2010–2019
Kuzipa Roho Zetu Udhibiti wa Miili Yetu
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


Kuzipa Roho Zetu Udhibiti wa Miili Yetu

Mojawapo ya mambo muhimu tunayoweza kujifunza katika maisha haya ni jinsi ya kutilia mkazo asili yetu ya milele na kudhibiti matamanio yetu maovu.

Wapendwa kaka na dada zangu, wakati mkutano mkuu wa Oktoba ulipokaribia mwaka jana, niliandaa hotuba yangu ya mkutano kuzungumzia maadhimisho ya miaka 100 ya ono la ulimwengu wa roho lililotolewa kwa Rais Joseph F. Smith mnamo Oktoba 3, 1918.

Siku chache baada ya kupeleka hotuba yangu kwa ajili ya tafsiri, mpendwa mwenza wangu wa milele, Barbara, alikamilisha safari yake ya duniani na kwenda katika ulimwengu wa roho.

Wakati siku zilipogeuka kuwa wiki, kisha miezi, na sasa mwaka tangu kifo cha Barbara, ninajikuta nikiyakubali kwa ukamilifu maandiko haya: “Nawe utaishi pamoja katika upendo, kwa kiasi kwamba utalia kwa ajili ya kupoteza wa wale wanaokufa.”1 Mimi na Barbara tulibarikiwa “kuishi pamoja kwa upendo” kwa miaka 67. Lakini nimejifunza katika njia binafsi kile inachomaanisha “kulia kwa ajili ya kupoteza” wale tunaowapenda. Oo, jinsi gani ninavyompenda na kumkumbuka!

Nadhani wengi wetu tunashindwa kuthamini kikamilifu kile wengine wanachokifanya kwetu mpaka wanapokuwa wamekufa. Nilijua Barbara mara zote alikuwa na shughuli nyingi, lakini sikuelewa kikamilifu uhitaji endelevu wa familia, Kanisa, na jamii kwenye muda wake. Kulikuwa na juhudi za kujitolea za kila siku zilizorudiwa mara nyingi kwa miaka mingi ambazo ziliifanya familia yetu kuendelea. Na kupitia yote hayo, kamwe hakuna yoyote katika familia yetu aliyewahi kumsikia akizungumza kwa ukali au kusema neno lisilo la ukarimu.

Wingi wa kumbukumbu umekuja juu yangu mwaka huu uliopita. Nimefikiri kuhusu uchaguzi muhimu wa kimwili alioufanya wa kuwa mama wa watoto saba. Kuwa mama wa nyumbani ilikuwa ni kazi pekee aliyoitaka daima, na alikuwa mbobezi katika kila nyanja.

Mara nyingi nimestaajabu jinsi alivyowafuatilia watoto wetu na mimi. Matayarisho ya mlo pekee yalikuwa kwa kweli kazi kubwa, bila kutaja shughuli kama kufua lundo la nguo familia yetu ilizovaa kila wiki na kutunza viatu na mavazi yenye vipimo sahihi kwa watoto. Sote tulimgeukia kwenye mambo mengine mengi ambayo yalikuwa muhimu kwetu. Na kwa sababu yalikuwa muhimu kwetu, yalikuwa pia muhimu kwake. Alikuwa, katika neno, adhimu—kama mke, kama mama, kama rafiki, kama jirani, na kama binti wa Mungu.

Sasa vile ameondoka, nina furaha kwamba nilichagua kukaa karibu naye wakati niliporudi nyumbani kutoka ofisini kipindi cha miezi ya mwisho ya maisha yake, kuushika mkono wake tulipokuwa tukitazama miisho ya baadhi ya matamasha yake pendwa ya muziki—tena na tena kwa sababu ugonjwa wa usahaulifu usingemruhusu kukumbuka kwamba alikwishayaona mchana uliopita. Kumbukumbu ya nyakati hizo za kushikana mikono sasa ni za thamani sana kwangu.

Akina kaka na akina dada, tafadhali msikose fursa ya kuangalia ndani ya macho ya wanafamilia yako kwa upendo. Watoto na wazazi, fikianeni kila mmoja na onesheni upendo wenu na shukrani. Kama mimi, baadhi yenu mnaweza kuamka siku moja na kugundua kwamba muda kwa ajili ya mawasiliano muhimu kama hayo umekwishapita. Ishini kila siku kwa mioyo iliyojawa na shukrani, kumbukumbu nzuri, huduma, na upendo mwingi.

Katika mwaka huu uliopita, Nimetafakari zaidi kwa kudhamiria kuliko hapo awali kuhusu mpango wa Baba yetu wa Mbinguni. Katika kumfundisha mwanaye Koriantoni, Alma aliuelezea kama “mpango mkuu wa furaha.”2

Neno ambalo linanijia mara kwa mara akilini mwangu sasa wakati ninapotafakari mpango ni “kukutana tena.” Ni mpango, ulioasisiwa na Baba yetu mpendwa wa Mbinguni, ambao katika kiini chake una uwezekano mtukufu wa kukutana kifamilia—wa kukutanika milele kwa waume na wake, wazazi na watoto, vizazi kwa vizazi katika kaya ya Mungu.

