2010–2019
Tukio Lako Kubwa
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


2:3

Tukio Lako Kubwa

Mwokozi anatualika, kila siku, kuweka kando faraja na usalama wetu na kuungana Naye katika safari ya ufuasi.

Vijitu

Kitabu pendwa cha hadithi za watoto kilichoandikwa miaka mingi iliyopita huanza na sentensi “Katika shimo ardhini aliishi kijitu.”1

Hadithi ya Bilbo Baggins inahusu kijitu cha kawaida na kisichosifika ambacho kilipatiwa fursa ya kusifika—nafasi nzuri kwenye tukio na ahadi yenye tuzo kubwa.

Tatizo ni kuwa vijitu wenye kujiheshimu sana hawataki kujishughulisha na matukio makubwa. Maisha yao yote ni juu ya starehe. Vinafurahia kula milo sita kwa siku vinapoweza kuipata na kutumia siku zao katika bustani zao, vikisimuliana hadithi na wageni, vikiimba, vikipiga ala za muziki, na vikifurahia sifa katika shangwe za kawaida za maisha.

Hata hivyo, wakati Bilbo anapoelezwa kuhusu tukio kubwa lisilo la kawaida, kitu fulani kinaanza kufura katika kina cha moyo wake. Anaelewa kutoka mwanzoni kabisa kwamba safari hiyo itakuwa yenye changamoto. Pengine hatari. Upo hata uwezekano wa yeye kutorejea.

Na bado, wito wa tukio kubwa umefika kwenye kina cha moyo wake. Na hivyo, hiki kijitu kinaacha starehe nyuma na kuingia njia ya tukio kubwa ambayo itakichukua moja kwa moja hadi “huko na kurudi tena”2

Tukio lako kubwa

Pengine moja ya sababu hadithi hii inatoa mwangwi kwa wengi ni kwa sababu ni hadithi yetu vile vile.

Miaka mingi, iliyopita, hata kabla hatujazaliwa, katika umri uliopitwa na wakati na kugubikwa na kiza kwenye kumbukumbu zetu, sisi pia tulialikwa kuingia kwenye tukio kubwa lisilo la kawaida. Ilipendekezwa na Mungu, Baba yetu wa Mbinguni. Kukubali tukio hili kubwa ingemaanisha kuacha starehe na usalama wa uwepo Wake wa karibu. Ingemaanisha kuja duniani kwenye safari iliyojaa hatari na majaribu tusiyoyajua.

Tulijua isingelikuwa rahisi.

Lakini pia tulijua kwamba tungepata hazina za thamani, ikiwa ni pamoja na mwili wa nyama na mifupa na uzoefu wa shangwe kuu na huzuni za maisha ya duniani. Tungejifunza kujitahidi, kutafuta, na kupambana. Tungegundua kweli juu ya Mungu na sisi wenyewe.

Ndiyo, tulijua tungefanya makosa mengi njiani. Lakini pia tulipewa ahadi: kwamba kwa sababu ya dhabihu kuu ya Yesu Kristo, tungeweza kuoshwa kutokana na uvunjaji wetu wa sheria, kusafishwa na kutakaswa katika roho zetu, na, siku moja kufufuliwa na kuungana tena na wale tuwapendao.

Tulijifunza ni kiasi gani Mungu anatupenda. Yeye alitupatia uhai, na anataka tufanikiwe. Kwa sababu hiyo, Yeye alimwandaa Mwokozi kwa ajili yetu. “Hata hivyo,” Baba yetu wa Mbinguni alisema, “waweza kujichagulia mwenyewe, kwani imetolewa kwako.”3

Lazima palikuwepo na sehemu za tukio hilo kubwa la maisha ya duniani ambazo ziliwapa wasiwasi na hata kuwatisha watoto wa Mungu, kwani idadi kubwa ya dada na kaka zetu wa kiroho waliamua kinyume na hilo.4

Kwa kipawa na nguvu za maadili ya haki ya kujiamulia, tuliazimia kwamba uwezekano wa kile ambacho tungejifunza na kile ambacho tungeliweza kuwa milele kilikuwa kinastahili uthubutu.5

Na hivyo, tukitumaini ahadi na nguvu za Mungu na Mwanaye Mpendwa, tuliikubali changamoto hiyo.

