Njoo, Unifuate 2024
Kiambatisho B: Kwa ajili ya Msingi—Kuwaandaa Watoto kwa Maisha Yote Kwenye Njia ya Agano ya Mungu


“Kiambatisho B: Kwa ajili ya Msingi—Kuwaandaa Watoto kwa Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2023)

“Kiambatisho B,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024

Kiambatisho B

Kwa ajili ya Msingi—Kuwaandaa Watoto kwa Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu

Katika miezi ambayo ina Jumapili tano, walimu wa Msingi wanahimizwa kubadili ratiba ya muhtasari wa Njoo, Unifuate wa Jumapili ya tano kwa shughuli moja au zaidi za kujifunza.

kanuni na Ibada za Injili ya Yesu Kristo

Injili ya Kristo hutufundisha jinsi ya kurudi kwa Mungu.

Wakati Yesu Kristo alipowatokea watu katika Amerika, aliwafundisha mafundisho Yake. Alisema kwamba tunaweza kuingia katika ufalme wa Mungu ikiwa tuna imani, tutatubu, kubatizwa, kupokea Roho Mtakatifu na kuvumilia hadi mwisho (ona 3 Nefi 11:31–40; Mafundisho na Maagano 20:29). Shughuli zilizo hapa chini zinaweza kukusaidia uwafundishe watoto kwamba kanuni na ibada hizi hutusaidia tumkaribie Mwokozi katika maisha yetu yote.

Ili kujifunza zaidi kuhusu mafundisho ya Kristo, ona 2 Nefi 31.

Shughuli Yamkini

  • Wape watoto picha ambazo zinawakilisha imani katika Yesu Kristo, toba, ubatizo na uthibitisho (ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 1, 111, 103, na 105). Soma au kariri na watoto makala ya nne ya imani na uwaombe wainue picha zao wakati kanuni au ibada hiyo inapotajwa. Wasaidie watoto waelewe jinsi kila kanuni na ibada hizi zinavyotusaidia tuwe zaidi kama Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.

  • Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto waelewe kwamba imani, toba, ubatizo na uthibitisho si matukio ya mara moja bali huathiri ukuaji wetu wa kiroho katika maisha yetu yote? Kwa mfano, unaweza kuwaonesha picha ya mbegu na mti mkubwa (au chora vitu hivi ubaoni). Wasaidie wafikirie mambo yanayosaidia mbegu ikue na kuwa mti mkubwa, kama vile maji, udongo na mwanga wa jua. Wasaidie waone kwamba haya ni kama mambo tunayofanya ili kusonga karibu na Mungu katika maisha yetu yote—kujenga imani yetu katika Yesu Kristo, kutubu kila siku, kuishi maagano yetu ya ubatizo na kumsikiliza Roho Mtakatifu.

  • Shiriki pamoja na watoto hadithi kuhusu fataki kutoka kwenye ujumbe wa Mzee Dale G. Renlund “Je, Kutubu Kunanisaidia Vipi Nihisi Furaha?Rafiki, Des. 2017, 12–13 au Liahona, Des. 2017, 70–71; ona pia video “Repentance: A Joyful Choice” [Maktaba ya Injili]).

    Katika sehemu mbalimbali wakati wa hadithi, waalike watoto wafikirie jinsi ambavyo Mzee Renlund yawezekana alihisi. Kwa nini tunahisi furaha tunapotubu? Shiriki pamoja na watoto furaha na upendo ambao umeuhisi wakati ulipomwomba Baba wa Mbinguni akusamehe.

Ubatizo

Yesu Kristo alinionesha mfano wakati alipobatizwa.

Japokuwa Yesu hakuwa na dhambi, alibatizwa ili aoneshe mfano kamili wa utiifu kwa Baba wa Mbinguni (ona 2Nefi 31:6–10).

Ili kujifunza mengi zaidi kuhusu ubatizo, ona Mafundisho na Maagano 20:37; Mada za Injili, “Ubatizo,” Maktaba ya Injili.

