Sura ya 35 Msamaria Mwema Yesu alisimulia hadithi nyingi, au mafumbo, ili kuwasaidia watu kujifunza ukweli. Siku moja kiongozi wa Wayahudi alimuuliza Yesu afanye nini ili apate uzima wa milele. Mwokozi alimuuliza maandiko yalisema nini. Kiongozi alisema kwamba mtu anapaswa ampende Mungu na pia ampende jirani yake. Yesu alisema kwamba alikuwa sahihi. Kisha kiongozi aliuliza, “Na jirani yangu ni nani?” Luka 10:25–29 Yesu alijibu kwa kumwambia mtu yule hadithi. Siku moja mtu Myahudi alikuwa akitembea barabarani kwenda mji wa Yeriko. Wezi walimpora na kumpiga. Walimuacha mtu yule barabarani, akiwa karibu ya kufa. Luka 10:30 Punde kuhani Myahudi alikuja na kumwona mtu yule. Kuhani alipita upande mwingine wa barabara. Hakumsaidia mtu yule. Luka 10:31 Mtu mwingine Myahudi aliyekuwa akifanya kazi hekaluni alipitia. Alimuona mtu aliyekuwa amejeruhiwa. Lakini yeye vilevile hakumsaidia mtu yule na akapita upande mwingine wa barabara. Luka 10:32 Kisha Msamaria alikuja. Wayahudi na Wasamaria hawakuwa marafiki. Lakini Msamaria alipomuona mtu yule, alihisi huzuni kwa ajili yake. Alihudumia majeraha ya mtu yule na kumvisha nguo. Luka 10:33–34; Yohana 4:9; Kamusi ya Biblia, “Wasamaria,” 768 Msamaria alimpeleka mtu yule kwenye nyumba ya wageni na kumhudumia hadi siku iliyofuata. Msamaria alipohitaji kuondoka, alimpa pesa mwenye nyumba ya wageni na kumwambia amhudumie mtu yule. Luka 10:34–35 Baada ya Yesu kueleza hadithi hii, alimuuliza kiongozi Myahudi nani kati ya watu hao watatu alikuwa jirani kwa mtu yule aliyekuwa amejeruhiwa. Luka 10:36 Kiongozi alisema kwamba Msamaria ndiye aliyekuwa jirani kwa sababu alikuwa amemsaidia mtu yule. Yesu alimwambia kiongozi Myahudi awe kama Msamaria. Luka 10:37