Mimi niliikubali.

Vivyo hivyo na wewe.

Tulikubali kuacha usalama wa hali yetu ya kwanza na kuingia katika tukio letu wenyewe kubwa la “huko na kurudi tena.”

Wito kwenye Tukio Kubwa

Na bado, maisha ya duniani yana njia za kutuvuruga, ama siyo? Tunafikia kupoteza mwelekeo wa tamanio letu kuu, tukipendelea starehe na raha zaidi kuliko kukua na kuendelea.

Bado, kunabakia kitu fulani kisichoepukika, katika kina cha mioyo yetu, ambacho ni njaa ya lengo la juu na bora zaidi. Njaa hii ni moja ya sababu kwa nini watu huvutiwa kwenye injili na Kanisa la Yesu Kristo. Injili ya urejesho ni, kwa fasihi ya dhana akilini, ni kufanywa upya kwa wito huu wa tukio tulilolikubali miaka mingi iliyopita. Mwokozi anatualika, kila siku, kuweka kando faraja na usalama wetu na kuungana Naye katika safari ya ufuasi.

Ziko kona nyingi katika njia hii. Kuna milima, mabonde, na michepuko. Yawezekana hata kuna buibui wa kufikirika, mazimwi, na hata dragoni mmoja au wawili. Lakini kama utabaki katika njia na kumtumaini Mungu, hatimaye utaipata njia iendayo kwenye hatma yako tukufu na kurudi kwenye nyumba yako ya mbinguni.

Sasa basi unaanzaje?

Ni rahisi mno.

Toa moyo wako kwa Mungu

Kwanza unahitaji kuchagua kutoa moyo wako kwa Mungu. Jitahidi kila siku kumtafuta Yeye. Jifunze kumpenda. Na kisha acha upendo huo ukuongoze kujifunza, kuelewa, na kujifunza kutii amri za Mungu. Injili ya urejesho ya Yesu Kristo imetolewa kwetu katika njia ya wazi na rahisi ili mtoto mdogo aweze kuelewa. Bado injili ya Yesu Kristo inayo majibu ya maswali magumu zaidi katika maisha na ina kina kirefu na ugumu usiofahamika kwa urahisi ambao hata kwa mafunzo na tafakuri ya maisha yote, tunaweza kwa nadra sana kuelewa hata sehemu iliyo ndogo zaidi.

Kama utasita katika tukio hili kwa sababu ya kutilia shaka uwezo wako, ukikumbuka kwamba ufuasi si kuhusu kufanya vitu kikamilifu; ni kuhusu kufanya vitu kwa kukusudia. Ni chaguzi zako ambazo zinaonesha wewe ni nani hasa, zaidi kuliko uwezo wako.6

Hata pale unaposhindwa, unaweza kuchagua kutokata tamaa, badala yake gundua ujasiri wako, songa mbele, na inuka. Hilo ndilo jaribio kubwa la safari.

Mungu anajua kwamba wewe si mkamilifu, kwamba wakati mwingine utaanguka. Mungu hakupendi kidogo wakati unapohangaika kuliko wakati unaposhinda.

Kama mzazi mwenye upendo, Yeye anakutaka wewe uendelee tu kujaribu kwa kukusudia. Ufuasi ni kama kujifunza kupiga kinanda. Pengine kile unachoweza tu kufanya mwanzoni ni kupiga sauti zinazofahamika za “Chopsticks.” Lakini kama utaendelea kufanya mazoezi, tuni hizi rahisi siku moja zinaweza kufungua njia na kuwa sonata, rhapsodi, na konseto za kupendeza.

Sasa, siku hiyo yawezekana isije katika maisha haya, lakini itakuja. Yote Mungu anayoomba ni kwamba uendelee kujaribu.