Shughuli Yamkini

  • Onesha picha ya ubatizo wa Mwokozi na ubatizo wa mtu mwingine (au ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 35 na huenda na. 103 au na 104). Waombe watoto washiriki utofauti na mfanano uliopo kati ya picha hizo mbili. Someni pamoja Mathayo 3:13–17 au “Sura ya 10: Yesu Anabatizwa” katika Hadithi za Agano Jipya, 26–29, au angalieni video inayohusiana kwenye Maktaba ya Injili.

    Waruhusu watoto wataje mambo katika picha ambayo yametajwa katika usomaji au video. Waambie watoto kuhusu upendo wako kwa Mwokozi na nia yako ya kumfuata Yeye.

  • Sikilizeni au imbeni wimbo kuhusu ubatizo, kama vile “When Jesus Christ Was Baptized” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto,102). Tunajifunza nini kuhusu ubatizo kutoka kwenye wimbo huu? Soma 2 Nefi 31:9–10, na waalike watoto wasikilize ni kwa nini Yesu Kristo alibatizwa. Waalike wachore picha zao wenyewe wakiwa kwenye siku yao ya ubatizo.

Ninaweza kuchagua kufanya agano na Mungu na kubatizwa.

Kujitayarisha kwa ajili ya ubatizo kunamaanisha mengi zaidi ya kujitayarisha tu kwa ajili ya tukio fulani. Inamaanisha kujitayarisha kufanya agano na kisha kulishika agano hilo kwa maisha yote. Tafakari jinsi unavyoweza kuwasaidia watoto waelewe agano watakalofanya na Baba wa Mbinguni pale watakapobatizwa, ambalo linajumuisha ahadi Anazotoa kwao na ahadi wanazotoa Kwake.

Shughuli Yamkini

  • Eleza kwamba agano ni ahadi kati ya mtu na Baba wa Mbinguni. Tunapojitahidi kutimiza ahadi zetu kwa Mungu, Mungu anaahidi kutubariki. Andika ubaoni Ahadi Zangu kwa Mungu na Ahadi za Mungu Kwangu. Someni pamoja Mosia 18:10, 13 na Mafundisho na Maagano 20:37, na wasaidie watoto watengeneze orodha ya ahadi wanazoziona chini ya vichwa vya habari vinavyofaa (ona pia Dallin H. Oaks, “Maagano Yako ya Ubatizo,” Rafiki, Feb. 2021, 2–3). Shiriki jinsi ambavyo Baba wa Mbinguni amekubariki wakati unapojitahidi kushika agano lako la ubatizo.

  • Waoneshe watoto picha za vitu ambavyo Yesu Kristo alivifanya akiwa duniani (kwa baadhi ya mifano, ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 33–49). Waombe watoto wazungumze kuhusu Yesu anafanya nini katika kila picha. Soma Mosia 18:8–10, 13, na waalike watoto wasikilize mambo ambayo wanaahidi kufanya wakati wanapobatizwa (ona pia “Agano la Ubatizo,” Rafiki, Feb. 2019, 7; Liahona, Feb. 2019, F3). Ahadi hizi zitashawishi vipi matendo yetu ya kila siku? Waalike watoto wachore picha yao wenyewe wakimsaidia mtu fulani kama vile ambavyo Yesu angefanya. Au unaweza kuwatengenezea watoto beji ndogo ya kuvaa yenye jina la Mwokozi.

    Picha
    mvulana akibatizwa

    Wakati tunapobatizwa, tunaweka ahadi na Mungu na Yeye anaweka ahadi na sisi.

Uthibitsho

Wakati ninapothibitishwa ninakuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho huleta baraka nyingi, ikiwa ni pamoja na fursa kwa watoto kuwa washiriki hai katika kazi ya Mungu.

Ili kujifunza zaidi kuhusu uthibitisho na kipawa cha Roho Mtakatifu, ona Gary E. Stevenson, “Ni Kwa Jinsi Gani Roho Mtakatifu Anakusaidia?,” Liahona, Mei 2017, 117–20; Mada za Injili, “Roho Mtakatifu,” Maktaba ya Injili.

