Hadithi za Maandiko
Sura ya 10: Yesu Anabatizwa


Sura ya 10

Yesu Anabatizwa

Yohana Mbatizaji akiwa jangwani

Yohana aliishi jangwani kwa miaka mingi. Alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa nywele za ngamia, na alikula asali na nzige. Watu walikuja kutoka mijini kumsikia akifundisha. Alijulikana kama Yohana Mbatizaji.

Yohana Mbatizaji akiwafundisha watu

Yohana Mbatizaji aliwafundisha watu kuhusu Yesu Kristo. Aliwaambia watubu dhambi zao na wabatizwe. Yohana aliwabatiza wale waliotubu dhambi zao.

Yohana Mbatizaji akiwafundisha watu

Watu walimuuliza Yohana Mbatizaji jinsi ya kuishi maisha bora. Aliwaambia washiriki na masikini, waseme ukweli, na wawe wenye haki kwa wengine. Alisema kwamba Yesu Kristo angekuja karibuni. Yesu angewapa kipawa cha Roho Mtakatifu.

Yohana Mbatizaji akizungumza na Yesu

Siku moja wakati Yohana Mbatizaji alikuwa akibatiza watu katika Mto Yordani, Yesu Kristo alimjia. Alimwomba Yohana ambatize. Yohana alijua kwamba Yesu daima alitii amri za Mungu na hakuhitaji kutubu. Yohana alifikiria kwamba Yesu hakuhitaji kubatizwa.

Yohana Mbatizaji akimbatiza Yesu

Lakini Mungu alikuwa ameamrisha kila mtu abatizwe, hivyo Yesu alimwambia Yohana ambatize. Yesu aliweka mfano kwetu kwa kutii amri ya Mungu ya kubatizwa.

Njiwa akiruka juu ya Yohana Mbatizaji na Yesu

Yesu alipotoka majini, Roho Mtakatifu alimjia. Mungu alizungumza kutoka mbinguni, akisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye.” Yohana Mbatizaji pia alishuhudia kwamba Yesu alikuwa Mwana wa Mungu.

Mathayo 3:16–17; Yohana 1:33–36; Yesu Kristo, 150