Wafikie Wengine kwa Upendo

Kuna kitu cha kufurahisha, ni kama fumbo la maneno, kuhusu njia hii uliyochagua: njia pekee ya wewe kuendelea katika tukio lako kubwa la injili ni kuwasaidia wengine waendelee vile vile.

Kuwasaidia wengine ndiyo njia ya ufuasi. Imani, tumaini, upendo, huruma, na huduma hutusafisha sisi kama wafuasi.

Kupitia jitihada zako za kuwasaidia maskini na wenye uhitaji, kuwafikia wenye dhiki, tabia yako wewe mwenyewe inatakaswa na kuundwa, roho yako inapanuliwa, na unatembea wima zaidi.

Lakini upendo huu hauwezi kuja kwa matarajio ya malipo. Haiwezekani kuwa aina ya huduma ambayo inatarajia kutambuliwa, kusifiwa au upendeleo.

Wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo humpenda Mungu na watoto Wake pasipo kutarajia kitu fulani kama malipo. Tunawapenda wale wanaotukatisha tamaa, ambao hawatupendi. Hata wale wanaotufanyia mzaha, wanaotunyanyasa, na wanaotafuta kutuumiza.

Mnapojaza mioyo yenu kwa upendo msafi wa Kristo, mnaondoa nafasi ya chuki, hukumu, na kuaibisha. Mnatii amri za Mungu kwa sababu mnampenda . Katika mchakato huo, kidogo kidogo mnakuwa kama Kristo katika mawazo na matendo yako.7 Na ni tukio gani kubwa lingeweza kuzidi hili?

Shiriki Hadithi Yako

Kitu cha tatu tunachojitahidi kukijua katika safari hii ni kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo na kutoona haya kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo .

Hatufichi imani yetu.

Hatuiziki.

Kinyume chake, tunazungumza kuhusu safari yetu na wengine katika njia za kawaida na za asili. Hivyo ndivyo marafiki wafanyavyo—wanazungumza kuhusu mambo yaliyo muhimu kwao. Mambo yaliyo karibu na mioyo yao na yenye kuleta tofauti kwao.

Hilo ndilo unalofanya wewe. Unaelezea hadithi na uzoefu wako kama muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Wakati mwingine hadithi zako hufanya watu wacheke. Wakati mwingine zinawatoa machozi. Wakati mwingine zitawasaidia watu kuendelea katika subira, kuvutiwa, na ujasiri wa kukabiliana na saa nyingine, siku nyingine, na kuja karibu zaidi na Mungu.

Simulia matukio yako wewe mwenyewe, katika mitandao ya kijamii, katika makundi, kila mahali.

Mojawapo ya vitu vya mwisho Yesu alivyowaambia wanafunzi Wake ilikuwa ni kwamba walipaswa kwenda ulimwenguni kote na kusimulia hadithi juu ya Kristo aliyefufuka.8 Leo sisi pia kwa furaha tunalikubali agizo hilo Kuu.

Ni ujumbe mtukufu ulioje tulionao kuushiriki: kwa sababu ya Yesu Kristo, kila mwanamume, mwanamke, na mtoto anaweza kurudi nyumbani salama kwenye nyumba yao ya mbinguni na huko kukaa katika utukufu na haki!

Kuna habari njema nyingine nyingi zaidi za kushiriki.

Mungu amemtokea mwanadamu katika siku yetu! Tuna nabii aliye hai.

Naomba niwakumbusheni kwamba Mungu hakuhitaji wewe “kuuza” injili ya urejesho au Kanisa la Yesu Kristo.

Yeye anategemea tu kwamba hutaificha chini ya pishi.

Na kama watu wataamua kuwa Kanisa si kwa ajili yao, huo ni uamuzi wao.

Haimaaniisha kuwa wewe umeshindwa. Endelea kuwatendea kwa ukarimu. Wala haikuzuii kuwaalika tena.

