Njoo, Unifuate 2024
Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani


“Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani,” Njoo, Unifuate——Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2023)

“Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024

Picha
familia ikijifunza maandiko

Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani

Nyenzo Hii Ni Kwa Ajili ya Nani?

Nyenzo hii ni kwa ajili ya mtu yeyote anayetaka kujifunza kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni—kama mtu binafsi au kama familia, na katika madarasa ya Kanisa. Kama hukuwa ukijifunza maandiko mara kwa mara huko nyuma, nyenzo hii inaweza kukusaidia uanze. Kama tayari una mazoea mazuri ya kujifunza maandiko, nyenzo hii inaweza kukusaidia upate uzoefu mwingi wenye maana.

Watu Binafsi na Familia Nyumbani

Mahali pazuri pa kujifunza injili ni nyumbani. Walimu wako kanisani wanaweza kukusaidia, na unaweza kupata uhamasisho kutoka kwa waumini wengine wa kata. Lakini kunusurika kiroho, wewe na familia yako mnahitaji kulishwa kwa “neno jema la Mungu” (Moroni 6:4: ona pia Russell M. Nelson, “Maneno ya Ufunguzi,” Liahona, Nov. 2018, 6–8).

Tumia nyenzo hii katika njia yoyote ambayo ina manufaa kwako. Mihutasari huangazia baadhi ya kweli za milele zinazopatikana katika Kitabu cha Mormoni, hupendekeza mawazo na shughuli za kukusaidia ujifunze maandiko wewe binafsi, pamoja na familia, au na marafiki. Unapojifunza, fuata mwongozo wa Roho ili kupata kweli za milele ambazo zinaleta maana kwako. Tafuta jumbe za Mungu kwa ajili yako, na kufuata misukumo unayopokea.

Walimu na Wanafunzi Kanisani

Kama unafundisha darasa la Msingi, vijana au darasa la watu wazima la Shule ya Jumapili, Ukuhani wa Haruni, au darasa la Wasichana, unahimizwa kutumia mihutasari katika nyenzo hii unapojiandaa kufundisha. Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani ni mtaala kwa ajili ya darasa lako la Jumapili. Mawazo katika nyenzo hii yamesanifiwa kwa ajili ya kujifunza nyumbani na kanisani. Unapojiandaa kufundisha, anza kwa kuwa na uzoefu wako mwenyewe katika maandiko. Maandalizi yako muhimu zaidi yatatokea wakati unapopekua maandiko na kutafuta mwongozo wa Roho Mtakatifu. Tafuta kweli za milele ambazo zinakusaidia uwe zaidi kama Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Njoo, Unifuate inaweza kukusaidia utambue baadhi ya kweli hizi na uelewe muktadha wa maandiko.

Kumbuka kujifunza injili, katika ubora wake, ni pale kiini chake kinapokuwa nyumbani na kusaidiwa na Kanisa. Kwa maneno mengine, jukumu lako kubwa ni kuwasaidia watu unao wafundisha katika juhudi zao za kujifunza na kuishi injili nyumbani. Wape fursa ya kushiriki uzoefu wao, mawazo, na maswali kuhusu vifungu vya maandiko. Waalike washiriki kweli za milele walizozipata. Hii ni muhimu zaidi kuliko kusoma tu kiasi fulani cha maelezo.

Msingi

Maandalizi yako kwa ajili ya kufundisha Msingi huanza kwa kujifunza kwako Kitabu cha Mormoni wewe binafsi na pamoja na familia yako. Unapofanya hivyo, sikiliza misukumo ya kiroho na umaizi kutoka kwa Roho Mtakatifu kuhusu watoto katika darasa lako la Msingi. Kuwa mwenye kuomba, na Roho anaweza kukupa mwongozo wa kiungu na mawazo ili uwasaidie wajifunze injili ya Yesu Kristo.

Unapojiandaa kufundisha, unaweza kupata mwongozo wa ziada kwa kuchunguza mawazo ya kufundishia katika nyenzo hii. Kila muhtasari katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani una sehemu yenye kichwa cha habari “Mawazo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto.” Fikiria mawazo haya kama mapendekezo ya kuchochea kupata mwongozo wako wa kiungu. Unawajua watoto katika darasa lako la Msingi—na utapata kuwajua hata vizuri zaidi pale unapochangamana nao darasani. Bwana anawajua pia, na Yeye atakupa mwongozo wa kiungu wa njia iliyo bora zaidi ya kuwafundisha na kuwabariki.