Shughuli Yamkini

  • Alika mtu ambaye alibatizwa na kuthibitishwa hivi karibuni aje darasani na kushiriki jinsi kuthibitishwa kulivyokuwa. Inamaanisha nini kwa mtu huyu kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho? Wasaidie watoto wafikirie njia wanazoweza kutunza agano lao la ubatizo kama waumini wa Kanisa (kama vile kuwatumikia wengine, kuwaalika wengine wajifunze zaidi kuhusu Yesu, kutoa sala katika mikutano na kadhalika). Shiriki jinsi ambavyo kufanya mambo haya kumekusaidia uhisi furaha ya kuwa muumini wa Kanisa la Kristo.

  • Onesha picha ya watu katika Maji ya Mormoni (ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 76), na waombe watoto waeleze kile wanachokiona kwenye picha. Simulia hadithi ya Alma na watu wake wakiwa wanabatizwa huko (ona Mosia 18:1–17; “Mlango wa 15: Alma Anafundisha na Kubatiza,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 43–44, au video inayohusiana kwenye Maktaba ya Injili).

    Rejea Mosia 18:8–9 na waalike watoto wafanye vitendo ili kuwasaidia wakumbuke mambo ambayo watu walikuwa radhi kufanya kama waumini wa Kanisa la Kristo. Shiriki uzoefu wako wakati uliposhuhudia waumini wa Kanisa wakihudumu kwa njia sawa na hizi.

Ninapothibitishwa, ninapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

Wakati tunapobatizwa na kuthibitishwa, Baba wa Mbinguni anaahidi kwamba “daima Roho Wake apate kuwa pamoja [nasi[” (Mafundisho na Maagano 20:77). Zawadi hii nzuri kutoka kwa Mungu inaitwa kipawa cha Roho Mtakatifu.

Shughuli Yamkini

  • Soma Mafundisho na Maagano 33:15, na waombe watoto wasikilize zawadi maalum ambayo Baba wa Mbinguni anatupatia wakati tunapobatizwa na kuthibitishwa. Ili kuwasaidia wajifunze zaidi kuhusu jinsi kipawa cha Roho Mtakatifu kitakavyowasaidia, rejeleeni pamoja Yohana 14:26; Wagalatia 5:22–23; 2 Nefi 32:5; 3 Nefi 27:20. Unaweza pia kurejelea makala isemayo “Roho Mtakatifu Ni …” (Rafiki, Juni 2019, 24–25; Liahona, Juni 2019, F12–F13).

  • Kabla ya darasa, waombe wazazi wa mtoto mmoja au zaidi washiriki jinsi walivyobarikiwa kwa sababu wana kipawa cha Roho Mtakatifu. Je, ni kwa jinsi gani Yeye aliwasaidia? Je, ni kwa jinsi gani wanaisikia sauti Yake?

  • Imbeni pamoja wimbo kuhusu Roho Mtakatifu, kama vile “Holy Ghost” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 105). Wasaidie watoto waelewe kile wimbo huu unachotufundisha kuhusu jinsi Roho Mtakatifu anavyotusaidia.

Roho Mtakatifu anaweza kuzungumza nami kwa njia nyingi.

Watoto ambao wanaweza kutambua sauti ya Roho watatayarishwa kupokea ufunuo binafsi ili uwaongoze katika maisha yao yote. Wafundishe kwamba kuna njia nyingi ambazo Roho Mtakatifu anaweza kuzungumza nasi.

Shughuli Yamkini

  • Wasaidie watoto wafikirie njia tofauti tofauti ambazo tunaweza kuzungumza na rafiki anayeishi mbali, kama vile kuandika barua, kutuma barua pepe au kuzungumza kwenye simu. Wafundishe kwamba Baba wa Mbinguni anaweza kuzungumza nasi kupitia Roho Mtakatifu. Tumia ujumbe wa Rais Dallin H. Oaks “Je, ni kwa Jinsi Gani Baba wa Mbinguni Huzungumza Nasi?” kuwasaidia watoto waelewe njia tofauti ambazo Roho Mtakatifu anaweza kuzungumza kwenye akili na mioyo yetu (Rafiki, Machi 2020, 2–3; Liahona, Machi 2020, F2–F3).

  • Shiriki uzoefu wakati ambapo Roho Mtakatifu aliwasiliana nawe, ama kupitia mawazo akilini mwako au kupitia hisia moyoni mwako (ona Mafundisho na Maagano 6:22–23; 8:2–3; ona pia Henry B. Eyring, “Fungua Moyo Wako kwa Roho Mtakatifu,” Rafiki, Agosti 2019, 2–3; Liahona, Agosti 2019, F2–F3). Shuhudia kwamba Roho Mtakatifu anaweza kuwasaidia kwa njia sawa na hizo.