Tofauti kati ya mawasiliano ya kawaida ya kijamii na ufuasi wa huruma, ujasiri ni— mwaliko!

Tunawapenda na kuwaheshimu watoto wote wa Mungu, bila kujali nafasi zao katika maisha, bila kujali rangi au dini, bila kujali maamuzi yao ya maisha.

Kwa ajili ya sehemu yetu, tutasema,”Njoo na uone! Jionee mwenyewe namna gani kutembea njia ya ufuasi itakavyokuwa yenye thawabu na ya kiungwana.”

Tunawaalika watu “kuja na kusaidia, tunapojaribu kuufanya ulimwengu kuwa mahali pazuri.

Na tunasema, “Njoo na ukae! Sisi ni kaka na dada zako. Sisi si wakamilifu. Tunamtumaini Mungu na tunatafuta kutii amri Zake.

“Ungana nasi, na utatufanya sisi kuwa watu bora zaidi. Na, katika mchakato huo, nawe utakuwa bora vile vile. Na tufanye tukio hili kubwa kwa pamoja.”

Je, napaswa kuanza lini?

Wakati rafiki yetu Bilbo Baggins alipohisi wito wa kwenda kwenye tukio kubwa ukisisimka ndani yake, aliamua kupata usingizi mnono usiku ule, kufurahia kifungua kinywa kizito, na kuanza mapema asubuhi.

Bilbo alipoamka, alitambua kuwa nyumba yake ilikuwa chafu, na ilikuwa karibu avutwe mbali na mpango wake madhubuti.

Lakini rafiki yake Gandalf alipokuja na kumwuliza, “Lini wewe utakuja?”9 Ili kuwa sambamba na rafiki yake, Bilbo alipaswa kuamua yeye mwenyewe nini cha kufanya.

Na hivyo, kile kijitu cha kawaida kisichosifika kilijikuta kikiruka nje ya mlango wa mbele wa nyumba yake hadi kwenye njia ya tukio kubwa kwa haraka kiasi kwamba hata kikasahau kofia yake, fimbo yake ya kutembelea, na kitambaa cha mfukoni. Na hata kiliacha kifungua kinywa chake cha pili bila kumalizika.

Pengine kuna somo kwa ajili yetu hapa vile vile.

Kama mimi na wewe tumehisi msisimko wa kujiunga kwenye tukio kubwa la kuishi na kusimulia kile Baba wa Mbinguni mwenye upendo alichokiandaa kwa ajili yetu miaka mingi iliyopita, ninawahakikishieni, leo ndiyo siku ya kumfuata Mwana wa Mungu na Mwokozi wetu kwenye njia Yake ya kuhudumu na ufuasi.

Tungeliweza kutumia muda wote wa maisha tukisubiri muda huo wakati kila kitu kinapojipanga kikamilifu. Lakini sasa ndio ule wakati wa kuweka msimamo kikamilifu wa kumtafuta Mungu, kuwahudumia wengine, na kushiriki na wengine uzoefu wetu.

Sahau kofia yako, fimbo yako ya kutembelea, kitambaa chako cha mkononi na nyumba yako iliyo chafu.10

Kwetu sisi wengine ambao tayari tunatembea njia hiyo, tuwe jasiri, tuwe na huruma, tujiamini, na tuendelee!

Kwa wale walioiacha njia hiyo, tafadhalini rudini, unganeni nasi tena, tufanyeni wenye nguvu zaidi.

Na kwa wale ambao bado hawajaanza, kwa nini kuchelewa? Ikiwa mnataka kupata uzoefu wa maajabu ya safari hii kubwa ya kiroho, weka mguu juu ya tukio lako kuu! Zungumza na wamisionari. Ongea na rafiki zako Watakatifu wa Siku za Mwisho. Zungumza nao juu ya kazi hii ya kushangaza na ya maajabu.11

Ni muda wa kuanza!

Njoo, Ujiunge Nasi!

