2010–2019
Maneno ya Kutamatisha
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


2:3

Maneno ya Kutamatisha

Ustahiki binafsi unahitaji uongofu wa jumla wa akili na moyo kuwa zaidi kama Bwana.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, tunapofikia tamati ya mkutano huu wa kihistoria, tunamshukuru Bwana kwa kuvuvia jumbe na muziki ambao umetuinua. Kwa kweli tumefurahia sherehe ya kiroho.

Tunajua injili ya urejesho ya Yesu Kristo italeta tumaini na shangwe kwa watu watakaosikia na kufuata mafundisho Yake. Tunajua pia kwamba kila nyumba inaweza kuwa kimbilio la kweli la imani, ambapo amani, upendo, na Roho wa Bwana vinaweza kukaa.

Ndiyo, taji la kito ya Urejesho ni hekalu takatifu. Ibada zake na maagano matakatifu ni ya msingi kwenye kuwaandaa watu walio tayari kumkaribisha Mwokozi kwenye Ujio Wake wa Pili. Kwa sasa tuna mahekalu 166 yaliyowekwa wakfu, na mengi yanakuja.

Maonesho ya ufunguzi yatafanywa kabla ya uwekaji wakfu wa kila hekalu jipya na lililorekebishwa. Marafiki wengi wasio wa imani yetu watashiriki katika utalii wa mahekalu hayo na watajifunza jambo kuhusu baraka za hekalu. Na baadhi ya wageni hao watashawishika kutaka kujua zaidi. Baadhi watauliza kwa dhati jinsi ambavyo wangeweza kustahili kwa ajili ya baraka za hekalu.

Kama waumini wa Kanisa, tutahitaji kuwa tumejiandaa ili kujibu maswali yao. Tunaweza kuelezea kwamba baraka za hekalu zinapatikana kwa yeyote na kwa watu wote ambao watajiandaa. Lakini kabla ya kuingia hekalu lililowekwa wakfu, wanahitaji kustahili. Bwana anataka watoto Wake wote kupata baraka za milele zinazopatikana ndani ya hekalu Lake. Yeye ameelekeza kile kila mtu lazima afanye ili kustahili kuingia nyumba Yake takatifu.

Mahala pazuri pa kuanzia fursa kama hiyo ya kufundisha ni kutilia umakini kwenye maneno yaliyochorwa sehemu ya nje ya hekalu: “Utakatifu kwa Bwana: Nyumba ya Bwana.” Ujumbe wa Rais Henry B. Eyring leo na zingine nyingi zimetuvuvia kuwa watakatifu zaidi. Kila hekalu ni mahala patakatifu; kila mwendaji hekaluni anajitahidi kuwa mtakatifu zaidi.

Vigezo vyote vya kuingia hekaluni vinahusiana na utakatifu binafsi. Kutathmini utayari huo, kila mtu anayetaka kufurahia baraka za hekalu atakuwa na mahojiano ya aina mbili: kwanza na askofu, mshauri wa uaskofu, au rais wa tawi; pili na rais wa kigingi au misheni au mmoja wa washauri wake. Katika mahojiano hayo, maswali kadhaa yataulizwa.

Baadhi ya maswali hayo hivi karibuni yamefanyiwa masahihisho kwa ajili ya usahihi. Ningependa kuyarejea kwa ajili yenu sasa:

  1. Je, una imani katika na ushuhuda wa Mungu, Baba wa Milele; Mwanaye, Yesu Kristo; na Roho Mtakatifu?

  2. Je, una ushuhuda wa Upatanisho wa Yesu Kristo na wa jukumu Lake kama Mwokozi na Mkombozi wako?

  3. Je, una ushuhuda wa Urejesho wa injili ya Yesu Kristo?

  4. Je, unamuidhinisha Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kama nabii, mwonaji, na mfunuzi na kama mtu pekee duniani aliyepewa mamlaka ya kutumia funguo zote za ukuhani?

    Je, unawaidhinisha washiriki wa Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili kama manabii, waonaji, na wafunuzi?

    Je, unawaidhinisha Viongozi Wakuu wengine wenye Mamlaka na viongozi wa maeneo husika wa Kanisa?