  • Wasaidie watoto wafikirie nyakati ambazo wanaweza kuwa wamemhisi Roho—kwa mfano, wakati wakiimba wimbo kuhusu Mwokozi au walipokuwa wakiwatendea wengine kwa ukarimu. Wasaidie watambue hisia za kiroho ambazo Roho Mtakatifu huleta. Unadhani kwa nini Roho Mtakatifu hutupatia hisia hizo? Wasaidie watoto wafikirie juu ya mambo ambayo tunahitajika tuyafanye ili tumsikie Roho Mtakatifu akizungumza nasi. Zungumza kuhusu kile unachofanya ili kumsikia Roho vizuri zaidi.

Sakramenti

Ninapopokea sakramenti, ninakumbuka dhabihu ya Mwokozi na kufanya upya maagano yangu.

Mwokozi alitupatia sakramenti ili atusaidie tukumbuke dhabihu Yake kwa ajili yetu na tufanye upya maagano yetu. Kwa sababu ya ibada hii ya kila wiki, tunaweza kuendelea kufurahia baraka za ubatizo wetu katika maisha yetu yote.

Ili kujifunza zaidi, ona Mathayo 26:26–30; 3 Nefi 18:1–12; Mafundisho na Maagano 20:77, 79.

Shughuli Yamkini

  • Waalike watoto wapake rangi “Yesu Alitambulisha Sakramenti kwa Wanefi” katika Kitabu cha Kupaka Rangi cha Hadithi za Maandiko: Kitabu cha Mormoni (2019), 26. Waombe waoneshe kile watu wanachofikiria kwenye picha. Wasomee watoto sehemu za 3 Nefi 18:1–12 au “Mlango wa 45: Yesu Kristo Anafundisha kuhusu Sakramenti na Sala,” Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 126–27, au angalia video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org. Je, tunaweza kufanya nini ili tumkumbuke Yesu wakati wa sakramenti?

  • Waombe watoto wakuambie baadhi ya mambo ambayo wanapaswa kukumbuka kufanya kila wakati, kama vile kufunga kamba za viatu vyao au kunawa mikono yao kabla ya kula. Kwa nini ni muhimu kukumbuka mambo haya? Soma Moroni 4:3 kwa watoto na waalike wasikilize kile tunachoahidi kukumbuka daima wakati tunapopokea sakramenti. Kwa nini ni muhimu kumkumbuka Yesu Kristo? Wasaidie watoto waelewe jinsi gani mkate na maji ya sakramenti hutusaidia tukumbuke kile ambacho Yesu amefanya kwa ajili yetu (ona Moroni 4:3; 5:2).

  • Andika ubaoni “Mimi ninaahidi …” Soma sala ya sakramenti kwa watoto (ona Mafundisho na Maagano 20:77, 79). Wakati wanaposikia ahadi tunayoitoa kwa Mungu, pumzika kidogo na uwasaidie wakamilishe sentensi ubaoni kwa ahadi waliyoisikia. Wasaidie waelewe kwamba tunapopokea sakramenti, tunafanya ahadi zile zile tulizozifanya wakati wa ubatizo.

  • Inamaanisha nini kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo? Ili kuwasaidia watoto wajibu swali hili, shiriki mfano wa kitu ambacho juu yake tunaweka majina yetu. Kwa nini tunaweka majina yetu juu ya vitu hivi? Kwa nini Yesu Kristo angetaka kuweka jina lake juu yetu? Fikiria kushiriki maelezo haya kutoka kwa Rais Russell M. Nelson: “Kujichukulia jina la Mwokozi juu yetu kunajumuisha kutangaza na kushuhudia kwa wengine—kupitia matendo na maneno yetu—kwamba Yesu ndiye Kristo” (“Jina Sahihi la Kanisa,” Liahona, Nov. 2018, 88).

Uwezo, Mamlaka na Funguo za Ukuhani

Mungu huwabariki watoto Wake kupitia nguvu za ukuhani.

