Sura ya 53 Yesu Anasulubiwa Askari wakimchapa Yesu kwa mijeledi. Walimvika joho la rangi ya zambarau. Walitengeneza taji ya miiba na wakamvika Yesu kichwani. Walimcheka na kumtemea mate. Walimwita “Mfalme wa Wayahudi.” Marko 15:15–20 Watu wengi waliwafuata askari walipokuwa wakimpeleka Yesu kwenye mlima karibu na Yerusalemu. Walimfanya abebe msalaba Wake mwenyewe. Walipiga misumari mikono na miguu Yake kwenye msalaba na kuuinua juu. Pia waliwasulubisha watu wengine wawili, ambao walikuwa wezi. Luka 23:27, 33; Yohana 19:17–18 Yesu alisali. Alimsihi Baba wa Mbinguni awasamehe askari waliomsulubisha. Hawakujua kwamba alikuwa ni Mwokozi. Luka 23:34 Mariamu, mama yake Yesu, alikuwa amesimama kando ya msalaba. Mtume Yohana alikuwa pale pia. Yesu alimwambia Yohana amtunze mama Yake. Yohana alimchukua mama yake Yesu nyumbani kwake. Yohana 19:25–27 Giza lilifunika nchi. Mwokozi aliteseka msalabani kwa masaa mengi. Hatimaye Roho Yake iliuacha mwili Wake, na akafa. Mathayo 27:45, 50 Alipokufa, tetemeko la ardhi lilivunja mawe makubwa vipande vipande. Pazia katika hekalu, iliyoitwa shela, ilipasuka vipande viwili. Askari wa Kirumi waliogopa. Mathayo 27:51, 54 Mmoja wa wanafunzi wa Yesu aliutoa mwili wa Mwokozi msalabani. Aliufunika kwa kitambaa na kuuweka kaburini, mahali ambapo watu huzikwa. Jiwe kubwa lilivingirishwa mbele ya kaburi. Mathayo 27:57–60