  5. Bwana amesema kwamba mambo yote lazima “yafanyike katika usafi” mbele Yake (Mafundisho na Maagano 42:41).

    Je, unajitahidi kwa usafi wa maadili katika mawazo na matendo yako?

    Je, unatii sheria ya usafi wa kimwili?

  6. Je, unafuata mafundisho ya Kanisa la Yesu Kristo katika matendo yako ya siri na ya hadharani kwa wana familia yako na wengine?

  7. Je, unaunga mkono au kudhamini mafundisho yoyote, matendo, au injili iliyo kinyume na ile ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa siku za Mwisho?

  8. Je, unajitahidi kuitakasa siku ya Sabato, kote nyumbani na kanisani; kuhudhuria mikutano yako; kujiandaa na kupokea sakramenti kwa kustahili; na kuishi maisha yako sawasawa na sheria na amri za injili?

  9. Je, unajitahidi kuwa mwaminifu katika yote unayofanya?

  10. Je, wewe ni mlipa zaka kamili?

  11. Je, unaelewa na kutii Neno la Hekima?

  12. Je, una wajibu wowote wa kifedha au wajibu mwingine kwa mwenza wa awali au kwa watoto?

    Ikiwa ndiyo, je, unatenda kwa wakati katika kukidhi wajibu huo?

  13. Je, unatunza maagano uliyofanya hekaluni, ikijumuisha kuvaa mavazi ya hekaluni jinsi ilivyoelekezwa katika endaumenti?

  14. Je, kuna dhambi nzito katika maisha yako ambazo zinahitaji kushughulikiwa na mamlaka ya ukuhani kama sehemu ya toba yako?

  15. Je, unajiona mwenye kustahili kuingia nyumba ya Bwana na kushiriki katika ibada za hekaluni?

Kesho, maswali haya yaliyopitiwa upya ya kibali cha hekaluni yatasambazwa kwa viongozi wa Kanisa kote ulimwenguni.

Kwa kuongezea kwenye kujibu maswali hayo kwa uaminifu, inaeleweka kwamba kila mtu mzima aliyekwisha kwenda hekaluni atavaa mavazi matakatifu ya ukuhani ndani ya nguo zao za kawaida. Hii ni ishara ya msimamo wa ndani kwenye kujitahidi kila siku kuwa zaidi kama Bwana. Pia inatukumbusha kubaki waaminifu kila siku kwenye maagano yanayofanywa na kutembea kwenye njia ya agano kila siku katika njia ya juu na takatifu.

Sasa, kwa dakika moja, ningependa kuzungumza na vijana wetu. Tunawahimiza muwe wenye kustahili kwa ajili ya vibali vya hekaluni vyenye ukomo wa matumizi. Utaulizwa maswali yale tu yanayohusika kwako katika maandalizi yako kwa ajili ya ibada za ubatizo na uthibitisho kwa niaba. Tuna shukrani kubwa kwa ustahili wenu na utayari wenu kushiriki katika kazi hiyo takatifu ya hekaluni. Tunawashukuru!

Ustahiki wa mtu binafsi kuingia nyumba ya Bwana unahitaji maandalizi mengi binafsi ya kiroho. Lakini kwa msaada wa Bwana, hakuna kinachoshindikana. Katika baadhi ya hali, ni rahisi kujenga hekalu kuliko ilivyo kuwajenga watu waliojiandaa kwa ajili ya hekalu. Ustahiki binafsi unahitaji uongofu wa jumla wa akili na moyo kuwa zaidi kama Bwana, kuwa raia mwaminifu, kuwa mfano mzuri, na kuwa mtu mtakatifu.