Watoto wote wa Mungu—wanawake kwa wanaume, vijana kwa wazee—wanapokea nguvu za Mungu pale wanaposhika maagano ambayo wamefanya Naye. Tunafanya maagano haya wakati tunapopokea ibada za ukuhani kama vile ubatizo (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho., 3.5, Maktaba ya Injili). Ili kujifunza zaidi, ona Russell M. Nelson, “Hazina za Kiroho,” Liahona, Nov. 2019, 76–79; “Kanuni za Ukuhani,” sura ya 3 kwenye Kitabu cha Maelezo ya Jumla.

Shughuli Yamkini

  • Wasaidie watoto watambue baraka wanazopokea kwa sababu ya ukuhani. Ili kuwapa baadhi ya mawazo, unaweza kuwaonesha video “Baraka za Ukuhani” (Maktaba ya Injili).

  • Fikiria kuorodhesha baraka hizi ubaoni. Kwa nini baraka hizi ni muhimu kwetu? Shuhudia kwamba baraka hizi huja kwetu kwa sababu ya Yesu Kristo na nguvu Yake ya ukuhani.

  • Andika vichwa vya habari vifuatavyo ubaoni: Uwezo wa Mungu na Uwezo na Mamlaka ya Mungu aliyopewa mwanadamu duniani. Waombe watoto waweke picha chini ya kichwa cha habari cha kwanza zinazotusaidia tuelewe jinsi ambavyo Mungu ametumia uwezo Wake kutubariki, kama vile kwa kuumba ulimwengu, kutulinda na kutuongoza, kutuonesha kwamba anatupenda na anatujua na anasikia na kujibu maombi yetu (ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 3, 68, 90111). Waombe waweke picha chini ya kichwa cha habari cha pili zinazotusaidia tuelewe jinsi wanaume wanaostahili duniani wanavyotumia uwezo na mamlaka ya Mungu kutubariki, kama vile kwa kubariki wagonjwa, kubatiza, kuthibitisha, kuhudumia sakramenti na kuunganisha familia (ona Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 46, 104, 105, 107120). Shiriki kwa nini una shukrani kwa ajili ya ukuhani na baraka zitokanazo na ukuhani.

  • Mojawapo ya njia kuu tunazopokea baraka za nguvu za Mungu katika maisha yetu ni kupitia ibada za ukuhani (ona Mafundisho na Maagano 84:20). Ili kuwasaidia watoto wajifunze ukweli huu, unaweza kuorodhesha maandiko yafuatayo ubaoni: 3 Nefi 11:21–26, 33 (ubatizo); Moroni 2 (uthibitisho); Moroni 4–5 (sakramenti). Watoto wanaweza kila mmoja kuchagua mojawapo ya vifungu hivi na wabainishe ibada inayoelezwa. Waalike watoto washiriki jinsi ambavyo wao binafsi wamebarikiwa kwa kupokea ibada za ukuhani.

  • Wasaidie watoto waelewe kwamba watapokea nguvu kutoka kwa Mungu pale wanapobatizwa na kushika maagano yao ya ubatizo. Waulize watoto jinsi nguvu hii inavyoweza kuwasaidia.

Kazi ya Mungu inaelekezwa kwa funguo za ukuhani na kutimizwa kwa mamlaka ya ukuhani.

Waumini wanaume wa Kanisa wanaostahili wanaweza kutawazwa kwenye ofisi katika ukuhani. Kwa kuongezea, wakati wowote mtu anapoitwa kwa ajili ya wito au kupewa kazi ya kusaidia katika kazi ya Mungu, mtu yule anaweza kutumia mamlaka ya ukuhani yahusianayo na kazi hiyo. Matumizi ya mamlaka yote ya ukuhani ndani ya Kanisa yanaelekezwa na watu wanaoshikilia funguo za ukuhani, kama vile rais wa kigingi, askofu na marais wa akidi. Funguo za ukuhani ni mamlaka ya kuelekeza matumizi ya ukuhani katika kufanya kazi ya Bwana.

