Mwanzoni mwa mkutano, rudieni kwa pamoja Dhamira ya Wasichana au Dhamira ya Akidi ya Ukuhani wa Haruni. Kisha ongoza mjadala kuhusu kazi ya wokovu na kuinuliwa ukitumia swali moja ua mengi ya yale yaliyopo hapo chini au yako mwenyewe (ona General Handbook, 10.2, 11.2, ChurchofJesusChrist.org). Panga njia za kutenda juu ya kile mnachojadili.

  • Ishi injili. Ni kwa jinsi gani kumgeukia Bwana hutusaidia kukabiliana changamoto zetu na majaribu yetu?

  • Utunzaji wa wale walio na mahitaji. Nani tunamjua ambaye anahitaji maombi yetu na urafiki wetu?

  • Waalike wote kuipokea injili. Ni mipango gani ya kushiriki injili iliyojadiliwa katika mikutano ya baraza la vijana la kata? Ni kwa jinsi gani darasa letu au akidi yetu inaweza kushiriki?

  • Unganisha familia milele. Ni kwa jinsi gani kazi ya historia ya familia imeimarisha mahusiano yetu na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo?

Mwishoni mwa somo, kama inafaa, fanya yafuatayo:

  • Shuhudia juu ya kanuni zilizofundishwa.

  • Wakumbushe washiriki wa darasa au akidi kuhusu mipango na mialiko iliyotolewa wakati wa mkutano.

Fundisha Mafundisho

Ikiongozwa na mtu mzima au kijana; dakika 25–35

Jiandae Binafsi Kiroho

Tunapohisi tuna hatia baada ya dhambi, tuna chaguo. Hisia hizi, ingawa zinaumiza, zinaweza kuwa baraka kama zitatufanya tutubu. Lakini Shetani anatuambia hisia hizi zinamaanisha kwamba Mungu hatupendi na hujaribu kutufanya tuhisi kukata tamaa na kukosa matumaini. Kunaweza kuwa na watu unaowafundisha ambao wana mzigo wa hisia kama hizo. Wanaweza kushangaa kama daima wanaweza kuwa wasafi na wenye furaha tena. Ni kwa jinsi gani ungeweza kuwasaidia kupata tumaini katika Upatanisho wa Mwokozi?

Nabii Isaya kwa ujasiri aliwarudi watu kwa sababu ya dhambi zao. Lakini yeye pia alishuhudia kwamba kwa sababu ya Mwokozi: “dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji (Isaya 1:18). Tafakari hili unaposoma Isaya 1–12 wiki hii. Nini kingeweza kuwapa mwongozo wale unaowafundisha kumgeukia Yesu Kristo kwa imani kwamba mizigo ya dhambi zao inaweza kuondolewa? Ungeweza pia kujifunza ushuhuda wa Dada Sharon Eubank juu ya Kristo katika ujumbe wake “Kristo: Nuru Ambayo Huangaza Gizani” (Liahona, Mei 2019, 73–76).

Picha
darasa la wasichana

Kwa sababu ya Yesu Kristo, mizigo yetu ya dhambi inaweza kuondolewa.

Jifunzeni Pamoja

Ili kujiandaa kwa ajili ya mjadala ambao unajenga juu ya Isaya 1–12, unaweza kumuomba kila kijana kuleta kwenye mkutano kitu chekundu na kitu cheupe. Unaweza kuvionyesha vitu hivi mnaposoma pamoja Isaya 1:16–18. Kisha vijana wanaweza kushiriki kwa maneno yao wenyewe kile walichojifunza kutoka kwa mistari hii. (Ona mjadala wa Dada Sharon Eubank wa mstari wa 18Kristo: Nuru Ambayo Huangaza Gizani.”) Hapa kuna baadhi ya shughuli zingine ambazo zinaweza kuleta imani katika nguvu za Mwokozi za kutufanya kuwa wasafi kiroho.

