2010–2019
Mguso wa Mwokozi
Mkutano Mkuu wa Oktoba 2019


2:3

Mguso wa Mwokozi

Wakati tunapokuja Kwake, Mungu atakuja kutuokoa, iwe kutuponya au kutupatia nguvu ya kukabiliana na hali yoyote.

Takribani miaka 2,000 iliyopita, Mwokozi alishuka kutoka mlimani baada ya kufundisha Mafundisho na kanuni zingine za injili. Wakati akitembea, alifuatwa na mtu ambaye alikuwa na ukoma. Mtu yule alionesha heshima na unyenyekevu wakati alipopiga magoti mbele ya Kristo, akitafuta msaada wa mateso yake. Ombi lake lilikuwa rahisi: “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.”

Kisha Mwokozi alinyoosha mkono wake na, kumgusa, akisema, “Nataka; takasika.”1

Tunajifunza hapa kwamba Mwokozi wetu mara zote anataka kutubariki. Baadhi ya baraka huja haraka, zingine huchukua muda, na baadhi zitakuja baada ya maisha haya, lakini baraka zitakuja kwa muda wake.

Kama vile mwenye ukoma, tunaweza kupata nguvu na faraja katika maisha haya kwa kukubali mapenzi Yake na kujua kwamba Yeye anataka kutubariki. Tunaweza kupata nguvu za kukabiliana na changamoto yoyote, kushinda majaribu, na kuelewa na kuvumilia hali zetu ngumu. Hakika, katika mojawapo ya nyakati za kuangamiza za maisha Yake, nguvu ya mwokozi ya kuvumilia iliongezwa pale Alipomwambia Baba Yake, “Mapenzi Yako yatimizwe.”2

Mwenye ukoma hakuomba kuponywa kwa njia ya kujikweza au kulazimisha. Maneno yake yalionesha tabia ya unyenyekevu, yenye matumaini makubwa lakini pia kwa nia ya dhati kwamba mapenzi ya Mwokozi yafatimie. Huu ni mfano wa tabia ambayo tunatakiwa kuja nayo kwa Kristo. Tunaweza kuja kwa Kristo tukiwa na uhakika kwamba nia Yake kwa sasa na mara zote itakuwa nzuri kwetu kwa ajili ya maisha ya hapa duniani na ya milele. Yeye ana mtazamo wa milele ambao sisi hatuna. Lazima tuje kwa Kristo tukiwa na nia ya dhati kwamba mapenzi yetu yamezwe katika mapenzi ya Baba kama vile ilivyokuwa kwake.3 Hii itatuandaa kwa ajili ya uzima wa milele.

Ni vigumu sana kufikiria maumivu ya mwili na hisia ambayo alikuwa nayo mwenye ukoma ambaye alikuja kwa Mwokozi. Ukoma huathiri neva na ngozi, ukisababisha uharibifu wa viungo na ulemavu. Kwa nyongeza, ilipelekea unyanyapaa mkubwa kutoka kwenye jamii. Mtu ambaye alipatwa na ukoma alitakiwa kuwaacha wapendwa wake na kuishi kwa kujitenga na jamii. Wenye ukoma walichukuliwa kama wachafu, vyote kimwili na kiroho. Kwa sababu hii, sheria ya Musa ilihitaji kwamba wenye ukoma wavae nguo zilizotatuka na kupaza sauti “Najisi!” wakati wakitembea.4 Wakiumwa na kudharauliwa, wenye ukoma waliishia kuishi katika magofu na mapango.5 Si vigumu kufikiria kwamba mwenye ukoma aliyemwendea Mwokozi alikuwa amevunjika moyo.

Wakati mwingine—katika njia moja au nyingine—sisi pia tunaweza kuhisi kuvunjika moyo, iwe ni kutokana na matendo yetu wenyewe au ya wengine, kutokana na hali ambazo tunaweza kuzidhibiti au la. Katika nyakati hizo, tunaweza kuweka mapenzi yetu katika mikono Yake.