Kama unahisi kwamba maisha yako yangekuwa na maana zaidi, kusudi la juu zaidi, mahusiano imara ya kifamilia, na uhusiano wa karibu zaidi na Mungu; tafadhali, njoo uungane nasi.

Kama unatafuta jumuiya ya watu ambao wanafanya kazi ili kuwa toleo lao bora zaidi, kuwasaidia walio kwenye uhitaji, na kuufanya ulimwengu huu kuwa mahali bora zaidi, njoo uungane nasi.

Njoo na uone kile safari hii ya kushangaza, ya maajabu, na ya tukio kubwa ni kitu gani hasa.

Ukiwa njiani utajitambua mwenyewe.

Utagundua maana.

Utamgundua Mungu.

Utagundua safari ya tukio kubwa zaidi na tukufu zaidi katika maisha yako.

Juu ya hili ninashuhudia katika jina la Mkombozi na Mwokozi wetu, Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. J. R. R. Tolkien, The Hobbit or There and Back Again (Boston: Houghton Mifflin, 2001), 3.

  2. Kichwa cha habari kidogo cha The Hobbit.

  3. Musa 3:17.

  4. Ona Ayubu 38:4–7 (wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha); Isaya 14:12–13 (“nitakiinua kiti changu juu kupita nyota za Mungu); Ufunuo 12:7–11 (kulikuwa na vita mbinguni).

  5. “Nabii Joseph Smith alielezea haki ya kujiamulia kama ‘utegemezi ule uhuru wa fikra ambao mbingu kwa rehema zimeutoa kwa familia ya mwanadamu kama moja ya kipawa chake cha juu’ [Mafundisho ya Nabii Joseph Smith, comp. Joseph Fielding Smith (1977), 49]. Huu ‘uhuru wa fikra,’ au haki ya kujiamulia, ni nguvu ambayo huwaruhusu watu kuwa ‘mawakala juu yao wenyewe ’ (M&M 58:28). Inajumuisha vyote kutumia haki ya kuchagua kati ya mema na mabaya au kutofautisha viwango vya wema na uovu na pia fursa ya kupata uzoefu wa matokeo ya uchaguzi huo. Baba wa Mbinguni anawapenda sana watoto Wake kiasi kwamba anataka sisi kufikia uwezekano wetu kamili—kuwa kama Yeye alivyo. Ili kuendelea, mtu lazima awe na hulka yenye uwezo wa kufanya uchaguzi wake anaotamani. Haki ya kujiamulia ni muhimu sana kwenye mpango Wake kwa ajili ya watoto Wake kwamba ‘hata Mungu hakuweza kuwafanya wanadamu wawe kama Yeye pasipo kuwafanya wawe huru’ [David O. McKay, “Twende Wapi?, Au Life’s Supreme Decision,” Deseret News, June 8, 1935, 1]” (Byron R. Merrill, “Agency and Freedom in the Divine Plan,” katika Window of Faith: Latter-day Saint Perspectives on World History [2005], 162).

  6. Katika riwaya yake Harry Potter na the Chamber of Secrets, mwandishi J. K. Rowling anamfanya Hogwarts headmaster Dumbledore kusema jambo linalofanana na Harry Potter mdogo. Ni ushauri wa kupendeza kwetu pia. Nimeutumia kwenye ujumbe kabla na ninafikiri una thamani kurudiwa.

  7. “Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa: lakini twajua ya kuwa, atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo” (1 Yohana 3:2; msisitizo umeongezwa).

    Wakati mabadiliko hayo yanaweza kuwa kupita uwezo wetu wa kuelewa, “Roho mwenyewe anashuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu:

    “Na kama tu watoto, basi tu warithi; warithi wa Mungu, na warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.

    “Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama ule utukufu utakaofunuliwa kwetu” (Warumi 8:16-18; msisitizo umeongezwa).

  8. Ona Mathayo 28:16–20.

  9. Tolkien, The Hobbit, 33.

  10. Ona Luka 9:59 –62.

  11. Ona LeGrand Richards, A Marvelous Work and a Wonder, rev. ed. (1966).