Inawezekana kwamba watoto katika darasa lako watakuwa tayari wamefanya baadhi ya shughuli hizi katika Njoo, Unifuate pamoja na familia zao. Hiyo ni SAWA. Kurudia rudia ni vyema. Fikiria kuwaalika watoto kushiriki wao kwa wao kile walichojifunza nyumbani—ingawa unapaswa pia kupanga njia za watoto kushiriki hata kama hawakujifunza nyumbani. Watoto hujifunza kweli za injili kwa ufanisi zaidi wakati kweli hizi zinapofundishwa kwa kurudiwa rudiwa kupitia shughuli mbalimbali. Ikiwa unaona kuwa shughuli fulani ya kujifunza inafaa kwa watoto, fikiria kuirudia, hasa ikiwa unawafundisha watoto wadogo zaidi. Unaweza pia kurejelea tena shughuli kutoka kwenye somo lililopita.

Katika miezi ambayo ina Jumapili tano, walimu wa Msingi wanahimizwa kubadilisha muhtasari wa Njoo, Unifuate uliopangwa kwenye Jumapili ya tano kwa shughuli moja au zaidi za kujifunza katika “Kiambatisho B: Kwa ajili ya Msingi—Kuwaandaa Watoto kwa Maisha Yote Kwenye Njia ya Agano ya Mungu.”

Madarasa ya Vijana na Shule ya Jumapili ya Watu Wazima

Sababu moja muhimu ya sisi kukutana katika madarasa ya Shule ya Jumapili ni kusaidiana na kuhimizana mmoja na mwingine pale tunapojitahidi kumfuata Yesu Kristo. Njia rahisi tunayoweza kufanya hivyo ni kuuliza swali kama vile “Roho Mtakatifu amekufundisha nini wiki hii wakati ulipojifunza Kitabu cha Mormoni ukitumia Njoo, Unifuate?” Majibu ya swali hili yangeweza kuongoza kwenye mazungumzo ambayo yanajenga imani katika Yesu Kristo na Injili Yake.

Kisha ungeweza kualika majadiliano yaliyojikita kwenye mapendekezo ya kujifunza katika Njoo, Unifuate. Kwa mfano, wazo la kujifunza lingeweza kupendekeza kupekua Alma 36 na kutengeneza orodha ya maneno ambayo yanafundisha kuhusu jukumu la Mwokozi katika toba. Unaweza kuwaomba washiriki wa darasa kushiriki na kuzungumza kuhusu maneno waliyopata. Ama mngeweza kutumia sehemu ya muda kutengeneza orodha pamoja kama darasa.

Akidi za Ukuhani wa Haruni na Madarasa ya Wasichana

Wakati akidi za Ukuhani wa Haruni na Madarasa ya Wasichana wanapokutana Jumapili, kusudi lao ni tofauti kiasi fulani na darasa la Shule ya Jumapili. Kama nyongeza ya kusaidiana kujifunza injili ya Yesu Kristo, makundi haya pia yanakutana ili kushauriana pamoja kuhusu kutimiza kazi ya wokovu na kuinuliwa (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 1.2). Wanafanya hivi chini ya maelekezo ya urais wa darasa na akidi.

Kwa sababu hii, kila mkutano wa akidi au darasa linapaswa kuanza na mshiriki wa urais wa akidi au darasa akiongoza mazungumzo kuhusu juhudi, kwa mfano, za kuishi injili, kuwahudumia watu walio na shida, kushiriki injili, au kushiriki katika kazi ya hekalu na historia ya familia.

Baada ya muda huu wa kushauriana pamoja, mwelekezi anaongoza darasa au akidi katika kujifunza injili pamoja. Viongozi watu wazima au washiriki wa darasa au akidi wanaweza kupangiwa kufundisha. Urais wa darasa au akidi, ukishauriana na viongozi watu wazima, hupanga majukumu haya.

Watu waliopangiwa kufundisha wanapaswa kujiandaa kwa kutumia mapendekezo ya kujifunza katika muhtasari wa kila wiki wa Njoo, Unifuate. Katika kila muhtasari, ikoni hii huonyesha shughuli ambayo kwa upekee inahusiana na vijana. Hata hivyo, mapendekezo yoyote katika muhtasari huu yanaweza kutumiwa kama shughuli kwa ajili ya vijana.

Kwa ajili ya mfano wa ajenda za mikutano ya akidi na madarasa, ona kiambatisho D.

Chapisha