Wazo hilo linaniletea faraja na uhakika kwamba nitakuwa na Barbara tena. Ingawa aliteseka kimwili kuelekea mwisho wa maisha yake, roho yake ilikuwa imara, adilifu, na safi. Alikuwa amejiandaa mwenyewe katika vitu vyote ili kwamba siku itakapofika, aweze kusimama mbele ya “kiti cha enzi cha Mungu,”3 akiwa amejaa ujasiri na hakikisho la amani. Lakini nipo hapa, ndani ya siku mbili, nitakuwa na umri wa miaka 91, na bado ninashangaa, “Je, nipo tayari? Je, ninafanya kila kitu ninachohitajika kufanya ili kuweza kuushika mkono wake kwa mara nyingine tena?”

Jambo rahisi mno, uhakika wa msingi wa maisha ni huu: sisi sote tutakufa. Kama tutakufa wazee au vijana, kirahisi au kwa shida, matajiri au masikini, tuliopendwa au wapweke, hakuna anayekwepa kifo.

Miaka michache iliyopita, Rais Gordon B. Hinckley alisema kitu fulani ambacho kina maana ya kipekee kuhusu hili: “Ni uhakika wa kupendeza kiasi gani, ni faraja kiasi gani ambayo huja kutoka katika uelewa kwamba kama tutaoa na kuolewa vyema na kuishi vyema, mahusiano yetu yataendelea, bila kujali kifo na kupita kwa muda.”4

Bila shaka nilioa vyema. Kwa hilo hapawezi kuwa na shaka. Lakini hiyo haitoshi, kulingana na Rais Hinckley. Mimi pia napaswa kuishi vyema.5

Leo, “kuishi vyema” kunaweza kuwa ni dhana kubwa ya kutatiza, hususani kama unatumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii, ambako sauti yoyote inaweza kutangaza ukweli halisi au fikra za uongo kuhusu Mungu na mpango Wake kwa ajili ya watoto Wake. Tushukuru, waumini wa Kanisa wana kanuni za kweli za injili ya milele kujua jinsi ya kuishi ili kwamba tuweze kuwa tumejiandaa vizuri wakati itakapobidi tufe.

Miezi michache tu kabla sijazaliwa, babu yangu Mtume, Mzee Melvin J. Ballard, alitoa hotuba kwamba, kwa baadhi ya watu, walivutiwa na umuhimu wa kile inachomaanisha kwa kuishi vyema. Ikiwa na kichwa cha habari “Mapambano kwa ajili ya Nafsi,” hotuba yake ililenga katika vita endelevu kati ya mwili wa nyama na mifupa na roho zetu za milele.

Alisema, “Mapambano makubwa mno ambayo mwanaume au mwanamke yeyote daima atakuwa nayo … yatakuwa ni mapambamo ambayo ni kati ya yeye mwenyewe,” akielezea kwamba Shetani, “adui wa nafsi zetu,” hutushambulia kupitia “tamaa, uchu, malengo ya mwili.”6 Kwa hivyo mapambano ya msingi ni kati ya utakatifu wetu na asili ya kiroho na tamaa za kimwili za mwanadamu wa tabia ya asili.” Akina kaka na akina dada, kumbukeni, tunaweza kupokea msaada wa kiroho kupitia uzoefu wa Roho Mtakatifu ambaye anaweza “kuwafundisha mambo yote.”7 Msaada unaweza pia kuja kupitia nguvu na baraka za ukuhani.

Sasa, ninauliza, ni kwa jinsi gani mapambano haya yanaendelea kwa kila mmoja wenu?

Rais David O. Mckay alisema: “Kuwepo kwa mwanadamu duniani ni jaribio kama ataweka juhudi zake, mawazo yake, nafsi yake, katika vitu ambavyo vinachangia kwenye faraja na kutosheleza asili ya mwili wake, au ikiwa ataweka kama [lengo] la maisha yake upatikanaji wa sifa za kiroho.”8

Mapambano haya kati ya asili zetu za kimwili na kiroho si jambo jipya. Katika mahubiri yake ya mwisho kwa watu wake, Mfalme Benjamini alifundisha kwamba “mwanadamu wa kawaida ni adui wa Mungu, na amekuwa tangu kuanguka kwa Adamu, na atakuwa, milele na milele, asipokubali ushawishi wa Roho Mtakatifu, na kumvua mtu wa kawaida na kuwa mtakatifu kupitia upatanisho wa Kristo aliye Bwana”9

Mtume Paulo alifundisha kwamba “wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho.

“Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani.”10

Inaonekana wazi kwangu kwamba mojawapo ya mambo muhimu tunayoweza kujifunza katika maisha haya ni jinsi ya kutilia mkazo asili yetu ya milele ya kiroho na kudhibiti matamanio yetu maovu. Hii haipaswi kuwa vigumu hivyo. Hata hivyo, roho yetu, ambayo imekuwepo muda mrefu zaidi kuliko mwili wetu, imefanikiwa katika kuchagua uadilifi juu ya uovu katika maisha kabla ya kuja duniani. Kabla ya dunia hii kuumbwa, tuliishi katika ulimwengu wa roho kama wana na mabinti wa Wazazi wa Mbinguni, waliotupenda na wanaoendelea kutupenda hata sasa.

Na ndiyo, ilitubidi kufanya maamuzi ya kubadili-maisha na chaguzi katika maisha yale kabla ya kuja duniani. Kila mtu aliyewahi kuishi au atakayewahi kuishi kwenye sayari hii alifanya uamuzi muhimu kuchagua kukubali mpango wa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya wokovu wetu. Kwa hiyo sote tulikuja duniani na rekodi iliyohakikiwa ya mafanikio ya asili ya kiroho na takdiri ya milele.

Fikiria kuhusu hilo kwa muda mfupi. Hivi ndivyo ulivyo na mimi hasa nilivyo na vile ambavyo umekuwa siku zote: mwana au binti wa Mungu, ukiwa na mizizi ya kiroho katika umilele na siku zijazo zilizofurika fursa zisizo na mwisho. Wewe ni—wa kwanza, wa muhimu, na daima—kiumbe wa kiroho. Na kwa hiyo wakati tunapochagua kuweka matamanio ya kimwili mbele ya asili yetu ya kiroho, tunachagua kitu ambacho ni kinyume na uhalisia, ukweli, halisi wa nafsi zetu kiroho.

Bado, hakuna ubishi kwamba mwili na misukumo ya kidunia vinatatiza ufanyaji wa maamuzi. Kukiwa na pazia la usahaulifu limewekwa kati ya ulimwengu wa roho kabla ya kuja duniani na ulimwengu huu tunaoishi, tunaweza kupoteza ulekeo wa uhusiano wetu na Mungu na asili yetu kiroho, na asili yetu ya kimwili inaweza kutoa kipaumbele kwenye kile tunachokitaka sasa. Kujifunza kuchagua mambo ya Roho juu ya mambo ya kimwili ni mojawapo ya sababu za msingi kwa nini uzoefu huu wa duniani ni sehemu ya mpango wa Baba wa Mbinguni. Ni sababu pia kwa nini mpango umejengwa juu ya msingi thabiti, wa uhakika wa Upatanisho wa Bwana na Mwokozi Yesu Kristo ili kwamba dhambi zetu, ikiwa ni pamoja na makosa tunayofanya wakati tunaporuhusu matamanio ya kimwili, ziweze kushindwa kupitia toba endelevu na tuweze kuishi tukiwa tumefokasi kiroho. Sasa ni muda wa kuthibiti hamu zetu za kimwili ili kukubaliana na mafundisho ya kiroho ya Kristo. Hiyo ndiyo sababu hatupaswi kuahirisha siku yetu ya toba.11

Toba, kwa hiyo, inakuwa silaha ya msingi katika mapambano yetu juu yetu wenyewe. Mkutano mkuu uliopita, Rais Russell M. Nelson alitaja mapambano haya na kutukumbusha kwamba “wakati tunapochagua kutubu, tunachagua kubadilika! Tunamruhusu Mwokozi kutubadilisha kuwa toleo zuri zaidi la sisi wenyewe. Tunachagua kukua kiroho na kupokea shangwe—shangwe ya ukombozi katika Yeye. Tunapochagua kutubu, tunachagua kuwa zaidi kama Yesu Kristo!12

Kila usiku ninapotafakari siku yangu katika sala kwa Baba yangu wa Mbinguni, ninaomba kusamehewa kama nilifanya chochote kibaya na kuahidi kujaribu kuwa mwema zaidi kesho. Ninaamini toba hii ya kawaida ya kila siku inasaidia roho yangu kuukumbusha mwili wangu kuhusu nani ana madaraka juu yangu.

Nyenzo nyingine ni fursa ya kila wiki ambayo sote tunayo kujifanya upya wenyewe kiroho kwa kushiriki sakramenti kwa ukumbusho wa Upatanisho na upendo mkamilifu ambao Bwana wetu na Mwokozi, Yesu Kristo anao kwetu.

Akina kaka na akina dada, ninawatia moyo kupunguza mwendo kidogo na kutafakari kuhusu wapi ulipo sasa katika kukomesha asili yako ya matamanio ya kimwili na kuwezesha asili yako takatifu, ya kiroho ili muda utakapofika, uweze kuingia katika ulimwengu wa roho kwenye muunganiko wa shangwe na wapendwa wako—kwa ajili ya hilo ninashuhudia na kwa unyenyekevu kuomba katika jina takatifu la Bwana Yesu Kristo, amina.

Chapisha