  • Kupitia tena mifano ya maandiko juu ya toba kunaweza kuwasaidia wale unaowafundisha kujenga imani yao kwamba Yesu Kristo anaweza kuwafanya wasafi kiroho. Ungeweza kuandika majina ubaoni kama vile Saulo (baadaye Paulo), Alma Kijana, Zeeziromu, na Anti-Nefi-Lehi. Unaweza pia kuandika makundi mawili ya marejeo ya maandiko: Matendo ya Mitume 8:3; Mosia 27:8–10; Alma 11:21–23; Alma 17:12–15 (watu hawa katika hali yao ya dhambi) na Matendo ya Mitume 9:13–20; Alma 36:17–24; Alma 15:5–12; Alma 23:6–12 (baada ya watu hawa kumgeukia Mwokozi na kutubu). Vijana wangeweza kuoanisha kila jina na maandiko yanayoelezea mtu yule. Watu walifanya nini ili kutubu? Matukio haya yanafundisha nini kuhusu utayari wa Mwokozi kusamehe? Je, tunaona mipangilio fulani tunayoweza kufuata?

  • Ili kuwasaidia wale unaowafundisha kuelewa vyema msamaha wa dhambi, unaweza kumpa kila mtu analojia au fumbo kujifunza. Haya yanaweza kujumuisha mwana mpotevu (ona Luka 15:11–24); Mwokozi kama Mchungaji wetu (aya ya 5–8 ya ujumbe wa Mzee Dale G. Renlund “Mchungani Wetu Mwema” [Liahona, Mei 2017, 29–32]); na kinanda kilichovunjika (mwanzoni mwa ujumbe wa Dada Cristina B. Franco “Nguvu za Uponyaji za Yesu Kristo” [Liahona, Nov. 2020, 60–62]). Vijana wanaweza kufanya muhtasari wa kila analojia au fumbo na kujadili kile linafundisha kuhusu upendo na nguvu za upatanisho za Mwokozi.

  • Kuhisi majuto kwamba tumetenda dhambi inasaidia na inatuongoza kuelekea toba. Kuhisi kukata tamaa au kutokuwa na thamani kwa sababu ya dhambi zetu haisaidii na inaweza kutuzuia kutubu. Darasa lako au akidi inaweza kusoma pamoja sehemu yenye kichwa “Huzuni za Kiungu” katika ujumbe wa Rais Dieter F. Uchtdorf “Unaweza Kufanya Hivyo Sasa!” (Liahona, Nov. 2013, 55–57). Ni nini tofauti kati ya huzuni kwa ajili dhambi unayoongoza kwenye toba na huzuni ambao inaongoza kwenye kukata tamaa? (ona pia 2 Wakorintho 7:9–10; Mormoni 2:12–14). Kama mtu anahisi kushindwa na hisia za kuwa na hatia na kukata tamaa kwa ajili ya dhambi, ni nini tungeweza kumwambia kumsaidia yeye kumgeukia Mwokozi? Waalike vijana kushiriki shuhuda zao za Mwokozi na rehema Zake.

Tenda kwa Imani

Watie moyo washiriki wa darasa au akidi kutafakari na kuandika kile watakachofanya juu misukumo waliyoipokea leo. Kama wangependa, wangeweza kushiriki mawazo yao. Waalike wafikirie kuhusu jinsi kutenda juu ya misukumo yao kutaimarisha mahusiano yao na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.

Nyenzo Saidizi

  • Dallin H. Oaks “Kutakaswa kwa Toba, Liahona, Mei 2019, 91–94

  • Toba kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo,” katika sura ya 3 ya Hubiri Injili Yangu (2019), 62–63

  • Repentance: A Joyful Choice” (video), ChurchofJesusChrist.org

Kufundisha katika Njia ya Mwokozi

“Ushuhuda binafsi wa Mwokozi uliwapatia mamlaka maneno Yake. … Unaposhuhudia mafundisho ya ukweli wa maandiko, Roho atathibitisha ukweli wa mafundisho katika mioyo ya wale unaowafundisha” (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 21).

Chapisha