Miaka kadhaa iliyopita, Zulma—mke wangu, nusu yangu ya kupendeza, sehemu yangu ya kupendeza—alipokea habari za kusikitisha wiki mbili tu kabla ya ndoa ya mmoja wa watoto wetu. Alikuwa na uvimbe katika tezi ya mate, na ulikuwa ukikua kwa kasi. Uso wake ulianza kuvimba, na alitakiwa mara moja kufanyiwa upasuaji. Mawazo mengi yalikuwa kichwani mwake na kujaza moyo wake. Je, uvimbe ulikuwa wa seli za saratani? Je, mwili wake ungeponaje? Je, uso wake ungepooza? Je, maumivu yangekuwa kiasi gani? Je, uso wake ungekuwa na kovu daima? Je, uvimbe ngerudi tena baada ya kuondolewa? Je angeweza kuhudhuria ndoa ya kijana wetu? Akiwa amelala kwenye chumba cha upasuaji, alihisi kuvunjika moyo.

Katika wakati huo muhimu, Roho alimnong’oneza kwamba alitakiwa kukubali mapenzi ya Baba. Kisha aliamua kuweka tumaini lake kwa Mungu. Alipata hisia zenye nguvu kamba iwe matokeo yoyote yale, mapenzi ya Bwana yangekuwa mazuri zaidi kwa ajili yake. Punde alizama usingizini kwa ajili ya upasuaji.

Baadaye, aliandika kishairi katika shajara yake: “Katika meza ya mpasuaji nilinyenyekea mbele Zako, na kukubali mapenzi Yako, nilisinzia. Nilijua ningeweza kukuamini Wewe, nikijua kwamba hakuna kibaya kinachoweza kutoka Kwako.”

Alipata nguvu na faraja kutokana na kusalimisha mapenzi yake kwenye yale ya Baba. Siku ile, Mungu alimbariki sana.

Bila kujali hali zetu zinavyoweza kuwa, tunaweza kutumia imani yetu kuja kwa Kristo na kumpata Mungu tunayeweza kumuamini. Kama mmoja wa watoto wetu, Gabriel, alivyowahi kuandika:

Kulingana na nabii, uso wa Mungu unag’aa kuliko jua

Na nywele Zake ni nyeupe kuliko theluji

Na sauti Yake inarindima kama mto utiririkao kwa kasi,

na mwanadamu si kitu katika Hayo. …

Ninanyenyekezwa wakati ninapotambua kuwa hata mimi si kitu.

Na hapo ndipo ninapotafuta tafuta kwenye njia yangu mungu ambaye ninaweza kumuamini.

Na hapo tu ndipo ninapompata Mungu ambaye ninaweza kumuamini.6

Mungu ambaye tunaweza kumuamini anatoa hamasa kwenye tumaini letu. Tunaweza kumuamini Yeye kwa sababu Anatupenda na anataka kile kilicho bora sana kwetu katika kila hali.

Mwenye ukoma alisonga mbele kwa sababu ya nguvu itokanayo na tumaini. Dunia haikumpatia suluhisho, wala faraja. Hivyo, mguso rahisi wa Mwokozi lazima ulikuwa kama mguso wa faraja kwa nafsi yake yote. Tunaweza tu kufikiria hisia za kina za shukrani mwenye ukoma alizokuwa nazo katika mguso wa Mwokozi, hasa pale aliposikia maneno “Nataka; takasika.”

Hadithi inasimulia kwamba “na mara ukoma wake ukatakasika.”7

Nasi pia tunaweza kuhisi mguso wa Mwokozi wa mkono wake wa upendo, wa uponyaji. Ni shangwe iliyoje, tumaini, na shukrani huja kwenye nafsi zetu kwa kujua kwamba Yeye anataka kutusaidia kuwa wasafi! Wakati tunapokuja Kwake, Mungu atakuja kutuokoa, iwe kutuponya au kutupatia nguvu ya kukabiliana na hali yoyote.

