Sura ya 59 Sauli Anajifunza kuhusu Yesu Sauli alikuwa amewaona watu wakimwua Stefano. Siku moja Sauli alikuwa akitembea kuelekea mji wa Dameski na marafiki kadhaa. Alikuwa akitaka kuwaweka baadhi ya wanafunzi wa Kristo gerezani. Matendo ya Mitume 7:58; 9:1–2 Ghafla mwangaza mkali uliong’aa kutoka mbinguni ulimzingira. Alianguka chini. Kisha Sauli alisikia sauti ya Yesu ikimuuliza ni kwa nini alikuwa akijaribu kuwadhuru Watakatifu. Sauli aliogopa. Alimuuliza Yesu kile alichopaswa kufanya. Mwokozi alisema Sauli alipaswa kwenda Dameski. Huko Sauli angeambiwa kile alichohitajika kufanya. Matendo ya Mitume 9:3–6 Sauli alifungua macho yake, lakini hakuweza kuona. Alikuwa kipofu. Rafiki zake walimpeleka Dameski. Matendo ya Mitume 9:8–9 Mwanafunzi wa Yesu Kristo aliyeitwa Anania aliishi Dameski. Katika ono, Yesu alimwambia Anania aende kwa Sauli. Matendo ya Mitume 9:10–11 Anania alikuwa na ukuhani. Aliweka mikono yake juu ya kichwa cha Sauli na kumbariki kwamba macho ya Sauli yangepata kuona. Baada ya kuponywa, Sauli alibatizwa na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Matendo ya Mitume 9:17–18 Sauli alibadilisha jina lake kuwa Paulo. Aliitwa kuwa Mtume. Alikuwa mmisionari wa Kanisa. Aliandika barua nyingi. Alikwenda kwenye nchi nyingi na alifundisha injili. Matendo ya Mitume 26:16–23; Warumi 1:1