Ninashuhudia kwamba maandalizi kama hayo huleta baraka zisizo na idadi katika maisha haya na baraka zisizoelezeka kwa ajili ya maisha yajayo, ikijumuisha uendelezaji wa umoja wa familia yako milele yote “katika hali ya furaha isiyo na mwisho.”1

Sasa ningependa kugeukia mada nyingine: mipango kwa ajili ya mwaka ujao. Katika majira ya kuchipua ya mwaka 2020, itakuwa miaka 200 tangu Joseph Smith alipopata ono dhahiri ambalo tunalijua kama Ono la Kwanza. Mungu Baba na Mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo, walimtokea Joseph, kijana wa miaka14. Tukio hilo lilianzisha mwanzo wenye nguvu wa Urejesho wa injili ya Yesu Kristo katika utimilifu wake, sawasawa na ilivyotabiriwa katika Biblia Takatifu.2

Kisha ulikuja mwendelezo wa matembezi kutoka kwa wajumbe wa mbinguni, ikijumuisha Moroni, Yohana Mbatizaji, na Mitume wa mwanzo Petro, Yakobo, na Yohana. Wengine walifuata, ikiwa ni pamoja na Musa, Elia, na Eliya. Kila mmoja alileta mamlaka matakatifu ili kubariki watoto wa Mungu duniani kwa mara nyingine.

Kimiujiza, sisi pia tumepokea Kitabu cha Mormoni: Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo, maandiko mwenza ya Biblia Takatifu. Mafunuo yaliyochapishwa kwenye Mafundisho na Maagano na Lulu ya Thamani Kuu pia yamestawisha kwa kiasi kikubwa uelewa wetu wa amri za Mungu na ukweli wa milele.

Funguo na ofisi za ukuhani zimerejeshwa, ikijumuisha ofisi za Mitume, Sabini, patriaki, kuhani mkuu, mzee, askofu, kuhani, mwalimu, na shemasi. Na wanawake wanaompenda Bwana wanatumikia kishujaa katika Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama, Msingi, Wasichana, Shule ya Jumapili, na miito mingine ya Kanisa—vipengele vyote muhimu vya Urejesho wa injili ya Yesu Kristo katika utimilifu wake.

Hivyo, mwaka 2020 utatajwa kama mwaka wa tukio muhimu la miaka mia mbili. Mkutano mkuu Aprili ijayo utakua tofauti na mkutano wowote wa nyuma. Katika miezi sita ijayo, ninatumaini kwamba kila muumini na kila familia itajiandaa kwa mkutano wa kipekee ambao utakumbusha misingi hasa ya injili iliyorejeshwa.

Unaweza kutamani kuanza maandalizi yako kwa kusoma upya maelezo ya Joseph Smith ya Ono la Kwanza kama ilivyoandikwa katika Lulu ya Thamani Kuu. Uelekeo wetu wa kujifunza kwa mwaka ujao katika Njoo, Unifuate ni Kitabu cha Mormoni. Unaweza kutamani kutafakari maswali muhimu kama vile, “Ni kwa jinsi gani maisha yangu yangekuwa tofauti ikiwa ufahamu wangu uliopatikana kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni ungetoweka ghafla?” au “Ni kwa jinsi gani matukio yaliyofuatia Ono la Kwanza yameleta tofauti kwangu na kwa wapendwa wangu?” Pia, pamoja na video za kitabu cha Mormoni sasa zikiwa zinapatikana, unaweza kutamani kuzijumuisha katika kujifunza kwako binafsi na kifamilia.

Chagua maswali yako mwenyewe. Buni mpango wako mwenyewe. Jitose mwenyewe katika nuru tukufu ya Urejesho. Unapofanya hivyo, mkutano mkuu Aprili ijayo hautakuwa tu wa kukumbukwa; utakuwa usiosahaulika.

Sasa katika hitimisho, ninawaachia upendo wangu na baraka yangu kwamba kila mmoja wenu aweze kuwa mwenye furaha zaidi na mtakatifu zaidi kwa kila siku ipitayo. Kwa sasa, tafadhali pata hakikisho kwamba ufunuo unaendelea katika Kanisa na utaendelea chini ya maelekezo ya Bwana mpaka “malengo ya Mungu yatakapotimizwa, na Yehova Mkuu atasema kazi imekamilika.”3

Ninawabariki hivyo, nikithibitisha tena upendo wangu kwenu, kwa ushuhuda wangu kwamba Mungu yu hai! Yesu ndiye Kristo! Hili ni Kanisa Lake na sisi ni watu Wake. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.