Shughuli Yamkini

  • Soma pamoja na watoto Marko 3:14–15, na waoneshe picha ya tukio lililoelezwa hapo (kama vile Kitabu cha Sanaa za Injili, na. 38). Waulize watoto kama wamewahi kuona mtu akitawazwa kwenye ofisi ya ukuhani au kutengwa kwa ajili ya wito (au waambie kuhusu uzoefu ambao umekuwa nao). Je, ni kwa jinsi gani hii inafanana na kile ambacho Mwokozi alikifanya kwa Mitume Wake? Wasaidie watoto waorodheshe ubaoni ofisi za ukuhani au miito ambayo inaweza kutolewa kwa waumini wa Kanisa, kama vile mwalimu au kiongozi katika kikundi. Pembeni ya kila ofisi au wito, unaweza kuandika kile ambacho mtu aliye na ofisi au wito huo ana mamlaka ya kukifanya. Waambie watoto jinsi gani kutengwa na mtu chini ya maelekezo ya funguo za ukuhani kumekusaidia katika kuhudumu.

  • Waalike watoto wafikirie juu ya kitu fulani kinachohitaji funguo, kama vile gari au mlango. Nini kitatokea ikiwa huna ufunguo? Someni pamoja Mafundisho na Maagano 65:2, na ushiriki ushuhuda wako kuhusu umuhimu wa kuwa na funguo za ukuhani duniani. Mnaweza pia kutazama video “Where Are the Keys?” (Maktaba ya Injili) na mtafute kile Mzee Stevenson anachofundisha kuhusu funguo za ukuhani.

  • Muombe mtu katika kata ambaye ana funguo aje darasani na kushiriki na watoto maana ya kushikilia funguo za ukuhani. Mwalike aeleze majukumu yake. Je, anaongoza sehemu gani ya kazi ya Bwana? Ni kwa jinsi gani Mwokozi anamsaidia?

Hekalu na Mpango wa Furaha

Hekalu ni nyumba ya Bwana.

Mahekalu ni sehemu ya mpango wa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya watoto Wake. Katika mahekalu, tunafanya Naye maagano matakatifu, tunapokea baraka ya nguvu ya ukuhani, tunapokea ufunuo, tunafanya ibada kwa niaba ya mababu zetu waliofariki na kuunganishwa na familia zetu kwa milele yote. Haya yote yanawezekana kwa sababu ya Yesu Kristo na dhabihu Yake ya upatanisho.

Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto unaowafundisha watambue utakatifu wa nyumba ya Bwana na wajitayarishe kustahili kushiriki katika ibada za hekaluni? Fikiria kurejelea nyenzo hizi: Mafundisho na Maagano 97:15–17; Russell M. Nelson, “Maneno ya Kutamatisha,” Liahona, Nov. 2019, 120–22; “Kwa nini Watakatifu wa Siku za Mwisho Wanajenga Mahekalu,” temples.ChurchofJesusChrist.org.

Picha
vijana nje ya hekalu

Mahekalu ni sehemu ya mpango wa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya watoto Wake.

Shughuli Yamkini

  • Onesha picha moja au zaidi za mahekalu. Waulize watoto ni kipi kinayafanya mahekalu yawe sehemu maalumu. Onesha kwamba kwenye kila hekalu kuna maandishi haya: “Utakatifu kwa Bwana: Nyumba ya Bwana.” Waulize watoto kile wanachofikiria “Utakatifu kwa Bwana” inaweza kumaanisha. Kwa nini hekalu linaitwa nyumba ya Bwana? Je, hii inatufundisha nini kuhusu hekalu? Ikiwa yeyote kati ya watoto amewahi kwenda hekaluni, wanaweza pia kushiriki jinsi walivyohisi walipokuwa huko. Ikiwa umewahi kwenda hekaluni, shiriki jinsi ambavyo umehisi uwepo wa Bwana ukiwa huko na zungumza kuhusu kwa nini hekalu ni mahali patakatifu kwako.

  • Someni pamoja Mafundisho na Maagano 97:15–17. Waombe watoto watafute kile ambacho Bwana anatarajia kutoka kwa wale wanaoingia katika nyumba Yake takatifu. Kwa nini tunahitaji kuwa wenye kustahili ili kuingia kwenye nyumba Yake? Kama sehemu ya mazungumzo haya, zungumza na watoto kuhusu kibali cha hekaluni, ikijumuisha jinsi ya kukipata. Unaweza kumwalika mshiriki wa uaskofu ashiriki nao jinsi mahojiano ya kibali cha hekaluni yalivyo na maswali ambayo yanaulizwa.