Kwa kiwango chochote, kukubali mapenzi Yake—na si mapenzi yetu—hutusaidia kuelewa hali zetu. Hakuna kibaya ambacho hutoka kwa Mungu. Yeye anajua kilicho bora sana kwetu. Labda Yeye hataondoa mizigo yetu kwa mara moja. Wakati mwingine Yeye anaweza kuifanya mizigo hiyo kuwa miepesi, kama ilivyokuwa kwa Alma na watu wake.8 Hatimaye, kwa sababu ya maagano, mizigo itainuliwa,9 aidha katika maisha haya au katika Ufufuo mtakatifu.

Nia ya dhati kwamba mapenzi Yake yatimizwe, pamoja na uelewa wa asili takatifu ya Mkombozi wetu, hutusaidia kukuza aina ya imani ambayo mwenye ukoma aliionesha ili kuweza kutakaswa. Yesu Kristo ni Mungu wa upendo, Mungu wa tumaini, Mungu wa uponyaji, Mungu ambaye anataka kutubariki na kutusaidia kuwa wasafi. Hicho ndicho Yeye alikitaka kabla ya kuja hapa duniani wakati Alipojitolea kutuokoa wakati tunapoanguka katika makosa. Hicho ndicho Yeye alichokitaka katika Gethsemane wakati Alipokabiliana na mauvivu yasiyoelezeka ya kibinadamu wakati wa majonzi ya kulipia gharama ya dhambi. Hicho ndicho anachokitaka sasa wakati anapotutetea mbele za Baba.10 Na ndiyo maana sauti Yake bado huita: “Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.”11

Anaweza kutuponya na kutuinua kwa sababu Ana uwezo wa kufanya hivyo. Yeye alijichukulia juu Yake maumivu ya mwili na roho ili kwamba Yeye angejazwa na rehema ili kwamba aweze kutusaidia katika mambo yote na kutuponya na kutuinua.12 Maneno ya Isaya, kama yalivyonukuliwa na Abinadi, yanaelezea vizuri na kwa ushawishi:

“Kwa hakika amejichukulia unyonge wetu, na kubeba huzuni zetu. …

“… Alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu; adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake; na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”13

Suala sawa na hili linafundishwa katika shairi hili:

“O Seremala wa Nazareti,

Moyo huu, uliovunjika mpaka kutopona,

Maisha haya, yaliyozongwa kukaribia kifo,

Oo, unaweza kuyatengeneza, Seremala?”

Na kwa mikono yake ya ukarimu na iliyo tayari,

Maisha yake mazuri yameshukwa katika

Maisha yetu yaliyoharibika, mpaka yanatengemaa

Uumbaji mpya—”vitu vyote vipya.”

“Kukata tamaa [tabia] ya moyo,

Hamu, malengo, tumaini, na imani,

Vifinyange kuwa sehemu sahihi,

O, Seremala wa Nazareti!”14

Ikiwa unahisi kwamba kwa njia yoyote ile hauko safi, ikiwa unahisi kuvunjika moyo, tafadhali jua kwamba unaweza kutakaswa, unaweza kurekebishwa, kwa sababu Yeye anakupenda. Amini kwamba hakuna chochote kibaya kinachoweza kutoka Kwake.

Kwa sababu Yeye “alishuka chini ya vitu vyote,”15 Yeye anafanya iwezekane kwa vitu vyote ambavyo vimevunjwa katika maisha yetu kutengenezwa, na hivyo tunaweza kupatanishwa na Mungu. Kupitia Yeye, vitu vyote hupatanishwa, vyote vilivyoko duniani na vilivyo mbinguni, akileta “amani kupitia damu ya msalaba wake.”16

Acha tuje kwa Kristo, tukipiga hatua zote muhimu. Tunapofanya hivyo, acha mtazamo wetu uwe ule wa kusema “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.” Kama tutafanya hivyo, tunaweza kupokea mguso wa uponyaji wa Bwana, pamoja na sauti Yake tamu: “Nataka; takasika.”

Mwokozi ni Mungu ambaye tunaweza kumuamini. Yeye ni Kristo, Mpakwa mafuta, Masiya, ambaye katika yeye ninashuhudia katika jina Lake takatifu, hata Yesu Kristo, amina.