Ndani ya Hekalu tunafanya maagano na Mungu.

Rais Russell M. Nelson alifundisha, “Yesu Kristo anatualika tufuate njia ya agano ili turejee nyumbani kwa Wazazi wetu wa Mbinguni ili tuwe na wale tunaowapenda” (“Njoo Unifuate,” Liahona, Mei 2019, 91). Wasaidie watoto waelewe kwamba njia ya agano inajumuisha ubatizo, uthibitisho na endaumenti ya hekaluni na kuunganishwa.

Shughuli Yamkini

  • Waombe watoto wakusaidie kupitia upya agano tunalofanya na Mungu wakati tunapobatizwa na ambalo tunalifanya upya pale tunapopokea sakramenti (ona Mosia 18:10; Mafundisho na Maagano 20:77, 79). Onesha picha ya hekalu na ueleze kwamba Baba wa Mbinguni ana baraka zaidi ambazo Yeye anataka kutupatia ndani ya hekalu.

  • Chora lango linaloongoza kwenye njia. Waulize watoto kwa nini wanadhani inasaidia kuwa na njia ya kutembea. Someni pamoja 2 Nefi 31:17–20, ambapo Nefi analinganisha agano la ubatizo na lango na anatualika tuendelee kwenye njia baada ya ubatizo. Kuna maagano mengi zaidi ya kufanya baada ya ubatizo, ikijumuisha maagano yanayofanywa hekaluni. Eleza kwamba Rais Nelson ameiita njia hii “njia ya agano.”

Hekaluni tunaweza kubatizwa na kuthibitishwa kwa niaba ya mababu waliofariki.

Injili ya Yesu Kristo hufanya iwezekane kwa watoto wote wa Mungu kurudi kuishi Naye, hata kama watakufa bila kuijua injili. Ndani ya hekalu, tunaweza kubatizwa na kuthibitishwa kuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo kwa niaba yao.

Shughuli Yamkini

  • Zungumza kuhusu wakati ambapo mtu alikufanyia jambo ambalo hukuweza kujifanyia mwenyewe. Waalike watoto washiriki uzoefu kama huo. Eleza kwamba tunapoenda hekaluni, tunaweza kupokea ibada takatifu kama vile ubatizo kwa niaba ya wengine ambao wamefariki. Je, ni kwa jinsi gani tunakuwa kama Yesu pale tunapofanya kazi kwa niaba ya wafu? Yesu amefanya nini kwa ajili yetu ambacho hatungeweza kujifanyia wenyewe?

  • Mwalike kijana mmoja au zaidi ambao wamebatizwa kwa niaba ya mababu zao ili washiriki uzoefu wao. Waulize ilikuwaje walipokuwa hekaluni. Wahimize washiriki jinsi walivyohisi kufanya kazi hii kwa niaba ya mababu zao.

  • Chora mti kwenye ubao, ikiwa ni pamoja na mizizi na matawi. Waombe watoto wafikirie jinsi ambavyo familia ni kama mti. Andika kwenye mizizi Mababu, andika kwenye matawi Vizazi, na andika kwenye shina la mti Wewe. Someni pamoja sentensi hii kutoka Mafundisho na Maagano 128:18: “Kwani sisi pasipo wao [mababu zetu] hatuwezi kukamilika; wala wao pasipo sisi hawawezi kukamilika.” Uliza maswali kama yafuatayo: “Kwa nini tunawahitaji mababu zetu? Kwa nini vizazi vyetu wanatuhitaji sisi? Ni kwa jinsi gani wazazi wetu, bibi na babu na mababu wengine wametusaidia?” Waalike watoto watafute sehemu iliyosalia ya Mafundisho na Maagano 128:18 kwa ajili ya kirai kinachoeleza jinsi tunavyoweza kuwasaidia mababu zetu.

  • Fikiria kufanya kazi na wazazi wa kila mtoto kutafuta jina la babu ili mtoto alipeleke hekaluni (ona FamilySearch.org).

Chapisha